ILIPOISHIA:
Huku nikitetemeka, nilisogea mpaka pale yule
mganga alipokuwa amelala, akiendelea kukoroma kwa nguvu, mimi nikamshika
miguuni na baba akamshika kichwani, tukaanza kumkokota kumtoa nje ya eneo letu,
tukaenda kumbwaga pembeni kabisa kwenye vichaka kisha tukarudi ndani. Ile
tunaingia ndani tu, tukasikia mlango ukigongwa kwa nguvu.
SASA ENDELEA...
“Nani!”
“Fungua!”
“Sifungui mpaka mjitambulishe na mueleze shida
yenu.”
“Ni mimi mzee Sifuni, mwenyekiti wa kijiji.”
“Unaonekana hauko peke yako!”
“Ndiyo, nimeongozana na wajumbe wa kamati ya
ulinzi na usalama ya kijiji, fungua tafadhali,” baada ya mwenyekiti huyo kusema
hivyo, baba alinioneshea ishara kwa mkono kwamba niende ndani kwa sababu
alishahisi wale watu wamekuja kwa shari. Nikatii nilichoambiwa na kwenda
chumbani lakini bado nilikuwa na shauku kubwa ya kutaka kuona kinachoendelea.
Baba alipofungua tu mlango, nilisikia
wakimuamrisha jambo:
“Upo chini ya ulinzi.”
“Kwa kosa gani?”
“Kwa kumshambulia mganga wa kienyeji aliyekuwa
anatimiza majukumu yake hapa kijijini kwetu.”
“Hivi nyie mna wazimu nini? Mbona
mnanifuatafuata sana? Sasa anayejiona mbabe aniguse,” nilimsikia baba akifoka
kwa jazba. Yule mwenyekiti akawa anaawamrisha mgambo wamkamate baba lakini kila
mmoja akawa anamtupia mpira mwenzake kwa hofu.
Nadhani lile tukio la ‘kumzimisha’ mganga
ambaye kila mmoja alikuwa akimuona kama ni kiboko, liliwajaza hofu kubwa ndani
ya mioyo yao. Baadaye niliwasikia wakiondoka huku wakitoa maneno ya kumtisha
baba kwamba eti siku zake zinahesabika, wakaelekea ule upande tulikomtupia yule
mganga ambaye bado alikuwa akiendelea kukoroma kama anayetaka kukata roho.
Wakamchukua na kuondoka naye ambapo taarifa
tulizozipata kesho yake ni kwamba alisafirishwa usiku huohuo kuelekea nyumbani
kwao, Malawi akiwa na hali mbaya sana. Siku zilizidi kusonga mbele, uhasama
kati ya familia yetu na wanakijiji wengine ukazidi kushamiri pale kijijini,
kila mtu akawa anatuchukia na kutusema vibaya.
Wiki kadhaa baadaye, siku hiyo nikiwa narejea
kutoka shuleni, nilipata taarifa kwamba yule mganga kutoka Malawi amerejea tena
na safari hii, amekuja na jeshi la waganga wengine kadhaa kwa lengo la kuja
kumkomesha baba kwa alichomfanyia.
Taarifa hizo zilinishtua sana, ikabidi
nimfikishie baba haraka lakini tofauti na nilivyotegemea, alizipokea kwa dharau
na kuendelea kusisitiza kwamba yeye siyo mchawi bali mganga na yeyote
atakayethubutu kumuingilia kwenye mambo yake, atamshikisha adabu.
Niliishiwa maneno, ikabidi nikae kimya
kusubiri kuona mwisho wa hayo yote utakuwa nini. Taarifa za ujio wa waganga hao
kutoka Malawi zilizidi kusambaa kwa kasi ya kimbunga, wanakijiji wengi wakawa
wanaonesha kufurahia ujio wao.
Hatimaye siku moja usiku, tukiwa tumemaliza
kupata chakula cha usiku, kundi la wanakijiji wengi liliwasili pale nyumbani
kwetu, wakiongozwa na wale waganga ambao jumla yao walikuwa watano.
Wakaizunguka nyumba yetu huku watu wakipiga
kelele kwa nguvu wakitaka eti baba akomeshwe. Siyo kwamba namtetea baba yangu
lakini binafsi, mpaka muda huo nilikuwa sielewi kwa sababu gani watu
wanamchukia kiasi hicho wakati hakuwa mchawi kama mwenyewe alivyokuwa anasema
bali mganga.
Vifo vya wanakijiji wawili, Mwankuga na
Mwashambwa havikuwa vigezo vya kumuita baba mchawi kwa sababu wao ndiyo
walioanza kumchokoza na mimi nilikuwepo siku hiyo. Nikawa nahisi kwamba huenda
ni chuki za watu ndizo zilizosababisha yote hayo.
“Anyolewe! Anyolewe!” ule umati uliokuwa nje
ya nyumba yetu ulikuwa ukipiga kelele kushinikiza eti baba anyolewe uchawi.
Baba akatutaka wote tutulie ndani na asiwepo wa kutoka nje hata mmoja, akaingia
kwenye chumba chake cha uganga na muda mfupi baadaye, alitoka mpaka nje
kulikokuwa na wale watu.
Hata sijui nini kilitokea lakini muda mfupi
baadaye tulisikia vishindo vya watu wakikimbia, huku wengine wakipiga kelele za
kuombamsaada, muda mfupi baadaye tukamsikia baba akiiingia ndani na kufunga
mlango, huku akitukana peke yake kuonesha jinsi alivyokuwa na hasira.
Muda mfupi baadaye alituita wanafamilia wote,
akiwemo na mama, akaanza kutuambia kwamba pale kijijini hapafai tena sisi
kuendelea kuishi kwa sababu tulikuwa na maadui wengi na kila mmoja alikuwa
akijitahidi kadiri ya uwezo wake kutuangamiza.
Akasema anajiamini kwamba anaweza kuilinda
vizuri familia yake kwa maana ya kujilinda yeye mwenyewe, sisi pamoja na mali
zetu zote lakini akasema kuwa si vizuri kuishi mahali ulipozungukwa na maadui.
“Sasa tutafanya nini mume wangu?”
“Inabidi tuhamie mjini,” alisema baba, wote
tukawa tunamtazama kwa macho ya shauku kubwa. Sisi tulizaliwa Makongorosi na
maisha yetu kwa asilimia kubwa yalikua pale kijijini, hakuna aliyewahi kuishi
nje ya pale, tukawa tunashangazwa na kauli ile ya baba ingawa kiukweli, mimi
binafsi nilikuwa natamani sana kuishi mjini.
Alitwambia kwamba kuna rafiki yake wa siku
nyingi waliyekuwa wakisoma pamoja, amewahi kumpa mwaliko wa kwenda kumtembelea
jijini dar es Salaam na kuahidi kumpa hifadhi, akatuambia kwamba anadhani huo
ndiyo muda muafaka wa sisi kuhamia Dar es Salaam.
Kiukweli, japokuwa nilikua nimeshinda nikiwa
kama mgonjwa kutokana na hali halisi ya matukio yaliyokuwa yakiendelea
kututokea, habari kwamba tunahama kutoka Makongorosi, Chunya mpaka Dar es
Salaam zilinifurahisha mno.
Baba alifunga kikao na kututaka wote tuanze
kujiandaa kwa sababu muda wowote mambo yatakapokuwa tayari, tutasafiri lakini
akatusisitiza kutomweleza yeyote kuhusu suala hilo, tukakubaliana naye.
Usingizi ulikuwa mtamu sana siku hiyo, kila mmoja akawa anafikiria namna
tutakavyoenda kuyaanza maisha mapya jijini Dar es Salaam.
Si mimi peke yangu ambaye nilikuwa nimechoshwa
na kashfa za kuitwa mtoto wa mchawi, famili ayetu nzima ilikuwa imechoshwa.
Basi siku hiyo ilipita, kesho yake tukaamka asubuhi lakini baba ndiye aliyekuwa
wa kwanza, tukamkuta yupo nje, akatusisitiza kwamba sote hatutakiwi kutoka
kabisa hapo nyumbani siku hiyo kwa sababu za kiusalama.
Alinisisitiza zaidi mimi kwa sababu mara zote
ndiyo nilikuwa namtoroka na kwenda mitaani, nikamuahidi kwamba sitaondoka. Basi
baadaye baba aliondoka, hatukujua ameenda wapi, tukaendelea na maandalizi ya
safari huku kila mmoja wetu akionesha kuwa na furaha kubwa moyoni mwake.
Baada ya kama saa mbili hivi kupita, tulimuona
baba akija akiwa ameongozana na wanaume wawili walioonesha kwamba siyo wakazi
wa Chunya, akaja nao mpaka pale nyumbani, akatutambulisha kwamba ni wateja
waliokuwa wanatafuta shamba la kununua. Baba akatuomba familia nzima tukubali
kuuza shamba letu moja kwa ajili ya kupata fedha za safari.
Nilichokuwa nampendea baba ni hapo tu, alikuwa
anapenda sana demokrasia linapokuja suala la mambo ya familia, tulikubali na
kwa akaniita mimi niongozane naye mpaka kwenye shamba letu moja. Wakaanza
kupimishiana na baada ya kukubaliana kila kitu, walihesabiana fedha,
wakaandikishana kisha tukaondoka kurudi nyumbani.
Wale wageni waliaga na kuondoka, baba akatuita
tena ndani na kuanza kuhesabu fedha zilizopatikana. Zilikuwa ni shilingi
milioni mbili na laki tatu, akasema zingetosha kabisa kwa safari yetu.
Tukakubaliana kwamba tumalizie maandalizi na asubuhi ya siku ya pili tuianze
safari ya kuelekea jijini Dar es Salaam.
Je, nini kitafuatia? Safari ya Dar
itawezekana? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment