ILIPOISHIA:
Mara
simu yake ilianza kuita mfululizo, akaishika na kutazama namba ya mpigaji
lakini katika hali ambayo sikuielewa, aliiachia simu hiyo, ikadondoka chini na
kufunguka betri ikaangukia kivyake, mfuniko kivyake na simu nayo kivyake.
Akaanza kuangua kilio kwa uchungu huku akiniomba nimsaidie, nilibaki nimepigwa
na butwaa.
SASA
ENDELEA…
“Nikusaidie nini Shenaiza?” nilimuuliza huku
nikiiokota ile simu na kuiunganisha upya.
“Nakuomba usiniache, fanya kila kinachowezekana
unitoroshe hapa hospitalini usiku huuhuu, watakuja kunimalizia,” alisema
msichana huyo na kuzidi kunichanganya.
“Watakuja kukumalizia? Akina nani? Na Kwa nini
tutoroke wakati hali yako bado siyo nzuri?”
“Naomba ufanye nilichokuomba mengine utaenda kuyajua
mbele ya safari,” alisema msichana huyo huku akiendelea kulia.
Nikiwa bado nimeduwaa, nikiwa sijui cha kufanya,
nilishtuka kumuona akichomoa sindano ya dripu aliyokuwa amechomwa mkononi mwake
na kusababisha damu zianze kumtoka mkononi, akajikongoja huku akionesha kuwa na
maumivu makali, akanitaka nimpe bega langu ili apate balansi ya kutembea.
Sikuwa na cha kufanya zaidi ya kukubaliana na
matakwa yake, japokuwa nilikuwa najua kwamba ninachokifanya ni hatari sana
lakini sikuwa na namna zaidi ya kumsaidia msichana huyo ingawa mpaka muda huo
sikuwa najua nini kinachomsumbua.
Huku damu zikimvuja na kudondokea sakafuni,
nilimsaidia kutembea, tukatoka mpaka nje ya wodi hiyo huku mara kwa mara
nikigeuka nyuma kutazama kama hakuna mtu aliyekuwa akitufuatilia.
Kwa bahati nzuri, kwa kuwa muda ulikuwa umeenda
sana, madaktari wengi walishaondoka sambamba na manesi ambapo waliosalia
walikuwa ni wale wenye ‘shift’ ya usiku ambao nao hawakuwa wengi.
“Heeei! Mnakwenda wapi usiku wote huu,” mwanaume wa
makamo ambaye bila hata kuuliza tulijua ni mlinzi wa hospitali hiyo kutokana na
kuvalia sare huku mkononi akiwa na kirungu, alituuliza huku akifunga geti la
kutokea nje.
Ilibidi nimdanganye kwamba nilimleta mgonjwa wangu
kutibiwa majeraha aliyoyapata kwenye ajali lakini hatukumkuta daktari kwa kuwa
alishaondoka, nikamdanganya kwamba tunaenda kujaribu kwenye hospitali nyingine
lakini hakutaka kuelewa. Akasema hawezi kuturuhusu kutoka mpaka tupate kibali
kutoka kwa daktari aliyekuwa zamu usiku huo.
Shenaiza ni kama alijua kilichokuwa ndani ya akili
yangu kwani alianza kuugulia kama anayesikia maumivu makali, nikatumia kigezo
hicho kuendelea kumshawishi yule mlinzi aturuhusu na alipozidi kukomaa,
nilichomoa noti moja ya shilingi elfu kumi na kumshikisha, nikamuona akiachia
tabasamu na kututaka kuwa makini.
Akafungua geti ambapo breki ya kwanza ilikuwa ni
kwenye kituo cha teksi kilichokuwa nje ya hospitali hiyo, tukaingia kwenye
teksi moja na kuondoka huku nikimuelekeza dereva kutupeleka nyumbani kwangu,
Mikocheni.
Kwa kuwa ulikuwa ni usiku na hakukuwa na foleni,
haikutuchukua muda mrefu tukawa tayari tumeshawasili Mikocheni, nilipotaka
kumlipa dereva teksi fedha zake tulizokubaliana, Shenaiza ambaye muda wote
alikuwa amejilaza huku kichwa chake akiwa amekiweka kwenye mapaja yangu,
aliniambia nisilipe.
“Nina fedha za akiba kwenye pochi yangu ndogo, hebu
fungua,” aliniambia, kweli nikafungua pochi yake ndogo aliyokuwa ameiweka
kwenye mfuko wa gauni refu alilokuwa amelivaa. Nilipoifungua, nilishangaa
kukuta kuna noti kadhaa za dola miamia za Kimarekani na noti mbili za shilingi
elfu kumi, zote mpya.
Nikatoa na kumpa dereva na kutaka kurudisha pochi
mahali pale lakini aliniambia kwamba nikae nayo mimi, nikakubali na kuiweka
kwenye mfuko wa suruali niliyokuwa nimeivaa.
Wakati wa kushuka, kama ilivyokuwa wakati wa
kupanda, ilibidi yule dereva teksi anisaidie kumtoa Shenaiza ambaye bado
alikuwa akiugulia maumivu makali, akapitisha mkono wake kwenye bega langu na
nikawa namsaidia kutembea kuelekea ndani kwangu.
Nilifungua mlango na kumkaribisha ndani, japokuwa
alikuwa kwenye maumivu makali, nilimuona akiachia tabasamu hafifu kisha
akanisifia: ”Mh! Jamani wewe msafi hadi raha, inatakiwa umpate mwanamke msafi
kama wewe ndiyo awe mke wako ndiyo mtaendana,” alisema huku akikodolea macho
huku na kule ndani ya sebule yangu.
Japokuwa sikuwa nimeoa lakini hakuna kitu
nilichokuwa nakipenda kama kuiweka nyumba yangu katika hali ya usafi, kuanzia
sebuleni mpaka chumbani huku nikinunua vitu vingi vya kisasa.
Nilimsaidia Shenaiza kukaa pale sebuleni kwenye sofa
kisha nikamvua viatu alivyokuwa amevaa pamoja na koti alilovaa juu ya gauni
lake na mtandio aliokuwa amejizibia lile jeraha la kichwani.
“Shenaiza mwenzio naogopa kulala na wewe ukiwa
kwenye hali hiyo, ukizidiwa usiku itakuwaje? Kwa nini tusiende hospitali
nyingine? Hapa siyo mbali na Hospitali ya Kairuki,” nilimwambia lakini alikataa
katakata na kuniambia kwamba hospitalini haikuwa sehemu salama kwake kwa wakati
huo.
“Basi kuna rafiki yangu anaishi hapo mtaa wa pili ni
daktari lakini bado hajaajiriwa, anafanya ‘field’ hapo Kairuki, unaonaje
nikamuite aje kutusaidia?”
“Hapana usijali, nitakuwa sawa kwa sababu kama ni
damu nimeshaongezewa ya kutosha, ondoa hofu,” alisema huku akiinua mkono wake
taratibu na kunigusa kwenye shavu langu la upande wa kushoto, akawa ananivutia
pale alipokuwa amekaa.
Kwa tahadhari kubwa nikiogopa nisije nikamtonesha
majeraha yake, niliulanisha mwili wangu, akanivutia mpaka nilipomsogelea
kabisa, akanibusu kwenye shavu langu na kuninong’oneza.
“Ahsante sana kwa msaada wako, ni Mungu pekee ndiye
atakayekulipa, upo tofauti sana,” nilitabasamu na kumtazama, macho yetu
yakagongana, naye akaachia tabasamu hafifu.
Kwa kuwa sikuwa nimekula chochote, ilibidi nimuage
kwamba naenda kubahatisha kama nitapa chipsi kwenye banda lililokuwa mtaa wa
pili kutoka pale nilipokuwa naishi. Nilitoka huku Shenaiza akinisisitiza niwahi
kurudi pia nifunge mlango kwa nje ikiwa ni pamoja na kuzima taa zote. Sikujua
kwa sababu gani bado alikuwa na hofu kubwa kiasi hicho. Nilifanya kama alivyoniambia
na kutoka, nikafunga mlango kisha nikafunga na geti la chuma kwa nje na
kuondoka kuelekea mtaa wa pili.
Kwa bahati nzuri nilikuta bado hawajafunga,
nikaagiza chipsi sahani mbili na vipande vya kuku kwani nilitaka nikambembeleze
Shenaiza naye ale japo kidogo. Dakika kadhaa baadaye chakula changu kilikuwa
tayari, nikalipa na kuanza kuondoka huku nikijitahidi kutembea haraka kwani
nilipoteza muda mwingi pale kusubiria chakula.
Katika hali ambayo sikuitegemea, nilipotokeza kwenye
uchochoro wa kuelekea kwangu, kwa mbali niliwaona wanaume kama watatu hivi
wakiwa wamesimama mlangoni kwangu, mmoja akiwa anagonga mlango kwa nguvu.
“Mungu wangu, akina nani tena hao usiku wote huu?”
nilijiuliza huku nikirudi nyuma na kujibanza pale uchochoroni, nikawaona wale
wanaume wakiendelea kugonga mlango kwa nguvu. Ugongaji wao ulionesha dhahiri
kwamba hawakuwa wamekuja kwa heri, nikawa natetemeka nikiwa sijui nitafanya
nini.
Je,
nini kitafuatia? Usikose next issue.
Nifollow kwenye mitandao ya kijamii kwa:
Facebook: Hash Power
Instagram: Hashpower7113
Twitter: Hash- Power.
No comments:
Post a Comment