ILIPOISHIA:
Kazi iliyokuwa imesalia, ilikuwa ni
kuvunja lile godauni kuangalia ndani kulikuwa na nini? Nilikuwa na shauku kubwa
ya kujua kilichokuwemo mle ndani kwani kwa jinsi nilivyosikia stori za mzee
huyo na mazingira ya ile ngome yake aliyokuwa akiishi, achilia mbali ulinzi wa
hali ya juu, ilionesha ana mambo mengi sana maovu.
SASA ENDELEA...
Askari waliokuwa na silaha,
walilizunguka godauni lote na wengine waliokuwa na vifaa maalum vya kuvunjia
mageti, walisogelea geti hilo na kuseti mitambo yao, tayari kwa kazi. Kwa muda
wote huo, yule mwandishi wa habari alikuwa bize kuhakikisha hakosi picha hata
moja.
Alikuwa akichakarika kisawasawa, akawa
anapiga picha za mnato na za video, kwa ajili ya kuwajuza wananchi juu ya
kilichokuwa kinaendelea. Wakati askari hao wakijiandaa kuvunja godauni hilo,
milio ya ving’ora vya magari mengi ya polisi vilisikika.
Kwa kuwa nilikuwa mwepesi, niliweza
kupaa juu na kutazama upande wa kule barabarani, nikashtuka kuona magari mengi
ya polisi, yakiwa naaskari wengi wenye silaha, yakija kwa kasi eneo lile.
Nadhani awali Junaitha alipowapelekea taarifa juu ya oparesheni hiyo, walidhani
ni tukio dogo tu lakini kilichotokea, kiliwafanya walipe tukio hilo uzito wa
juu.
Binafsi hata sikuona umuhimu wa wao
kufika muda huo kwa sababu tayari jeshi la mtu mmoja nilikuwa nimesafisha njia.
Wale askari waliendelea na kazi yao na muda mfupi baadaye, walifanikiwa kuvunja
geti hilo.