ILIPOISHIA:
Nikamuongoza baba mpaka kwenye kaburi la
Alfred ambalo juu yake kulikuwa na msalaba ulioandikwa jina lake kamili, tarehe
ya kuzaliwa na tarehe ya kufa kwake. Akaniambia niwe makini kwa kila
atakachokuwa anakifanya, nikatingisha kichwa huku hofu kubwa ikiwa imetanda
ndani ya moyo wangu kwani kiukweli nilikuwa nikiogopa sana makaburi na maiti.
SASA ENDELEA:
Baba alianza kufukuafukua ule upande wa
kichwani kwenye lile kaburim akaingiza mkono mfukoni na kutoa kichupa
kilichokuwa na ungaunga mweusi, akaumwaga kuanzia upande wa kichwani mpaka
miguuni, kisha akaniambia tuanze kulizunguka lile kaburi kwa kuanzia kushoto
kwenda kulia.
Alianza yeye, na mimi nikafuatia, tukawa
tunazunguka lakini kwa kutembea kinyumenyume, baada ya kuzunguka raundi sana,
nilianza kusikia kizunguzungu kikali, baba akaniambia nikae, yeye akarudi
kusimama palepale alipokuwa amesimama.
“Hebu muite jina lake mara tatu kwa sauti
kubwa,” alisema baba, nikawa simuelewi anamaanisha nini. Yaani mtu alishakufa
siku nyingi zilizopita halafu ananiambia nimuite jina lake, tangu lini maiti
ikaitika? Hata hivyo, ilibidi tu nitii kile alichoniambia, nikamuita.
Nililitaja jina lake kwa mara ya kwanza, baba
akawa ananionesha ishara kwamba niongeze sauti, nikamuita kwa mara ya pili
kisha kwa mara ya tatu. Cha ajabu kabisa, nilisikia akiitikia, tena niliweza
kuthibitisha kabisa kwamba ni yeye kwa sababu nilikuwa naijua sauti yake na
hata akizungumza neno moja tu, nakuwa nimeshamtambua.
Nilitetemeka kuliko kawaida, nikawa nageuka
huku na kule kwa sababu alivyoitikia, ilionesha kwamba hayupo pale kwenye
kaburi bali yupo umbali wa mita kadhaa pembeni. Nikiwa bado siamini, baba
alinionesha kwa kidole, akaniambia nitazame chini ya mti mkubwa wa mjohoro
uliokuwa pembeni kidogo ya makaburi.
Nilitazama lakini sikuona kitu, nikamgeukia
baba, akaniambia niendelee kutazama bila kupepesa macho. Katika hali ambayo
sikuitegemea, nilimuona Alfred akiwa amesimama chini ya mti, nywele zake zikiwa
zimekuwa ndefu na chafu sana, rangi ya ngozi yake ikiwa imebadilika na kuwa
utafikiri amejipaka unga wa mkaa usoni. Akiwa ni kama na yeye amegundua kwamba
nimemuona, Alfred aligeuka na kuanza kutimua mbio, muda mfupi baadaye
akapotelea kwenye msitu mkubwa uliokuwa pemebi ya makaburi hayo.
Nilibaki nimepigwa na butwaa, nikiwa siamini
kabisa nilichokiona, baba akanigeukia na kunitazama usoni.
“Unaona sasa? Mambo mengine usiwe unakuwa
mbishi tu,” alisema, nikawa bado nimepigwa na butwaa, nikihisi kama nipo kwenye
ndoto za kutisha ambazo sikuwa najua mwisho wake utakuwa nini.
Ilibidi baba anishike mkono na kuanza
kunivuta, akili zangu zikarudi sawa, nikawa bado nageukageuka kutazama kule
Alfred alikokuwa amepotelea. Nitakuja kueleza zaidi juu ya mazingira ya kifo
cha Alfrted ambapo sasa na mimi nilianza kuamini kwamba hakikuwa kifo cha
kawaida. Baba ni kama alikuwa amenifumbua macho.
Tulirudi mpaka nyumbani, tukakuta bado watu
wanazidi kuongezeka pale kwenye msiba wa Mwankuga.
Tulienda mpaka nyumbani lakini kwa kuwa bado
nilikuwa na maswali mengi kuhusu kifo cha mzee huyo, ilibidi nimtoroke tena
baba na kwenda pale msibani. Safari hii watu walikuwa tayariw ameshakaa pale
nje kwa kujipanga, kila mmoja akiwa na uso wa huzuni.
Kitendo cha mimi kuonekana tu eneo hilo,
nilishangaa watu wakiacha kila walichokuwa wanakifanya na kunikodolea macho.
Hata wale waliokuwa wanalia, wote walinyamaza, wakawa wananitazama. Sikuelewa
kwa sababu gani hali hiyo imetokea, hofu kubwa ikatanda ndani ya moyo wangu.
Kwa mbali nikaanza kusikia minong’ono huku
watu wakiendelea kunitazama. Mzee mmoja ambaye naye siku za nyuma nimewahi
kusikia kwamba ana tabia ya kuwaibia watu fedha kwa uchawi wa ‘chuma ulete’,
alisimama na kuongea kwa jazba.
“Baba yako alichokifanya ameona hakitoshi
ameamua kukutuma na wewe uje kuendeleza uchawi wenu hapa. Mwaka huu mtaisoma
namba, kamwambie anajikaanga kwa mafuta yake mwenyewe, mwisho wake umekaribia,”
alisema mzee huyo na kusababisha watu karibu wote pale msibani wamuunge mkono,
zogo kubwa likatokea huku wengine wakiinuka na kutaka kuja kunishushia kipigo.
Ni hapo ndipo nilipoelewa kwa nini watu
walikuwa wakinitazama kwa macho ya chinichini nilipofika msibani hapo. Kumbe
walikuwa wanahisi baba amenituma mwenda kufanya uchawi! Maskini, nilibaki
natetemeka kwa hofu kubwa kwa sababu sikuwa najua chochote kuhusu uchawi wala
kuroga.
Ili kuokoa maisha yangu, ilibidi nitimue mbio,
wakaendelea kunisindikiza kwa maneno makali wakimtuhumu baba na sisi familia
nzima kwamba tunahusika na mambo ya kishirikina na kwamba eti sisi ndiyo tumemuua
mzee Mwankuga kutokana na ugomvi wetu wa kugombea mpaka wa shamba.
Nilirudi nyumbani nikiwa natweta, mtu wa
kwanza kuniona alikuwa ni baba ambaye alikuwa amekaa nje ya nyumba yetu, kwenye
gogo kubwa la mti wa mvule akiandaa dawa zake, akashangaa kuniona naingia
mbiombio huku nikilia. Alinisimamisha lakini sikusimama kwa hofu kwamba wale
watu watakuwa wananifuatilia, nikapitiliza mpaka ndani na kwenda kujifungia
chumbani kwetu.
Nilijuta kwa kutosikiliza kile alichokuwa
ameniambia, nikawa natetemeka kwa hofu kubwa ndani ya moyo wangu. Niliendelea
kujifungia chumbani kutwa nzima, nikijiuliza maswali mengi yasiyo na majibu.
Kwa mujibu wa maelezo ya baba, kama Mwankuga
alikuwa amekufa, mwalimu Mwashambwa ambaye naye alikuwa naye kwenye lile tukio
la kule porini, naye angekufa, jambo ambalo kidogo lilikuwa gumu kwangu
kuliamini.
Kilichotokea siku hiyo, kuanzia kule porini
tulikokuwa tumeenda kuchimba dawa na baba, kifo cha Mwankuga, kilichotokea kule
makaburini na kelele za watu waliokuwa wakiituhumu familia yetu kuwa ya
kichawi, vilinifanya nianze kumtazama baba kwa jicho la tofauti.
Basi siku hiyo ilipita nikiwa na mawazo mengi
sana kuhusu yale matukio yaliyotokea, kila nilipokuwa nikifikiria, nilikosa
majibu. Gumzo kubwa liliendelea kutawala kijijini kwetu kuhusu uchawi wa baba,
kuna ambao walidiriki hadi kuja jirani na nyumba yetu na kuanza kutoa vitisho
kwamba dawa yetu inachemka.
Nilifedheheka sana moyoni mwangu. Siku tatu
baadaye, Mwankuga alizikwa kwenye makaburi ya kijiji huku msiba wake
ukitawaliwa na vituko vya kishirikina vya hapa na pale ambavyo bado watu wengi
waliendelea kuamini kwamba familia yetu inahusika.
Hatimaye Mwankuga alizikwa na kidogo zile
kelele tulizokuwa tunapigiwa zikaanza kupungua. Hata hivyo, siku ya kwenda
shule ilipofika (kipindi hicho bado nilikuwa nasoma Shule ya Msingi
Makongorosi, Chunya) nilikumbana na unyanyapaa mkubwa sana shuleni.
Wanafunzi wenzangu walikuwa wakinitenga na
kuniita mchawi, wakawa wanaituhumu familia yetu kwamba inahusika na vifo vya
watu wengi waliokuwa wanakufa katika mazingira ya kutatanisha pale kijijini
kwetu. Hata hivyo, kama baba alivyotufundisha wanafamilia wote, hatukutakiwa
kujibizana na mtu yeyote, nikawa nasikiliza tuhuma zote bila kujibu chochote.
Shauku yangu kubwa ilikuwa ni kutaka kumuona
mwalimu Mwashambwa kwa sababu kwa mujibu wa baba, na yeye alikuwa pamoja na
marehemu Mwankuga siku waliyokuwa wanapigana kichawi na baba kule porini.
Nilikuwa na shauku kubwa ya kumuona mwalimu huyo kwa sababu nilitaka kujifunza
kitu juu ya uchawi na wachawi.
Niliamini kwa kumtazama tu, naweza kugundua
kitu kilichokuwa kimejificha nyuma ya maisha yake. Hata hivyo, baadaye
ulipowadia muda wa kipindi cha hesabu, mwalimu wa darasa alikuja na kutuambia
kwamba mwalimu Mwashambwa alikuwa anaumwa sana hivyo asingeweza kuja shuleni
wala kuingia darasani mpaka atakapopona.
“Kumbe ni kweli!” nilijikuta nimeropoka kwa
sauti kubwa, kauli iliyosababisha wanafunzi wote pamoja na mwalimu wanigeukie
pale nilipokuwa nimekaa, nikasikia miguno ya chinichini ikitawala darasa zima.
“Ni kweli nini?” mwalimu wetu wa darasa, Madam
Timbuka alihoji huku akinifuata pale nilipokuwa nimekaa. Nilijisikia aibu kubwa
iliyochanganyikana na hofu, sikujua nimjibu nini mwalimu huyo kwani ndani ya
akili yangu, nilikuwa nimezipokea taarifa hizo za ugonjwa wa mwalimu Mwashambwa
na kile alichoniambia baba kwamba mwalimu huyo alikuwa mchawi na walikuwa
wakishirikiana na marehemu Mwankuga.
“Naongea na wewe Togolai, ni kweli nini?”
alihoji tena Madam Timbuka, safari hii akiwa amenikaribia kabisa pale
nilipokuwa nimekaa, nikaanza kubabaika huku hofu kubwa ikishindwa kujificha
kwenye uso wangu.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye
Championi Jumatatu.
No comments:
Post a Comment