ILIPOISHIA:
“Mbona
unavuja damu nyingi hapo, umepatwa na nini?” alisema Rahma, nilipojitazama pale
ubavuni, nilishtuka sana baada ya kuona damu nyingi nzito zikiwa zimenitoka
bila mimi mwenyewe kujua chochote na kulowanisha kabisa shati langu.
SASA
ENDELEA...
Sikujua nini cha kufanya, nilitamani
nirudi haraka ndani kabla mambo hayajazidi kuharibika lakini Rahma
akaning’ang’ania, kwanza akitaka kujua kwa nini yule muuzaji alikuwa
akinikimbia lakini pili nini kimetokea mpaka shati langu lilowe damu kiasi
kile.
Kiukweli sikuwa na majibu, nikawa
naendelea kuhangaika kuzuia damu isiendelee kunitoka. Rahma alivua kitenge
chake na kunipa, naye akawa ni kama haelewi kilichokuwa kinaendelea.
Tukiwa tunaendelea kuhangaika, mara
nilisikia ile hirizi yangu mkononi ikinibana sana, nikajua mambo
yameshaharibika. Nilishaambiwa kwamba nikiona inanibana ghafla, ujue mahali
nilipo kuna mtu mwenye nguvu za giza na kuna jambo baya anataka kulifanya.
Harakaharaka nilifanya kama nilivyokuwa
nimeelekezwa, niliunganisha kidole gumba na kidole kidogo kwenye mkono wa
kushoto, nikafanya hivyo kwenye mkono wa kulia, nikaviminya kwa nguvu huku
nikigeuka huku na kule kuangalia ni nani atakayeonesha dalili zisizo za
kawaida.
Nilifundishwa kwamba kama kuna mtu
yeyote anataka kukujaribu kwa nguvu za giza, ukifanya hivyo basi umemkomesha na
kama nguvu zake ni ndogo, anaweza kuumbuka hadharani.
“Mmefuata nini hapa?” sauti ya mwanaume
ilisikika kutoka kwenye lile duka, wote tukageuka kutazama ni nani aliyekuwa
akitusemesha.
“Shikamoo mzee!” Rahma alimsalimu
mwanaume mzee aliyekuwa ndani ya duka hilo kwa uchangamfu. Ilionesha
wanafahamiana. Badala ya kujibu, yule mzee alimuuliza Rahma mimi ni nani na
nimefuata nini pale.
“Ni kaka yangu, anaitwa Togo, tuna
mazungumzo ya kifamilia tulitaka tunywe soda huku tukiendelea kuzungumza.”
“Hapana! Hatuuzi soda hapa, ukitaka
huduma uje peke yako, siyo na huyo,” alisema mwanaume huyo huku akiwa
amenikazia macho, Rahma akashtuka na kunigeukia. Kadiri yule mzee alivyokuwa
akizidi kunitazama, na mimi ndivyo nilivyozidi kuminya vidole huku nikiwa
nimemkazia macho kwani nilihisi ndiye mbaya wangu mwenyewe.
“Ondokeni! Ondokeni,” alisema mzee huyo
kwa kupaza sauti, wateja wengine waliokuwa pembeni wakawa wanashangaa kwa
sababu hakukuwa na jambo lolote baya tulilofanya. Rahma aligeuka na kutaka
kuondoka huku akishangaa iweje mzee huyo atubadilikie kiasi hicho lakini mimi
wala sikutishika kwa sababu nilishaanza kuiona hofu ilivyomjaa ghafla.
Niliendelea kumtazama huku nikiendelea
kuminya vidole vyangu kwa nguvu, nikashangaa kumuona akianza kutokwa na jasho
jingi huku akitingisha kichwa kama kunipa ishara kwamba niache nilichokuwa
nakifanya. Mara alianza kutetemeka, jasho likazidi kumtoka na kufumba na
kufumbua, akaanza kutapatapa kama anayetaka kupandwa na kifafa, akadondoka
chini kama mzigo, puh!
Kitendo hicho kilinishtua sana kwani
alipodondoka tu, ile hirizi nayo iliacha kunibana, sijui nini kilinituma
niangalie juu ya mlango wa kuingilia kwenye duka hilo ambalo lilikuwa limejaza
vitu vingi vya thamani, nikashtuka mno kuona kitu kama fuvu la mtoto mdogo
likiwa limeninginizwa juu ya mlango.
Nikiwa bado nimepigwa na butwaa,
nilisikia sauti ya baba kutokea nyuma. Kumbe wakati nikiendelea kuvutana na
yule mzee, Rahma alikimbilia nyumbani na kwenda kumuita baba yake pamoja na
baba, harakaharaka wakaja.
“Unafanya nini Togo?” baba aliniuliza
kwa sauti ya chini, nadhani hakutaka asikike kwa watu ambao walishaanza
kukusanyika kwa lengo la kutoa huduma ya kwanza na kutaka kujua nini kimetokea.
“Hamna kitu baba, tulikuwa tunataka
kuagiza soda, hakuna kingine,” nilisema huku nikiendelea kukitazama kile kitu
kama fuvu.
“Ondoka haraka, hili eneo si salama,
fanya haraka,” alisema baba, nikageuka na kukutana ana kwa ana na Rahma ambaye
naye alikuwa ananionesha ishara ya kutaka tuondoke haraka eneo hilo maana
tayari watu walishajaa.
Nikarudi kinyumenyume, nikajichanganya
kwenye umati wa watu waliokuwa wakiendelea kujaa, Rahma akanishika mkono na
kuanza kunivuta haraka tuelekee nyumbani.
“Togo, kuna kitu unanificha si ndiyo?
Nataka leo unieleze ukweli, ngoja kwanza nikaangalie kinachoendelea, nakuomba
usitoke, baba amesema ikibidi nikufungie chumbani kwako na funguo,” Rahma
aliniambia huku akipumua kwa kasi, akarudia kunisisitiza kwamba nisitoke kisha
harakaharaka akaondoka.
Nilikaa kitandani na kuvua shati ambalo
lilikuwa limelowa damu, nikawa najitazama pale damu ilipokuwa inanitoka.
Ilikuwa ni kwenye kile kidonda changu, nikawa nashangaa iweje nitokwe na damu
nyingi kiasi kile wakati sikuwa nimejitonesha? Nilijiuliza maswali mengi ambayo
yote hayakuwa na majibu.
“Ina maana yule ndiyo mmiliki wa lile
duka? Kwa nini anatumia uchawi kwenye biashara yake? Kile pale mlangoni ni fuvu
kweli? Ina maana alimuua mtoto ili kuvutia wateja kwenye biashara yake?
“Kwa nini yule mdada amekimbia tena kwa
mara nyingine, tena akiwa mtupu? Ina maana ndiyo mchezo wake kuuza akiwa hana
nguo mwilini?” niliendelea kujiuliza kwa sauti ya chini, maswali yalikuwa mengi
sana ndani ya kichwa changu, hata sikujua ni nani atakayenipa majibu.
Dakika kadhaa baadaye, niliwasikia baba
na baba yake Rahma wakirejea wakiwa wanazungumza kwa sauti za chinichini. Muda
mfupi baadaye, Rahma naye akarejea na kuja moja kwa moja mpaka chumbani kwangu.
“Vipi, nini kimeendelea?” nilimuuliza
Rahma huku nikisimama, nikiwa kifua wazi, akashusha pumzi ndefu na kabla
hajanijibu chochote, macho yake yakatua kwenye ile hirizi niliyokuwa nimeivaa
mkononi, akashtuka kidogo kisha akahamishia macho pale kwenye jeraha dogo
ambalo bado lilikuwa likichuruzika damu.
“Hapo umefanya nini?” alisema huku
akinisogelea na kuinama kunitazama vizuri, nikarudi nyuma huku nikimuonesha
ishara kwamba asiniguse. Akanitazama usoni na kuyagandisha macho yake, tukawa
tunatazamana.
“Hizo damu zimetoka wapi?” sauti ya baba
ndiyo iliyotuzindua. Kumbe wakati nikipita pale koridoni kuelekea chumbani
kwangu, matone ya damu yalikuwa yakidondoka chini mpaka kwenye mlango wangu.
Alipoingia na kunikuta nipo kifua wazi,
tukitazamana na Rahma, alinisogelea na kitu cha kwanza, macho yake yalitua pale
kwenye jeraha langu, akapatazama kwa sekunde kadhaa kisha akanitazama usoni,
naye tukawa tunatazamana.
“Rahma hebu kamuite baba yako haraka,”
alisema baba, harakaharaka Rahma akatoka.
“Haya ndiyo mambo niliyokuwa siyataki
mimi, umeona huo utajiri unaoutaka ulivyo na mambo magumu? Hutakiwi
kutembeatembea mpaka zipite siku saba, siku nyingine utakutana na magwiji
watakuua, una bahati yule mzee bado hajakomaa kwenye haya mambo,” alisema baba,
akaingiza mkono mfukoni na kutoa karatasi alilokuwa amelikunja, akalifungua na
kutoa ungaunga mweusi, akachukua kidogo na kunipaka huku akinitaka kuwa makini.
“Naona na wewe umeanza kuonesha ukidume
wako, unawaona watu si ndiyo?” alisema baba huku akiachia tabasamu hafifu.
Ilikuwa ni nadra sana kwa baba kutabasamu, akanipigapiga mgongoni huku
akiendelea kutabasamu.
Muda mfupi baadaye, baba yake Rahma
aliingia, nikashangaa wote wanacheka na kugongesheana mikono, naye akarudia
kuniambia kwamba niwe makini na nisiende tena kwenye lile duka, kama nahitaji
soda ni bora niagize niletewe nyumbani. Hawakukaa sana, wakatoka na kuniacha
mle chumbani, sekunde chache Rahma akaingia tena.
“Nataka uniambie ukweli Togo, nini
kinachoendelea?”
“Hujanijibu swali langu kuhusu
kilichotokea.”
“Watu wanasema eti yule mzee ni mchawi
na biashara zake amekuwa akiziendesha kwa uchawi sasa leo amekutana na kiboko
yake, wamempeleka kwa mganga lakini hali yake siyo nzuri,” alisema rahma,
nikashusha pumzi ndefu na kukaa vizuri, Rahma akanisogelea huku bado akionesha
kuwa na shauku kubwa ndani ya moyo wake.
“Togo wewe ni mchawi?” Rahma aliniuliza
swali ambalo lilinishtua mno moyo wangu, nikamtazama, akarudia tena swali lake
huku akisisitiza kwamba anataka mimi mwenyewe ndiyo nimweleze ukweli kama kweli
nampenda.
Nikashusha pumzi ndefu huku nikijiuliza,
nimweleze ukweli? Uamuzi niliofikia, ilikuwa ni kumweleza tu maana hayo ndiyo
yalikuwa malengo yangu tangu jana yake, sikutaka kujali ataupokeaje ukweli,
nikameza mate na kumtazama.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
67 na kuendelea bado!!??
ReplyDeleteDahh_vitabu vipooo tuambie tuje kununua
ReplyDeleteNamba 67 inatoka lini kaka.!?
ReplyDelete67 vipi bado
ReplyDelete