ILIBIDI nisogee mpaka kwenye maegesho ya bodaboda
nikiamini pale itakuwa rahisi kuzungumza na dereva yeyote ili aniwahishe kabla
ile ‘ambulance’ haijapotea kabisa. Nilipopiga hatua moja, nilijiona kuwa
mwepesi sana halafu tambo lilikuwa refu sana tofauti na kawaida.
Sehemu ambayo ningetembea hata hatua ishirini,
nilipiga hatua mbili tu, nikawa nimeshafika pale kwenye bodaboda.
SASA ENDELEA…
“OYA mambo vipi mkubwa!” nilimsalimu dereva wa
bodaboda aliyekuwa pembeni yangu kwa bashasha kubwa lakini hakuniitikia, akawa
anaendelea kuifutafuta bodaboda yake.
Nilirudia kumsalimu lakini bado hakunijibu chochote
na wala hakuonyesha kama ananisikia. Nilimgusa begani lakini bado ilikuwa ni
kazi bure, aliendelea kufutafuta bodaboda yake, nikabaki nimepigwa na butwaa.
Ilibidi nimsogelee dereva mwingine wa bodaboda, naye nikamsalimia kwa bashasha lakini hakunijibu, nikarudia tena na tena lakini bado hali ilikuwa ileile, nikaenda kwa watatu ambaye alikuwa akipiga stori na wenzake, naye akaonyesha kutonisikia.
Ilibidi nimsogelee dereva mwingine wa bodaboda, naye nikamsalimia kwa bashasha lakini hakunijibu, nikarudia tena na tena lakini bado hali ilikuwa ileile, nikaenda kwa watatu ambaye alikuwa akipiga stori na wenzake, naye akaonyesha kutonisikia.
“Kwani imekuwaje? Mbona sielewi kinachoendelea?”
nilijisemea huku nikianza kutetemeka kwa hofu kubwa, mwisho niliamua kufanya
jambo moja, nilipaza sauti kwa nguvu nikiita ‘bodabodaaa!’ niliamini yeyote
ambaye atakuwa wa kwanza kuniona basi nitamchukua huyohuyo lakini wapi! Kila
mmoja aliendelea na mambo yake.
Ni hapo ndipo nilipogundua kwamba huenda nilikuwa
sionekani kwa macho ya kawaida wala sauti yangu haisikiki licha ya ukweli
kwamba mwenyewe nilikuwa najisikia vizuri tu.
“Sasa nitafanyaje?” nilisema huku nikigeuka kuitazama
ile ‘ambulance’, tayari ilishapotea kwenye upeo wa macho yangu lakini akili
zangu zilinituma kuamini kwamba lazima itakuwa imeupeleka mwili wangu Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili.
“Nataka nikashuhudie kila kitu kinachoendelea,” nilisema
huku nikianza kutafuta mbinu nyingine ya kunifikisha hospitalini hapo. Sijui
nilipata wapi akili hizo lakini nilijikuta tu nikiamua kuanza kutimua mbio
kuelekea kule ile ambulance ilikoelekea.
Nilipopiga hatua chache tu, nilijikuta nikiwa
napaa angani kwa kasi kubwa, nikawa naitazama mitaa ya jiji kutokea angani.
Kuna wakati akili zangu zilinituma kuamini kabisa kwamba nilikuwa kwenye ndoto
ya kutisha ambayo muda wowote itaisha lakini akili nyingine zikawa zinaniambia
kwamba siyo ndoto, kila kitu kilikuwa kikitokea kwa uhalisia.
Wakati ambulance ikiwasili kwenye geti kuu la
kuingilia Muhimbili, na mimi tayari nilikuwa nimeshafika eneo hilo, geti
likafunguliwa na likaingia moja kwa moja mpaka kwenye eneo la ‘emergency’ ambalo
wagonjwa wenye hali mbaya ndipo walipokuwa wanafikia.
Milango ya ambulance ilifunguliwa, manesi waliokuwa
ndani ya ile ambulance pamoja na wengine waliokuwa pale mapokezi, walisaidiana kuushusha
mwili wangu na kukimbizwa mpaka ndani, nikawa nashuhudia kila kitu kilichokuwa kinaendelea.
Harakaharaka nilianza kupewa huduma ya kwanza,
nikamuona nesi mmoja akichukua mkasi na kukata shati nililokuwa nimevaa,
nilipoliona jeraha lililokuwa kifuani wangu,
nilisisimka mno. Nilijiuliza iweje mtu anifanyie ukatili mkubwa kiasi hicho,
tena bila sababu ya msingi?
Japokuwa vitabu vya dini vinakataza kulipa kisasi,
nilijikuta nikipandwa na ari kubwa ya kulipa kisasi, nilikuwa nimejeruhiwa
sana. Niliwaona hata wale manesi akitetemeka kila walipokuwa wanalitazama jeraha
langu.
Kwa bahati nzuri, madaktari wa kiume waliingia, huwa
naamini siku zote kwamba sisi wanaume Mungu ametuumba na ujasiri mkubwa kuliko wanawake.
Wakaanza kunifanyia kile ambacho
kitaalamu huwa kinaitwa ‘dressing’, yaani
kusafisha jeraha kabla ya kuanza kutibiwa. Muda mfupi baadaye, tayari nilikuwa nimesafishwa
jeraha hilo, nikahamishwa na kupelekwa chumba cha wagonjwa mahututi nikiwa bado
sijitambui huku madaktari na manesi wakiendelea kuhangaika kudhibiti damu
zilizokuwa zinaendelea kunitoka kwa wingi.
Nilipoingizwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi,
harakaharaka niliunganishwa kwenye mashine ya kunisaidia kupumua huku dripu ikitiririka
kwa kasi kuingia kwenye mishipa yangu.
“He has lost a great deal of blood, he need an urgent
transfusion,” (Amepoteza damu nyingi sana, anahitaji kuongezewa damu haraka
iwezekanavyo) alisema daktari mmoja kwa Kiingereza, kwa kuwa na mimi shule
ilikuwepo kiasi chake kichwani, nilimuelewa vizuri.
Niendelee kusisitiza kwamba wakati haya yote yakitokea,
katika ulimwengu wa kawaida sikuwa na fahamu hata kidogo, nilikuwa nimefumba macho
na kulala pale kitandani kama maiti, nikiwa nimeunganishwa na mashine ya
kunisaidia kupumua lakini katika ulimwengu mwingine ambao hata sijui niuiteje,
nilikuwa nimesimama kwenye pembe moja ya ile wodi, nikishuhudia kila kilichokuwa
kinaendelea.
Kazi ya kuokoa maisha yangu iliendelea, madaktari
na manesi wakawa wanapishana huku na kule, huyu kabeba dawa, huyu kabeba chupa
ya damu, huyu mikasi na sindano, ilimradi kila mmoja alikuwa bize.
Nilijisikia ahueni kubwa ndani ya moyo wangu kuona
watu ambao pengine hata hawakuwa wakinijua, wakipigana kuokoa maisha yangu. Niliendelea
kuwatazama wanavyohangaika, kuna wakati machozi ya uchungu yalikuwa yakinitoka kwa
sababu ya kilichotokea, nikawa naendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa
majibu.
Nilivuta kumbukumbu ya jinsi mambo yote
yalivyoanza kutokea.
***
Januari 16, 2012
Mikocheni, Dar es Salaam.
“Haloo!”
“Haloo, nani mwenzangu.”
“Mh! Kwani namba yangu hujaisevu Moses, mbona una
visa wewe.”
“Samahani, utakuwa umekosea namba, mimi siitwi
Moses wala sikufahamu.”
“Ooh! Basi samahani kaka yangu nitakuwa nimechanganya
namba. Samahani sana.”
“Usijali, kuwa makini,” yalikuwa ni mazungumzo kati
yangu na mtu aliyepiga simu na kunifananisha.
Nilikata simu na kubonyeza kitufe kwenye rimoti ya
runinga yangu kubwa (flat screen) niliyokuwa nimekata sauti (mute) baada ya
kuona simu yangu inaita. Nikawa naendelea kutazama muvi kwani miongoni mwa vitu
nilivyokuwa navipenda, ilikuwa ni kutazama muvi, kuangalia mpira na kusikiliza muziki,
hasa muda ninaokuwa nyumbani baada ya kutoka kazini.
Haukupita muda mrefu, simu yangu ikawa inaita tena,
nilikasirika kwa sababu muvi ilikuwa imefika sehemu nzuri na sikutaka inipite
hata sehemu moja, safari hii nilibonyeza kitufe cha ‘pause’ kuisimamisha ili
isiendelee, nilipotazama namba ya mpigaji, ilikuwa ni ileile ya yule mtu
aliyedai kukosea namba.
“Samahani mpendwa najua nakusumbua, nimeangalia
vizuri simu yangu na kugundua kuwa ni kweli nilikosea namba wakati nakupigia.”
“Usijali dada, tufanye yameisha.”
“Ahsante kwa kunisamehe kaka yangu, japo sikujui
lakini unaonekana mstaarabu sana. Mimi naitwa Shenaiza sijui mwenzangu unaitwa
nani.”
“Naitwa Jamal au kwa kifupi Jay,” nilimjibu kwa kifupi
kwa sababu niliona kama ananiletea stori zisizo na kichwa wala miguu.
“Ooh! Nimefurahi kukufahamu kaka Jamal. Unaishi
wapi vile?”
“Mikocheni,” nilimjibu na safari hii niliamua kubonyeza
tena rimoti, muvi ikaendelea kwani niliona hana chochote cha maana cha
kuniambia, nikawa nimeiweka simu sikioni huku nikiendelea kuangalia muvi.
“Mbona kuna kelele kwani uko wapi?” alihoji msichana
huyo lakini sikumjibu chochote, naona baadaye alijishtukia mwenyewe, akaamua
kukata simu. Nikaiweka simu pembeni na kuendelea kutazama muvi.
Baadaye ilipoisha, nilichukua simu yangu na kugundua
kuwa kulikuwa na meseji nyingi zimeingia bila mwenyewe kushtukia, nikaanza
kuzisoma moja baada ya nyingine.
Nilishangaa kugundua kwamba ukiachilia mbali meseji
mbili za rafiki zangu, Justice na Prosper, nyingine zote zilikuwa zimetoka kwa
yule msichana aliyekosea namba ya simu, nikashusha pumzi ndefu na kuanza
kuzisoma, moja baada ya nyingine nikiwa
na shauku kubwa ya kutaka kuona ameandika nini.
Je, nini kitafuatia? Meseji zinahusu nini? Usikose
next issue.
No comments:
Post a Comment