ILIPOISHIA:
Junaitha alimkokota mpaka bafuni na
kufunga mlango kwa ndani, nikabaki nimesimama pale koridoni. Ghafla nikaanza
kusikia sauti ya Firyaal akilia kama mtu anayekabwa na kitu, nikakurupuka mpaka
kwenye kile chumba walichokuwa wamelala wote, nikafunga breki za ghafla
mlangoni, nikiwa siamini kile nilichokuwa nakiona.
SASA ENDELEA...
Firyaal alikuwa amejikaba shingoni kwa
kutumia mikono yake miwili, macho yakiwa yamemtoka pima, akikoroma kama mtu
anayeelekea kukata roho. Sikuwahi kusikia hata mara moja kama kuna mtu amewahi
kufanikiwa kuyakatisha maisha yake kwa kujikaba mwenyewe lakini kwa Firyaal
ilionesha kama hilo linaweza kutokea muda wowote.
Kwa kasi ya ajabu nilisukuma mlango na
kwenda kumkamata Firyaal, kwa jinsi alivyokuwa na mwili ‘teketeke’, niliamini
itakuwa rahisi kwangu kumtoa ile mikono yake shingoni lakini kumbe nilikuwa
najidanganya.
Nilishangaa nilipomgusa Firyaal kukuta
mwili wake umekakamaa na kuwa mgumu kama mti, nikaanza kuhaha kujaribu kumnasua
bila mafanikio, aliendelea kukoroma huku wenzake wakiwa wamelala fofofo.
Ilibidi nitoke na kumkimbilia Junaitha
ambaye muda mfupi baadaye naye alikuja na kushuhudia kile kilichokuwa
kikiendelea.
“Umemfanya nini?”
“Sijui chochote, mi nimemkuta tu
anajikaba,” nilisema, akamsogelea kwa hatua za harakaharaka na katika hali
ambayo sikuitegemea, nilishangaa kumuona akimzibua kibao cha nguvu upande wa
kushoto, akahamia upande wa kulia, akamzibua kwa nguvu zaidi!
“Utamuumiza?”
“Hapa ndiyo namsaidia, nyamaza?”
Junaitha alinifokea, akamuongeza kibao kingine cha upande wa kushoto, nikafumba
macho kwani sikutaka kuona jinsi msichana huyo mrembo alivyokuwa akiadhibiwa.
“Eeeh! Hapa ni wapi? Jamal, Jamal,”
sauti ya Firyaal iliyokuwa inatoka kwa kukoroma, ndiyo iliyonifanya nifumbue
macho, nikashangaa kumuona akiwa amefumbua macho, akijishangaa yeye mwenyewe na
kutushangaa sote mle ndani.
“Firyaal,” nilisema huku nikisimama, na
yeye akajikongoja na kusimama, tukawa tunataka kwenda kukumbatiana lakini
Junaitha alitukataza, akasema Firyaal amevamiwa na pepo wachafu kwa hiyo lazima
asafishwe kwanza ndiyo tutakaporuhusiwa kugusana naye.
Maelezo yale yalinishtua sana,
nikakumbuka kauli ya Junaitha kwamba lazima kuna mmoja wetu atapoteza maisha
kama kafara, nikawa nasali moyoni kwamba asiwe Firyaal kwa sababu nilimuona
kama mrembo sana, tena binti mbichi ambaye alikuwa tayari kunipa zawadi ya kuwa
mwanaume wake wa kwanza, kama ilivyokuwa kwa Raya.
“Nakuomba msaidie,” nilimwambia
Junaitha, akanitazama tu usoni bila kunijibu chochote. Tukiwa tunatazamana,
mara tulishtuka kumuona Shenaiza akiingia ndani ya kile chumba akiwa amejifunga
taulo tu, naye akapigwa na butwaa kumuona mdogo wake, Firyaal naye akashtuka
mno kumuona dada yake akiwa amesimama, wote tukawa tunashangaana, ukimya
ukapita kati yetu.
“Naombeni mnisikilize kwa makini,
tumefikia hatua nzuri sana lakini kama tusipokuwa makini, tutasababisha
matatizo makubwa zaidi, Jamal shughulika na Shenaiza, mimi ngoja nikamalizane
na Firyaal, angalizo! Hamtakiwi kugusana kwa sasa,” alisema Junaitha,
nikatingisha kichwa kuonesha kukubaliana naye.
“Bado sielewi Jamal, mdogo wangu
amefikaje huku halafu mbona kama hayupo sawa?”
“Shenaiza, tulikotoka ni mbali sana
kuliko tunakoelekea, amini kila kitu kitakuwa sawa kabisa, twende,” nilisema
kwa sauti iliyojaa matumaini makubwa ingawa ukweli hata mimi nilikuwa sijui
mwisho wa sarakasi zote zile ungekuwa nini.
Kama alivyosema Junaitha, sikutakiwa
kumgusa Shenaiza ingawa mwenyewe alionesha kuwa na shauku kubwa ya kutaka
tukumbatiane, tukaongozana mpaka chumbani kwake. Kwa kuwa siku zote hizo hakuwa
na fahamu, hata chumba chake kilikuwa kizito mno, tulipoingia tu mwenyewe ndiyo
alikuwa wa kwanza kuligundua hilo.
“Mbona humu ndani hewa nzito sana?”
alisema, sikumjibu chochote zaidi ya kumsaidia kufungua madirisha na kuwasha
feni, yeye akakaa kwenye kiti kilichokuwa pembeni ya kitanda, akiendelea
kunitazama kama anayetamani kuzungumza jambo na mimi.
“Unajua bado najihisi kama nipo kwenye
ndoto, kumbukumbu zangu zinarudi taratibu sana kichwani.”
“Usiwe na wasiwasi, kila kitu kitakuwa
sawa.”
“Wewe si ulikuwa unaumwa hoi
hospitalini?” aliniuliza, nikatingisha kichwa huku nikifungua vifungo vya shati
langu, nikamuonesha jeraha akubwa lililokuwa kifuani ambalo sasa lilikuwa
limepona na kubakiza ganda la juu kubanduka ili lipone kabisa na kuacha kovu,
akapigwa na butwaa.
“Mh! Kwa hiyo nilipoteza fahamu kwa muda
mrefu kiasi hicho mpaka umepona?”
“Ni stori ndefu Shenaiza, hebu tuliza
kwanza kichwa chako, nimeshakwambia kila kitu kitakuwa sawa.
“Sasa ulitokaje hospitalini na mimi
nilitokaje? Yule daktari aliyekuwa akinichoma sindano za kwenye mishipa alikuwa
akichanganya na nini mbona zilikuwa zikiuma sana halafu nikawa nalala sana
baada ya kuchomwa?”
“Jamani Shenaiza, si nimekwambia
nitakueleza kila kitu? Kuwa mpole,” nilimwambia. Kwa kuwa shuka lililokuwa limetandikwa
pale kitandani lilikuwa limechafuka, ilibidi nifungue kabati na kuchukua
jingine safi, nikabadilisha na kumwambia apumzike kitandani.
Kweli alifanya hivyo lakini akataka na
mimi nilale naye pale kitandani, jambo ambalo sikukubaliana naye, nikamwambia
ni lazima tufuate masharti kwa sababu tulikuwa kwenye kipindi kigumu. Kweli
alijilaza pale kitandani kihasarahasara, mimi nikakaa pale alipokuwa amekaa
yeye.
Bado alikuwa na maswali mengi lakini
niliendelea kumkatisha na kumtaka apumzike. Kutokana na jinsi alivyokuwa
amechoka, hazikupita dakika tatu, akapitiwa na usingizi mzito.
Muda mfupi baadaye, Junaitha alirejea
akiwa na Firyaal ambaye sasa alionesha kurudi kwenye hali yake ya kawaida.
“Kwa nini umemruhusu huyo alale tena
wakati hajala chochote? Hebu muamshe, anaweza kupitiliza tena akatupa kazi ya
ziada,” alisema Junaitha na hakusubiri mimi nifanye kazi hiyo, alimsogelea
mwenyewe pale kitandani na kuanza kumtingisha.
Shenaiza akakurupuka usingizini na kukaa
kitako, macho yake yakatua kwa mdogo wake, safari hii Junaitha aliwaruhusu
wakumbatiane, wakafanya hivyo na kila mmoja wao akaanza kuangua kilio kwa sauti
ya juu mithili ya watu waliopokea taarifa za msiba.
Cha ajabu, walipokumbatiana na kuanza
kulia tu, mvua kubwa ilianza kunyesha ghafla, akina Raya na Shamila waliokuwa
usingizini nao wakazinduka na kuja mbiombio kwenye kile chumba tulichokuwemo,
yule mwanamke wa ajabu aliyekuwa amefungiwa naye akaanza kunguruma kwa sauti
kubwa.
Kila kitu kilibadilika kwa kasi kubwa
mno, mvua kubwa ikaendelea kumwagika, huku wingu kubwa jeusi likitanda kila
kona na kuimeza kabisa nuru iliyokuwepo, ungeweza kudhani tayari ni usiku.
“Kuna kitu kinataka kutokea siyo kizuri,
hebu nifuateni haraka,” alisema Junaitha, wote tukakurupuka na kusimama, tukatoka
na kuanza kumfuata Junaitha, tukiwa hatuelewi tunaenda wapi.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment