ILIPOISHIA:
“Naongea na wewe Togolai, ni kweli nini?”
alihoji tena Madam Timbuka, safari hii akiwa amenikaribia kabisa pale
nilipokuwa nimekaa, nikaanza kubabaika huku hofu kubwa ikishindwa kujificha
kwenye uso wangu.
SASA ENDELEA...
“Kwamba mwalimu wetu anaumwa. Nilisikia
asubuhi nikawa siamini,” nilidanganya, nikamuona mwalimu Timbuka akishusha
pumzi ndefu, wanafunzi wenzangu waliokuwa wakinitazama kwa shauku, nao
walionesha kuridhika na majibu yangu.
Baada ya kutoa taarifa hizo, mwalimu Timbuka
alitutaka tusipige kelele bali tuutumie muda huo kujisomea, akatoka na kutuacha
wote tukiwa kimya. Moyoni mwangu niliendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa
majibu.
“Kwa hiyo mwalimu Mwashambwa naye atakufa?”
nilijiuliza moyoni wakati nikiendelea kutafakari taarifa za ugonjwa wa mwalimu
wetu. Nilijaribu kuunganisha matukio, hofu ikazidi kuongezeka ndani ya moyo
wangu. Bado sikutaka kuamini kwamba baba alikuwa mchawi na alikuwa akihusika na
kilichokuwa kinaendelea.
Muda ulizidi kusonga mbele, hatimaye ukawadia
muda wa mapumziko. Kwa kawaida, ilikuwa ikifika muda wa mapumziko, kengele
inagongwa mara mbili kuashiria wanafunzi wote tutoke madarasani lakini siku
hiyo, kengele iligongwa tofauti. Iligongwa mfululizo huku walimu wakiwa wameshatoka
na kusimama mstarini, kila mmoja akionekana kuwa ‘siriasi’.
“Kuna nini kwani?” nilijiuliza wakati
nikisimama na kutoka pamoja na wanafunzi wenzangu, tukaelekea mstarini huku
kila mmoja akiwa na shauku kubwa ya kusikia kilichofanya tukusanyike muda huo,
jambo ambalo siyo la kawaida.
Mwalimu mkuu wetu, Nyerema alisimama na
kututaka wote kutulia na kumsikiliza alichokuwa anataka kutuambia.
“Ni siku mbaya kwetu, najua wote mnajua kwamba
mwalimu wenu, Mwashambwa alikuwa anaumwa sana, taarifa mbaya ni kwamba hatunaye
tena, tumepokea taarifa za kifo chake muda huu, nawaomba nyote mtulie na muwe
wavumilivu katika kipindi hiki kigumu, taratibu nyingine mtatangaziwa baadaye,”
alisema mwalimu Nyerema, vilio vikaanza kusikika kutoka kwa wanafunzi.
Siyo siri nilipatwa na mshtuko mkubwa sana,
sikutaka kuamini kwamba mwalimu Mwashambwa ameondoka. Niliunganisha matukio na
kile nilichoelezwa na baba, nikawa siamini.
“Ina maana baba ndiye anayehusika na kifo cha
mwalimu wetu pia?” nilijiuliza moyoni nikiwa bado nimesimama palepale. Nikiwa
katika hali ile, nilihisi kuna mtu ananitazama, nikageukia kule mtu huyo
alipokuwepo. Hakuwa mwingine bali mwalimu Timbuka ambaye alikuwa akinitazama
kwa makini. Kwa ilivyoonesha, alikuwa akinitazama kwa muda mrefu, nikabaki
kubabaika kwa sababu sikuelewa kwa sababu gani ananitazama namna ile.
Ili kuvunga, nilijichanganya na wanafunzi
wengine na kuondoka eneo hilo, nikarudi darasani ambako wanafunzi wengi
walikuwa wakiendelea kulia kwa uchungu. Baadaye kengele iligongwa tena, tukatoka
na kwenda mstarini ambapo tulipewa utaratibu wa namna ya kushiriki msiba wa
mwalimu wetu.
Wakati wanafunzi wengine wakifunga safari
kuelekea kwa mwalimu Mwashambwa, mimi nilichepuka na kukimbilia nyumbani,
moyoni nikiwa na dukuduku kubwa.
“Amekufa kama ulivyosema.”
“Si nilikwambia? Umeamini sasa!”
“Kwa hiyo wewe ndiyo umemuua? Kwani baba wewe
ni mchawi?” nilijikuta nikimuuliza baba swali ambalo hata yeye hakulitegemea,
akanitazama kwa macho ya ukali.
“Nani aliyekwambia mimi ni mchawi?”
“Nimesikia watu wakisema, hata shuleni kwetu
kote watu wananinyooshea vidole wakisema eti mimi na wewe tunashirikiana
uchawi,” nilisema huku nikitetemeka, baba akanisogelea kisha akashusha pumzi
ndefu.
“Mwanangu Togolai, lazima ujue kwamba hapa
kijijini sisi tuna maadui wengi sana kwa sababu ya kazi ninayofanya baba yako.
Watu wengi wananionea wivu kwa sababu hakuna mganga mwenye nguvu kama mimi
ukanda wote huu. Sasa maadui zangu wameanza kunizushia na kunichafulia sifa
nionekane mchawi lakini siyo kweli, mimi ni mganga wala siyo mchawi,” alisema
baba kwa sauti iliyojaa busara na upole.
Licha ya maneno yote yaliyokuwa yanazungumzwa
na watu, nilikuwa nikiamuamini sana baba. Niliyaamini maelezo yote aliyonipa
kwa asilimia mia moja, na mimi nikashusha pumzi ndefu kisha tukawa tunatazamana
na baba.
“Ikitokea mtu mwingine yeyote anakutania au
anakuzodoa kuhusu uchawi, naomba uje unieleze moja kwa moja, wakati mwingine
inabidi tuwe wakali ili kulinda heshima yetu,” alisema baba kisha akainuka na
kuniacha nimekaa palepale, nikawa naendelea kuyatafakari maneno aliyoniambia.
Japokuwa nilikuwa nampenda sana mwlimu
Mwashambwa, sikuweza kuhudhuria kwenye msiba wake nikihofia macho ya watu kwani
tayari maneno yalikuwa yamesambaa sana kwamba baba alikuwa anahusika na vifo
vya ghafla vya watu wawili, Mwankuga na Mwashambwa vilivyotokea mfululizo.
Hatimaye mazishi yalifanyika lakini
manenomaneno yalizidi kuwa mengi kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele. Siku
moja nikiwa shuleni, nilisikia wanafunzi wenzangu wakinitena kwamba mwisho wa
ubabe wa familia yetu ulikuwa umefika kwa sababu wanakijiji walikaa kikao cha
pamoja na kufikia maazimio ya kwenda kumleta mganga mashuhuri kutoka Chitipa,
Malawi kwa ajili ya kuja ‘kuwanyoa’ uchawi watu wote waliokuwa wakihisiwa
kuhusika na ushirkina pale kijijini kwetu, akiwemo baba.
“Baba nimesikia eti kuna mganga amefuatwa
Malawi kuja kuwanyoa uchawi watu wote wanaotajwa kuhusika kusababisha viofo vya
watu wasio na hatia hapa kijijini, ukiwemo wewe,” nilimwambia baba baada ya
kurejea kutoka shuleni.
Tofauti na nilivyotegemea, baba hakuonesha
kushtushwa na kitu chochote, akawa anaendelea kukatakata mizizi ya dawa nje ya
nyumba yetu huku akisema kwamba wanajisumbua kwa sababu yeye siyo mchawi.
“Watanyoana wenyewe kwa wenyewe, mimi hakuna
mtu anayeweza kunigusa,” alisema baba kwa kujiamini, nikakosa cha kuendelea
kuzungumza. Maisha yaliendelea kusonga mbele, siku saba baadaye, mkutano wa
wanakijiji ulitishwa kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Makongorosi ambapo
wanakijiji wengi walikusanyika.
“Baba wewe huendi kwenye mkutano?”
“Siendi, kama unataka nenda kaniwakilishe,
nina shughuli zangu muhimu siwezi kuziacha kwenda kusikiliza upumbavu wa watu
wa kijiji hiki,” alisema baba kwa kujiamini.
Kwa kuwa siku hiyo sikuwa na kazi, ilibidi
nifanye kama baba alivyoniambia, nikaenda kumuwakilisha ingawa nililazimika
kukaa nyumanyuma, sikutaka watu wajue kwamba niko pale. Niweke wazi kwamba
tuhuma zilizokuwa zinamkabili baba na familia yetu kwa jumla zilitufanya
tuikose amani kabisa.
Kila tulipokuwa tukionekana, ilikuwa ni lazima
tunyooshewe vidole, jambo ambalo binafsi liliniathiri sana kisaikolojia.
Nikapoteza kabisa uwezo wa kujiamini, nikawa naishi kama digidigi, hali
kadhalika kwa ndugu zangu wengine ingawa kwa baba yeye alionekana kutojali
chochote.
“Tumechoshwa na uchawi hapa kijijini kwetu.
Kwa pamoja tumefanikisha ujio wa mganga Mabwanji kutoka Malawi kwa lengo la
kusafisha kijiji chetu. Wale wote waliokuwa wanaringia uchawi wao, kiboko yao
amewasili, karibu uwasalimie wanakijiji,” alisema mzee wa kimila pale kijijini
ambaye tulizoea kumuita Mwene.
Mwanaume mzee mwenye macho mekundu sana na
midomo myeusi, akiwa amejifunga shuka refu lenye rangi nyekundu na nyeusi,
kichwani akiwa amejifunga kitambaa cheusi, shingoni akiwa na hirizi kadhaa na
shanga, alisimama na kunyoosha juu mkia wa mnyama ambaye sikuwa namjua, watu
wote wakashangilia kwa nguvu.
“Sina mengi ya kuzungumza, naomba ushirikiano
wenu tuwakomeshe wachawi wa kijiji hiki,” alisema mwanaume huyo kwa Kiswahili
kibovu, watu wakashangilia tena kwa nguvu kisha Mwene akaendelea na maelezo,
akisisitiza kwamba kazi lazima ianze siku hiyohiyo usiku.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment