Monday, September 3, 2018

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 5


ILIPOISHIA:
Nilikimbia na kujaribu kuruka ukuta lakini kabla sijaruka, nikasikia wale askari wakifungua milango na kuruka kwenye gari lao kwa kasi kubwa, mmoja kati yao akatoa amri ya kunitaka nisimame na kuinua mikono juu, jambo ambalo niliona kama haliwezekani.
SASA ENDELEA...
Yaani nisalimu amri kirahisi namna hiyo? Nijivalishe mwenyewe kitanzi kwenye shingo yangu? Lilikuwa ni jambo lisilowezekana kwa hiyo ilikuwa ni lazima nifanye kitu, tena haraka iwezekanavyo.
Pale nilipokuwa nimesimama, karibu na ukuta, kulikuwa na mtaro, ile inayochimbwa kandokando ya barabara. Kwa sababu maeneo mengi ya Masaki na Mikocheni yana kama asili ya majimaji, mitaro mingi iliyochimbwa ni mirefu na ina maji.
Kwa kasi ya kimbunga, nilijirusha kwenye mtaro, nikasikia risasi kadhaa zikipita mita chache kutoka pale nilipo, nikaangukia ndani ya mtaro. Kwa jinsi nilivyochukua uamuzi huo kwa kasi kubwa, nadhani hata polisi wenyewe hawakutegemea.
Katika medani za kivita, adui anapokuwa sehemu ambayo yupo chini kuliko wewe, kama kwenye shimo au handaki na ana silaha ya moto, huwa ni hatari sana kwa wewe uliyesimama juu ya ardhi kwa sababu yeye anaweza kukupiga risasi lakini wewe huwezi.

Wale polisi walilitambua hilo kwa sababu nadhani huwa wanafundishwa, kwa hiyo walichokifanya, ilikuwa ni kukimbia haraka kurudi nyuma ili kutafuta sehemu ya kujikinga na mashambulizi ya wazi ya risasi.
Nilikuwa na uwezo wa kufanya chochote lakini sikuona sababu ya msingi ya kuingia kwenye matatizo na polisi kwa muda huo, kwa hiyo nilichokifanya, nilifyatua risasi moja hewani ili kuwatisha wasije kichwakichwa kisha nikautumia muda huo kutambaa kwa kasi kama nyoka kwenye ule mtaro.
Nilifanikiwa kuibukia mita kadhaa mbele na kwa sababu wao waliamini lazima nitakuwa palepale niliporukia, waliendelea kufyatua risasi huku wakisogea, safari hii wakiwa makini zaidi. Nikatoka kwenye mtaro na kukimbia huku nikiwa nimeinama, nikatokezea kwenye ukuta wa jengo lingine ambalo linatumika kama ‘godauni’ la kuhifadhia mizigo, nikaruka ukuta mrefu na kuangukia kwa ndani.
Niliona ni afadhali kupambana na walinzi wa godauni hilo kuliko kupambana na polisi ambao kila mmoja alikuwa na silaha.
Kama nilivyoeleza awali, uzembe uleule wa walinzi, ambao sijui kwa wakati huo walikuwa wapi, pengine nao walijificha baada ya kusikia milio ya risasi, uliniwezesha kukatiza eneo lote la godauni bila kuonwa, nikaenda kuruka ukuta wa upande wa pili na kutokea mtaa wa pili, nikawa nakimbia huku mwili wangu wote ukiwa umelowa kwa maji machafu ya ule mtaro.
Nilikimbia kwa tahadhari kubwa huku nikiendelea kusikia milio ya risasi kule nilikotoka, nadhani polisi bado walikuwa wakijiaminisha kwamba nipo palepale niliporukia. Baada ya dakika kadhaa, nilitokezea kwenye Barabara ya Cocacola, ile inayotokea Mwenge kwenda Mikocheni.
Nilijua kabisa kwamba nikiwa nakimbia pembeni ya barabara ni rahisi kuonekana, kwa hiyo nikavuka na kuingia upande wa pili wenye viwanda na magodauni mengi, ambao kwa wakati huo ulikuwa kimya kabisa.
Nilikimbia kwa umbali mrefu huku nikimuomba Mungu wasishtukie nilikokimbilia, lengo langu likiwa ni kufanya kila kinachowezekana kufika Kibaha usiku huohuo. Baada ya kukimbia kwa umbali mrefu, niliona mwanga wa bodaboda ikija kwa kasi mbele yangu, nikajua hiyo ndiyo nafasi yangu ya kujiokoa.
Nilijitokeza na kusimama katikati ya barabara na kuinua bunduki juu huku mkono mmoja nikimuamuru dereva wa bodaboda kusimama. Nilipoona anaongeza mwendo, niliikamata bunduki vizuri na kumnyooshea, nikiwa tayari kufanya lolote kumsimamisha kama atakaidi ninachokitaka.
Akiwa ni kama hakutegemea alichokuwa anakiona mbele yake, dereva alifunga breki za ghafla, akaruka kwenye bodaboda na kuiacha ianguke, akaanza kukimbia kurudi kule alikotoka huku akiwa ameinua mikono juu, nadhani aliogopa zaidi baada ya kugundua kwamba nilikuwa na bunduki.
Sikutaka kushughulika naye, harakaharaka niliifuata ile bodaboda ambayo bado ilikuwa inanguruma pale chini huku taa zikiwa zimewaka, nikaiinua na kuhakikisha kama ipo salama, nikapanda na kuiondoa kwa kasi kubwa huku bunduki yako nikiwa nimeivaa begani.
Niliendesha kwa kasi kubwa mno, kwenye matuta nikawa nainuka bila kupunguza mwendo na kuyafukia kama ‘nimesimama’, muda mfupi baadaye nikawa tayari nimeshafika Afrikana.
Nilikunja kona kushoto, nikawa narudi upande wa mjini kwa sababu awali nilikuwa kwenye ile Barabara ya Old Bagamoyo, ile inayopita kule kwenye Ofisi za Times FM.
Nilirudi mpaka njia panda ya... nikakata kona na kuingia upande wa kulia, nikawa nakimbia kwa kasi kubwa kwenye barabara ya kuelekea Mbezi, ambayo kipindi hocho bado ilikuwa haijawekwa lami kama ilivyo sasa hivi. Kwa wanaoijua barabara hii, inaenda kukutana na Morogoro Road eneo la Mbezi Mwisho.
Basi nilikamua kwelikweli, sikuwa na uhakika kama mafuta yaliyomo kwenye bodaboda hiyo yatatosha kunifikisha ninakoenda kwa sababu pale yule dereva alipoitupa na kukimbia, mafuta yalimwagikia barabarani.
Baada ya kama dakika ishirini hivi, tayari nilikuwa nimeshafika Mbezi, nikaingia kwenye barabara ya lami na kuendelea kukimbia kwa kasi kubwa, mpaka ikafika mahali nikawa nahisi bodaboda inaweza kulipuka. Sikuwa dereva mzuri wa bodaboda lakini nilikuwa na uelewa wa kutosha wa namna ya kuendesha na kwa sababu usiku huo hakukuwa na magari mengi barabarani, basi sikupata sana shida.
Baada ya kukimbia kwa muda mrefu, hatimaye niliwasili Kibaha Maili Moja, nikapita na mbele kidogo, nilikunja upande wa kulia kwenye viwanda, nikanyoosha na barabara na kuanza kupandisha kuelekea Machinjio ya Zamani, wenyeji wa Bagamoyo watakuwa wanakufahamu vizuri. Ni nje kabisa ya Mji wa Kibaha.
Muda ulikuwa umeyoyoma sana na kwa mbali nikaanza kuona kama ule mwanga wa alfajiri umeanza kulifukuzia mbali giza totoro la usiku. Niliendelea kusonga mbele, nikipita kwa kasi kwenye barabara yenye mchanga mwingi na kusababisha muda mwingine pikipiki iwe inaniyumbisha kwa nguvu.
Mpaka nafika Machinjioni, tayari kulikuwa kumeshaanza kupambazuka na nikajua fika kwamba sitaweza kuikamilisha kazi hiyo kwa siku hiyo, kwa sababu muda mzuri ulikuwa ni usiku wa giza totoro.
Kwa kuwa nilikuwa nalifahamu vizuri shamba nilikoelekezwa kwamba Saima ndiko alikopelekwa, nilitafuta sehemu ya kuificha pikipiki, nikaiingiza ndanindani kabisa kwenye mashamba ya mikorosho na kuipaki, nikashuka na kukaa chini kwa sababu upepo uliosababishwa na spidi kubwa niliyokuwa naendeshea pikipiki hiyo, ulisababisha kifua changu kiwe ni kama kinataka kupasuka.
Tayari mapambazuko yalishawadia kwa hiyo nilichokifanya, ilikuwa ni kuhakikisha hakuna mtu anayeweza kuiona pikipiki hiyo, nikaanza kutembea kwa miguu kuelekea kwenye shamba kubwa lenye zaidi ya ekari hamsini, ambalo ndiko yalikokuwa maficho niliyoelekezwa kwamba Saima atakuwa amefichwa akiteswa.
Mmiliki wa shamba hilo kubwa, alikuwa ni mfanyabiashara mkubwa, Mutesigwa au maarufu kama Bosi Mute, ambaye naweza kukiri kwamba licha ya awali kuwa msaada mkubwa kwangu wakati nafika mjini kwa mara ya kwanza, sasa alikuwa ndiyo adui yangu mkubwa na nilishajiapiza kwamba popote nitakapopata bahati ya kukutana naye kwenye kumi na nane zangu, lazima nimuue, tena kwa mikono yangu mwenyewe.
Kwa nje lilikuwa linaonekana kama ni shamba, likiwa limezungushiwa uzio mrefu wa matofali na nyaya lakini kwa ndani, ilikuwa ni kama kambi ya waasi.
Mipango yote michafu ilikuwa ikifanyikia ndani ya shamba hilo, mali nyingi za wizi, yakiwemo magari, yalikuwa yakifichwa ndani ya shamba hilo na kwa sababu Mutesigwa alikuwa anajua namna ya kula na wakubwa, hakuna mtu yeyote aliyekuwa anaweza kulisogelea shamba lake.
Miongoni mwa makosa makubwa aliyoyafanya, ilikuwa ni kuanza kuniandama, akiamini sina cha kumfanya. Nilishamtumikia kwa kipindi kirefu, kwa hiyo nilikuwa namjua kuliko mtu mwingine yeyote na siyo kumjua yeye tu, bali mpaka familia yake na watu wote aliokuwa akishirikiana nao. Kwa kuwa yeye alikuwa amenianza, nilijiapiza kummaliza kwa sababu wahenga wanasema akuanzaye mmalize.
Maisha yangu na kila nilichokuwa nakipitia, ilikuwa ni kwa sababu yake, yeye ndiye aliyenibadilisha kutoka kuwa kijana mzuri, mpole na mstaarabu mpaka kuja kuwa mnyama na sasa silaha aliyoitengeneza, ilikuwa inarudi kumuangamiza yeye mwenyewe.
Nilitafuta sehemu nzuri, upande wa nyuma kabisa wa shamba hilo kubwa, nikajificha na kuanza kupanga namna ya kwenda kutimiza azma yangu. Ilikuwa ni lazima nimuokoe Saima kwa gharama yoyote, hasa ukizingatia kwamba ndani ya tumbo lake, alikuwa na kiumbe, mwanangu mtarajiwa, ambaye angekuja kuyabadilisha kabisa maisha yangu na kunifanya na mimi nianze kuitwa baba.

Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Championi Ijumaa.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...