Monday, December 18, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 56


ILIPOISHIA:
“Tunaenda Chunya, hutakiwi kwenda kinyume na maelekezo tunayokupa, ukifanya uzembe tu, kitakachokutokea ni juu yako,” alisema baba kwa sauti ya msisitizo, nikawa natingisha kichwa kukubaliana naye. Tulikaa chini na kuweka kama duara hivi, tukashikana mikono kisha nikaambiwa nifumbe macho.
SASA ENDELEA...
Kweli nilifumba macho, baba na baba yake Rahma wakawa wanazungumza maneno fulani ambayo sikuwa nayaelewa kwa kuyarudiarudia, kisha nikaanza kusikia kama upepo mkali ukianza kuvuma kwa nguvu, sikuelewa tena kilichoendelea mpaka niliposikia baba akinitingisha kwa nguvu.
“Tumeshafika! Fumbua macho,” alisema baba, nikafumbua macho na kujikuta nikiwa kwenye mazingira tofauti kabisa. Sikuelewa tumetumia muda gani maana ninachofahamu mimi kuna umbali mrefu sana kutoka Mbeya mpaka Dar es Salaam, ni safari ya kutoka alfajiri na mapema na kufika usiku.

“Unashangaa nini tumeshafika!” baba alisema huku akinivuta mkono maana kiukweli nilikuwa nimepigwa na butwaa, nikishangaa huku na kule, nikijaribu kukumbuka kama eneo lile nalifahamu.
“Mungu wangu!” nilijisemea moyoni baada ya kugundua kwamba tulikuwa kwenye shule ya msingi niliyosoma pale Chunya, chini ya mti mkubwa uliokuwa nyuma ya shule ambao kwa kipindi kirefu nilikuwa nikisikia watu wakisema kwamba una majini.
“Tumefikaje huku?” niliuliza nikiwa bado nashangaashangaa nikiwa siamini. Yaani nifumbe macho nikiwa kwenye makaburi ya Wagiriki, Kunduchi jijini Dar halafu ninapofumbua macho muda mfupi baadaye, usiku huohuo nijikute nipo Chunya, ilikuwa ni zaidi ya maajabu.
“Huu si muda wa maswali,” baba aliniambia huku akinitaka niongeze mwendo, tukawa tunatembea kuelekea upande wa Magharibi mwa shule, kulipokuwa na njia ya kuingilia na kutokea shuleni hapo.
Baba alikuwa mbele, mimi katikati na nyuma alikuwepo baba yake Rahma, tukawa tunatembea na baadaye tukafika kwenye eneo la uwanja wa shule. Japokuwa ilikuwa ni usiku, uwanja ulionesha kuwa na pilikapilika nyingi sana, watu wengi walikuwa wamekusanyika na kuweka makundi matatu, kundi la kwanza lilikuwa upande wa goli la kwanza, wengine walikuwa katikati ya uwanja na wengine kwenye goli jingine.
Ilionesha kama kuna shughuli fulani zinaendelea ingawa zilionesha kwamba si za kawaida kwa sababu watu wengine walikuwa watupu, wengine walikuwa wakicheza ngoma za kienyeji na wengine walikuwa wamekaa chini.
“Hutakiwi kugeuka nyuma, ni mwiko,” baba aliniambia wakati tukiendelea kuchanja mbuga, tukawa tunapita kwenye njia ambayo wakati nasoma, ndiyo niliyokuwa nikiitumia kwenda na kurudi shule.
Tulipita kwenye vichaka kadhaa na baadaye tukatokezea kwenye nyumba za nyasi zilizokuwa pembezoni mwa kijiji, tukasimama ambapo baba aliniambia kwa sababu mimi ndiye ninayefahamu nyumbani kwa huyo rafiki yangu, Sadoki ambaye ndiye niliyemchagua kumtoa kafara, nitangulie mbele.
Akarudia kunisisitiza kwamba sitakiwi kugeuka nyuma wala kuzungumza hovyo, kazi yangu ni moja tu, kuongoza njia. Nilitii nilichoambiwa huku nikitetemeka sana. Mara kwa mara taswira ya Sadoki ilikuwa ikinijia ndani ya kichwa changu, nikawa najisikia uchungu mno ndani ya roho yangu hasa kutokana na ukweli kwamba yeye ndiye aliyekuwa tegemeo la familia yao.
Niliongoza njia na kwa sababu vichochoro vyote vya Chunya nilikuwa navijua kwa sababu hapo ndipo nilipozaliwa na kukulia, sikupata tabu. Baada ya kutembea kwa dakika kadhaa, hatimaye tuliwasili kwenye nyumba chakavu ya akina Sadoki. Nikaonesha kwa ishara kwamba tayari tumeshafika, baba akanivuka na kutangulia mbele.
Kwa muda wote huo, baba yake Rahma alikuwa kimya kabisa, baba akaanza kutoa maelekezo kwamba tunatakiwa kuizunguka nyumba hiyo mara saba, kutokea upande wa kulia kwenda kushoto. Nilichojifunza, mambo mengi yanayofanywa na watu wa jamii hizi, huwa yanakwenda kinyume na utaratibu wa kawaida, tukaanza kufanya vile baba alivyosema.
Tulikuwa tukipiga hatua fupifupi huku baba na baba Rahma wakiimba nyimbo fulani za kutisha ambazo hata sikuwa nazielewa, tukazunguka mpaka ilipofika raundi ya saba, tukamalizia pale kwenye kona ya nyuma tulipoanzia kuzunguka.
Baba alipiga mguu wa kushoto chini, mara ukuta ukawa kama umefunguka, akatangulia yeye kuingia kinyumenyume, akapotelea ndani.
Tukabaki mimi na baba Rahma, akaniambia na mimi nipige mguu wa kushoto chini kwa nguvu, nikafanya hivyo, ule uwazi ukatokea tena, akanielekeza kuingia kinyumenyume, nikafanya hivyo na kujikuta nipo ndani, pembeni ya baba ambaye alikuwa amesimama akitusubiri.
Mara baba yake Rahma naye akaingia kwa mtindo uleule. Wasichokijua wengi ni kwamba watu wabaya wanapoamua kuingia ndani ya nyumba yako, huwa hawatumii mlango kwa hiyo hata ufunge milango kwa makufuli makubwa, ujenge fensi hata yenye umeme na uweke walinzi wenye silaha nzito, huwezi kuwazuia watu wenye nguvu za giza kuingia ndani kwako.
Maisha waliyokuwa wakiishi akina Sadoki yalikuwa ya chini sana maana hata sebuleni kwao hakukuwa na kitu chochote cha maana zaidi ya viti vya mbao na meza ndogo, na vyombo vya jikoni. Japokuwa nyumba yote ilikuwa giza, cha ajabu ni kwamba nilikuwa na uwezo wa kuona kila kitu, mpaka kijiko.
Tulianza kutafuta chumba anacholala Sadoki na kwa sababu nilishawahi kuwa naingia mpaka chumbani kwake, niliwaongoza, tukaenda mpaka kwenye chumba chake na kumkuta Sadoki akiwa amelala na mdogo wake wa kiume juu ya kitanda cha kamba.
Kwa wale waliowahi kuishi vijijini watakuwa wananielewa vizuri ninapozungumzia kitanda cha kamba. Maskini! Sadoki alikuwa akikoroma pamoja na mdogo wake, wakiwa hawaelewi chochote kinachoendelea.
Baba alinielekeza kukizunguka kitanda hicho na kusimama upande ambao kichwa cha Sadoki kilikuwepo, nikafanya hivyo, baba akasimama upande wa miguuni na baba yake Rahma akasimama pale katikati.
Moyo ulikuwa ukiniuma sana na sikuelewa natakiwa kufanya nini, nikawa nasubiri maelekezo tu, huku moyo wangu ukijihisi kuwa na hatia kubwa mno. Sadoki hakuwa amefanya kosa lolote baya kustahili adhabu kali kiasi kile maana kama ni kupishana maneno, kilikuwa ni kitu cha kawaida kabisa kwa marafiki walioshibana.
Baba alinielekeza kuinamisha kichwa kumuelekea Sadoki pale kitandani, nao wakafanya hivyohivyo kisha baba akaanzisha wimbo ambao mimi sikuwa naujua, baba yake Rahma akawa anaitikia. Niliogopa sana kwa sababu walikuwa wakiimba kwa sauti ya juu ambayo ingeweza kuwaamsha watu waliokuwa ndani ya nyumba hiyo.
Baada ya kuimba mara kadhaa, baba alitoa kichupa kidogo kilichokuwa na ungaunga mweusi ndani, akakitingisha kwa nguvu kisha akampa baba Rahma ili anipe mimi, kikanifikia ambapo alinipa maelekezo kwa ishara kwamba nikitingishe kwa nguvu kisha nichukue ungaunga kidogo na kumpaka Sadoki kwenye paji la uso wake.
Nilifanya kama nilivyoelekezwa, nikampaka kwenye paji la uso kwa kuchora ishara kama ya msalaba hivi, kisha baba akanipa maelekezo kwamba natakiwa kugeuka na kumpa mgongo Sadoki, nikageuka, na wao wakageuka kisha baba akapiga makofi akiashiria tugeuke tena.
Tulipogeuka, nilishtuka sana kumuona Sadoki akiwa amekaa kweye kitanda chake lakini akiwa amefumba macho. Baba akanielekeza kwamba nimshike mkono, kweli nikafanya hivyo, nikamshika, akasimama kisha baba akanionesha ishara kwamba nimuangalie kwa makini anachokifanya.
Alisogea kwenye pembe moja ya chumba na kupiga mguu chini kwa nguvu, ukuta ukafunguka ambapo alitoka nje kinyumenyume, huku nikitetemeka na mimi nikasogea kwenye ile kona huku nikiwa nimemshika Sadoki mikono yake yote miwili. Japokuwa alikuwa amesimama, bado alikuwa amefumba macho.
Nikapiga mguu chini kwa nguvu na kugeuka, nikawa nataka kutoka lakini nilishangaa mwili wangu ukiwa mzito kama ninayevutwa na kitu kurudi ndani. Sijui nini kilitokea kwani nilishtukia baba Rahma ameyeyuka, nikabaki mimi na Sadoki, nikapiga tena mguu kwa nguvu na kutaka kutoka lakini safari hii, ukuta haukufunguka kabisa, kijasho chembamba kikaanza kunitoka.
Nikiwa bado nashangaa nikiwa sijui nini cha kufanya, Sadoki alifumbua macho, tukawa tunatazama ana kwa ana. Ni kama fahamu zake zilikuwa zimemrejea kwani alishtuka sana kuniona ndani ya chumba chake, akageuka huku na kule huku akijaribu kujitoa kwenye mikono yangu kwa hofu kubwa.
“Togoo! Umeingiaje humu?” aliniuliza kwa sauti ya juu, nikasikia mlango wa chumba cha pili ukifunguliwa kuashiria kwamba kuna mtu alikuwa amesikia na sasa anatoka.
“Nimekwisha!” nilijisema huku nikigeuka huku na kule, sikumuona baba wala baba yale Rahma, Sadoki akanibadilikia na kunishika kwa nguvu ii nisipate nafasi ya kukimbia.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...