ILIPOISHIA:
Niliondoka kazini nikiwa ni kama
nimechanganyikiwa, sikuwa namjua Shenaiza lakini sijui kwa nini nilihisi kama
matatizo yake yalikuwa yakinihusu sana. Nikiwa kwenye kituo cha daladala
nikiendelea kusubiri usafiri, ujumbe mfupi uliingia kwenye simu yangu, ulisomeka:
“Mwenye simu hii amelazwa Hospitali ya Amana,
Ilala. Hali yake ni mbaya, hawezi kuzungumza.”
SASA ENDELEA…
“Mungu wangu,” nilisema baada ya kumaliza
kuusoma ujumbe huo. Nilijaribu kuipiga tena namba hiyo, ikapokelewa lakini
sauti haikuwa ya Shenaiza, akaniambia yeye ni Rozina, nesi katika hospitali ya
Amana na kwamba yeye ndiye aliyekuwa akimhudumia msichana huyo.
Nilimuomba anitajie wodi aliyolazwa msichana
huyo, akaniambia niende tu nikifika hospitalini hapo nipige kupitia namba
hiyohiyo atakuja kunipokea. Niliita bodaboda na kumuelekeza kukimbia kadiri
awezavyo kuelekea Amana. Abiria wengine waliokuwa pale kituoni wakisubiri
daladala, walibaki kunishangaa lakini mwenyewe sikujali.
Nikaondoka na bodaboda huku nikimhimiza
kuongeza mwendo ili tuwahi kufika. Baada ya kuhangaika sana kwenye foleni, kama
ujuavyo Jiji la Dar es Salaam nyakati za jioni, hatimaye tuliwasili Amana.
Nikapiga namba ya Shenaiza ambapo yule nesi alipokea tena, nikamweleza kwamba
tayari nilikuwa nimefika, akaniambia nimsubiri mapokezi.
Sikuwa hata naijua sura ya huyo Shenaiza
mwenyewe kwa sababu hatukuwahi kuonana zaidi ya kusikia sauti yake tu kwenye
simu.
Muda mfupi baadaye, alitoka nesi mmoja,
mwembamba, mrefu mwenye rangi ya weusi wa asili, akaniuliza kama mimi ndiye
niliyekuwa nawasiliana naye kwenye simu. Nilipomjibu kwamba ni mimi, aliniuliza
nilikuwa na uhusiano gani na mgonjwa?
Nikamjibu kwamba mimi ni kaka yake, nikamuona
akiguna huku akinitazama kwa macho ya udadisi. Sikuelewa kwa nini ananitazama
hivyo, nikajikaza kiume na kuonyesha kutobabaika.
“Nifuate!” alisema huku akianza kutembea
kuelekea wodini, na mimi nikawa namfuata. Tulipita kwenye korido na kutokezea
kwenye wodi za wanawake, nikawa naangaza macho huku na kule wakati tukipita
pembeni ya vitanda walivyolazwa wanawake wengi, tukapita na kwenda kwenye wodi
iliyokuwa imejitenga peke yake. Yule nesi akafungua mlango na kunipa ishara
kwamba niingie.
Japokuwa kulikuwa na vitanda vinne ndani ya
wodi hiyo, ni kimoja tu kilichokuwa kimelaliwa na mgonjwa aliyeonesha kutokuwa
na fahamu. Yule nesi alinipa ishara kwamba yule ndiyo mgonjwa mwenyewe,
nilimtazama kwa mshangao nikiwa kama siamini macho yangu.
Hakuwa Shenaiza yule ambaye nilimjengea picha
kichwani mwangu, alikuwa mtu mwingine tofauti kabisa kiasi cha kunifanya nihisi
huenda nesi amekosea kunipeleka au hatukuelewana katika mazungumzo yetu.
Hakuwa msichana wa Kitanzania kama nilivyokuwa
nimemfikiria, alikuwa na mchanganyiko ambao siwezi kueleza moja kwa moja kama
ni Mzungu au ni Mwarabu lakini alikuwa katikati ya jamii hizo mbili. Kiumri
alionesha kuwa bado ni binti mdogo tofauti na nilivyomfikiria kwamba anaweza
kuwa ni mwanamke mwenye kati ya miaka 25 hadi 30.
Alikuwa amelala tuli kitandani huku akiwa
amefungwa bandeji kubwa kichwani, huku jicho lake moja likiwa limebadilika
rangi na kuwa na weusi na wekundu kwenye ngozi inayolizunguka jicho kuonesha
kwamba damu zilikuwa zimevilia kwa ndani. Pia mkono wake mmoja ulikuwa
umezungushiwa bandeji kubwa kuanzia juu kidogo ya kiganja mpaka kwenye kiwiko
cha mkono.
Dripu moja sambamba na chupa ya damu vilikuwa
vikitiririka kwa kasi kuingia kwenye mishipa yake ya damu, nikajikuta nikipatwa
na hali ambayo siwezi kuielezea kwa urahisi. Kwa kifupi, japokuwa bado sikuwa
na uhakika kwamba yule ndiye Shenaiza tuliyekuwa tukiwasiliana naye, nilijikuta
nikimuonea huruma sana kutokana na hali aliyokuwa nayo.
Nilitamani kujua nini kimemfika mpaka akawa
kwenye hali hiyo. Nilitamani pia nimjue yeye ni nani na asili yake ni wapi hasa
kwani hakuonesha kuwa Mtanzania japokuwa alikuwa akizungumza vizuri Kiswahili.
“Mbona unamshangaa sana? Kwani mlikuwa
mnafahamiana kabla?” yule nesi aliniuliza baada ya kuniona hali niliyokuwa
nayo, nilishusha pumzi ndefu na kuzugazuga, nikasogea pembeni ya kitanda cha
Shenaiza na kumpa ishara kwamba tusogee pembeni ili tuzungumze zaidi.
“Samahani nesi, hebu nieleze nini kimetokea?”
“Nitakueleza lakini nataka na wewe unieleze
ukweli, usije ukanisababishia matatizo kwenye kazi yangu, huyu ni nani kwako?”
“Nimeshakwambia kwamba ni dada yangu.”
“Hapana, siyo kweli! Hebu ngoja kwanza,”
alisema huku akienda kuchukua simu iliyokuwa pembeni ya kitanda cha Shenaiza,
akanifuata na kuniuliza kama simu yangu nilikuwa nayo, nikamjibu kwamba ninayo,
akaniambia nipige namba ya Shenaiza. Nikatoa simu yangu na kutafuta namba yake
kisha nikampigia.
“Unaona amekusevu vipi?” aliniuliza yule nesi
huku akinionesha jina lililotokea kwenye simu yake, nikabaki nimepigwa na
butwaa kutokana na jinsi alivyokuwa amenisevu.
Sikutaka kuendelea kumbishia yule nesi kwa
sababu angeweza kupata sababu ya kukataa kunipa ushirikiano baada ya kuamini
kwamba nilikuwa nikimdanganya, nikaamua kukubali yaishe, nikamuacha aamini kile
mwenyewe alichotaka kukiamini (nitafafanua zaidi baadaye jinsi alivyokuwa
amenisevu).
Baada ya kuelewana na nesi huyo, alianza
kunieleza kwamba walimpokea mgonjwa huyo majira ya saa tisa za jioni baada ya
kuletwa na wasamaria wema ambao walidai wamemkuta amepigwa na kujeruhiwa vibaya
nje ya nyumba yao.
“Alikuwa akitokwa na damu nyingi huku pia
akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake, ikabidi tumpokee hivyohivyo
na kuanza kumpatia matibabu lakini mpaka sasa hakuna anayejua jina lake,
ametokea wapi na nini kilichomsibu, tunasubiri labda akirejewa na fahamu au
ndugu zake wakija ndiyo watueleze kilichotokea,” alisema yule nesi, nikashusha
pumzi ndefu na kugeuka kumtazama Shenaiza pale kitandani.
Baada ya kumaliza kuzungumza na nesi,
nilimuomba niende kukaa pembeni ya Shenaiza mpaka atakaporejewa na fahamu zake
lakini aliniambia kuwa ni kinyume na taratibu za hospitali hiyo, akanitaka
nikakae nje ya wodi na kama kuna chochote, atanipa taarifa lakini akasisitiza
kwamba mgonjwa alikuwa anahitaji damu zaidi kwa sababu amepoteza nyingi,
akanitaka kama nipo tayari kumchangia anielekeze nini cha kufanya.
Sikuwa na kipingamizi, nilikubali kumchangia
damu, yule nesi akanichukua mpaka kwenye wodi nyingine ambapo alinitambulisha
kwa madaktari wenzake na kuwaeleza kwamba nilikuwa nataka kumtolea damu mgonjwa
wangu Shenaiza. Nikachukuliwa vipimo vya awali na baada ya kuonekana nilikuwa
fiti, niliingizwa kwenye chumba kingine na kuanza kutolewa damu.
Nikiwa naendelea kutoa damu, niliendelea
kujiuliza maswali mengi kuhusu Shenaiza yaliyokosa majibu. Kuna wakati
nilijilaumu sana kukataa kuonana naye mapema kwani niliamini pengine ningeweza
kumsaidia asipatwe na kilichomtokea. Hata hivyo nilijipa moyo kwamba sikuwa
nimechelewa, nikawa namuombea kwa Mungu apone na kurudi kwenye hali yake ya
kawaida.
Baada ya kumaliza kutolewa damu, nilirudi pale
nje ya wodi na kukaa huku nikiendelea kutafakari mambo mengi. Tayari kigiza cha
jioni kilishaanza kuingia lakini moyo wangu haukuwa radhi kuondoka hospitalini
hapo, nilijiapiza kwamba hata ikibidi kukesha usiku kucha, nitafanya hivyo
mpaka nifahamu kilichomsibu Shenaiza.
Ilipofika majira ya kama saa moja za jioni,
yule nesi, Rozina alinifuata na kunipa habari ambazo zilinifanya mapigo ya moyo
yanilipuke kuliko kawaida. Aliniambia Shenaiza amerejewa na fahamu na jambo la
kwanza alilouliza ni kama nilikuwa nimempigia simu.
“Nimemwambia kwamba upo hapa nje, akaniomba
sana akuone, lakini anazungumza kwa shida sana,” alisema nesi huyo, nikainuka
na kuanza kumfuata harakaharaka kuelekea wodini.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment