Monday, February 5, 2018

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 61



ILIPOISHIA:
Kila kitu kilibadilika kwa kasi kubwa mno, mvua kubwa ikaendelea kumwagika, huku wingu kubwa jeusi likitanda kila kona na kuimeza kabisa nuru iliyokuwepo, ungeweza kudhani tayari ni usiku.
“Kuna kitu kinataka kutokea siyo kizuri, hebu nifuateni haraka,” alisema Junaitha, wote tukakurupuka na kusimama, tukatoka na kuanza kumfuata Junaitha, tukiwa hatuelewi tunaenda wapi.
SASA ENDELEA...
Kila kitu kilibadilika kwa kasi kubwa mno, mvua kubwa ikaendelea kumwagika, huku wingu kubwa jeusi likitanda kila kona na kuimeza kabisa nuru iliyokuwepo, ungeweza kudhani tayari ni usiku.
“Kuna kitu kinataka kutokea siyo kizuri, hebu nifuateni haraka,” alisema Junaitha, wote tukakurupuka na kusimama, tukatoka na kuanza kumfuata Junaitha, tukiwa hatuelewi tunaenda wapi.
“Asibaki mtu nyuma, kuweni makini,” alisisitiza Junaitha huku akipiga hatua za harakaharaka, tukazidi kuelekea ndani ya nyumba hiyo, tukafika mpaka sehemu kulipokuwa na korido nyembamba, tukaenda mpaka mwisho wa korido ambako hakukuwa na mlango wala sehemu ya kupita, nikawa sielewi lengo la Junaitha.

“Leso trebos replicas nimbus,” alisema Junaitha na kutuambia na sisi tumfuatishe maneno hayo mara saba kwa kasi, tukaanza kurudia maneno hayo ambayo hakuna aliyeyajua maana yake zaidi ya yeye mwenyewe.
Cha ajabu, tuliporudia kwa mara ya saba, lile eneo ambalo tuliona kama ni ukuta, lilibadilika na kuwa mlango, ukajifungua ambapo alituelekeza kwamba tunatakiwa kuingia kinyumenyume, akaanza yeye huku akituhimiza kufanya haraka kuingia.
Tulipoingia wote, alitamka maneno fulani ambayo hakuna aliyeelewa maana yake, pale palipokuwa na mlango pakajifunga, kule ndani giza likatanda kila sehemu. Hakuna ambaye aliweza hata kumuona mwenzake aliyekuwa naye sentimita kadhaa tu pembeni.
Bado tuliweza kusikia ngurumo za radi na upepo mkubwa vilivyokuwa vikiendelea kusikika, kuonesha kwamba mvua ilikuwa ikiendelea kunyesha. Nikasikia vishindo vya Junaitha na muda mfupi baadaye, tukasikia akiwasha swichi ya ukutani, taa ikawaka, kila mtu akawa anageuka huku na kule kutazama vizuri mandhari ya pale tulipokuwepo.
Kilikuwa ni chumba kikubwa ambacho kwa ilivyoonesha, ni kama kilikuwa sebule ambayo haijatumika kwa miaka mingi iliyopita, ‘matandabui’ yalikuwa yametapakaa kila sehemu, mpaka kwenye ile taa ambayo nayo ilikuwa na mwanga hafifu kutokana na kuzingirwa na vumbi pamoja na matandabui.
Pembeni kulikuwa na samani za kale, makochi ya kizamani, meza ya mbao, kabati dogo lililokuwa na vyombo vichache vya udongo. Kila kitu ndani ya sebule hiyo kilikuwa cha kizamani, vumbi na matandabui vikazidi kupafanya pawe na mwonekano wa kutisha sana.
“Kaeni hapo mtulie kimya, asiondoke yeyote kati yenu,” alisema Junaitha na kufumba na kufumbua, tulishangaa tu ameyeyuka, hakuna aliyejua ameenda wapi.
“Kwani kuna nini kinaendelea jamani? Mbona sielewi?”
“Tumeambiwa tutulie,” nilimjibu Raya ambaye alionesha kuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua nini kimetokea. Muda mfupi baadaye, ile taa ilizimika, giza likawa nene kuliko hata mwanzo. Hakuna aliyemsemesha mwenzake, kila mmoja alikuwa kimya kabisa.
Ukimya ulikuja kukatishwa na kelele za mlango uliokuwa ukifunguliwa, Junaitha akaingia na kwenda kuwasha tena taa, wote tukashangaa akiwa amelowa chapachapa na mwili wake kubadilika rangi na kuwa mweusi. Hata maji yaliyokuwa yakichuruzika kwenye mwili wake yalikuwa meusi mithili ya mtu aliyeogea maji ya mkaa.
Cha ajabu, zile ngurumo za radi hazikusikika tena, kukawa kimya kabisa.
“Twendeni,” alisema Junaitha huku akitetemeka kutokana na kulowana, harakaharaka wote tukainuka na kuelekea kwenye ule mlango, tukatoka na Junaitha akawa wa mwisho kutoka. Alipotoka tu, ule mlango nao ulipotea, eneo lote likawa kama lilivyokuwa mwanzo, ukuta.
“Washenzi sana hawa, kazi imekwisha sasa,” alisema Junaitha huku akigeuka na kumtazama Shenaiza ambaye muda wote alikuwa kimya kabisa, kama hayupo.
“Vipi unajisikiaje?”
“Najisikia vizuri lakini bado nina maswali mengi.”
“Hayo mambo ya maswali achana nayo. Jamal wewe kuna waandishi wa habari unaofahamiana nao?”
“Waandishi wa habari? Wa nini tena?”
“Hili suala tunaelekea kulimaliza lakini polisi wa nchi hii nawajua, tunaweza kuwapa ushahidi wote lakini bado wakashirikiana na wahalifu kubadilisha ukweli kuwa uongo kwa hiyo nimewaza kwamba ni bora tuwe na mwandishi wa habari mmoja na mwanasheria mmoja, siku chache zijazo nchi yote hii itatingishika,” alisema Junaitha.
Cha ajabu, Firyaal na Shenaiza ambaye mtuhumiwa mkuu tuliyekuwa tukihangaika kuhakikisha anafikishwa mbele ya sheria ambaye ni baba yao mzazi, walionesha kufurahishwa zaidi na taarifa hizo, wakatazamana na kuachia tabasamu kisha wakawa ni kama wanapeana ishara fulani.
Junaitha alituongoza mpaka sebuleni, kila mtu akawa na shauku ya kuchungulia nje kwani hali ya hewa ilikuwa imebadilika na kurudi kama mwanzo, yaani usingeweza kudhani kwamba muda mfupi uliopita hali ilikuwa tete.
Mimi ndiyo nilikuwa wa kwanza kusimama na kwenda mpaka dirishani, nikafungua pazia na kuchungulia nje. Cha ajabu, hakukuwa na dalili zozote za mvua, nikapigwa na butwaa nikiwa ni kama siamini. Nilifikicha macho yangu nikihisi huenda nilikuwa ndotoni lakini haikuwa hivyo; hakukuwa na dalili yoyote ya mvua kunyesha na jua lilikuwa likiwaka.
Niligeuka na kuwatazama Shamila, Raya, Firyaal na Shenaiza ambao ni kama walikuwa wakisubiri nitawajibu nini, nikatingisha tu kichwa, hali iliyowafanya wainuke haraka na kuja pale dirishani, nao wakapigwa na butwaa kwani hakukuwa na dalili zozote za mvua.
“Kwani mama’ako mdogo ni mchawi?” Raya alimuuliza Shamila lakini kabla hajajibu, Junaitha akaingilia kati.
“Ndiyo, mimi ni mchawi, hata wewe ni mchawi ndiyo maana upo hapa, unafikiri umefika kwa bahati mbaya hapa?” alijibu Junaitha ambaye tayari alishabadilisha nguo na kuvua zile zilizokuwa zimelowa ingawa bado mwili wake ulikuwa mweusi sana.
“Haya njooni huku kila mtu aulize maswali yote aliyonayo, nipo tayari kuwajibu kwa sababu kesho ndiyo siku ya kuhitimisha kila kitu kilichokuwa kikiendelea,” alisema Junaitha, wote tukainuka na kuanza kumfuata, mimi ndiyo nilikuwa nyuma kabisa, nikamuona Shamila akipunguza mwendo kwa makusudi, wote wakapita, tukabaki wawili tu nyuma, akageuka na kunitazama usoni, macho yetu yakagongana.
“Nashindwa kujizuia mpenzi wangu.”
“Vipi tena Shamila.”
“Nimekumisi mpenzi wangu.”
“Lakini si tupo pamoja mama?”
“Ndiyo, lakini mambo yenyewe ndiyo kama hivi, hatupati hata dakika chache za kuwa pamoja, mi nimechoka bwana,” alisema Shamila na kunisogelea mwilini, nikawa naiona hatari iliyokuwa mbele yetu endapo Junaitha atageuka na kugundua kwamba tulibaki koridoni tumesimama, tena tukiwa tumesogeleana mithili ya majogoo yanayotaka kupigana.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...