ILIPOSHIA:
Aliniambia
Shenaiza amerejewa na fahamu na jambo la kwanza alilouliza ni kama nilikuwa
nimempigia simu.
“Nimemwambia
kwamba upo hapa nje, akaniomba sana akuone, lakini anazungumza kwa shida sana,”
alisema nesi huyo, nikainuka na kuanza kumfuata harakaharaka kuelekea wodini.
SASA
ENDELEA…
Muda mfupi baadaye, tulikuwa pembeni ya kitanda
alichokuwa amelazwa msichana huyo, nesi Rozina akaniambia ananipa dakika chache
za kuzungumza na mgonjwa, akatoka na kufunga mlango wa wodi hiyo. Kwa muda wote
huo, macho yangu yalikuwa juu ya uso wa msichana huyo ambaye naye alikuwa
akinitazama, tukawa tunatazamana.
Tofauti na nilivyofika mara ya kwanza hospitalini
hapo, safari hii niliweza kumuona vizuri msichana huyo. Kitu ambacho naomba
nikiseme wazi, japokuwa alikuwa kwenye maumivu makali, akiwa amefungwa bandeji
kubwa kichwani na jicho lake moja likiwa limevilia damu na kuwa jekundu,
Shenaiza alikuwa na sura nzuri mno.
Nilijikuta
nikivutiwa naye na kuendelea kumtazama, naye akawa ananitazama bila kusema kitu
chochote mpaka nilipoamua kuvunja ukimya.
“Pole dada Shenaiza! Pole sana,” nilisema kwa sauti
ya upole, kauli yangu ikawa kama mkuki ndani ya moyo wake kwani badala ya
kujibu, alianza kuangua kilio kikali cha kwikwi, machozi mengi yakawa
yanachirizika kupitia kwenye pembe za macho yake na kuishia kwenye shuka jeupe
alilokuwa amelala juu yake.
Ikabidi nimsogelee zaidi na kumuinamia pale
kitandani, kwa kutumia mkono wangu mmoja nikawa namfuta machozi huku nikiendelea
kumpa maneno ya kumfariji, nikamuona naye akitoa mkono wake mmoja kwenye shuka
na kuushika mkono wangu huku akiendelea kulia, akauvutia kifuani kwake huku akinitazama
usoni.
Macho yake ni kama yalikuwa na sumaku kwani katika
mazingira ambayo sikuyategemea, na mimi nilijikuta nikianza kulengwalengwa na
machozi. Nilijikuta nikimuonea mno huruma msichana huyo na kuwa na shauku kubwa
ya kutaka kusikia nini kilichomtokea.
Mpaka muda huo, hakuwa amefumbua mdomo wake na
kuzungumza neno hata moja zaidi ya kuendelea kulia tu huku akinitazama kwa
macho yaliyobeba ujumbe. Japokuwa na mimi nilijisikia uchungu sana, nilijitahidi
kujikaza kiume na kuendelea kumbembeleza.
“Nashukuru kwa upendo wako ulionionesha, kumbe
nilivyokuwa nimekutafsiri baada ya kusikia sauti yako mara ya kwanza
nilipokosea namba yako ya simu nilikuwa sahihi kabisa,” alisema Shenaiza kwa
sauti ya chini mno lakini iliyosikika vizuri kabisa masikioni mwangu.
“Usijali Shenaiza, nipo kwa ajili yako na
nitaendelea kuwepo pembeni yako kwa shida na raha,” nilimwambia, kauli ambayo
ilimfanya aachie tabasamu hafifu, akaubusu mkono wangu ambao muda wote alikuwa
bado ameung’ang’ania.
Kilichonishangaza kwa Shenaiza, japokuwa ndiyo
kwanza tulikuwa tunakutana kwa mara ya kwanza, tena akiwa kwenye maumivu
makali, alionesha kama ana hisia fulani juu yangu kwa sababu siyo rahisi
kumshika mkono kisha ukaubusu kwa mtu ambaye wala hujawahi kumuwazia akilini
mwako.
“Halafu kumbe wewe ni kijana mzuri namna hiyo, kwa
nini hujaoa mpaka leo,” alisema Shenaiza kwa lafudhi nzuri japo alionesha kuwa
na maumivu, nikajikuta nikitabasamu na kukosa cha kumjibu.
“Kwani nini kimekutokea dada’angu?”
“Ni stori ndefu, ngoja nitakusimulia kila kitu
nikipata nafuu lakini naomba umwambie na nesi kwamba sihitaji mtu yeyote ajue
kwamba nimelazwa hapa, naweza kupata matatizo mengine bure. Naomba wewe ndiyo
uwe mtu pekee wa kunisimamia mpaka nitakapopona,” alisema msichana huyo kwa
sauti ya chini iliyoonesha bado yupo kwenye maumivu, nikawa natingisha kichwa
kuonesha kukubaliana naye.
Kwa muda mfupi niliozungumza na Shenaiza, niligundua
kwamba huenda ana jambo zito sana lililokuwa likiusumbua moyo wake na kweli alikuwa
akihitaji mtu wa kumsaidia ingawa bado sikuwa najua ni nini kilichokuwa
kinamsumbua.
“Nikuulize swali jingine?” nilimhoji, akatingisha
kichwa kuonesha kukubali. Nilitaka kumuuliza kuhusu jinsi alivyokuwa amenisevu kwenye
simu yake lakini nikahisi huenda nikam-boa kwa swali hilo.
“Uliza tu,” alinisisitiza baada ya kuona nasitasita.
“Kwa nini umenisevu vile kwenye simu yako?”
“Simu yangu? Mungu wangu, we umeonaje wakati hata
simu yangu huijui,” alisema msichana huyo huku aibu za kikekike zikiwa
zimetawala kwenye uso wake, akawa anakwepesha macho yake ili yasigongane na
yangu, tabasamu hafifu likiwa limechanua kwenye uso wake.
Aliendelea kulikwepakwepa swali hilo lakini na mimi
niliendelea kumbana hapohapo. Nilichokifanya, niliamua kuipiga namba yake na
kwa kuwa simu yake ilikuwa pembeni ya kitanda chake ingawa mwenyewe hakuiona,
muda mfupi baadaye ilianza kuita, namba yangu ikiwa imeseviwa ‘My Husband’!
Akazidi kujisikia aibu za kikekike na mwisho akafunguka:
“Niliamua kukusevu hivyo kwa sababu ya matatizo
yanayonikabili, naomba suala hilo tusilizungumze leo, ipo siku utanielewa,”
alisema na kugeukia pembeni kuonesha hakuwa akitaka tuendelee kuzungumzia suala
hilo, nikabadilisha mada haraka.
Kingine kilichonishangaza kwa Shenaiza, kila
nilichokuwa namuuliza alikuwa akikwepa kunijibu, hakuna jambo hata moja ambalo
nilitaka kulijua na akanijibu bila wasiwasi, nilipomuuliza anaishi wapi na
anakaa na nani, alikwepa swali hilo kwa maelezo kwamba tutazungumza siku
nyingine akiwa amepona.
Nilipomuuliza pia nini kilichomtokea mpaka akaumia
hivyo mpaka kulazwa hospitalini hapo, bado hakuwa tayari kunieleza, kisingizio
kikawa kilekile kwamba mpaka atakapopona ndiyo atanieleza kila kitu.
Kwa kuwa bado mwili wake haukuwa na nguvu hasa baada
ya kupoteza damu nyingi kama alivyonieleza nesi Rozina, nilikubaliana naye.
Nilipomuuliza kama angehitaji nini usiku huo kwa ajili ya chakula kwa sababu
nilikuwa na uhakika kwamba hajala chochote, aliiambia nikamtafutie juisi tu,
inamtosha.
Tayari nesi alishaingia na kunitaka nitoke kwani
mgonjwa alikuwa akihitaji mapumziko ya kutosha, nikamwambia kwamba kuna vitu
ameniagiza naenda kumnunulia nitarejea baada ya muda mfupi, nesi akaniruhusu
huku akisisitiza niwahi kwani kuna muda ukishafika, watu wa kawaida
hawaruhusiwi tena kuingia wodini.
Nilitoka haraka na kwenda kwenye maduka yaliyokuwa
jirani na hospitali hiyo, nikamnunulia juisi maboksi mawili na keki laini
ambazo niliamini atazipenda. Nikarudi wodini na muda mfupi baadaye niliruhusiwa
tena kuingia wodini, nikamkuta Shenaiza ametulia pale kitandani, akionesha
kuanza kupata ahueni kubwa. Aliponiona tu, tabasamu pana lilichanua kwenye uso
wake, nikamsogelea mpaka pale kitandani, nikatoa maboksi ya juisi na keki na
kuweka kwenye droo ya pembeni ya kitanda na kumtaka akijisikia ahueni ajitahidi
kunywa.
Kwa kuwa muda nao ulikuwa umeyoyoma, nilimuaga
kwamba narudi nyumbani lakini nitakuja kumtembelea asubuhi lakini alionesha
kuwa mgumu kukubaliana na hilo.
Mara simu yake ilianza kuita mfululizo, akaishika na
kutazama namba ya mpigaji lakini katika hali ambayo sikuielewa, aliiachia simu
hiyo, ikadondoka chini na kufunguka betri ikaangukia kivyake, mfuniko kivyake
na simu nayo kivyake. Akaanza kuangua kilio kwa uchungu huku akiniomba
nimsaidie, nilibaki nimepigwa na butwaa.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment