“Nimepata salamu zako kwamba umechagua kuwa tajiri, ombi lako limekubaliwa lakini kuna masharti inatakiwa kabla siku zako saba hazijaisha, uwe umeshaanza kuyafuata, vinginevyo utakufa,” alisema yule mwanamke, macho yakanitoka pima.
SASA ENDELEA...
Nilijiweka vizuri pale chini nikiwa na shauku kubwa ya kutaka kusikia ataniambia nini, akanitazama machoni kisha akashusha pumzi ndefu na kunisogelea.
“Kwa nini umeamua kupita njia hii?” aliniuliza kwa sauti ya upole, nikashindwa kuelewa alikuwa anamaanisha nini.
“Unalingana na kijana wangu ambaye mwezi wa kumi na mbili angekuwa anatimiza miaka 21, makosa yangu yamesababisha niishi maisha ya kujuta kila siku, sitaki mtu mwingine apite njia kama niliyowahi kupita mimi na kusababisha nimpoteze mwanangu kipenzi,” alisema lakini wala maneno yake hayakuniingia akilini.
“Umeshawishiwa na mtu yeyote au ni maamuzi yako mwenyewe?”
“Nimeamua mwenyewe, wala hakuna aliyenishawishi.”
Kwa jinsi majibu yangu yalivyokuwa, yule mwanamke alishindwa kuendelea kunihoji maana nilishafikia uamuzi ndani ya moyo wangu na hakukuwa na jinsi yoyote ambayo ningebadilisha uamuzi huo.
“Unatakiwa kuwa makini sana na aina ya maisha utakayokuwa unaishi, hutakiwi kunywa pombe wala kuvuta sigara, hutakiwi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke yeyote mpaka utakapooa, hutakiwi kulala kitandani, utakuwa unalala chini na hutakiwi kula nyama nyekundu, mengine ni ya vitendo zaidi, nisubiri,” alisema mwanamke huyo na kutoka.
Nilibaki nayatafakari yale masharti aliyonipa, sikuona jambo lolote la kunizuia kwa sababu kama ishu ya ulevi, sikuwa nakunywa pombe wala kuvuta sigara, achilia mbali bangi ingawa katika makuzi ya ujana, kuna wakati nimewahi kujaribu na kuishia kudhalilika.
Suala la uhusiano wa kimapenzi, nilichokuwa nimekiamua kutoka ndani ya moyo wangu, ni kwamba kama Rahma akikubaliana na mimi, nitamuoa awe mke wangu wa ndoa maana alikuwa na kila kitu nilichokuwa nakihitaji, achilia mbali tofauti yetu ya umri. Suala la kutolala kitandani, nalo pia halikuwa tatizo kwangu kwa sbaabu maisha yetu ya kule kijijini, tulishazoea kulala kwenye vitanda vya kamba au kulala chini kwenye mkeka kwa hiyo hilo pia halikuwa tatizo kwangu.
Suala la kula nyama nalo sikuona kama ni shida kwa sababu maisha ya kule kijijini kwetu, nyama tulikuwa tunakula siku za sikukuu au mara chache tunapoenda kuwinda, mboga yetu kubwa ilikuwa ni samaki.
Kimsingi masharti hayo aliyonipa, yalinifanya ile hofu yote niliyokuwa nayo kuhusu kumiliki utajiri, iyeyuke kama theluji iyeyukavyo juani, hamu ya kutamani kuwa na utajiri mkubwa, ikazidi kunijaa.
Moyoni nilijiambia kama masharti yenyewe ndiyo hayo, kwa nini wachawi wanaogopa kuwa matajiri? Wanachokiogopa ni nini hasa? Akilini nilianza kuvuta picha ya jinsi nitakavyokuwa ‘tajiri mtoto’, nikiendesha magari ya kifahari na kuishi kwenye majumba ya gharama kubwa.
Hata ule ushauri alionipa Mkuu pamoja na baba yake Rahma, kwamba kama nataka mambo yasiwe magumu kwangu, nisitamani kuwa na utajiri mkubwa, bali fedha za kawaida tu za kuniwezesha kuishi bila shida, niliutupilia mbali, tabasamu pana likachanua kwenye uso wangu.
Dakika kadhaa baadaye, yule mwanamke alirejea, nikashtuka kumuona akiwa na kisicho cha kawaida. Shingoni alikuwa amebeba nyoka mdogo aliyejiviringisha huku kichwa chake akiwa amekielekezea mbele, akamshika na kumshusha chini, akajiviringisha na kuinua kidogo kichwa chake.
Nilishtuka sana, kama nilivyowahi kueleza, pamoja na ujanja wangu wote, hakuna kitu nilichokuwa naogopa kama nyoka.
“Unashtuka nini? Huyu itabidi umzoee tu,” alisema yule mwanamke, nikawa nimekaa kwa tahadhari kubwa, nikimtazama kwamba akinisogelea tu nikimbie kuelekea nje. Cha ajabu, nilipomchunguza vizuri yule nyoka, alikuwa na madoadoa sawasawa na ya yule nyoka ambaye Mkuu alinichanja na kumlambisha damu yangu.
“Itabidi umtunze na kumheshimu kwa moyo wako wote, huyu ndiye atakayeamua hatima ya utajiri unaoutaka, kadiri anavyozidi kuwa mkubwa ndivyo unayoyataka yatakavyokuwa yanatimia,” alisema mwanamke huyo, bado nikawa najiuliza maswali mengi yasiyo na majibu.
“Unamshangaa kwani ndiyo mara yako ya kwanza kumuona? Hebu vua shati huko,” alisema mwanamke yule, ni hapo ndipo nilipoamini kwamba ni kweli nyoka yule ndiyo yuleyule aliyelambishwa damu yangu na Mkuu.
Nilivua shati, yule mwanamke anachukua wembe na kusogelea, akanichanja kwenye mbavu upande wa kushoto, damu zikaanza kunitoka kwa sababu alivyonichanja alikandamiza mkono, akamchukua yule nyoka ambaye sasa alikuwa akitoa ulimi wake na kuchezesha.
Akamsogeza mpaka pale kwenye jeraha langu, hofu niliyokuwa nayo ilikuwa haielezeki. Simulizi kuhusu nyoka nilizowahi kuzisikia, achilia mbali matukio niliyowahi kushuhudia jinsi watu na mifugo inavyopoteza maisha baada ya kung’atwa na nyoka, vilinifanya niwe mwoga sana kwa viumbe hawa.
Alipomsogeza tu kwenye jeraha, alijikunjua na kunigusa kwa ulimi wake, akaanza kuilamba ile damu kwa kasi kubwa. Muda mfupi tu baadaye, jeraha lilibaki kuwa alama tu, damu zote alizilamba nyoka yule na wala nyingine hazikuendelea kunitoka.
“Utamzoea tu wala usijali, si umeamua mwenyewe?” alisema yule mwanamke huku akitingisha kichupa chenye dawa ya majimaji, akanipaka pale kwenye jeraha kisha akamchukua yule nyoka, safari hii alimuingiza kwenye mfuko uliotengenezwa kwa kipande cha gunia, akatoka na kuniacha nikiwaza sana.
Nimewahi kusikia simulizi za watu waliokuwa wakifuga nyoka wakubwa ndani ya nyumba zao kwa ajili ya imani za kishirikina, sikutaka kuamini kwamba na mimi ndiyo naelekea kwenye maisha hayo, nikaanza kuelewa hatari iliyokuwa mbele yangu.
Hata hivyo, bado shauku ya kuwa tajiri haikuniisha, nilijipa moyo kwamba kama wapo watu ambao wanaweza, kwa nini mimi nishindwe? Muda mfupi baadaye, yule mwanamke alirejea na kuendelea kunielekeza mambo mbalimbali, yaani alivyokuwa akiongea na mimi ni kama tayari nimeshakuwa tajiri maana alikuwa akinipa masharti ya namna ya kutumia fedha.
Aliniambia hata niwe na fedha nyingi kiasi gani, sitakiwi kutoa kumpa mtu yeyote fedha siku za Jumatatu, Jumanne na Jumapili, akaniambia hata kama kuna mtu amepatwa na dharura kubwa na kiwango kidogo tu cha fedha kinaweza kumsaidia, sitakiwi kabisa kutoa hata shilingi kumi kwenye siku hizo alizonitajia.
Akaniambia pia kwamba katika siku hizo nilizokuwa na uwezo wa kutoa fedha, muda wa kutoa fedha kumpa mtu yeyote au kufanya kitu chochotye kinachohusiana na fedha, ni saa kumi na mbili jioni, kabla jua halijazama. Maelezo hayo yalinishangaza sana, nikawa najiuliza maswali mengi kichwani yaliyokosa majibu.
Baadaye, aliniambia kwamba natakiwa kurudi tena nyumbani kwake hapo baada ya siku sita kwa ajili ya kwenda kukamilisha baadhi ya mambo. Alinipa mkono na kunitakia maisha mema ya utajiri, mimi bado macho yangu yakawa kwenye ule mfuko aliomuweka yule nyoka mdogo.
Baadaye baba na baba yake Rahma walikuja kunichukua, wakamshukuru mwanamke huyo, tukatoka na safari ya kurejea nyumbani ikaanza. Tayari ilishagonga saa nane za usiku, tukawa tunatembea kwa miguu kuelekea kwenye barabara kubwa ya lami.
Kutoka nyumbani kwa mwanamke huyo mpaka kwenye barabara ya lami, kulikuwa na umbali mrefu sana na kibaya zaidi, ni kwamba tulikuwa tunapita kwenye pori kubwa ambalo kwa usiku ule lilikuwa likitisha sana.
Tukiwa tunaendelea kuchanja mbuga, baba akiwa mbele na baba yake Rahma akiwa nyuma, mara tulianza kusikia sauti za ajabu kutoka ndani ya pori lile, huku kukiwa na purukushani kubwa, mapigo ya moyo wangu yalilipuka na kuanza kunienda mbio kuliko kawaida.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment