ILIPOISHIA:
“Ni
stori ndefu Rahma ila naomba unielewe nitakachokwambia,” nilisema, nikashusha
pumzi ndefu na kuamua liwalo na liwe. Nilitaka kwenda moja kwa moja, kwamba
baba yake na baba yangu walikuwa wachawi. Cha ajabu, kila nilipotaka kusema
hivyo, mdomo ulikuwa mzito, nikawa naumauma maneno, hali iliyosababisha
anikazie macho.
SASA
ENDELEA...
“Mbona sikuelewi Togo?”
“Ni kuhusu wazazi wetu.”
“Wamefanya nini?”
“Wanajihusisha na...” kabla sijamalizia
nilichotaka kukisema, jambo la ajabu lilitokea. Yule muuzaji wa lile duka,
alifungua mlango na kutoka huku akikimbia, cha ajabu, hakuwa amevaa nguo hata
moja.
“Vipi kwani mbonaumeshtuka?”
“Umemuona?”
“Nani? Vero? Nini cha ajabu kwani?”
Rahma alinishangaa sana, na mimi nikawa namshangaa. Yaani mtu atoke dukani
akiwa mtupu, halafu aanze kukimbia mitaani, siyo jambo la kushangaza hilo?”
“Itakuwa labda kuna anaenda kuomba
chenji, tuendelee na mazungumzo yetu,” Rahma alizidi kunishangaza. Sikuelewa
kwamba alikichukuliaje kitendo kile kiasi cha kutokipa uzito hata kidogo, hata
baadhi ya wateja waliokuwa wamekaa upande wa pili, nao wakipata vinywaji,
hawakuonesha kushtuka kabisa.
“Ndiyo atoke bila nguo?”
“Togo, umeanza kuchanganyikiwa nini?”
“Rahma, ina maana huoni kama hajavaa
nguo yule? Kwa hiyo kumbe ndiyo maana alikuwa anajificha dukani?”
“Nani hajavaa nguo? Una matatizo gani
Togo? Usije kunitia aibu hapa, hebu maliza twende,” alisema Rahma huku
akimalizia soda yake. Nadhani alihisi huenda nikatokewa na maruweruwe kama yale
yaliyokuwa yakinitokea.
“Basi Rahma, tuendelee na mazungumzo
yetu,” nilijaribu kumsihi lakini alishaonesha kama ameingiwa na hofu ndani ya
moyo wake, hakutaka kukaa tena eneo lile, ikabidi nimalizie soda yangu na
kusimama.
Sikuwa nimemlipa yule muuzaji, lakini
Rahma aliniambia kwamba nisijali yeye atampa hata baadaye. Nilijisikia vibaya
sana ndani ya moyo wangu kwa jinsi Rahma alivyonipuuza ila sikutaka kumuonesha.
Kwa jinsi alivyonichukulia, hata kama
ningemweleza kile kilichofanya nikakutana naye pale, huenda pia angenipuuza kwa
hiyo nilichokifanya, niliamua kunyamaza na dukuduku langu moyoni.
“Hujamalizia ulichotaka kuniambia,”
alisema Rahma wakati tukitembea kurudi ndani, nikamwambia asiwe na wasiwasi
nitamueleza siku nyingine.
“Kwani siku hizi umeshapata mwanamke
mwingine anayekuzuzua?”
“Hapana Rahma, na ndiyo maana nilitaka
kuzungumza na wewe, lakini basi tuyaache.”
“Sikuelewi Togo na kama unaona
ulichokifanya kwangu ni sawa, wala mimi sina cha kusema ila kumbuka chozi langu
haliwezi kwenda bure,” alisema Rahma, nikajaribu kumbembeleza lakini ilikuwa
sawa na kazi bure.
Mpaka tunaingia ndani, Rahma alikuwa
akiendelea kulalamika tu, akaniambia anashukuru kwa yote niliyomfanyia na
kumuumiza moyo wake. Nilishindwa cha kusema, ikabidi ninyamaze tu, bado wale
madereva bodaboda na Bajaj pale nje hawakuwa wamerejea.
Tuliingia ndani lakini Rahma hakutaka
kabisa kujishughulisha na mimi, alienda moja kwa moja sebuleni, mimi nikaenda
chumbani huku nikiwa nimekosa kabisa furaha. Nilijilaza kitandani, nikaanza
kutafakari tukio la yule muuzaji wa lile duka.
Nilichokihisi kwa harakaharaka, huenda
alikuwa akitumia nguvu za kishirikina kwenye biashara yake maana nimewahi
kusikia kwamba kuna wafanyabiashara ambao ukiingia kwenye duka lake au sehemu
anayofanyia biashara, hata kama umevaa nguo, anakuona kila kitu lakini wapo
wengine ambao inakuwa kinyume chake, kwamba muuzaji anakaa kwenye biashara
akiwa hana nguo hata moja ingawakwa macho ya kawaida anaonekana amevaa nguo.
Lengo la kufanya hivyo inakuwa ni kuvutia
wateja na kiukweli hata kwenye lile duka la pale nje, lilikuwa kubwa lenye kila
kitu unachokihitaji na kiukweli alikuwa akifanya sana biashara kwa sababu kwa
muda mfupi tu tuliokaa pale, wateja walikuwa hawakauki.
“Ulitaka kumwambia nini Rahma,” sauti ya
baba ilinizindua kutoka kwenye lindi la mawazo. Alikuwa amesimama pembeni ya
kitanda changu, hata sikukumbuka ameingia saa ngapi, nilichoshtuka ni kumuona
akiwa ndani.
“Mimi?” niliongea kwa kubabaika huku
nikiinuka pale kitandani.
“Kwani nazungumza na nani?” baba
aliniuliza akionesha kuwa na jazba, nikawa nababaika. Kwa jinsi ilivyoonesha,
alikuwa anajua kwamba nilitaka kumweleza Rahma ukweli, jambo ambalo walinionya
sana kwamba sitakiwi kutoa siri za jamii yetu kwa mtu yeyote asiyehusika.
“Tulikuwa tunapiga stori za kawaida tu.”
“Stori za kawaida ndiyo muende dukani?”
baba alinihoji huku akinitazama kwa macho ya ukali, sikuwa na cha kujibu na kwa
jinsi baba alivyo, nilitegemea kabisa kwamba pale lazima angenizibua makofi,
nikawa nimekaa ‘attention’.
“Kuna maagizo yako kutoka kwa Mkuu,
usiku itabidi tukupeleke sehemu, umeyaanza mwenyewe lazima uyamalize,” baba
alisema huku akigeuka na kuanza kuondoka, nikabaki na mshangao mkubwa, nikiwa
sijui alichokimaanisha. Akiwa anamalizikia kutoka, aligeuka na kunitazama kwa
macho makali.
“Ole wako ufumbue domo lako!” Nilishusha
pumzi ndefu, mambo yalianza kuwa mengi na kunielemea kwa sababu kabla moja
halijaisha, lingine lilikuwa likiibuka. Kwa jinsi nilivyozungumza na baba yake
Rahma, nilitambua kwamba hizo salamu kutoka kwa Mkuu lazima zitakuwa zinahusu
masharti ya uamuzi nilioufanya.
Niliona kama muda unaenda taratibu sana,
sikutoka chumbani, hata chakula nililetewa kulekule na Rahma ingawa safari hii
alionesha kuwa na chuki za waziwazi kwangu maana hakutaka hata kunisemesha wala
kunitazama usoni.
Hatimaye jioni iliwadia, baba na baba
yake Rahma, wakiwa tayari wameshajiandaa, walinifuata chumbani na kuniambia
muda wa safari umewadia, wakanitaka nijiandae, baba Rahma akanipa koti kubwa
jeusi.
“Kwani tunaenda wapi?”
“Jiandae bwana, maswali mengi ya nini?”
alisema baba kama kawaida yake, nikajiandaa na muda mfupi baadaye, safari
ilianza. Kwa jinsi nilivyokuwa nimevaa, haikuwa rahisi kwa mtu yeyote
kunitambua, lile koti lilinibadilisha kabisa. Tulitoka na kuelekea moja kwa moja
kwenye stendi ya mabasi ya Makumbusho, tukapanda kwenye ‘coaster’ moja ambayo
mbele ilikuwa imeandikwa kwamba inaenda Bagamoyo. Sikuwa nimewahi kufika
Bagamoyo zaidi ya kusoma tu darasani kuhusu mji huo wa kihistoria.
Basi tulienda mpaka tulipofika sehemu
moja iitwayo Mlingotini, tukateremka kwenye gari na kuvuka barabara, tukaanza
kutembea kwa miguu. Tulienda umbali mrefu sana maana mpaka inafika saa tano za
usiku, bado tulikuwa tukitembea.
Hatimaye tuliwasili kwenye eneo
lililokuwa na nyumba kama tatu hivi, moja ikiwa imeezekwa kwa bati na zile
nyingine kwa makuti, baba akabisha hodi ambapo sauti ya mwanamke ilisikika
ikitukaribisha.
Muda mfupi baadaye, mwanamke mmoja mzee
alitoka, ilionesha alikuwa akifahamiana vizuri na baba na baba yake Rahma kwani
aliwakaribisha kwa uchangamfu, tukaingia ndani na kukaa kwenye jamvi lililokuwa
pale sebuleni.
“Ndiyo huyu?” aliuliza yule mwanamke,
baba akamjibu kwamba ndiyo mimi, sikuelewa kwamba ndiyo mimi nimefanyaje na kwa
nini ameniuliza, ikabidi niwe mpole.
“Mchumba hujambo? Ukifanikiwa na mimi
nataka uninunulie gari,” alisema yule mwanamke huku akitabasamu, mapengo yake
yakaonekana. Sikuelewa kwa nini amesema vile, nikazidi kuwa gizani. Alinishika
mkono na kuwapa ishara akina baba kwamba wamsubiri, tukatoka nje na kwenda kwenye
kibanda cha makuti.
Wakati tunatoka, nilimsikia baba
akimwambia baba Rahma kwamba kuwana mtoto kama mimi ni hasara, wakacheka.
Sikuelewa kwa nini baba amesema vile lakini sikujisikia vibaya maana mimi na
baba kukwaruzana ni jambo la kawaida kabisa, ingawa mimi ndiyo nilikuwa mwanaye
kipenzi.
“Nimepata salamu zako kwamba umechagua
kuwa tajiri, ombi lako limekubaliwa lakini kuna masharti inatakiwa kabla siku
zako saba hazijaisha, uwe umeshaanza kuyafuata, vinginevyo utakufa,” alisema
yule mwanamke, macho yakanitoka pima.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment