Thursday, October 26, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 49


ILIPOISHIA:
Nilipofika, na mimi nilijifanya ni mwombolezaji wa kawaida tu, nikawasalimia baadhi ya watu kisha nikajichanganya na waombolezaji wengine. Ghafla nilishtuka baada ya kuona kitu ambacho sikukitarajia, nikahisi kijasho chembamba kikianza kunitoka, mara hirizi yangu ikaanza kunibana kwa nguvu, kufumba na kufumbua kamba yake ikakatika, ikadondoka chini!
SASA ENDELEA...
“Mungu wangu!” nilijikuta nimetamka kwa sauti, hali iliyofanya watu wote washtuke, hata wale ambao hawakuwa wameniona nikiwasili eneo hilo, waligeuka na kunitazama, nikajihisi mwili ukiishiwa nguvu na kunyong’onyea kama nimepigwa na shoti ya umeme.
Sikujua nifanye nini kwa wakati huo, watu wakawa bado wamenikazia macho, kila mtu akiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua mimi ni nani na nini kimetokea mpaka nikashtuka kiasi hicho.
“Wasalimu watu wote kwa heshima kisha wape pole,” nilisikia sauti ya baba masikioni mwangu, ghafla nikajikuta nimepata nguvu na kuwa na imani kubwa kwamba hata iweje, baba ameshajua kinachoendelea kwa hiyo atanisaidia.

“Shikamooni jamani na poleni sana kwa msiba!” nilizungumza kwa kujitutumua huku sauti yangu ikiwa bado na dalili za kutetemeka. Wengine walijibu salamu yangu na wengine walikaa kimya lakini kwa kiasi kikubwa, kitendo cha mimi kuwasalimu, kiliwafanya wengi wanione kama muombolezaji wa kawaida.
Wengine waliendela na mazungumzo yao na wachache walibaki wakinitazama, nikawa natafuta ‘taiming’ ya kuiokota ile hirizi. Kwa harakaharaka niligundua kwamba kulikuwa na zaidi ya watu saba waliokuwa bado wamenikazia macho, nikawa najaribu kuzuga, sikutaka kutazamana na mtu yeyote usoni kwa sababu nilihisi ile hatia niliyokuwa nayo isingeweza kufichika.
Kwa bahati nzuri, nikiwa bado nazugazuga pale nikitafuta namna ya kuiokota ile hirizi pale chini, kulisikika sauti za wanawake wakilia kwa nguvu mara tu baada ya kushuka kwenye gari kwani msiba haukuwa mbali na barabara kuu ya lami ya kuelekea Morogoro.
Watu karibu wote waligeukia kule vile vilio vilikokuwa vinatokea, nikaona huo ndiyo muda pekee wa kufanya kile nilichokusudia. Kwa kasi kubwa niliinama na kuikwapua ile hirizi pale chini kisha nikaisokomeza kwenye mfuko wa suruali. Wakati nikiamini kwamba hakuna mtu aliyeniona, nilishtuka kugundua kwamba wale watu niliokuwa nahisi kwamba wananitazama, wala hawakujishughulisha kuwatazama wale watu waliokuwa wakilia, kumbe bado walikuwa wamenikazia macho na kitendo cha kuikota ile hirizi pale chini, walikishuhudia live bila chenga, kwa mara nyingine nikajikuta nikiishiwa nguvu.
Japokuwa ilikuwa ni asubuhi, nilihisi nikilowa kwapani kwa kijasho chembamba.
“Usipokuwa makini utakiona cha mtema kuni leo, nani aliyekutuma kwenda msibani? Ni mwiko kabisa kwa sheria zetu, bora hata ungeenda makaburini,” sauti ya baba ilisikika tena masikioni mwangu na kuzidi kunipa hofu kubwa ndani ya moyo wangu.
Niligeuka huku na kule, nikagundua kwamba kumbe kulikuwa na watu wengine nyuma yangu waliokuwa bado wakinitazama, nikazidi kuingiwa na hofu. Sikuwa najua natakiwa kufanya nini, nikaamua kuchukua maamuzi magumu.
Kwenye moja kati ya maturubai yaliyokuwa yakiendelea kufungwa, kulikuwa na mshumaa wa rangi ya zambarau ambao tayari ulishawashwa na pembeni yake, kulikuwa na picha kubwa iliyowekwa kwenye fremu ya kioo, sambamba na daftari na kibakuli kilichokuwa na fedha.
Bado watu wengi walikuwa wanawatazama wale waombolezaji waliokuwa wakiendelea kulia kwa uchungu huku wakisaidiwa na wenyeji wao kupelekwa pale msibani, nikatembea kwa hatua za kusuasua mpaka pale kwenye ile picha ya marehemu, nikaitazama.
Kiukweli hakuna siku ambayo nimewahi kujihisi kuwa na hatia kubwa ndani ya moyo wangu kama siku hiyo. Maskini ya Mungu, bado alikuwa binti mdogo kabisa na kwenye picha hiyo alikuwa ameachia tabasamu pana, akionesha kuwa na matumaini mwengi kwenye maisha yake ya baadaye.
Nilijisikia vibaya sana kushiriki kuyakatisha maisha ya msichana yule mdogo asiye na hatia, nikashindwa kujizuia, machozi yakanitoka kwa wingi na kulowanisha uso wangu.
Sikukumbuka tena kama kuna watu walikuwa wakinifuatilia hatua kwa hatua, kwa uchungu niliokuwa nao, niligeuka haraka na kutafuta sehemu ya kujificha kwa sababu huwa sipendi kabisa mtu yeyote ayaone machozi yangu. Kwa kutumia viganja vya mikono yangu nilijiziba usoni, nikasogea mbali kabisa na wale waombolezaji wengine, nikasimama chini ya mwembe uliokuwa jirani, donge kubwa likiwa limeniganda kooni.
“Kijana, wewe ni nani na hapa umefuata nini?” sauti nzito ya mwanaume nisiyemjua ndiyo iliyonizindua kutoka kwenye hali ile, harakaharaka nikajifuta machozi na kugeuka kumtazama.
Alikuwa ni mwanaume wa makamo, mweusi tii, akiwa na macho mekundu sana, huku mishipa mingi ikiwa imesimama kwenye kichwa chake. Kabla ya kumjibu, haraka sana nilimtazama kwenye mikono yake. Cha ajabu, nilimuona akiwa ameweka ile ishara kama ambayo baba alinifundisha, alikuwa ameziba kucha ya kidole chake kidogo kwa dole gumba.
Alipoona nimekazia macho kwenye mkono wake, aliuficha kwa nyuma kisha akarudia tena kuniuliza swali lake.
“Usimjibu chochote, mkazie macho usoni,” nilisikia sauti ya baba, nikafanya kama alivyoniambia. Japokuwa alikuwa na sura ngumu, nilijikakamua kisabuni nakumkazia macho usoni, akashtuka kuona namtazama machoni.
Cha kushangaza, na yeye aliponikazia macho kwa sekunde kadhaa na kurudia tena kuniuliza swali lile, alipoona bado nimekomaa kumtazama machoni, aliachia vile vidole vyake alivyokuwa amevibana, akawa ni kama anababaika machoni maana hakuweza tena kunitazama machoni.
“Usifikiri watu wote hapa ni wajinga, kwa usalama wako ondoka haraka,” alisema kwa sauti ya kukwamakwama lakini sikumjibu chochote zaidi ya kuendelea kumkazia macho, nikamuona akiufyata mkia na kugeuka, akatembea harakaharaka na kwenda kujichanganya na wenzake.
Nikiwa bado namtazama, alipokaa tu niliona wazee wengine kadhaa ambao walikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakinitazama kwa macho ya ukali wakimfuata pale alipokuwa amekaa, wakawa wanazungumza kisha nikaona wote wamegeuka na kunitazama.
“Iweke hiyo hirizi chini ya ulimi na kimbia haraka uwezavyo kuondoka eneo hilo kabla hawajakufikia,” sauti ya baba ilisikika tena masikioni mwangu. Harakahara nikaingiza mkono mfukoni na kuitoa ile hirizi, japokuwa ilikuwa kubwa niliingiza mdomoni na kuibana chini ya ulimi.
Kabla hata sijamaliza kufanya kitendo hicho, nilishtukia lile kundi la wale wazee likija kwa kasi pale chini ya mwembe, nikageuka haraka na kuanza kutimua mbio, sikuwa naijua mitaa ya Mlandizi lakini kwa jinsi baba alivyoongea kwa msisitizo na hali halisi ilivyokuwa, nilijua nikilemaa, kweli nitaadhirika.
Kila mtu alibaki amepigwa na butwaa pale msibani maana ilikuwa ni zaidi ya kituko, nilitimua mbio ambazo sikumbuki kama nimewahi kukimbia maishani mwangu, nikawa nakatiza mitaani huku watu wengine wakishtuka wakidhani labda nilikuwa mwizi, kwa nyuma nikawa nasikia kelele kwa wingi kuonesha kwamba wale watu walikuwa wameniungia tela.
Sikujua nini kitanipata endapo watanitia mikononi na kugundua kwamba mimi ndiye niliyesababisha kifo cha yule mtoto huku mama yake akiwa mahututi, na kusababisha watui wote wawe na huzuni kiasi kile.
Sijisifii lakini ukweli ni kwamba katika suala la mbio, nilikuwa na uwezo mkubwa sana, dakika chache baadaye nikawa nimeshatokomea kwenye mashamba ya mikorosho na minazi, kelele za wale watu waliokuwa wakinifukuza zikiwa bado zinaendelea kusikika, sauti ya baba ikasikika tena masikioni mwangu lakini safari hii, ilikuwa na maelezo ambayo yalinimaliza kabisa nguvu, nikajua mwisho wangu umewadia. Niliujutia sana uamuzi wangu wa kujipeleka mwenyewe kwenye mdomo wa mamba.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Championi Jumatatu.



1 comment:

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...