ILIPOISHIA:
Maneno yake yalinipa nguvu sana,
akaniambia kwamba aliwalaza usingizi mzito kwa makusudi wale wengine ili
tukamalizie kazi ya kumzindua Shenaiza lakini akanipa taarifa ambazo
zilinishtua mno. Aliniambia baba yake Shenaiza amejizatiti vilivyo kwa nguvu za
nje na ndani na ili tufanikishe azma yetu, ilikuwa ni lazima mtu mmoja kati
yetu afe.
“Afe?”
“Ndiyo, lazima afe mtu kwenye kafara.”
SASA ENDELEA...
“Sasa mambo ya makafara yanaingiaje tena
hapa? Kama ni hivyo basi mimi najitoa.”
“Ukijitoa maana yake wewe ndiyo utakufa.
Wasiwasi wa nini na wewe ni mwanaume? Hebu acha woga, nitakufundisha cha
kufanya wala usiwe na wasiwasi,” alisema Junaitha lakini kiukweli alikuwa
amenichanganya mno.
Mmoja kati yetu lazima afe? Nani sasa!
Kama siyo mimi ni nani? Raya? Haiwezekani. Shenaiza? Hapana. Shamila? Noo! Au
Firyaal? Nilijiuliza maswali mengi ambayo yote hayakuwa na majibu.
Nilichokifanya ilikuwa ni kujaribu kupambana na hofu ambayo sasa ilikuwa
inanitafuna ndani kwa ndani.
Hakuna kitu ambacho binadamu hawezi
kukizoea kama kifo! Miaka yote watu wanakufa lakini kwa nini kila mtu anapokufa
kunakuwa na msiba mzito kwa watu wanaomzunguka? Ni dhahiri kwamba kifo
hakizoeleki.
“Mbona kama umepoteza umakini Jamal?
Kwani wewe unaelewa nini kuhusu kifo?” aliniuliza Junaitha, swali ambalo
lilinizindua kutoka kwenye lindi la mawazo.
“Kifo? Kifo si ni kufa?”
“Ndiyo ni kufa, unaelewa nini kuhusu kufa?”
“Ndiyo ni kufa, unaelewa nini kuhusu kufa?”
“Mtu anakufa na huo ndiyo unakuwa mwisho
wa maisha yake,” nilimjibu Junaitha, nikiwa nimemkodolea macho.
“Huna haja ya kuogopa kuhusu kifo kwa
sababu kinachotokea inakuwa ni kuhama tu kutoka kwenye ulimwengu mmoja kwenda
kwenye ulimwengu mwingine, ni kama hivi tu sisi tunavyofanya lakini tofauti
yake ukifa unakuwa huwezi kurudia kwenye mwili wako lakini hakuna tofauti sana.”
“Sijakuelewa.”
“Utanielewa tu wala usiwe na haraka,
sitaki kabisa kusikia ukiogopa kuhusu kifo, umenielewa?”
“Nitaachaje kuogopa Junaitha?”
“Sasa unaogopa nini? Mbona huogopi
tunavyohama kutoka ulimwengu mmoja kwenda mwingine?” alisema Junaitha lakini
bado alichokuwa anakisema hakikuingia kabisa akilini mwangu.
“Hebu tuachane na haya mambo kwanza,
tuna kazi kubwa mbele yetu,” alisema, akanibusu mdomoni, nikashusha pumzi ndefu
na kuinuka pale tulipokuwa tumelala, naye akainuka, tukatoka na kuelekea kwenye
chumba alichokuwa amelala Shenaiza.
“Hebu niambie ukweli, hujawahi kufanya
mapenzi na huyu msichana kweli?” Junaitha aliniuliza, akimaanisha Shenaiza,
nikamjibu kwa kutingisha tu kichwa.
“Hebu nitazame usoni,” alisema Junaitha
lakini sikutaka kumtazama kwa sababu ambazo nazijua mwenyewe.
“Kwa nini tusimalize kazi kwanza halafu
hayo mengine yatafuata baadaye?” nilisema huku nikionesha kutofurahishwa na
swali lake, ilivoonesha naye hakutaka kuniudhi kwani alibadilisha mada haraka.
“Simama kwa kule,” aliniambia,
akinioneshea upande uliokuwa na miguu ya Shenaiza, nikafanya kama
alivyoniambia. Yeye alisimama upande wa kichwani kwa msichana huyo, akapiga
magoti na kunitaka na mimi nifanye hivyohivyo.
“Katika vidole vyako kumi vya mikono,
nataka kila kimoja kiguse kidole cha Shenaiza na ushikilie hivyohivyo, usiachie,”
aliniambia, nikafanya kama alivyoniambia. Kweli nilishika vidole vyote vya
Shenaiza, nikawa namtazama Junaitha kusubiri maelekezo zaidi.
“Fumba macho,” alisema Junaitha na
kusisitiza kwamba nisimuachie vidole wala nisifumbue macho, nikamsikia akianza
kuongea maneno ambayo hata sijui ni ya lugha gani au yalikuwa yakimaanisha
nini, akaendelea kuyarudiarudia na kadiri alivyokuwa anazidi kuongea ndivyo
sauti yake ilivyoanza kuwa ya kutisha, ikawa inasikika kama ile aliyoitoa kule
kwenye ulimwengu mwingine ambayo ama kwa hakika ilikuwa ikitisha.
Nilianza kuhisi vitu kama upepo mkali
ukivuma mle ndani, sikuelewa umetokea wapi, ukabadilisha na kuanza kuwa kama
kimbunga kikali, vitu vikawa vinapeperushwa huku na kule. Upepo ulizidi kuwa mkali,
Junaitha naye aliendelea kuyarudiarudia maneno yake kwa ukali, mara ikaanza
kusikika miungurumo ya ajabu mle ndani, ikafuatiwa na radi kubwa iliyopiga kwa
nguvu kubwa mno, nilijikuta nikipoteza mwelekeo, nikarushwa mpaka ukutani,
nikajibamiza na kudondoka chini.
Ninachoshukuru ni kwamba sikufumbua
macho kama Junaitha alivyoniambia, nikajikuta nimepoteza fahamu, nikawa sielewi
kinachoendelea.
“Wewe ni nani?”
“Na wewe ni nani?” nilijikuta nikirejewa
na fahamu lakini nusunusu, jitu kubwa ambalo sikuweza kuona mwisho wake,
lilikuwa limesimama mbele yangu, likiniuliza kwa sauti nzito. Cha ajabu, eti
wala sikuogopa chochote na badala ya kujibu, na mimi nikaliuliza swali.
“Kwa nini mnaingilia mambo yasiyowahusu?
Mnamjua huyu binti? Kwa nini mnataka kumsaidia?”
“Na nyie kwa nini mnamtesa? Si
ameshawaambia hataki kushirikiana nanyi?”
“Wewe ndiyo unamsemea? Kwa nini asiseme
mwenyewe?”
“Nasema mwenyewe sasa, sitaki
kushirikiana na nyie, Jamal nisaidie baba?” sauti ambayo niliitambua vyema
kwamba ni ya Shenaiza ilisikika lakini nilipogeuka huku na kule, sikumuona
zaidi ya lile jitu.
“Unasemaje wewe?”
“Nimesema sitaki kushirikiana na nyie,
niacheni na maisha yangu,” sauti ya Shenaiza ilisikika tena, ghafla ikasikika
tena radi kali ambayo safari hii niliona kama imepiga jirani kabisa na pale
nilipokuwa.
Fahamu zikanirudia vizuri, nikajikuta
nimelala sakafuni, huku Shenaiza akipiga kelele kwa nguvu pale kitandani,
Junaitha akikazana kumtuliza.
“Njoo unisaidie Jamal, inuka njoo,”
alisema Junaitha, nikainuka pale sakafuni kwa kujikongoja, nikasogea pale
nilipokuwa nimesimama awali, Junaitha akaniambia nimshikilie Shenaiza ambaye
alikuwa akirusha miguu na kutapatapa.
“Tulia Shenaiza, kila kitu kitakuwa
sawa,” alisema Junaitha, msichana huyo ambaye muda wote alikuwa amefumba macho,
alifumbua na ghafla akawa ni kama amezinduka, macho yake yakatua kwangu.
“Jamal!”
“Shenaiza.”
“Hapa ni wapi na nimefikaje?”
“Ooh! Ahsante kazi imekamilika,” alisema
Junaitha huku akimuachia Shenaiza, akawa anajifuta jasho jingi lililokuwa
linamtoka.
“Na huyu ni nani?”
“Tulia Shenaiza, kwanza pole kwa yote
yaliyokutokea, pumzika kwanza utajua kila kitu,” nilimwambia, akawa bado ni kama
ana mawenge, akawa ananitazama mimi, anamtazama Junaitha, anakitazama kile
chumba, anajitazama yeye mwenyewe katika namna ya kushangaa sana.
“Inabidi nikamuogeshee maji ya maiti,
amka binti,” alisema Junaitha na kumshika mkono Shenaiza ambaye bado alikuwa
ameduwaa. Kiukweli hata mimi nilikuwa na maswali mengi sana lakini ilibidi nijikaze
ili Shenaiza atulie. Nilishangaa kwamba iweje ndani ya muda mfupi tu namna
hiyo, kutokee mambo ya kutisha kiasi kile mle ndani halafu watu waliopo nje
wasijue chochote?
Nini kimefanyika mpaka Shenaiza ambaye
kwa siku kadhaa alikuwa amepoteza kabisa fahamu, leo arudiwe na fahamu zake
kama hakuna kilichotokea? Wanaosema uchawi haupo, nawapa pole. Uchawi upo na
una nguvu kwelikweli.
“Njoo kwanza Jamal,” alisema Shenaiza
baada ya kuwa ameshasimama kwa msaada wa Junaitha, mwili wake ukiwa hauna nguvu
kabisa. Nilimsogelea, akanikumbatia kwa nguvu na kunibusu mdomoni, tukio ambalo
Junaitha alilishuhudia ‘laivu’.
“Nakupenda sana, naamini wewe ndiyo
umeyapigania maisha yangu mpaka muda huu,” alisema, nikamuona Junaitha
akimshika mkono bila kusema kitu na kuanza kumvuta kuelekea bafuni.
Mate ya Shenaiza yalikuwa machungu
kuliko klorokwin, nikawa najikaza tu huku nikijitahidi kuachia tabasamu kwenye
uso wangu. Junaitha alimkokota mpaka bafuni na kufunga mlango kwa ndani,
nikabaki nimesimama pale koridoni.
Ghafla nikaanza kusikia sauti ya Firyaal
akilia kama mtu anayekabwa na kitu, nikakurupuka mpaka kwenye kile chumba
walichokuwa wamelala wote, nikafunga breki za ghafla mlangoni, nikiwa siamini
kile nilichokuwa nakiona.
Je, nini kitaendelea? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment