Tuesday, January 30, 2018

SEVEN DAYS IN HELL (Siku Saba Kuzimu)- 58




ILIPOISHIA:
“Yule kule aliyekuwa ananguruma kama mnyama ni nani?” Firyaal aliuliza swali, nikawaona wenzake wote wakitingisha vichwa, kuunga mkono swali hilo.
“Ni stori ndefu kidogo, ngoja nitawaeleza lakini njooni kwanza huku niwape dawa,” alisema.
SASA ENDELEA...
Wote wakamfuata mpaka kule kwenye kile chumba walichokuwa wamelala, akawaamuru wote wakae kwenye mkao wa kutengeneza duara, akatoka na kuelekea chumbani kwake, aliporudi muda mfupi baadaye, alikuwa na kichupa kidogo kilichokuwa na mafuta yaliyokuwa yananukia vizuri sana, akaanza kumpaka mafuta yale kichwani na usoni mmoja baada ya mwingine.
“Itabidi mkae dakika ishirini kisha mkaoge, baada ya hapo tutakamilisha kazi ya kumzindua Shenaiza, tumeelewana?”
“Mi nasikia njaa inaniuma sana.”
“Hatutakiwi kula chchote mpaka tukamilishe kwanza kazi hii, ukishakula tu utasababisha nguvu kubwa ambazo zinatakiwa kutumika kichwani mwako, zielekezwe tumboni kwa ajili ya mmeng’enyo wa chakula, jambo linaloweza kusababisha tukakwama, tumeshakula mbuzi mzima, hatuwezi kushindwa kumalizia mkia,” alisema Junaitha akimjibu Firyaal.

Wote walionesha kuelewa walichoambiwa na kwa sababu shauku ya kila mmoja ilikuwa ni kumuona Shenaiza akisimama tena, walikubaliana naye. Ilibidi mimi niwaache wakiendelea kusubiri hizo dakika ishirini ziishe, nikaenda kwenye chumba changu ambacho tangu niingie ndani ya nyumba hiyo nilikitumia kwa muda mfupi sana.
Kwa jinsi nilivyokuwa nikijisikia uchovu, nilipoingia tu, nilienda kujibwaga kitandani, nikawa najisikia jinsi mwili ulivyokuwa ukivuta kwa uchovu. Nilitulia nikitafakari mambo mengi ndani ya kichwa changu. Sikujua mwisho wa yote yale ungekuwa nini, nilishachoka kutangatanga, nilitamani haya mambo yafike mwisho ili nirudie maisha yangu ya kawaida kama zamani.
“Vipi umelala?”
“Hapana, nimejipumzisha tu,” alisema Junaitha huku akifungua mlango na kuingia ndani ya kile chumba. Nilijihisi kukosa amani kwa sababu nilijua kwa vyovyote, lazima akina Raya watamuona Junaitha akitoka chumbani kwangu na kuwafanya waanze kutuhisi vibaya.
Ni kweli alikuwa amenilambisha asali ambayo sikuwa tayari kuiacha lakini suala la tofauti ya umri kati yetu, lilinifanya niwe na aibu sana kuwa naye. Nilitaka kila kitu kati yetu kiendelee kuwa siri kwa sababu niliamini umebaki muda mfupi kabla ya kukamilisha mambo yote yaliyokuwa yametuelemea kisha kila mtu akaendelee na maisha yake.
Niliamini nitakuwa huru zaidi nikiwa kwangu ambapo kichwani nilishapanga kwamba mambo yakitulia tu, naenda kutafuta chumba sehemu nyingine na kuhama kabisa eneo lile.
“Najua umebaki na maswali mengi kuhusu kile ulichokiona kule ndani lakini halikuwa lengo langu kukuficha ndiyo maana nimekuja ili tuzungumze.”
“Ok sawa Junaitha lakini sidhani kama huu ni muda muafaka wa sisi kuzungumza, watatushtukia.”
“Usijali, nimewapa dawa maalum ya usingizi, hakuna atakayeamka sasa hivi, inabidi walale ili tupate nafasi nzuri ya kukamilisha hiki tulichokianza,” alisema Junaitha huku akinisogelea pale kitandani nilipokuwa nimelala, akanibusu kwenye paji la uso wangu na kunifanya nisisimke kiasi. Sikusisimka sana kama kawaida yangu kwa sababu ya uchovu na maswali mengi yaliyokuwa yakitembea ndani ya kichwa changu.
“Niulize chochote unachotaka kujua,” alisema huku naye akijilaza pembeni yangu, akawa anatazama juu kama mimi nilivyokuwa nimelala.
“Ndani ya kile chumba kuna nini?”
“Kuna vitu vingi vinavyohusu mambo ya kichawi.”
“Kwani wewe ni mchawi?” nilimuuliza swali ambalo lilimfanya ashushe pumzi ndefu, akajigeuza na kuwa ananitazama.
“Sisi sote ni wachawi ingawa tunatofautiana kiwango cha uchawi.
“Sikuelewi, una maanisha nini?”
“Sikupenda kukwambia hili lakini ngoja tu nikwambie, mimi hapa ninapoishi, ndipo alipokuwa anaishi marehemu baba yangu na mama yangu. Ndani ya familia yetu, sisi tulizaliwa watoto wawili tu, mimi na dada yangu aitwaye Munaitha, ambaye ndiyo mama mzazi wa Shamila, rafiki yako,” alisema.
“Hata hivyo, kwa kipindi kirefu kumbe baba yetu alikuwa akijihusisha na mambo ya kichawi bila sisi kujua, mpaka alipokuja kufariki ndiyo tukaja kuambiwa ukweli na marehemu mama yetu ambaye naye alifariki muda mfupi baadaye na kutuacha mimi na dada yangu tu.
“Kwa kuwa mambo ya kichawi lazima apatikane mtu wa kurithi mikoba, mimi ndiyo nilichaguliwa kurithi lakini kwa kipindi hicho, nilikuwa pia tayari nimeshafika mbali kwenye masomo ya utambuzi.”
“Masomo ya utambuzi? Ndiyo yapi?”
“Ni kama uchawi tu lakini wenyewe unafundishwa darasani, unatumika sana kwenye nchi za Magharibi. Utambuzi unakuwa ni kwa lengo la kujifunza kuhusu mwili wako na nguvu tunazozalisha, ziwe ni nzuri au mbaya na huu una nguvu kuliko hata uchawi wenyewe unaoujua.
“Kwa hiyo nikawa na nguvu mara mbili, uchawi wa darasani na uchawi mweusi ambao ndiyo huu wa kutumia matunguli, mafuvu na madawa ya kienyeji. Kile chumba ndiyo ilikuwa ofisi ya baba yangu, tangu aanze kuitumia, hakuna mtu mwingine yeyote aliyewahi kuingia zaidi ya mimi na sasa hivi wewe, wengine huwa wanaingia wakiwa mateka kama tulivyomfanya yule mshenzi.
“Kuna siri nyingi sana ndani ya kile chumba, kimsingi ni kama ikulu inayojitegemea,” alisema Junaitha, akawa ni kama amezidi kunichanganya. Nilianza kutafakari kwa kina kuhusu hicho alichoniambia kuwa ni uchawi wa darasani na uchawi mweusi. Nilitaka kujua mambo mengi kwa wakati mmoja kwa sababu kuna siku nakumbuka alituambia kuwa hata ukitaka kuingia benki na kuchukua fedha kisha ukatoka bila kuonwa, inawezekana.
“Najua una shauku ya kutaka kujua vitu vingi lakini usiwe na wasiwasi, kila kitu utakijua vizuri kabisa ilimradi umeshatua kwenye himaya yangu, kinachotakiwa hapa ni kushirkiana kwanza kulimaliza suala la Shenaiza,” alisema, na mimi nikashusha pumzi ndefu na kumgeukia.
“Muda unazidi kusonga mbele Junaitha na hakuna kinachoeleweka, nahitaji kurudi kwenye maisha yangu ya kawaida kama zamani,” nilimwambia, akaniambia nisiwe na wasiwasi mbona kila kitu kimeshakaribia mwisho!
Aliniambia kwamba tukishamaliza kazi ya kumzindua Shenaiza ambayo ingefanyika muda mfupi baadaye, tutaandaa mpango maalum wa kumkamatisha baba yake Shenaiza kwenye mikono ya dola ili kukomesha biashara hatari aliyokuwa anaifanya.
“Usione kama unapoteza muda, nakuhakikishia baada ya kufanikisha hili suala la kumkamata baba yake Shenaiza, utakuwa maarufu sana wewe, dunia nzima itakujua na kukuheshimu na huo ndiyo utakuwa muda mzuri wa wewe kuishi maisha unayotaka kwa sababu kichwa chako kinazalisha nguvu kubwa sana ambayo ina uwezo hata wa kuhamisha milima,” aliniambia.
Maneno yake yalinipa nguvu sana, akaniambia kwamba aliwalaza usingizi mzito kwa makusudi wale wengine ili tukamalizie kazi ya kumzindua Shenaiza lakini akanipa taarifa ambazo zilinishtua mno. Aliniambia baba yake Shenaiza amejizatiti vilivyo kwa nguvu za nje na ndani na ili tufanikishe azma yetu, ilikuwa ni lazima mtu mmoja kati yetu afe.
“Afe?”
“Ndiyo, lazima afe mtu kwenye kafara.”
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

1 comment:

  1. Kwa zaidi ya miaka 13 ya ndoa sikuweza kuzaa, naendelea kuharibika hata nikipata mimba, madaktari wote hawakuweza kunisaidia, hadi dada yangu akanielekeza kwa Dr DAWN, ambaye alinisaidia nikapata ujauzito na sasa hivi kuwa na mtoto mzuri wa kike,
    Anasaidia pia marafiki zangu wengi niliowaelekeza, Dr DAWN ni baraka kwa kila mtu anayewasiliana naye,
    *Kama unataka kupata mimba.
    *Ukitaka kuacha kuharibika kwa mimba.
    *Ukitaka kumrudisha mpenzi wako.
    *Kama unataka mume/mkeo arudishwe.
    *Kama unataka kurejesha mali yako iliyoibiwa au Pesa.
    *Ukitaka kutibu aina yoyote ya ugonjwa,
    Wasiliana naye kwa WhatsApp: +2349046229159

    ReplyDelete

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...