ILIPOISHIA:
Tukiwa
tunaendelea kuchanja mbuga, baba akiwa mbele na baba yake Rahma akiwa nyuma,
mara tulianza kusikia sauti za ajabu kutoka ndani ya pori lile, huku kukiwa na
purukushani kubwa, mapigo ya moyo wangu yalilipuka na kuanza kunienda mbio
kuliko kawaida.
SASA
ENDELEA...
“Nakufaaa! Naku...fa...aa,” sauti ya
mwanamke ilisikika, aliporudia mara ya pili kuimba msaada, sauti yake ilikuwa
ikikwamakwama na muda mfupi baadaye akaanza kukoroma kuonesha kwamba mtu au
watu waliokuwa wakitaka kumdhuru tayari walishafanikisha lengo lao.
Tofauti na hali niliyokuwa nayo mimi,
baba na baba yake Rahma hawakuonesha kushtuka chochote, yaani ilikuwa ni kama
hakuna kilichotokea na wala hakuna aliyeshughulika kwa chochote.
Muda mfupi baadaye, harufu ya damu
mbichi ilitawala eneo lote lile, milio ya bundi na midege mingine ya ajabu
ikazidi kuifanya hali iwe ya kutisha mno. Baba aliendelea kupiga hatua
ndefundefu, hukumoyo wangu ukiwa umepondwapondwa kwa hofu na mshtuko, na mimi
nikawa naongeza mwendo, miguu yangu ikitetemeka kuliko kawaida.
“Unaogopa nini? Hili linaitwa pori la
kafara, huku ndiyo watu wanakokuja kutolea makafara ili mambo yao yafanikiwe,”
alisema baba yake Rahma huku tukiendelea kusonga mbele, sikumjibu chochote
maana bado nilikuwa natetemeka sana.
Jambo ambalo mpaka leo huwa silipatii
majibu, ni kwa nini watu wenye imani za giza hawaoni hatari kabisa kuyakatisha
maisha ya mtu mwingine? Ni kweli kwamba sote tutakufa na kifo hakiepukiki
lakini kwa nini uyakatishe maisha ya mtu mwingine kwa sababu zako binafsi?
Japokuwa na mimi nimefanya sana huo
mchezo, natamani kama utokee muujiza nguvu zote za giza zipotee. Ukweli ambao
watu wengi hawaujui, katika vifo vinavyotokea kila siku, iwe ni kwa ajali,
magonjwa, watu kujinyonga au kuuana, nguvu za giza zinahusika kwa asilimia
kubwa sana.
Kuna matukio mengine unaweza kuona kama
ni kifo cha kawaida tu lakini mtu mwenye uwezo wa kuona mambo kwa jicho la
tatu, anakuwa anaelewa mchezo mzima ulivyotokea. Si kila kifo kinachotokea kipo
kama unavyoweza kudhani, humu duniani kuna mambo mengi sana yaliyojificha na
kuna watu wanawaonea sana wenzao na kundi kubwa linaloonewa sana, ni wale watu
wasio na imani thabiti ndani ya mioyo yao.
Basi tulifika mpaka barabarani, kwa kuwa
muda ulikuwa umeenda sana, hakukuwa na magari yoyote yaliyokuwa yakipita,
barabara ilikuwa kimya kabisa. Nilitegemea baba atasema tutafute sehemu ya
kuondokea kama kawaida yetu maana nilikuwa nimchoka sana lakini safari hii
alizungumza kitu cha tofauti.
Alisemakwa sababu tulikuwa tumebeba kitu
cha muhimu sana, ilikuwa ni lazima tufike nyumbani kwa njia za kawaida.
Aliposema tumebeba kitu muhimu sikumuelewa kwa sababu kiukweli hakuna hata
mmoja kati yetu aliyekuwa na mzigo wowote. Tulianza kutembea pembezoni mwa
barabara ileile ya lami tuliyojia, huku wote tukiwa kimya kabisa. Utaratibu
wetu ulikuwa uleule, baba mbele, mimi katikati na baba Rahma nyuma.
Kwa bahati nzuri, tulipofika mbele
kidogo, kuna Fuso lilikuwa likitokea upande wa mashambani, likiwa na shehena ya
mananasi, kama ujuavyo tena Bagamoyo kunalimwa sana matunda.
Harakaharaka baba alimpungia mkono dereva,
akasimamisha gari kabla hajaingia kwenye barabara ya lami, akamfuata na
kuzungumza naye ambapo sekunde chache baadaye, baba alitupa ishara kwamba
tupande.
Nadhani walishakubaliana, ikawa ahueni
maana nilikuwa nikiiwazia sana ile safari. Gari lilikuwa limejaza mananasi
mpaka juu kabisa, ikabidi tupande na kukaa juu ya mabomba na kujishikilia
vizuri, dereva akaliingiza gari kwenye barabara ya lami na safari ikaendelea.
Japokuwa kule juu kulikuw ana upepo
mkali unaochoma mpaka ndani ya kifua, ilibidi tuvumilie maana ilikuwa bora
kuliko kutembea kwa miguu. Baada ya kama dakika hamsini hivi, tuliwasili jijini
Dar, tukateremka kwenye kituo cha Mwenge, tukamshukuru sana yule dereva, yeye
akaendelea na safari yake na sisi tukaanza kutembea kuelekea nyumbani.
Kitu kingine ambacho nilijifunza lakini
nisingependa kukizungumzia sana leo, maduka mengi, hasa yale makubwa, yanakuwa
na ulinzi wa nguvu za giza hasa nyakati za usiku ambapo kama una uwezo wa kuona
mambo yaliyojificha, unaweza kustaajabu sana.
Hii dunia ina mambo mengi sana
yaliyojificha, kama nioivyosema, sitaki kuelezea sana kuhusu hili. Basi
tuliendelea na safari yetu mpaka tulipofika nyumbani, tayari ilishagonga saa
tisa na nusu.
“Unatakiwa kuwa mtulivu na msiri, hakuna
kitu cha ajabu tena kwako, umenielewa,” baba aliniambia kwa kauli ya msisitizo
wakati tukiagana kwa ajili ya kila mmoja kwenda kulala lakini sikumuelewa
anamaanisha nini.
“Kuanzia leo utakuwa unalala peke yako,
chumba chako kinatakiwa kuwa kimefungwa muda wote na usiruhusu watu kuingiaingia,
hata awe nani, umenielewa?” alisema baba, baba yake Rahma akawa anatingisha
kichwa kuonesha kwamba anaunga mkono kile alichokisema baba.
Bado sikuwa naelewa kwa nini wananiambia
vile, baba akahitimisha kwa kuniambia kwamba eti hategemei kunisikia nikifanya
jambo lolote la ajabu. Tuliagana, nikaingia chumbani kwangu, kweli yule ndugu
yangu niliyekuwa nalala naye siku mojamoja hakuwepo, kwa hiyo nilikuwa peke
yangu.
Kwa jinsi nilivyokuwa nimechoka,
sikutaka hata kufanya kitu kitu chochote, nikavua nguo zote, nikazima taa na
kujilaza kitandani. Mwili wangu ulikuwa na maumivu sehemu mbalimbali, lakini
pale yule mwanamke aliponichanja usiku huo palikuwa na maumivu makali zaidi.
Nikiwa bado natafakari mambo chungu
nzima yaliyotokea kwa siku nzima, nilisikia kitu kilichonishtua sana. Chini ya
kitanda changu kulikuwa kama na purukushani fulani hivi kwa mbali, ikabidi
harakaharaka niinuke na kwenda kuwasha taa.
Nikainama chini kwa tahadhari kubwa na
kuchungulia uvunguni, katika hali ambayo sikuitegemea kabisa, nilikiona kile
kimfuko kilichotengenezwa kwa kipande cha gunia, nilichokionakule kwa yule
mtaalamu kikiwa chini ya kitanda changu.
Ni kimfuko hichohicho ndicho yule
mtaalamu tuliyetoka kwake usiku huo, alichomuweka yule nyoka mdogo baada ya
kumlambisha damu yangu. Kilichonishtua zaidi, kimfuko kilikuwa tupu, kwa akili
za harakaharaka nikahisi kwamba lazima zile purukushani nilizokuwa nazisikia,
zilikuwa ni za yule nyoka akihangaika kutoka.
Sasa kimfuko kimefikaje chumbani kwangu?
Na kama kile nilichokuwa nakihisi ni kweli, yule nyoka alikuwa mle ndani,
ningelalaje? Nilijikuta usingizi wote ukiniisha, harakaharaka nikapanda juu ya
kitanda na kukaa kwenye uchago wa kitanda ili hata akipanda kitandani, asiweze
kunifikia.
Ni hapo ndipo nilipoanza kuelewa kauli za
baba zilikuwa na maana gani, kuanzia ile ya kule njiani kwamba ‘tumebeba kitu
muhimu sana’, mpaka yale maneno aliyoyazungumza muda mfupi uliopita kabla kila
mmoja hajaenda kulala.
Nilijiapiza kwamba sitalala mpaka
kupambazuke, na ukizingatia tayari muda ulishaenda sana, niliona isiwe tabu.
Lakini waliosema usingizi ndugu yake kifo hawakukosea, hata sijui nini
kilitokea, nilipokuja kushtuka baadaye, nilijikuta nimelala kitandani na kibaya
zaidi, hata taa ilikuwa imezimwa.
Mshtuko nilioupata ulikuwa hauelezeki,
nikafumbua macho na kuyakodoa kama nitaona chochote lakini nilijitahidi
nisitingishike hata sehemu moja kwenye mwili wangu. Nikiwa nimejikausha kama
gogo, nilihisi hali fulani kwenye ile sehemu yule mwanamke aliponichanja usiku
huo.
Nilihisi kama kuna kitu kinanilamba
hivi, nikaanza kutetemeka huku nikiendelea kujikausha nisisababishe mtikisiko
wa aina yoyote, nilipozidi kuvuta utulivu, nikahisi kuna kitu cha baridi
kinatingishikatingisha upande ule niliokuwa nalambwa, mapigo ya moyo yakawa
yanadunda kama nimetoka kukimbia mbio za mita mia moja.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment