Monday, February 5, 2018

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 62



ILIPOISHIA:
“Ndiyo, lakini mambo yenyewe ndiyo kama hivi, hatupati hata dakika chache za kuwa pamoja, mi nimechoka bwana,” alisema Shamila na kunisogelea mwilini, nikawa naiona hatari iliyokuwa mbele yetu endapo Junaitha atageuka na kugundua kwamba tulibaki koridoni tumesimama, tena tukiwa tumesogeleana mithili ya majogoo yanayotaka kupigana.
 SASA ENDELEA...
“Please Shamila, huu siyo muda muafaka, kama inawezekana tutafute muda baadaye,” nilisema kwa sauti ya chini, akashusha pumzi ndefu na kunitazama usoni kwa macho yake mazuri, tukaendelea kutembea lakini alionesha kweli amemaanisha kile alichokisema.
Tuliingia kwenye kile chumba ambacho tulikuwa tukikutania kila panapokuwa na shughuli maalum, Junaitha akatuelekeza kukaa kwa duara kama ilivyokuwa kawaida yetu kisha akatuambia wote tuanze kuvuta hewa kwa wingi kwa kutumia pua na kuitoa kwa kutumia mdomo.
“Inatakiwa wote tufumbe macho na tuendelee kupumua taratibu, vuta pumzi ndefu kwa kutumia tumbo na sio kifua, unajua kuna watu wengi wanaishi lakini hawajui hata namna ya kupumua, badala yake wao wanahema,” alisema Junaitha na kuanza kutufafanulia kile alichokisema.

Alisema kwa kawaida, unapovuta pumzi inatakiwa hewa iende kujaa kwenye mapafu, ambayo kimsingi yanapatikana chini ya mfupa wa chini wa kifua kwa ndani au kwa Kiingereza diaphragm.
“Unapovuta hewa kwa kutumia kifua, maana yake haifiki kwenye mapafu kama inavyotakiwa na unapoitoa, inakuwa imeishia njiani na kama mjuavyo pumzi ndiyo uhai wenyewe kwa hiyo mtu ambaye hapumui vizuri hawezi kuwa na afya nzuri ya mwili au akili.
“Nataka na nyie mjifunze kuanzia leo, unapopumua tumia tumbo, unapovuta hewa hakikisha tumbo limejaa na unapotoa hakikisha linabaki tupu, hapo ndiyo utakuwa na uhakika kwamba pumzi zimefika sehemu husika na hewa imefika kwenye mapafu,” alisema Junaitha, elimu ambayo awali sikuwa naifahamu.
“Unapotulia kwenye hali hii kwa muda, huku ukiizuia akili yako kufikiria kitu kingine chochote zaidi ya pumzi unazovuta na kutoa, utapata utulivu mkubwa mno wa akili na mwili na hiki ndicho wengine wanachokiita tahajudi au meditation, sasa kabla sijaruhusu maswali nataka wote tufanye kwa dakika kadhaa, nataka wote tufumbe macho na tutaendelea kupumua kwa utulivu mpaka nitakapowapa ishara,” alisema Junaitha, wote tukatii alichotuambia.
Kiukweli kwa upande wangu, nilipoanza kutuliza akili tu, nilijisikia hali ambayo haijawahi kutokea maishani mwangu. Akili yangu ilitulia, mwili nao ukatulia, nikawa najihisi kama nipo kwenye ulimwengu mwingine wa tofauti kabisa. Niliendelea kuifurahia hali hiyo, nikajikuta nikisahau kila kitu, ikafika kipindi nikawa hata sijui pale nipo wapi na nafanya nini, nikawa najisikia raha tu.
Ni mpaka Junaitha alipopiga makofi na kutuambia kwamba inatosha ndipo akili zangu ziliporudi mahali pake, nikagundua kumbe nilikuwa nimekaa juu ya zulia, nikawa najishangaa sana.
“Enhee! Mmejisikiaje?” aliuliza Junaitha, mimi ndiyo nikawa wa kwanza kumjibu kwamba nimejisikia vizuri sana, wenzangu wote nao walijibu hivyohivyo, tukamshukuru Junaitha kwa kutufundisha kitu kizuri namna ile.
“Kwa hiyo mmeanza kuona kwamba kumbe kila mmoja wetu ana nguvu fulani ndani ya mwili wake ingawa wengi hawajui namna ya kuzitumia na ukionesha kujua kidogo ndiyo kila mtu anakuona wewe ni mchawi, hata nyie si mnaamini mimi ni mchawi sana si ndiyo?” alisema Junaitha, akaanza kututolea ufafanuzi kama ule alionipa awali.
Akatuambia kwamba baba yake mzazi alikuwa na nguvu za giza na ndiye aliyemrithisha lakini wakati anarithishwa, tayari na yeye alikuwa ameshaanza mafunzo ya elimu ya utambuzi, ambayo yalimfanya awe na uwezo mkubwa wa kutumia nguvu zisizoonekana.
Kwa jinsi alivyokuwa anajua kujieleza, tulijikuta wote tukiishiwa maswali, Shenaiza yeye akataka kujua kuhusu hali yake aliyokuwa nayo na nini kilichotokea mpaka alipojikuta pale ndani.
Kwa kuwa Junaitha alikuwa ametoa mwenyewe ruhusa ya kuulizwa maswali, alimfafanulia kila kitu, akamueleza mpaka jinsi tulivyoenda kumtorosha Shamila hospitalini baada ya kuwa anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kunitorosha mimi na Shenaiza hospitalini, kwa kushirikiana na Raya na Firyaal.
Mazungumzo yalikuwa marefu lakini mwisho wa yote, Junaitha alituhakikishia kwamba kesho yake ndiyo ingekuwa mwisho wa baba yao akina Shenaiza na shirika lake la kishetani la Black Heart.
“Leo mnajiona kama watu wadogo lakini nawahakikishieni kesho kila mtu atawaona mashujaa kwa kuibua sakata hili,” alisema Junaitha na kutusisitiza kwamba inatakiwa tupambane pamoja maana mzee huyo alikuwa na nguvu kubwa ambazo angeweza kuzitumia kutushinda.
“Kinachonifanya niamini kwamba tutamzidi nguvu ni kwa sababu kwanza mchawi wake yupo mikononi mwetu tunamshikilia na huyo ndiyo alikuwa akimpa jeuri kwa kipindi chote kwa hiyo sasa hivi atabaki kuwa na nguvu za nje tu lakini nguvu za giza hakuna kitu,” alisema Junaitha.
Suala la kuwa na mwandishi wa habari mmoja pamoja na mwanasheria tayari lilishatimia kwa sababu nilimuunganisha na mwandishi mahiri wa habari za uchunguzi, Richard Bukos na kwa kuwa yeye alikuwa akifahamiana na mwanasheria, basi kazi haikuwa ngumu.
Baada ya hapo, alituruhusu kila mmoja akapumzike kwa ajili ya kujiandaa kwa shughuli ya kesho, huku akinitaka mimi nibaki mle ndani ya kile chumba kwanza. Nilimuona Shamila ni kama hajaifurahia kauli hiyo kwa sababu tayari alishanionesha kwamba ananihitaji, nikamkonyeza kama ishara ya kumwambia asiwe na wasiwasi, tutapata tu muda wa kuwa pamoja.
“Unajua kazi kubwa tumeshaikamilisha kwa hiyo huu ni muda mzuri wa mimi na wewe kupumzika, natangulia chumbani kwangu nakuomba uje lakini hakikisha hakuna anayekuona ukiingia,” alisema Junaitha, nikatingisha kichwa kumkubalia. Nilikubali tu japokuwa nilikuwa najua anachokihitaji na japokuwa haikuwa sahihi kufanya vile, nilijikuta tu na mimi nikipenda kuwa karibu naye kwani niliamini nitajifunza mambo mengi zaidi nikiwa naye.
Nilisimama na kuelekea kwenye chumba changu, nikawapita Firyaal na Shenaiza ambao wao walikuwa kwenye chumba kimoja, nikawasikia wakizungumza kwa furaha ndani ya chumba chao, wakinitaja jina langu.
Nilipita pia kwenye chumba alichokuwemo Raya, yeye alikuwa kimya kabisa, nikapita kwenye mlango wa chumba cha Shamila kwa sababu cha kwangu kilikuwa mwishomwisho, nikashangaa kumuona Shamila amesimama mlangoni.
Aliponiona tu, alinivamia, akanivutia ndani ya chumba chake na kufunga mlango kwa ndani, akanikumbatia huku akipumua kama mtu aliyetoka kukimbia mbio za marathon.
“Nakupenda sana Jamal, njoo uutibu moyo wangu,” alisema huku akinimwagia mvua ya mabusu. Kwa hali aliyokuwa nayo, hakukuwa na njia ambayo ningeweza kumkwepa tena, hasa ukizingatia kwamba hata mimi nilikuwa nampenda kutokana na jinsi alivyonisaidia, kuanzia kule hospitalini mpaka muda huo na pia kutokana na jinsi alivyokuwa mzuri.
Sikujivunga, na mimi nilimuonesha ushirikiano wa nguvu, muda mfupi baadaye tukagusanisha ndimi na kuanza kuelewa kwenye ulimwengu wa tofauti kabisa. Shamila alionesha kuwa na papara mno, muda mfupi baadaye akawa tayari yupo kama alivyoletwa duniani, akahamia upande wangu na kuanza kufanya kama alivyofanya kwake.
Muda mfupi baadaye, wote tulikuwa ‘saresare maua’, akanisukuma kwa nguvu kwenye uwanja wa fundi seremala, nikaangukia mgongo, akaja juu yangu kwa kasi, maandalizi ya mechi ya kirafiki isiyo na jezi wala refa yakaendelea huku akionesha kunikamia kama Simba na Yanga zinavyokamiana zinapokutana uwanjani.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

3 comments:

  1. Vipi kitabu Kip???? Au itaendelea lini

    ReplyDelete
  2. Tunaomba usituweke mda mwing kusubir muendelezo mana yakaribia miez 3 sas huwa tunajipa moyo itatokakesho Kesho hatimae leo

    ReplyDelete

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...