ILIPOISHIA:
WALE wageni waliaga na kuondoka, baba akatuita
tena ndani na kuanza kuhesabu fedha zilizopatikana. Zilikuwa ni shilingi
milioni mbili na laki tatu, akasema zingetosha kabisa kwa safari yetu.
Tukakubaliana kwamba tumalizie maandalizi na asubuhi ya siku ya pili tuianze
safari ya kuelekea jijini Dar es Salaam.
SASA ENDELEA...
KWELI usiku huo hakuna hata aliyepata lepe la
usingizi, ‘kimuhemuhe’ cha safari kilitufanya tukae macho mpaka jogoo la kwanza
lilipokuwa linawika. Baba alituagiza kwamba tubebe vile vitu vya muhimu tu kwa
sababu maisha ya kijijini yalikuwa tofauti sana na maisha ya mjini.
Akatuambia vitu vingine tuviache palepale na
vitakuwa salama kwa sababu kuna walinzi anawaacha kwa ajili ya kutulindia mji
wetu. Aliposema walinzi sikumuelewa kwa haraka anamaanisha nini, akili nyingine
zikanituma kuamini kwamba labda watakuwa ni mgambo lakini nilijiuliza anaweza
kuwaacha mgambo ndiyo walinde nyumba yetu wakati hawakuwa wakielewana? Sikupata
majibu.
Saa kumi na nusu za usiku, tulitoka na kuanza
kutembea kuelekea stendi, kila mmoja akiwa na mzigo wake. Tukaenda mpaka stendi
ambapo tulipanda gari la kwanza kabisa ambalo lilikuwa likielekea Mbeya mjini,
lakini cha ajabu, wakati wote tumeshapanda kwenye gari, baba yeye alibaki
chini.
Tukawa tunasubiri na yeye apande lakini
hakufanya hivyo, sanasana tukamuona akiwa anazungumza na mama, kupitia dirisha
la gari lile tulilokuwa tumepanda, nadhani alikuwa akimpa maelekezo muhimu sana
kwa sababu muda wote mama alikuwa akitingisha kichwa kuashiria kuelewa kile alichokuwa
akiambiwa.
Baada ya kumaliza kuzungumza na mama, baba
alikuja moja kwa moja pale nilipokuwa nimekaa mimi, akanipa mkono na kuniambia
kwamba tutangulie yeye atafuata, akaniambia ananiamini mimi zaidi kwa hiyo
lazima niwe makini kuwalinda ndugu zangu.
Nilijisikia fahari sana kwa jinsi baba
alivyokuwa akinipa kipaumbele kwenye mambo ya msingi japokuwa nilikuwa na kaka
zangu na mimi ndiyo nilikuwa mdogo. Baada ya dakika chache, dereva aliingia
ndani ya gari, akawasha na safari ya kutoka Makongorosi kuelekea Mbeya mjini
ikaanza.
Safari haikuwa nyepesi, kwa sababu sehemu
kubwa ya njia ya kutokea Chunya kuelekea Mbeya mjini, ni milima na mabonde
makubwa, ikiambatana na miteremko ambayo kama dereva hayupo makini hamuwezi
kufika salama. Ukizingatia na lile giza la alfajiri ile, kila mmoja alikuwa
akiomba moyoni tufike salama. Baada ya safari ndefu, hatimaye tuliwasili
Mbalizi, gari likashusha baadhi ya abiria na kuingia Barabara Kuu ya
Mbeya-Tunduma ambayo ni ya lami, likaendelea na safari ya kuelekea Mbeya Mjini.
Nikiri kwamba hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya
kwanza kufika mjini na kila kitu kwangu kilikuwa kigeni. Sikuwahi kuona
barabara ya lami, sikuwahi kuona magari mengi ya kila aina wala sikuwahi kuona
nyumba nzuri na za kisasa, nyingine zikiwa na maghorofa.
Ilikuwa ni safari ambayo iliufurahisha mno
moyo wangu, nikawa nachekacheka tu mwenyewe. Hali ilikuwa hivyohivyo kwa ndugu
zangu wengine ambao nao walikuwa na ushamba ulioonekana waziwazi kwenye sura
zao. Safari yetu ilienda kuishia kwenye Stendi Kuu ya Mabasi ya Mbeya au
maarufu kama Mbeya Terminal.
Cha ajabu, wakati gari likikata kona kuelekea
sehemu ya kushushia abiria, nilimuona baba akiwa chini, akilitazama gari
tulilokuwa tumepanda. Nikabaki na maswali mengi yasiyokuwa na majibu, kwamba
alifikaje kabla yetu? Kumbukumbu zangu zilinionyesha kwamba kule Chunya, stendi
kulikuwa na gari moja tu ambalo ndiyo hilo ambalo sisi tulipanda.
Na safari nzima, hatukupitwa na gari lingine
lolote, wala chombo kingine cha usafiri, si bodaboda wala Bajaj, sasa baba alifikaje
pale kabla yetu? Yalikuwa ni maswali ambayo sikuwa na majibu yake. Lakini cha
ajabu, nilipomgeukia mama wala hakuonyesha kushtushwa na uwepo wa baba eneo
lile, nikamuona akimpungia mkono kama anayemwambia ‘tuko hapa’.
Gari liliposimama, baba ndiye aliyekuwa
akitupokea mizigo, ndugu zangu wote walionekana kuchukulia uwepo wa baba eneo
lile kama kitu cha kawaida, kwa kifupi hakuna aliyekuwa na akili ya udadisi
kama niliyokuwa nayo mimi, nadhani ndiyo maana baba alikuwa akinipenda zaidi
yao.
Alitupokea mizigo na kutusaidia kushuka,
tukasimama pembeni ya gari, mimi nikawa namtazama nikiwa sina majibu ya maswali
yangu kabisa. Mimi na ndugu zangu wote tulikuwa tumechafuka miili yetu kwa
sababu ya kusafiri kwenye barabara ya vumbi kutoka Chunya lakini baba yeye
alikuwa msafi kabisa.
“Tunasafiri na basi lile pale,” alisema baba
kwa sauti ambayo wote tuliisikia vizuri, akatuonyesha kwenye basi kubwa
lililokuwa limeinama upande wa mbele kama ndege ya kijeshi, wote tukawa
tunalitazama basi lile kwani muundo wake ulikuwa wa aina yake na sidhani kama
kuna yeyote kati yetu ambaye aliwahi kuliona basi kama hilo kwa macho.
Basi tulibeba vifurushi vyetu na kuanza
kumfuata baba ambaye alitupeleka mpaka kwenye lile basi, yeye akawa wa kwanza
kuingia, akawa anatusaidia kupanda ngazi mmoja baada ya mwingine. Wa mwisho
alikuwa mama ambaye alikuwa na mzigo mkubwa, baada ya kuingia, baba alianza
kusoma namba za siti zilizokuwa zimeandikwa upande wa juu wa basi hilo kubwa,
mpaka alipozipata.
Kila mtu alikuwa na siti yake, akawa
anatuelekeza sehemu za kukaa, akampa mama tiketi zetu wote kisha nikamuona
akizungumza naye mambo fulani, akaingiza mkono mfukoni na kutoa noti kadhaa za
shilingi elfu kumikumi, mama akamshukuru, kisha akamuinamia sikioni na
kumuongelesha mambo ambayo hakuna aliyesikia.
Wakati akimnong’oneza mama, macho ya baba
yalikuwa kwangu, nilipoona ananiangalia, ikabidi nikwepeshe macho yangu kwani
tulifundishwa kwamba siyo heshima kuwatazama baba na mama wanapokuwa na
mazungumzo yao ya siri.
Baada ya hapo, alikuja pale nilipokuwa
nimekaa, akaniinamia na kurudia kuniambia maneno yaleyale aliyoniambia wakati
tukiondoka kule Chunya. Aliniambia kwamba ukimtoa mama, mimi ndiye niliyepaswa
kuwa mkuu wa msafara na lazima nihakikishe tunafika salama salmini tuendako,
akanipigapiga mgongoni kisha akanipa mkono.
Alifanya hivyohivyo kwa ndugu zangu wengine
pia, akawapa mkono mmoja baada ya mwingine kisha akarudi kwangu na kuniambia
kwamba tutangulie yeye anafuata.
“Lakini baba... sisi wote ni wageni huko tunakoenda,
kwa nini usikae na sisi kwenye hili basi? Tukipotea je?” nilimuuliza, swali
lililomfanya anitazame usoni kwa makini, nikakwepesha macho yangu kwa sababu
baba alikuwa na hali fulani ambayo akikukazia macho lazima utazame pembeni.
“Kwani kutoka Chunya kuja hapa nani alikuwa wa
kwanza kufika?” aliniuliza, swali lililonifanya nipate nafasi ya kutoa dukuduku
nililokuwa nalo moyoni.
“Tena nilitaka kukuuliza, kwani ulikuja na
usafiri gani na kwa nini wewe hujachafuka kama sisi?”
‘Wewe ni mwanaume, lazima ujifunze kuwa na
akiba ya maneno, siyo kila unachokiona ukizungumze au uulize, sijakuzaa kuja
kuwa msindikizaji maishani mwako,” alisema kwa sauti ya chini ambayo ni mimi tu
niliyeisikia lakini iliyokuwa imebeba ujumbe mzito sana ndani yake, nikashusha pumzi
na kukaa vizuri kwenye siti yangu.
Tayari dereva alishaanza kupiga ‘resi’ nyingi
na kupiga honi, kuonyesha kwamba muda mfupi baadaye safari ingeanza. Baba
akatembea harakaharaka kuelekea kwenye mlango wa kushukia, akateremka mpaka
chini na kusimama upande ule tuliokuwa tumekaa, gari likaanza kuondoka ambapo
alitupungua mikono, na sisi tukafanya hivyo.
Safari ikaanza, hiyo ilikuwa ni karibu saa
kumi na mbili na nusu, basi likaanza kuchanja mbuga kuelekea Dar es Salaam.
Baada ya kusafiri umbali mfupi, tukiwa
tumefika eneo maarufu liitwalo Mlima Nyoka, lililokuwa kilometa chache kutoka
Uyole mjini, tulishangaa kuanza kuona gari likiyumbayumba. Nilikuwa nikisikia
sifa za eneo hilo mara kwa mara kwamba magari mengi, hasa ya abiria yalikuwa
yakipata ajali na kuua abiria wengi, mapigo ya moyo yakawa yananienda mbio
kuliko kawaida.
Kulikuwa na mteremko mkali wenye kona za
hatari, na baada ya kuvuka daraja kulikuwa na mlima mkali pia, jambo ambalo
lilimaanisha kama dereva akishindwa kulimudu gari, ajali yake ingekuwa si ya
mchezo. Dereva alizidi kuyumba huku gari likiongeza kasi, hali iliyofanya
abiria waanze kupiga kelele kwa nguvu, wengi wakilitaja jina la Mungu.
Gari lilizidi kuongeza kasi, likawa linashuka
kwenye mteremko huo kwa kasi kubwa huku likiendelea kuyumba huku na kule,
kelele ndani ya basi zikazidi kuongezeka.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
bUY bEST
ReplyDelete