ILIPOISHIA:
Nilihisi kama kuna kitu kinanilamba
hivi, nikaanza kutetemeka huku nikiendelea kujikausha nisisababishe mtikisiko
wa aina yoyote, nilipozidi kuvuta utulivu, nikahisi kuna kitu cha baridi
kinatingishikatingisha upande ule niliokuwa nalambwa, mapigo ya moyo yakawa
yanadunda kama nimetoka kukimbia mbio za mita mia moja.
SASA ENDELEA...
Nilitulia tuli huku nikiendelea
kutetemeka, mara nikaanza kuhisi kile kitu kikitambaa na kunivuka mwili, kutoka
upande mmoja kuelekea upande mwingine. Japokuwa kulikuwa na giza niliweza
kukitambua vizuri kiumbe hicho kuwa alikuwa ni nyoka. Hata sijui ushujaa wa
kutulia vile niliupata wapi maana kama nilivyowahi kusema, hakuna kitu
nilichokuwa nakiogopa maishani mwangu kama nyoka.
Basi yule nyoka mdogo alinitambuka na
kupotelea upande wa pili wa kitanda, nikashusha pumzi ndefu kisha kwa tahadhari
kubwa nikainuka pale nilipokuwa nimelala, nikasimama kwenye uchago wa kitanda
na kujivuta mpaka kwenye swichi ya taa, nikaiwasha.
Japokuwa kulikuwa na baridi kali ya
usiku, mwili wote ulikuwa umelowa jasho, nikajitazama kwenye lile jeraha langu
ubavuni, nikashtuka kugundua kwamba lilikuwa limeanza kujichimba na kutengeneza
kidonda. Kumbe wakati yule nyoka akinilamba, alikuwa akitoa ganda la juu ambalo
lilikuwa likiashiria kuanza kupona, nikashtuka mno huku nikiwa sielewi nini
hatma yangu.
Cha ajabu ni kwamba safari hii sikuwa
nasikia maumivu kabisa. Nikageuka na kutazama pale kitandani, hapakuwa na kitu
zaidi ya shuka, nikalivuta na kujaribu kujikung’uta nikihofia kwamba yule nyoka
anaweza kuwa bado yupo lakini hakukuwa na chochote.
Nikashuka na kuchungulia chini ya
kitanda, pale palipokuwa na ule mfuko uliotengenezwa kwa kipande cha gunia. Cha
ajabu, ulikuwa umefungwa vilevile, nikashusha pumzi ndefu na kurudi kitandani.
Kama ingekuwa amri yangu, siku hiyo
nisingelala kabisa lakini usingizi ulikuwa ukinitesa sana. Nilichoamua, ilikuwa
ni kufungua mlango na kuuegesha ili kama hali ikitokea tena, nitoke mbio mpaka
nje. Sikuzima tena taa kama mwanzo, nikataka kuona nini kitatokea tena.
Nilipojiegesha kitandani tu, usingizi
mzito ulinipitia, nilipokuja kuzinduka, tayari kulishakuwa kumepambazuka
kabisa, harakaharaka nikashuka kitandani na kuchungulia kule chini ya kitanda.
Cha ajabu ni kwamba ule mfuko haukuwepo,
niliangaza kila kona lakini sikuuona, nikahisi labda yule nyoka alitambaa nao
na kujifuicha kwenye nguo zilizokuwa chini, nikapekua kila sehemu lakini
sikuona dalili zozote.
“Unatafuta nini?” sauti ya baba
ilinizindua kutoka kwenye lindi la mawazo, nikashusha pumzi ndefu na kumtazama
usoni, naye akawa ananitazama.
“Kuna kitu kimenitokea usiku
sijakielewa.”
“Kitu gani?” baba aliniuliza kwa mkato,
ikabidi niinue shati na kumuonesha pale ubavuni palipokuwa na kidonda, nikaanza
kumueleza jinsi nilivyoshtuka na kukutana na mauzauza ya yule nyoka chumbani
kwangu na jinsi alivyokuwa akinilamba pale kwenye kidonda.
Tofauti na nilivyotegemea, baba alicheka
kwa dharau, akaniambia kama naipenda pepo kwa nini naogopa kufa? Sikumuelewa
anamaanisha nini, ikabidi nimhoji, akanijibu kwa mafumbo na kutoka zake,
akaniacha nikiwa na mawazo tele kichwani mwangu.
Baadaye nilitoka na kwenda kuoga,
nikarudi na kujiandaa kisha nikatoka na kwenda kibarazani ambako baba yake
Rahma alikuwa amekaa akisoma kitabu. Nilipomsalimia, aliacha kila alichokuwa
anakifanya na kuitikia salamu yangu kwa uchangamfu.
Kwa jinsi alivyonipokea, nilipata nguvu
ya kumuuliza kwa kina kuhusu mambo mbalimbali ambayo nilikuwa siyaelewi,
akaniambia jambo ambalo lilinishtua sana. Aliniambia kwamba usiku wakati
tukirejea nyumbani kutoka Bagamoyo, kuna sehemu tulipita na kusikia mwanamke
akipiga kelele za kuomba msaada.
Akaniambia kwenye msitu ule ndipo mahali
watu waliochagua njia kama yangu, ya kuwa na utajiri wa kichawi, wanapoenda
kutolea makafara yao, akaniambia hata mimi mambo yakichanganya nitakuwa naenda
kutoa kafara kwenye msitu huo. Nilishtuka sana kutokana na maneno aliyoniambia,
nikawa nahisi kama nipo ndotoni.
“Ukiwa mwanachama wa kawaida, unatoa
kafara za kawaida, kama ambazo tayari wewe umeshazitoa, si unakumbuka umeshatoa
mara ngapi?” aliniuliza baba yake Rahma huku akigeuka huku na kule kuhakikisha
hakuna anayetusikiliza.
“Mara mbili!” Nilimjibu. Kiukweli mpaka
wakati huo tayari nilikuwa nimesababisha matukio yaliyoondoa nafsi za watu
wasio na hatia wawili, la kwanza lilikuwa ni lile la ajali iliyoyakatisha
maisha ya yule mtoto wa Mlandizi na ya pili ikiwa ni ile ya bodaboda aliyepata
ajali mbaya baada ya kugongana na mimi, mita chache kutoka pale kwenye msiba wa
yule mtoto.
Jaribio lingine la kumtoa kafara Sadoki,
rafiki yangu kipenzi wa Chunya lilikuwa limegonga mwamba huku ikibakia kidogo
nidhalilike kutokana na nguvu ya upako aliyokuwa nayo Sadoki na mama yake.
“Sasa ka njia uliyochagua, utatakiwa
kuwa unatoa sadaka za damu mara nyingi kadiri iwezekanavyo, ndiyo maana kuanzia
mwanzo nilikwambia kwamba utajiri huo ni mgumu sana, bora ubaki maskini,”
alisema baba yake Rahma.
Japokuwa kweli niliogopa kwa kiasi
fulani, lakini tamaa ya utajiri ilishawaka ndani ya moyo wangu kiasi kwamba
sikuwa nataka kusikia jambo lingine lolote la kunirudisha nyuma. Nilimkatisha
kijanja na kumuuliza kuhusu kile kilichotokea usiku kuhusu yule nyoka.
Alinifafanulia kwamba ni kawaida ya mtu
yeyote anayemiliki au anayetaka kumiliki utajiri kwa nguvu za giza, kufuga
mnyama huyo na kuongeza kwamba chakula chake kikubwa, ukiachana na vyakula vya
kawaida ambavyo nyoka hupewa, ni lazima kila siku awe anakunywa damu yangu.
“Mungu wangu!” nilishtuka sana na
kujikuta nimelitaja jina la Mungu. Kwa maneno hayo ya baba yake Rahma, ni
kwamba kile kilichotokea usiku haukuwa muujiza na kwamba ni jambo ambalo
litakuwa linatokea kila siku kwa kipindi chote cha maisha yangu, nilijikuta
nikichoka.
“Kadiri utakavyokuwa unamtunza vizuri na
kumpa mahitaji yake yote, ndivyo atakavyokuwa anaongezeka ukubwa na kadiri atakavyokuwa
anaongezeka ndivyo utajiri wako utakavyokuwa unaongezeka kwa hiyo ukiwa
mvumilivu, unaweza kufika mbali,” alisema baba yake Rahma, nikawa na shauku
kubwa ya kuendelea kumuuliza, hasa
kuhusu nyoka huyo lakini mazungumzo yetu yalikatishwa na Rahma.
“Kaka Togo za asubuhi? Naomba
unisindikize dukani mara moja,” alisema Rahma kwa heshima, baba yake akanipa
ishara kwamba niende, nikainuka na kutoka naye.
Tofauti na siku zote, pale nje palikuwa
peupe kabisa, wale madereva Bajaj na bodaboda hawakuwepo, Rahma akaniambia eti
walikuwa wameamua kuhamisha kituo chao na kukipeleka sehemu nyinginekwa sababu
pale hakuna abiria.
Nilijikuta nikicheka tu maana ukweli
haukuwa hivyo, moyoni nilibaki nikijiuliza, ina maana nimekuwa na nguvu kiasi
cha kuwatisha watu kiasi kile?
“Mlikuwa mnazungumza nini na baba? Maana
naona mnaelewana sana, sijawahi kumuona baba yangu akiwa karibu na mtu kama
ilivyo kwako, siku hizi hata mimi hanipendi kama anavyokupenda wewe,” Rahma
alisema wakati tukitembea taratibu kuelekea dukani.
Sikumjibu kitu chochote cha maana zaidi
ya kuleta masihara kwa sababu jana yake nilipotaka kumweleza ukweli aliniona
kama nimechanganyikiwa.
“Mbona mimi nakuuliza maswali ya msingi
wewe unanijibu kimasihara?” Rahma alinihoji, ikabidi niache kuchekacheka na
kuvaa ‘usiriasi’, nikamwambia hata mimi mwenyewe sielewi.
“Tunaenda wapi kwani?”
“Nataka twende pale tulipokaa jana,
nahitaji kuzungumza na wewe,” aliniambia, moyo wangu ulisita kwani niliamini
naweza kukutana na hali kama ya jana Rahma akaendelea kuniona mwendawazimu.
Hata hivyo nilishindwa kumkatalia, tukaelekea mpaka pale dukani.
Cha ajabu, tulipofika tu, yule dada
tuliyemkuta jana yake, aliponiona tu alikurupuka kwa kasi na kukimbia huku
akiacha mlango wazi. Hakuwa amevaa nguo na nadhani hiyo ndiyo sababu
iliyomfanya akimbie, Rahma akawa anashangaa akiwa haelewi kinachoendelea.
“Mbona unavuja damu nyingi hapo,
umepatwa na nini?” alisema Rahma, nilipojitazama pale ubavuni, nilishtuka sana
baada ya kuona damu nyingi nzito zikiwa zimenitoka bila mimi mwenyewe kujua
chochote na kulowanisha kabisa shati langu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment