ILIPOISHIA:
MWANAUME mzee mwenye macho mekundu sana na
midomo myeusi, akiwa amejifunga shuka refu lenye rangi nyekundu na nyeusi,
kichwani akiwa amejifunga kitambaa cheusi, shingoni akiwa na hirizi kadhaa na
shanga, alisimama na kunyoosha juu mkia wa mnyama ambaye sikuwa namjua, watu
wote wakashangilia kwa nguvu.
SASA ENDELEA...
“Sina mengi ya kuzungumza, naomba ushirikiano
wenu tuwakomeshe wachawi wa kijiji hiki,” alisema mwanaume huyo kwa Kiswahili
kibovu, watu wakashangilia tena kwa nguvu kisha Mwene akaendelea na maelezo,
akisisitiza kwamba kazi lazima ianze siku hiyohiyo usiku.
Baada ya maelezo marefu yaliyojaa vitisho kwa
watu waliokuwa wakitajwa kuhusika na uchawi, mkutano uliahirishwa, watu
wakatawanyika huku kiongozi huyo wa kijiji akiwataka watu wote kutoa
ushirikiano kwa mganga Mabwanji atakapoenda kuwatembelea kwenye nyumba zao.
Hofu niliyokuwa nayo ilikuwa kubwa mno, kwa
jinsi watu walivyokuwa wanatuchukia pale kijijini nilijua lazima moto utawaka.
Baadhi ya wazee waliokuwa wanaheshimika pale kijijini, walianza maandalizi ya
kumsaidia mganga huyo kwa kila alichokuwa anakihitaji, dawa zikaandaliwa na
hatimaye muda uliokuwa ukisubiriwa na wengi ukawadia.
Saa tatu juu ya alama usiku, kazi ya kuzunguka
kwenye nyumba za watu waliokuwa wakishukiwa kuwa wachawi ilianza, kutokana na
jinsi nilivyokuwa na shauku kubwa ya kutaka kuona kazi hiyo inavyofanyika,
nilichomoka nyumbani kimyakimya na kwenda kushuhudia licha ya kwamba baba
alitutaka wote tukae ndani kwa sababu siku hiyo ilikuwa mbaya kwa familia yetu.
Mtu wa kwanza kufuatwa alikuwa ni mwanamke
mjane ambaye tulizoea kumuita mama Chinga, Mmakonde kutoka Kusini ambaye
alikuwa akifanya kazi ya kupika pombe za kienyeji.
Kwa kipindi kirefu nilikuwa nikisikiasikia
kwamba eti mwanamke huyo alikuwa akitumia viungo vya binadamu kupikia pombe
zake ndiyo maana alikuwa na wateja wengi sana hapo kijijini. Tangu nikiwa mdogo
niliaminishwa kwamba eti ule ambao huwa tunaona kama ni mwiko mkubwa anaoutumia
kukorogea mapipa yake ya pombe, ulikuwa ni mkono wa binadamu.
Watu hao walipofika, huku ngoma ikipigwa na
pembe za wanyama zikipulizwa, kila mtu akiwa ameshika tochi za kienyeji ambazo
hutengenezwa kwa kuviringisha matambara mbele ya kipande cha mti kisha kuchovya
kwenye mafuta ya taa, nyumba yake ilizungukwa kisha mganga akaanza kazi yake.
Akawa anafanya uchawi wake pale, mara afukue
kwenye kona ya nyumba na kutoa hirizi kubwa, mara afukue pembeni ya mlango na
kutoa fuvu la mnyama wa ajabu, yaani ilikuwa ni patashika nguo kuchanika.
Mwanamke huyo na yeye akatolewa na kukalishwa
chini, mbele ya nyumba yake, akapakwa unga mweupe kichwani na kuanza kunyolewa
nywele huku ngoma zikiendelea kupigwa, mganga akawa anaimba nyimbo za ajabu na
kumtolea vitisho vingi mwanamke huyo kwamba akirudia tena kujihusisha na uchawi
lazima atakufa.
Baada ya zoezi hilo lililochukua karibu saa
zima, watu wote waliondoka na kumuacha mwanamke huyo akilia kwa uchungu, huku
akiendelea kusisitiza kwamba yeye siyo mchawi wala haujui uchawi. Safari ya
kuelekea kwenye nyumba nyingine ikaanza, na mimi nikawa nawafuata kwa nyuma.
Cha ajabu, niliwaona wakielekea nyumbani
kwetu, mapigo ya moyo yakawa yananienda mbio kuliko kawaida, sikujua mwisho
wake utakuwaje. Walipofika, walifanya kama walivyofanya kwa yule mwanamke,
wakaizunguka nyumba yetu huku wakiimulika na tochi za kienyeji, ngoma ikawa
inapigwa huku mganga akiimba nyimbo ambazo hakuna aliyekuwa anazielewa.
Akawa anazunguka huku na kule kama anayetafuta
kitu fulani pale nje kwetu, ghafla nikaona mlango ukifunguliwa, baba akatoka
kwa kasi na kuwapita watu wote, akasogea mpaka pale yule mganga alipokuwa
amesimama, wakawa wanatazamana.
“Ni nani aliyekupa mamlaka ya kuingia kwenye
miji ya watu na kutapeli ukijifanya unawatoa watu uchawi?”
“Wewe ni nani wa kunihoji maswali hayo? Wewe
ni mchawi na wanakijiji wenzako wamekuchoka hapa kijijini. Hii safari ya ujio
wangu ni kwa ajili yako, lazima nikunyooshe.”
“Wewe bado ni mwepesi sana kwangu, huna ubavu
wa kushindana na mimi. Isitoshe mimi siyo mlozi kama wewe, mimi ni mtaalamu,
tena gwiji,” alisema baba kwa sauti ambayo niliisikia vizuri kisha baada ya
hapo akageuka na kurudi ndani, nikamuona yule mganga akivuta na kutoa pumzi
ndefundefu kama anayejiandaa kufanya tukio moja kubwa sana.
Alipoingia ndani na kufunga mlango, huku nje
yule mganga aliendelea kuzunguka huku na kule, wasaidizi wake wakawa wanampigia
manyanga na kumuimbia nyimbo ambazo walizielewa wenyewe.
“Inatakiwa tumkamate kwa nguvu na kumtoa nje,
anaonyesha ni jeuri sana,” alisema mganga huyo kwa Kiswahili kibovu, watu wote
wakawa wanatingisha vichwa kuonyesha kukubaliana na alichokuwa anakisema.
Nilijikuta nikitetemeka sana pale nilipokuwa
nimejibanza, nikajua arobaini za baba zilikuwa zimewadia. Japokuwa bado sikuwa
na majibu kamili kichwani mwangu kama baba ni mganga au mchawi, bado
sikukubaliana na kitendo alichokuwa anataka kufanyiwa kwa sababu ulikuwa ni
udhalilishaji wa hali ya juu.
Wakati kundi la wanaume wakijiandaa kuingia
ndani kwa nguvu na kuvunja mlango, nilimuona baba akitoka kwa kujiamini, kifua
akiwa amekitanguliza mbele na kusimama tena mbele ya mganga, wale watu wote
wakamzunguka kisharishari.
“Mnataka kutumia nguvu kunikamata? Hivi mna
akili timamu nyie? Haya mwenye ubavu anyooshe mkono wake na kunigusa,” alisema
baba kwa hasira. Nilibaki namshangaa baba kwani sikujua amepata wapi ujasiri wa
kiasi kile. Kauli hiyo iliwashtua hata wale watu waliokuwa wanataka kumkamata,
nikaona wote wakirudi nyuma lakini mganga aliendelea kusisitiza kwamba ni
lazima wamkamate kwa nguvu.
Watu wote walipojaribu kufanya hivyo,
tulishtuka kuona kimbunga kikubwa ambacho hata sikujua kimetokea wapi, kikianza
kuvuma kwa nguvu pale baba alipokuwa amesimama, vumbi jingi na takataka za kila
aina zikawa zinarushwa huku na kule, kufumba na kufumbua, baba hakuwepo tena
eneo hilo.
Wale watu wote, akiwemo na mganga mwenyewe,
walibaki wamepigwa na butwaa, kila mmoja akawa anajifuta vumbi. Sikuwahi
kushuhudia kimbunga kikubwa kikitokea, tena usiku kama ule, nikabaki na maswali
mengi yaliyokosa majibu.
“Ametukimbia! Ametukimbia!” alisema yule
mganga kwa sauti ya juu, huku na yeye akionyesha dhahiri kuwa na taharuki kubwa
ndani ya moyo wake.
“Siwezi kuwakimbia kwa sababu hakuna wa
kunitisha hata mmoja kati yenu,” ilisikika sauti ya baba kisha nikashangaa
kumuona akitokea gizani na kurudi tena pale alipokuwa amesimama awali, nikaona
watu wote wakianza kurudi nyuma kwa hofu kubwa kwa sababu walishajua baba
anaweza kufanya chochote muda wowote.
“Nataka hili liwe funzo kwako na kwa watu
wengine wenye akili kama zako,” alisema baba kwa kujiamini huku akiendelea
kumsogelea yule mganga, akafanya ishara kama ananyonga kitu kwa nguvu, kufumba
na kufumbua mganga yule alidondoka chini na kuanza kutapatapa kama anataka
kukata roho.
Kuona hivyo, watu wote waliokuwa wameandamana
na mganga huyo, walitimua mbio, kila mmoja kuelekea njia yake na muda mfupi
baadaye, wote walikuwa wametokomea gizani, ikabidi nitoke pale nilipokuwa
nimejibanza huku na mimi nikiwa na hofu kubwa ndani ya moyo wangu.
“Hebu beba huko miguuni tuutoe huu mzoga
hapa,” alisema baba, akimaanisha tumtoe yule mganga.
Huku nikitetemeka nilisogea mpaka pale yule
mganga alipokuwa amelala, akiendelea kukoroma kwa nguvu, mimi nikamshika
miguuni na baba akamshika kichwani, tukaanza kumkokota kumtoa nje ya eneo letu,
tukaenda kumbwaga pembeni kabisa kwenye vichaka kisha tukarudi ndani. Ile
tunaingia ndani tu, tukasikia mlango ukigongwa kwa nguvu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment