Friday, February 2, 2018

Kivuruge wa Tandale- 5



ILIPOISHIA:
Sikukumbuka hata kumalizana na Shija, harakaharaka nikavuka barabara kuelekea upande ule aliokuwa amekaa yule mrembo, huku nikiwa na shauku kubwa ya kutaka kusikia anataka kuniambia nini.
“Mambo kivuruge?” alinisalimia huku akitabasamu, nikashtuka amelijulia wapi jina hilo? Uso wangu ukajawa na aibu.
SASA ENDELEA...
“Nancy!”
“Mh! Umewezaje kulikumbuka jina langu haraka hivyo?”
“Aa! Kawaida tu, unajua kitu au mtu muhimu kwenye maisha yako huwezi kumsahau kirahisi,” nilijikakamua kiume na kujaribu kuyatawala mazungumzo.
“Karibu tupate vinywaji,” alisema msichana huyo huku akinionesha sehemu ya kukaa, nikashindwa kukataa, nikajisogeza na kukaa naye meza moja, tukawa tunatazamana. Si kawaida yangu kumuonea aibu mwanamke, hata awe mzuri kiasi gani lakini siku hiyo nilijikuta nikipoteza kabisa ujasiri mbele ya Nancy.
Kulikuwa na mambo mengi ambayo yalifanya nipoteze ujasiri, kwanza siku hiyo ndiyo ilikuwa ya kwanza kukutana na msichana huyo mrembo, muda ule nilipotoka kwenda kula ‘lunch’.

Hilo halikuwa tatizo kwangu kwa sababu nilikuwa na uzoefu wa kukutana na warembo kadhaa huko nyuma, ambao muda huohuo tuliokutana niliwafanya wanizoee utafikiri tunafahamiana miaka kibao nyuma na hivyo kutimiza malengo yangu kwa urahisi.
Tatizo lilikuwa mazingira niliyokutana na Nancy na alichonifanyia. Kwanza alikataa kabisa kunipa namba zake za simu licha ya kujitahidi kumchombeza kwa maneno ya hapa na pale lakini alinichomolea, tena kwa maneno ambayo niliyaona kama ni dharau kubwa kwangu! Lakini kama hiyo haitoshi, aliamua kunitukana kiutu uzima kwa kulipia bili yangu ya chakula bila kuniambia chochote, yaani ni kama aliyeamua kusema ‘utanipa nini maskini wewe!’
Lakini kingine kilichofanya nipoteze ujasiri, ni kwamba nilikuwa nimetoka matukio ambayo nilihisi kila nitakayetazamana naye usoni, anaweza kugundua kwamba nimetoka kufanya nini.
Kitendo cha kuwavuruga Madam Bella na Salma, tena ndani ya muda huohuo, wakipishana dakika chache tu, kilinifanya nijihisi kuwa na hatia ndani ya moyo wangu, nikawa nahisi nikitazamana sana na nancy anaweza kuyaona niliyotoka kuyafanya na pengine nikapoteza kabisa nafasi hata ya kukaa naye mezani nakunywa soda.
“Nambie, mbona sasa hivi huna porojo kama muda ule kule kantini?” aliniuliza huku akionesha kuchangamka sana, akavuta juisi kwa kutumia mrija aliokuwa ameushika kisistaduu na kumeza funda moja, akawa bado anaendelea kuchekacheka mwenyewe kwa furaha.
“Aliyekwambia kwamba mimi naitwa Kivuruge ni nani?”
“Mh! Kwani ukiwa na tabia mbaya unajificha? Kila mtu anakufahamu na habari zako zinasambaa kwa kasi.”
“Tabia mbaya kivipi? Na hayo yote yanakujaje?” nilisema huku nikijitahidi kuuvaa uso wa usiriasi. Nancy akanitazama, alipoona nimeanda kubadilika usoni alipunguza masihara.
“Mhudumu, hebu njoo umsikilize mgeni wangu,” alisema Nancy, nikawa nageuka na kutazama huku na kule. Kwa ufupi ni kwamba utulivu uliniisha kabisa ndani ya motyo wangu kwa sababu ukiachilia ukweli kwamba pale tulipokaa watu wengi walikuwa wakinijua, ilikuwa ni jirani pia na ofisini kwetu.
Kwa sababu nilifanya kuondoka kijanja, nilijua Salma au Madam Bella, yeyote kati yao atakayekuwa wa kwanza kutoka, lazima ataniona nikiwa nimekaa na Nancy.
“Hamna bana mi nakutania, yule dada wa pale kantini ndiyo aliyeniambia eti wewe wanakuita Kivuruge kwa tabia yako ya kupenda wanawake.”
“Mimi! Jamani, mbona wau wanapenda sana kunisingizia?” nilisema huku nikivaa sura ya upole ambayo ni miongoni mwa silaha nyingine ambazo hunisaidia sana ninapokuwa kwenye mawindo yangu.
“Unataka kusema anakusingizia? Mbona mimi kuniona leo tu umenitongoza?” alisema Nancy na kuzidi kunibana. Sikukubali kushindwa, nilitumia mwanya huo kujitetea lakini pia kuendelea kujitengenezea mazingira.
Kitendo cha Nancy kujileta mwenyewe pale na kunichangamkia baada ya kuniona, kilikuwa ni ishara nzuri kwangu, nikajua nikiongeza juhudi kidogo tu naweza kufanikiwa kumuopoa mrembo huyo ambaye kiukweli alikuwa akiyafanya mapigo ya moyo wangu yapishane ‘steps’ kama hatua za mlevi.
“Kwani wewe unaishi wapi?” aliniuliza Nancy, nikaona nishai kumjibu kwamba naishi Tandale kwa sababu mrembo mwenyewe alionekana kutoka kwenye familia bora kisawasawa, nikazugazuga lakini kumbe tayari alikuwa anazo taarifa zangu zote.
“Si nimesikia unaishi Tandale wewe? Sasa mbona unasema unaishi Sinza?”
“Naishi kwenye mpaka wa Sinza na tandale lakini upande wa tandale,” nilikuta nimezungumza kitu ambacho hata sikuwa nimekifikiria kichwani.”
“Kwa hiyo wewe unaishi Tandale au Sinza?” nancy alizidi kunikalia kooni, huku akicheka sana. Alionekana kufurahishwa sana na ujanjaujanja wangu katika mazungumzo, ikafika mahali akawa anacheka mpaka analeta mkono kugonga na mimi, nikawa nafurahia ulaini wa viganja vya mikono yake na kajoto f’lani hivi alikokuwa nako.
“Nimefurahi sana kukufahamu Kivuruge!”
“Nimefurahi pia kukufahamu mrembo Nancy.”
“Kwani mimi mrembo?”
“Ndiyo, tena sana! Mungu amekupendelea vitu vingi sana, ‘trust me’,” nilianza kumsifia Nancy, basi akawa anacheka kwa sauti ya juu mpaka watu waliokuwepo pale pembeni yetu wakawa wanageuka na kututazama.
Halikuwa jambo dogo kukaa na msichana mrembo kama Nancy na kumfanya muda wote awe na furaha kiasi kile, wale wahudumu wa kiume nikaona wananitazama kwa macho yaliyoonesha wazi kwamba wana chuki na mimi. 
“Sasa Nancy, mi naomba nikuache, kuna kazi inatakiwa nikaifanye nyumbani, si unajua tena maisha ya kigetogeto jioni ndiyo muda wa kufanya kazi za ndani,” nilimuaga kijanja, akacheka sana, mwisho akaniambia nisubiri tuondoke wote.
“Mh!” niliguna, kiukweli nilikuwa namtaka sana Nancy lakini siyo kwa muda huo, nilikuwa nimechoka vibaya sana na kama kweli angekubali kuondoka na mimi, maana yake tungejikuta wote tumeishia Tandale, kwenye nyumba ninayoishi na kwangu mimi hilo lilikuwa ni kosa sawa na kuwapita mabeki wote na kubaki mimi na kipa tu golini.
Kabla hata sijajibu chochote, Nancy alisimama na kuchukua mkoba wake wa kijanja, akaufungua na kutoa noti ya shilingi elfu kumi, akamuita mhudumu na kulipa kisha akanionesha ishara kwambe ‘twen’zetu’.
“Kwani unaishi na nani kwako?”
“Naishi mwenyewe Nancy.”
‘Huwa unatumia usafiri gani ukiwa unatoka?”
“Daladala tu, si unajua mimi mgumu,” nilisema kwa kujitutumua, akacheka sana, akaniambia siku hiyo anataka kunipa ofa ya kupanda Ubber.
“Ubber ndiyo nini?” nilimuuliza kwa sababu kiukweli sikuwa najua, akanielekeza kwamba ni teksi ambazo hazina nembo kama teksi hizi za kawaida na mteja anatumia mtandao kuiita na hata malipo yake yapo tofauti kidogo, akanielekeza kwamba huwa mteja analipa kulingana na kilometa na muda aliotumia barabarani.
Alinizidi maarifa katika hilo, tukatoka na kuelekea barabarani, muda wote nikawa nageukageuka kutazama kama hakuna mtu yeyote atakayetoka pale ofisini kwetu na kuniona. Kwa mbali nilimuona mlinzi wetu, Shija akinionesha alama ya dole kama anayesema ‘nimekukubali kaka’.
Uzuri wa Nancy ulisababisha kila tulipokuwa tunapita, midume igeuka na kumtazama, alikuwa amejaaliwa haswaa! Basi muda mfupi baadaye, tayari tulikuwa ndani ya gari dogo lenye ‘kipupwe’ ndani, akaniambia mimi ndiyo nimuelekeze dereva wapi kwa kutupeleka.
“Tandale kwa Mtogole kaka,” nilisema, yule dereva akageuka na kunitazama akiwa ni kama haamini nilichomwambia. Nadhani kwa hadhi ya mrembo niliyekuwa naye, alitegemea nimwambie tupeleke Masaki au Mbezi, sijui kwa nini sisi watu wa Tandale tunadharaulika sana.
Basi tulitoka na safari ikaanza, nikiwa nimekaa siti ya nyuma na Nancy, tukawa tunaendelea kupiga stori, safari hii akinilalia kifuani mara kwa mara na kunifanyia vituko ambavyo viliniweka katika wakati mgumu sana.
Sijui kulitokea nini, nikashtukia amenibusu, nikamgeukia nakumtazama, akawa ananitazama kwa macho yaliyobeba hisia nzito sana za mapenzi, moyoni nikawa nasema ‘hunijui vizuri wewe’.
Ni kweli nilikuwa nimechoka sana lakini kamwe nisingeweza kuacha nafasi adhimu kama ile inipite, nikiwa bado najiongeza kichwani nini cha kufanya, nilishtukia tukiwa tumegusanisha ndimi zetu, akionekana kuwa na hisia nzito sana za mapenzi.
Kila kitu kilikuwa kikitokea kwa kasi kubwa kiasi kwamba kama hunifahamu, ungeweza kudhani nimemfanyia dawa dada wa watu anipende ghafla, kichwani nikawa nafikiria kwamba tukishuka tu dukani, fasta naenda dukani kwa Mangi ‘kujibusti’ kwanza kuondoa uchovu wote kisha ndiyo nianze kudili naye.
“Tumeshafika bro!” alisema yule dereva wa Ubber, kauli yake ndiyo iliyotuzindua kutoka kwenye dimbwi la huba, kucheki pembeni, kweli tayari tulikuwa Tandale kwa Mtogole.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Risasi Mchanganyiko.


No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...