ILIPOISHIA:
Tulipokaribia nyumbani kwa mzee huyo, baba
alinionesha ishara kwamba nisimame, nikafanya hivyo, tukawa tunasikia sauti za
watu wengi wakilia kutoka nyumbani kwa mzee huyo, baba akanionesha ishara kama
anayesema ‘unaona?’, nikashika mdomo kwa mshangao. Sikutaka kuamini kwamba
kweli mzee Mwankuga alikuwa amefariki dunia.
SASA ENDELEA...
Nilijikuta nikishusha lile furushi la dawa na
panga, nikawa nataka niende kushuhudia mwenyewe kama ni kweli lakini baba
aliniambia nisithubutu kufanya hivyo, hasa kutokana na uhasama uliokuwepo kati
yetu na familia hiyo. Bado niliendelea kuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua
kama ni kweli yule mzee amekufa.
Ilibidi baba anishike mkono, tukaenda mpaka
nyumbani ambapo baba aliingia kwenye chumba chake cha uganga na kuanza kuchambua
zile dawa tulizotoka nazo porini. Ni kama alijua kwamba nitamtoroka na kurudi
kule msibani kwenda kushuhudia kilichotokea kwani aliniambia nikae palepale,
nimuangalie jinsi alivyokuwa akichambua dawa.
Kweli nilitii maagizo yake, nikakaa pale
lakini bado nilikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kilichoendelea.
Nilipomuona baba amezama kwenye kazi yake hiyo, niliinuka na kuanza kuelekea
mlangoni, akaniwahi na kuniuliza ninakokwenda.
“Naenda kujisaidia baba,” nilimdanganya baba,
akanitazama usoni kisha akaendelea na kazi yake. Nilitoka na kwenda chooni
ambako nako nilizunguka nyuma, nikatokomea huko na kwenda kutokea upande wa
pili, nyumbani kwa mzee Mwankuga.
Kwa kuwa watu walikuwa wengi, hakuna
aliyenitazama vizuri, kwa hiyo nikapata nafasi ya kujichanganya na waombolezaji
ambao kadiri muda ulivyokuwa unazidi kusonga mbele ndivyo walivyokuwa wakizidi
kuongezeka.
“Kwani alikuwa anaumwa?”
“Hapana alikuwa mzima wa afya kabisa na
alikuwa akiendelea na kazi zake, mara akaanza kulalamika kwamba kichwa
kinamuuma sana, damu zikawa zinamtoka puani na mdomoni, ghafla akadondoka na
kugeuza macho, muda mfupi baadaye moyo wake ukasimama,” nilimsikia ndugu mmoja
wa Mwankuga akimuelezea mmoja wa waombolezaji.
Ni hapo ndipo nilipoamini kwamba kweli
Mwankuga alikuwa amekufa, kwa kuhofia kuonekana na watu, hasa ndugu zake ambao
kama nilivyosema tangu awali hatukuwa na uhusiano nao mzuri, nilirudi
kinyumenyume, kisha nikaondoka haraka kurudi nyumbani.
Nilimkuta baba akiwa amesimama nje ya nyumba
yetu, akinitazama, nadhani alishashtukia kwamba nimemtoroka, aliponiona tu
natokeza, akanibana kwa maswali magumu.
“Ulikuwa wapi?”
Nilikosa cha kujibu, nikawa najiumauma, baba
akaniambia nina bahati sana vinginevyo angenifunza adabu, tukaingia ndani
ambapo tulienda mpaka kule kwenye chumba cha uganga, baba akanikalisha chini na
kuanza kuzungumza na mimi.
“Unajua wewe ndiyo mwanangu kipenzi na sasa
umeshakuwa mkubwa, sina sababu ya kuendelea tena kukuficha mambo yangu ndiyo
maana leo nimekuonesha baadhi ya mambo.
“Dunia imebadilika sana mwanangu, binadamu
tunaishi kwa ubaya sana, hakuna anayemtakia mwenzake mema, watu wanawaonea
wengine bila sababu, watu wasio na hatia wanakufa kila siku, ukienda
makaburini, yaliyojaa ni makaburi ya watu wasio na hatia! Kila mmoja lazima
ajilinde mwenyewe na ukishaweza kujilinda mwenyewe, unaweza pia kuwalinda
wenzako,” alisema baba, maneno ambayo yaliniingia lakini bado sikuwa naelewa
kile alichokuwa anakimaanisha.
Bado nilikuwa nataka ufafanuzi wa kifo cha
mzee Mwankuga kwa sababu kwa akili yangu, niliona kama hakuwa amefanya jambo
lolote kubwa kustahili adhabu ya kifo. Ni kama baba aliyaona mawazo yangu,
akaniambia anajua najiuliza maswali mengi yasiyo na majibu kuhusu kilichotokea
kule msituni.
“Kuna yule rafiki yako aliyekufa kwa
kutumbukia kwenye kisima mwaka jana, unamkumbuka?”
“Alfred? Ndiyo namkumbuka,” nilimjibu baba
huku nikiwa na shauku ya kutaka kusikia anachotaka kukisema. Akaniambia
mazingira ya kifo cha Alfred, yalikuwa yamejaa utata wa hali ya juu na kwamba
baada ya kuchunguza kwa kina, aligundua kwamba Alfred hakufa kifo cha kawaida,
bali aliuawa.
Akaendelea kuniambia kwamba hata huko kuuawa
kwenyewe, japokuwa kila mtu alikuwa anajua ni kweli amekufa na kuzikwa, lakini
ukweli ni kwamba hakuwa amekufa bali alichukuliwa msukule.
“Kwani kuna tofauti gani kati ya mtu aliyekufa
na mtu aliyechukuliwa msukule?” Nilimuuliza baba, akaniambia kwamba mtu
aliyekufa kwa kifo cha amri ya Mungu, huwa mwili unatengana na roho, mwili
unaenda kuzikwa kaburini na huo ndiyo unakuwa mwisho wa maisha ya kawaida ya hapa
duniani.
Akaniambia pia kwamba kwa kawaida, nafsi au
roho ya mtu huwa haiishi ila baada ya kutengana na mwili, huhama kutoka kwenye
ulimwengu wa kawaida na kwenda kwenye ulimwengu mwingine. Nilipotaka kumuuliza
kuhusu huo ulimwengu mwingine, aliniambia kwamba atanifafanulia siku nyingine.
Akaendelea kunieleza kwamba mtu anayechukuliwa
msukule, huwa hafi bali anabadilishwa kichawi kiasi cha kila mmoja kuamini
kwamba ni kweli amekufa lakini kinachotokea, huwa anachukuliwa na wachawi na
kwenda kutumikishwa kichawi kwenye kazi mbalimbali, mpaka siku ambayo atakufa
kwa amri ya Mungu lakini kwa kipindi chote hicho, huwa anaishi kama msukule.
“Sasa mbona Alfred alipokufa tulienda kumzika
makaburini na hata siku ya kuaga mwili wake, wote tulipita kwenye jeneza lake
na mimi mwenyewe nilimshuhudia akiwa amelala ndani ya jeneza?”
“Ni vigumu sana kunielewa hiki ninachokisema
kwa maneno, lakini nataka nikuhakikishie kwamba rafiki yako hakufa na
aliyefanya yote hayo ni huyu mshenzi Mwankuga,” alisema baba akionesha kuwa na
jazba, akaendelea kunieleza kwamba, licha ya Alfred, walikuwepo watu wengine
wengi tu ambao wengine waliuawa kwelikweli lakini kwa ushirikina, ikiwa ni
uonevu unaofanywa na wachawi hasa wanapokaribia kutoa makafara yao, na wengine
huchukuliwa misukule.
Bado sikuwa namuelewa anachokisema, akaniambia
anataka akanithibitishie kwamba Alfred hakufa. Aliacha kila alichokuwa
anakifanya, tukatoka nje ambapo watu walikuwa wakizidi kufurika kwenye msiba wa
Mwankuga na sasa vilio vya wanawake vilikuwa vikizidi kuongezeka.
Wala baba hakujali chochote, tukatoka na
kuelekea makaburini ambayo yalikuwa eneo maarufu linalofahamika kama msalabani,
nilikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujionea mwenyewe kile alichokuwa anakisema
baba kama ni kweli.
“Unakumbuka alizikwa kwenye kaburi gani?” baba
aliniuliza, nikamwambia nakumbuka vizuri kwa sababu enzi za uhai wake, Alfred
alikuwa rafiki yangu mkubwa na kifo chake cha ghafla, kiliniumiza mno moyo
wangu. Kwa kuwa hata siku ya mazishi yake nilikuwepo mpaka makaburini, nilikuwa
nalikumbuka vizuri kaburi lake.
Nikamuongoza baba mpaka kwenye kaburi la
Alfred ambalo juu yake kulikuwa na msalaba ulioandikwa jina lake kamili, tarehe
ya kuzaliwa na tarehe ya kufa kwake. Akaniambia niwe makini kwa kila
atakachokuwa anakifanya, nikatingisha kichwa huku hofu kubwa ikiwa imetanda
ndani ya moyo wangu kwani kiukweli nilikuwa nikiogopa sana makaburi na maiti.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment