JINA langu naitwa Togolai Mahimba, ni mtoto wa
mwisho kati ya watoto saba wa baba yetu, Sinai Mahimba ambaye kwa sasa ni
marehemu. Baba yetu alifariki miaka mitatu iliyopita baada ya kuugua ghafla.
Kifo chake kilitawaliwa na utata mkubwa na
hata siku ya mazishi yake, kulitokea mambo mengi ya ajabu ambayo mpaka leo
siwezi kuyaeleza. Ninayo mambo mengi ambayo ningependa kukusimulia ndugu
msomaji lakini kwa kuanzia, naomba nikueleze mambo machache yaliyotokea kabla
ya kifo cha baba yetu ambaye mimi ndiye nilikuwa mtoto anayenipenda zaidi.
Kabla hajafikwa na mauti, baba yetu alikuwa
mtu maarufu sana kijijini kwetu, Makongorosi, Chunya mkoani Mbeya tulikokuwa
tukiishi. Kilichofanya awe maarufu kiasi hicho, ni kazi yake ya uganga
aliyokuwa anaifanya ambapo mbali na mambo mengine, alikuwa akiwafanyia
matambiko wachimbaji wengi wa dhahabu ili wakiingia mgodini, wapate dhahabu kwa
urahisi sambamba na wafanyabiashara wengine.
Umaarufu wa baba ulisababisha hata
sisi watoto wake tuwe maarufu sana, hasa mimi ambaye muda mwingi nilikuwa
nikiongozana naye kila alikokuwa anakwenda, kuanzia kwenye matambiko maporini,
kwenye mazindiko migodini, kuchimba dawa msituni mpaka kilingeni kwake
alikokuwa akifanyia shughuli zake za uganga.
Wengi walikuwa wakifupisha jina langu kwa
kuniita Togo na hilo ndiyo lililokuwa maarufu kuliko hata jina langu halisi.
Nakumbuka maisha yangu ya utotoni yalikuwa ya raha sana kutokana na jinsi baba
alivyokuwa akinipenda. Hata ndugu zangu wengine tuliozaliwa pamoja, walikuwa
wakinionea gere kwa jinsi nilivyokuwa nikipendwa.
Maisha yaliendelea vizuri, nikawa naendelea
kukua huku pia nikijifunza mambo mengi aliyokuwa akiyafanya baba katika kazi
zake. Mambo yalianza kubadilika siku moja tukiwa msituni na baba kutafuta dawa.
Baba akiwa ameinama akichimba mizizi ya mti wa
mtangetange ambao ulikuwa ukitumika kwa kutibu magonjwa mengi, hata yale
yaliyoshindikana hospitalini, ghafla alivamiwa na kundi la popo waliokuwa
wanapiga kelele kwa nguvu. Baba akawa anahangaika kujaribu kuwazuia popo hao
ambao waliendelea kumzonga hasa sehemu za kichwani.
Akiwa anaendelea kupambana nao, nilimshuhudia
akifanya tukio ambalo sikuwahi kumuona baba akilifanya hata mara moja. Kwa kasi
ya kimbunga, aliyeyuka na kupotea eneo hilo, nikabaki nimepigwa na butwaa,
nikiwa ni kama siamini.
Ghafla wale popo baada ya kuona baba amepotea
kimiujiza, walitawanyika na kupotea eneo hilo huku wakiendelea kupiga kelele
kwa nguvu. Nikawa nageuka huku na kule kumtazama baba bila mafanikio, hofu
kubwa ikatanda kwenye moyo wangu.
“Unashangaa nini Togolai,” sauti ya baba ndiyo
iliyonizindua kutoka kwenye lindi la mawazo, nikashtuka kwa nguvu. Cha ajabu,
baba alikuwa amesimama palepale alipokuwepo, akiendelea na kazi yake ya
kuchimba mizizi ya mtangetange kama hakuna kilichotokea.
“Baba mbona sielewi?”
“Huelewi nini tena?”
“Popo.”
“Popo? Wamefanya nini?”
“Hawajakuumiza?”
“Mbona sikuelewi Togo?” alisema baba huku
akiacha kazi aliyokuwa anaifanya na kunisogelea. Sikutaka kuamini kama kweli
baba alikuwa haelewi nilichokuwa nakizungumza, akanisogelea na kunishika
begani.
“Uko sawa?”
“Ndi..yo baba, niko sawa,” nilibabaika kidogo,
nikamuona baba akigeuka huku na kule kama anayeangalia kitu fulani. Na mimi
nikawa nageuka kufuata usawa wa macho yake, ghafla macho yetu yakaganda eneo
moja, nilipigwa na butwaa kubwa kwa nilichokuwa nakiona, nikajikuta nikianza
kutetemeka.
Wanaume wawili waliokuwa uchi wa mnyama,
walikuwa wakining’inia kwenye tawi la mti mkubwa uliokuwa mita chache kutoka
pale tulipokuwa, wote wakitukodolea macho yao mekundu.
“Unawaona wale washenzi?” baba alisema huku
akionyesha kutokuwa na hata chembe ya wasiwasi. Nikatingisha kichwa kama ishara
ya kumjibu ‘ndiyo nawaona’.
“Wale ni wachawi wanaosumbua watu kijijini
kwetu, naona wametangaza vita na mimi, hawanijui hawa,” alisema baba na kama
ilivyotokea mara ya kwanza, aliyeyuka na kupotea eneo lile, wale wachawi nao wakapotea
kwenye upeo wa macho yangu, nikasikia kelele za watu waliokuwa wakilia kwa
sauti kubwa kama wanaolalamikia maumivu makali.
“Ndiyo dawa yao, na siku nyingine wakirudia
watanikoma,” alisema baba, nikashtuka tena baada ya kumuona amesimama palepale
alipokuwa mara ya kwanza, pembeni yangu lakini safari hii alikuwa akihema kwa
nguvu kama mtu aliyetoka kukimbia. Nilijihisi kama nipo ndotoni.
“Baba mbona sielewi kinachotoke...” nilisema
lakini kabla sijamalizia kauli yangu, macho yangu yalitua kwenye mkono wa baba
uliokuwa na jeraha na alama kama ameng’atwa na mnyama mkali, huku damu nyeusi
zikimtoka kwa wingi.
“Ninii!” baba alinihoji baada ya kuona macho
yangu yameganda kwenye mkono wake.
“Umeumia baba, pole,” nilisema lakini baba
hakunijibu kitu zaidi ya kuusogeza ule mkono wenye jeraha karibu na uso wake,
akawa analichunguza vizuri lile jeraha.
Akasogea pale kwenye mti wa mtangetange na
kuchuma majani yake, akayatia mdomoni na kuanza kuyatafuna kisha muda mfupi
baadaye, aliyatoa mdomoni na kuyabandika juu ya kidonda chake, nikamuona
akifumba macho kama ishara ya kuonyesha jinsi alivyokuwa akihisi maumivu.
“Nitakuwa sawa usijali, nimeshazoea kusumbuana
na hawa wachawi. Inabidi na wewe uwe jasiri,” alisema baba huku akiendelea
kujisafisha pale kwenye jeraha lake. Zile damu nyeusi zilizokuwa zinamtoka
zikakata, akashusha pumzi ndefu na kuendelea na kazi ya kuchimba dawa.
Kwa kweli matukio yale niliyoyashuhudia
yaliufanya moyo wangu uingiwe na hofu kubwa mno. Sikuwahi kudhani baba anaweza
kuwa na nguvu za giza kiasi kile, siku zote niliamini alichokuwa anakifanya ni
kutibu watu kwa mitishamba tu, basi! Hata hivyo, nilijikaza kiume na kuuficha
mshtuko nilioupata, nikaendelea kumsaidia baba na hatimaye tukamaliza kazi
yetu.
Wakati tunarudi kutoka msituni, baba alinisisitiza
njiani kwamba sitakiwi kumwambia mtu yeyote kuhusu nilichoshuhudia, hata ndugu
zangu wa tumbo moja. Akaniambia kwa kilichotokea, anahisi kuna madhara makubwa
yatakuwa yametokea kijijini kwetu.
“Unamaanisha nini baba?”
“Wale wachawi waliotuvamia kule msituni, mmoja
nimemuumiza sana sijui kama anaweza kuwa yupo hai mpaka muda huu.”
“Kwani ni akina nani wale?”
“Kwani wewe huwajui wale? Au hujawatazama
vizuri?” baba alinihoji na kuanza kunifafanulia, akaniambia yule mmoja ni mzee
wa kanisa pale kijijini kwetu, aliponitajia jina lake ndiyo nikamtambua vizuri.
Alikuwa ni mzee Mwankuga, ambaye mara kwa mara alikuwa akiingia kwenye migogoro
na baba kutokana na kugombea mpaka wa shamba kwa sababu shamba letu na lake
yalikuwa yemepakana.
Nakumbuka kuna kipindi waliwahi kupelekana
mpaka kwa balozi kutokana na ugomvi wao huo. Hata familia zetu hazikuwa na
uhusiano mzuri, sisi tulikatazwa kabisa kuongea wala kucheza na watoto wa mzee
Mwankuga na yeye hali kadhalika.
“Kwa hiyo unataka kusema mzee Mwankuga naye ni
mchawi? Si mtumishi wa Mungu yule na kila Jumapili anaenda kanisani tena anakaa
siti za mbele?”
“Mwanangu dunia ina mengi hii! Hutakiwi
kumuamini mtu, pale kanisani waumini karibu wote huwa wanakuja kutafuta dawa
kwangu, wengine wanataka wapandishwe vyeo, wengine wanataka kujikinga na
wengine wana shida mbalimbali, usiwaamini binadamu,” alisema baba, nikabaki
nimeduwaa. Hizo zikawa ni habari nyingine za kushangaza sana kwangu.
“Sasa pale si walikuwa wawili? Huyo mwingine
ni nani?”
“Si yule mwalimu wenu, Mwashambwa?”
“Mwalimu wetu Mwashambwa anayetufundisha
hesabu naye ni mchawi?” niliuliza kwa mshangao mkubwa huku mdomo nikiwa
nimeuacha wazi.
“Ndiyo, hata ule mguu wake anaochechemea
nasikia alikutana na kombora la kichawi ndiyo likampa ulemavu wa kudumu, siyo
mtu mzuri kabisa, we turudi nyumbani utasikia chochote kuhusu watu hao wawili,”
baba alisema kwa kujiamini, ukimya mrefu ukatanda kati yetu, hakuna
aliyezungumza chochote.
Niliendelea kutembea huku nikiwa na furushi
langu la dawa kichwani pamoja na panga, baba yeye alikuwa ametangulia mbele,
naye akiwa amebeba dawa na jembe tulilokuwa tunalitumia kuchimbia dawa.
Ili kufika nyumbani kwetu, ilikuwa ni lazima
upite nyumba kadhaa za nyasi na nyingine za bati zilizokuwa pembezoni mwa
kijiji ndiyo uelekee nyumbani. Miongoni mwa nyumba hizo, ilikuwepo pia na
nyumba ya mzee Mwankuga ambaye muda mfupi uliopita baba alikuwa akinisimulia
mambo yake kwamba ni mchawi.
Tulipokaribia nyumbani kwa mzee huyo, baba
alinionyesha ishara kwamba nisimame, nikafanya hivyo, tukawa tunasikia sauti za
watu wengi wakilia kutoka nyumbani kwa mzee huyo, baba akanionyesha ishara kama
anayesema ‘unaona?’, nikashika mdomo kwa mshangao. Sikutaka kuamini kwamba
kweli mzee Mwankuga alikuwa amefariki dunia.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment