Tuesday, July 25, 2017

Graves of the Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 7


ILIPOISHIA:
WALE wageni waliaga na kuondoka, baba akatuita tena ndani na kuanza kuhesabu fedha zilizopatikana. Zilikuwa ni shilingi milioni mbili na laki tatu, akasema zingetosha kabisa kwa safari yetu. Tukakubaliana kwamba tumalizie maandalizi na asubuhi ya siku ya pili tuianze safari ya kuelekea jijini Dar es Salaam.
SASA ENDELEA...
KWELI usiku huo hakuna hata aliyepata lepe la usingizi, ‘kimuhemuhe’ cha safari kilitufanya tukae macho mpaka jogoo la kwanza lilipokuwa linawika. Baba alituagiza kwamba tubebe vile vitu vya muhimu tu kwa sababu maisha ya kijijini yalikuwa tofauti sana na maisha ya mjini.
Akatuambia vitu vingine tuviache palepale na vitakuwa salama kwa sababu kuna walinzi anawaacha kwa ajili ya kutulindia mji wetu. Aliposema walinzi sikumuelewa kwa haraka anamaanisha nini, akili nyingine zikanituma kuamini kwamba labda watakuwa ni mgambo lakini nilijiuliza anaweza kuwaacha mgambo ndiyo walinde nyumba yetu wakati hawakuwa wakielewana? Sikupata majibu.
Saa kumi na nusu za usiku, tulitoka na kuanza kutembea kuelekea stendi, kila mmoja akiwa na mzigo wake. Tukaenda mpaka stendi ambapo tulipanda gari la kwanza kabisa ambalo lilikuwa likielekea Mbeya mjini, lakini cha ajabu, wakati wote tumeshapanda kwenye gari, baba yeye alibaki chini.

Graves of The Innocents (Makaburi Yasiyo na Hatia)- 6


ILIPOISHIA:
Huku nikitetemeka, nilisogea mpaka pale yule mganga alipokuwa amelala, akiendelea kukoroma kwa nguvu, mimi nikamshika miguuni na baba akamshika kichwani, tukaanza kumkokota kumtoa nje ya eneo letu, tukaenda kumbwaga pembeni kabisa kwenye vichaka kisha tukarudi ndani. Ile tunaingia ndani tu, tukasikia mlango ukigongwa kwa nguvu.
SASA ENDELEA...
“Nani!”
“Fungua!”
“Sifungui mpaka mjitambulishe na mueleze shida yenu.”
“Ni mimi mzee Sifuni, mwenyekiti wa kijiji.”
“Unaonekana hauko peke yako!”
“Ndiyo, nimeongozana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya kijiji, fungua tafadhali,” baada ya mwenyekiti huyo kusema hivyo, baba alinioneshea ishara kwa mkono kwamba niende ndani kwa sababu alishahisi wale watu wamekuja kwa shari. Nikatii nilichoambiwa na kwenda chumbani lakini bado nilikuwa na shauku kubwa ya kutaka kuona kinachoendelea.
Baba alipofungua tu mlango, nilisikia wakimuamrisha jambo:
“Upo chini ya ulinzi.”
“Kwa kosa gani?”
“Kwa kumshambulia mganga wa kienyeji aliyekuwa anatimiza majukumu yake hapa kijijini kwetu.”

Monday, July 24, 2017

Seven Days In Hell (Siku Saba Kuzimu)- 6


ILIPOISHIA:
Mara simu yake ilianza kuita mfululizo, akaishika na kutazama namba ya mpigaji lakini katika hali ambayo sikuielewa, aliiachia simu hiyo, ikadondoka chini na kufunguka betri ikaangukia kivyake, mfuniko kivyake na simu nayo kivyake. Akaanza kuangua kilio kwa uchungu huku akiniomba nimsaidie, nilibaki nimepigwa na butwaa.
SASA ENDELEA…
“Nikusaidie nini Shenaiza?” nilimuuliza huku nikiiokota ile simu na kuiunganisha upya.
“Nakuomba usiniache, fanya kila kinachowezekana unitoroshe hapa hospitalini usiku huuhuu, watakuja kunimalizia,” alisema msichana huyo na kuzidi kunichanganya.
“Watakuja kukumalizia? Akina nani? Na Kwa nini tutoroke wakati hali yako bado siyo nzuri?”
“Naomba ufanye nilichokuomba mengine utaenda kuyajua mbele ya safari,” alisema msichana huyo huku akiendelea kulia.
Nikiwa bado nimeduwaa, nikiwa sijui cha kufanya, nilishtuka kumuona akichomoa sindano ya dripu aliyokuwa amechomwa mkononi mwake na kusababisha damu zianze kumtoka mkononi, akajikongoja huku akionesha kuwa na maumivu makali, akanitaka nimpe bega langu ili apate balansi ya kutembea.
Sikuwa na cha kufanya zaidi ya kukubaliana na matakwa yake, japokuwa nilikuwa najua kwamba ninachokifanya ni hatari sana lakini sikuwa na namna zaidi ya kumsaidia msichana huyo ingawa mpaka muda huo sikuwa najua nini kinachomsumbua.

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 5


ILIPOSHIA:
Aliniambia Shenaiza amerejewa na fahamu na jambo la kwanza alilouliza ni kama nilikuwa nimempigia simu.
“Nimemwambia kwamba upo hapa nje, akaniomba sana akuone, lakini anazungumza kwa shida sana,” alisema nesi huyo, nikainuka na kuanza kumfuata harakaharaka kuelekea wodini.
SASA ENDELEA…
Muda mfupi baadaye, tulikuwa pembeni ya kitanda alichokuwa amelazwa msichana huyo, nesi Rozina akaniambia ananipa dakika chache za kuzungumza na mgonjwa, akatoka na kufunga mlango wa wodi hiyo. Kwa muda wote huo, macho yangu yalikuwa juu ya uso wa msichana huyo ambaye naye alikuwa akinitazama, tukawa tunatazamana.
Tofauti na nilivyofika mara ya kwanza hospitalini hapo, safari hii niliweza kumuona vizuri msichana huyo. Kitu ambacho naomba nikiseme wazi, japokuwa alikuwa kwenye maumivu makali, akiwa amefungwa bandeji kubwa kichwani na jicho lake moja likiwa limevilia damu na kuwa jekundu, Shenaiza alikuwa na sura nzuri mno.

Thursday, July 20, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 4


ILIPOISHIA:
Niliondoka kazini nikiwa ni kama nimechanganyikiwa, sikuwa namjua Shenaiza lakini sijui kwa nini nilihisi kama matatizo yake yalikuwa yakinihusu sana. Nikiwa kwenye kituo cha daladala nikiendelea kusubiri usafiri, ujumbe mfupi uliingia kwenye simu yangu, ulisomeka:
“Mwenye simu hii amelazwa Hospitali ya Amana, Ilala. Hali yake ni mbaya, hawezi kuzungumza.”
SASA ENDELEA…
“Mungu wangu,” nilisema baada ya kumaliza kuusoma ujumbe huo. Nilijaribu kuipiga tena namba hiyo, ikapokelewa lakini sauti haikuwa ya Shenaiza, akaniambia yeye ni Rozina, nesi katika hospitali ya Amana na kwamba yeye ndiye aliyekuwa akimhudumia msichana huyo.
Nilimuomba anitajie wodi aliyolazwa msichana huyo, akaniambia niende tu nikifika hospitalini hapo nipige kupitia namba hiyohiyo atakuja kunipokea. Niliita bodaboda na kumuelekeza kukimbia kadiri awezavyo kuelekea Amana. Abiria wengine waliokuwa pale kituoni wakisubiri daladala, walibaki kunishangaa lakini mwenyewe sikujali.
Nikaondoka na bodaboda huku nikimhimiza kuongeza mwendo ili tuwahi kufika. Baada ya kuhangaika sana kwenye foleni, kama ujuavyo Jiji la Dar es Salaam nyakati za jioni, hatimaye tuliwasili Amana. Nikapiga namba ya Shenaiza ambapo yule nesi alipokea tena, nikamweleza kwamba tayari nilikuwa nimefika, akaniambia nimsubiri mapokezi.

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 3


ILIPOISHIA:
NILISHANGAA kugundua kwamba ukiachilia mbali meseji mbili za rafiki zangu, Justice na Prosper, nyingine zote zilikuwa zimetoka kwa yule msichana aliyekosea namba ya simu, nikashusha pumzi ndefu na kuanza kuzisoma, moja baada ya nyingine nikiwa na shauku kubwa ya kutaka kuona ameandika nini.
SASA ENDELEA…
YA kwanza ilisomeka: “Samahani kaka Jamal naomba tuchati kama hutajali.” Nikaisoma na kuirudia zaidi ya mara mbili, sikuelewa maana ya yeye kuomba tuchati ni nini kwa sababu tayari nilishamwambia amekosea namba na mwenyewe akakiri hilo.
Hakuishia hapo, meseji nyingine ikasomeka: “Nina tatizo kubwa nilikuwa nahitaji mtu wa kumshirikisha ndiyo maana nikawa nimempigia simu ndugu yangu mmoja aitwaye Moses lakini baada ya kusikia sauti yako, naamini na wewe unaweza kuwa na busara na kunisaidia nini cha kufanya.”

Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na hatia) - 5


ILIPOISHIA:
MWANAUME mzee mwenye macho mekundu sana na midomo myeusi, akiwa amejifunga shuka refu lenye rangi nyekundu na nyeusi, kichwani akiwa amejifunga kitambaa cheusi, shingoni akiwa na hirizi kadhaa na shanga, alisimama na kunyoosha juu mkia wa mnyama ambaye sikuwa namjua, watu wote wakashangilia kwa nguvu.
SASA ENDELEA...
“Sina mengi ya kuzungumza, naomba ushirikiano wenu tuwakomeshe wachawi wa kijiji hiki,” alisema mwanaume huyo kwa Kiswahili kibovu, watu wakashangilia tena kwa nguvu kisha Mwene akaendelea na maelezo, akisisitiza kwamba kazi lazima ianze siku hiyohiyo usiku.
Baada ya maelezo marefu yaliyojaa vitisho kwa watu waliokuwa wakitajwa kuhusika na uchawi, mkutano uliahirishwa, watu wakatawanyika huku kiongozi huyo wa kijiji akiwataka watu wote kutoa ushirikiano kwa mganga Mabwanji atakapoenda kuwatembelea kwenye nyumba zao.
Hofu niliyokuwa nayo ilikuwa kubwa mno, kwa jinsi watu walivyokuwa wanatuchukia pale kijijini nilijua lazima moto utawaka. Baadhi ya wazee waliokuwa wanaheshimika pale kijijini, walianza maandalizi ya kumsaidia mganga huyo kwa kila alichokuwa anakihitaji, dawa zikaandaliwa na hatimaye muda uliokuwa ukisubiriwa na wengi ukawadia.

Makaburi ya Wasio na Hatia (The Graves of the Innocents)- 4


ILIPOISHIA:
“Naongea na wewe Togolai, ni kweli nini?” alihoji tena Madam Timbuka, safari hii akiwa amenikaribia kabisa pale nilipokuwa nimekaa, nikaanza kubabaika huku hofu kubwa ikishindwa kujificha kwenye uso wangu.
SASA ENDELEA...
“Kwamba mwalimu wetu anaumwa. Nilisikia asubuhi nikawa siamini,” nilidanganya, nikamuona mwalimu Timbuka akishusha pumzi ndefu, wanafunzi wenzangu waliokuwa wakinitazama kwa shauku, nao walionesha kuridhika na majibu yangu.
Baada ya kutoa taarifa hizo, mwalimu Timbuka alitutaka tusipige kelele bali tuutumie muda huo kujisomea, akatoka na kutuacha wote tukiwa kimya. Moyoni mwangu niliendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.
“Kwa hiyo mwalimu Mwashambwa naye atakufa?” nilijiuliza moyoni wakati nikiendelea kutafakari taarifa za ugonjwa wa mwalimu wetu. Nilijaribu kuunganisha matukio, hofu ikazidi kuongezeka ndani ya moyo wangu. Bado sikutaka kuamini kwamba baba alikuwa mchawi na alikuwa akihusika na kilichokuwa kinaendelea.
Muda ulizidi kusonga mbele, hatimaye ukawadia muda wa mapumziko. Kwa kawaida, ilikuwa ikifika muda wa mapumziko, kengele inagongwa mara mbili kuashiria wanafunzi wote tutoke madarasani lakini siku hiyo, kengele iligongwa tofauti. Iligongwa mfululizo huku walimu wakiwa wameshatoka na kusimama mstarini, kila mmoja akionekana kuwa ‘siriasi’.

Wednesday, July 19, 2017

MAKABURI YA WASIO NA HATIA (GRAVES OF THE INNOCENTS)- 3


ILIPOISHIA:
Nikamuongoza baba mpaka kwenye kaburi la Alfred ambalo juu yake kulikuwa na msalaba ulioandikwa jina lake kamili, tarehe ya kuzaliwa na tarehe ya kufa kwake. Akaniambia niwe makini kwa kila atakachokuwa anakifanya, nikatingisha kichwa huku hofu kubwa ikiwa imetanda ndani ya moyo wangu kwani kiukweli nilikuwa nikiogopa sana makaburi na maiti.
SASA ENDELEA:
Baba alianza kufukuafukua ule upande wa kichwani kwenye lile kaburim akaingiza mkono mfukoni na kutoa kichupa kilichokuwa na ungaunga mweusi, akaumwaga kuanzia upande wa kichwani mpaka miguuni, kisha akaniambia tuanze kulizunguka lile kaburi kwa kuanzia kushoto kwenda kulia.
Alianza yeye, na mimi nikafuatia, tukawa tunazunguka lakini kwa kutembea kinyumenyume, baada ya kuzunguka raundi sana, nilianza kusikia kizunguzungu kikali, baba akaniambia nikae, yeye akarudi kusimama palepale alipokuwa amesimama.
“Hebu muite jina lake mara tatu kwa sauti kubwa,” alisema baba, nikawa simuelewi anamaanisha nini. Yaani mtu alishakufa siku nyingi zilizopita halafu ananiambia nimuite jina lake, tangu lini maiti ikaitika? Hata hivyo, ilibidi tu nitii kile alichoniambia, nikamuita.
Nililitaja jina lake kwa mara ya kwanza, baba akawa ananionesha ishara kwamba niongeze sauti, nikamuita kwa mara ya pili kisha kwa mara ya tatu. Cha ajabu kabisa, nilisikia akiitikia, tena niliweza kuthibitisha kabisa kwamba ni yeye kwa sababu nilikuwa naijua sauti yake na hata akizungumza neno moja tu, nakuwa nimeshamtambua.

Nilitetemeka kuliko kawaida, nikawa nageuka huku na kule kwa sababu alivyoitikia, ilionesha kwamba hayupo pale kwenye kaburi bali yupo umbali wa mita kadhaa pembeni. Nikiwa bado siamini, baba alinionesha kwa kidole, akaniambia nitazame chini ya mti mkubwa wa mjohoro uliokuwa pembeni kidogo ya makaburi.

Tuesday, July 18, 2017

MAKABURI YA WASIO NA HATIA (GRAVES OF THE INNOCENTS)- 2


ILIPOISHIA:
Tulipokaribia nyumbani kwa mzee huyo, baba alinionesha ishara kwamba nisimame, nikafanya hivyo, tukawa tunasikia sauti za watu wengi wakilia kutoka nyumbani kwa mzee huyo, baba akanionesha ishara kama anayesema ‘unaona?’, nikashika mdomo kwa mshangao. Sikutaka kuamini kwamba kweli mzee Mwankuga alikuwa amefariki dunia.
SASA ENDELEA...
Nilijikuta nikishusha lile furushi la dawa na panga, nikawa nataka niende kushuhudia mwenyewe kama ni kweli lakini baba aliniambia nisithubutu kufanya hivyo, hasa kutokana na uhasama uliokuwepo kati yetu na familia hiyo. Bado niliendelea kuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kama ni kweli yule mzee amekufa.
Ilibidi baba anishike mkono, tukaenda mpaka nyumbani ambapo baba aliingia kwenye chumba chake cha uganga na kuanza kuchambua zile dawa tulizotoka nazo porini. Ni kama alijua kwamba nitamtoroka na kurudi kule msibani kwenda kushuhudia kilichotokea kwani aliniambia nikae palepale, nimuangalie jinsi alivyokuwa akichambua dawa.
Kweli nilitii maagizo yake, nikakaa pale lakini bado nilikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kilichoendelea. Nilipomuona baba amezama kwenye kazi yake hiyo, niliinuka na kuanza kuelekea mlangoni, akaniwahi na kuniuliza ninakokwenda.

“Naenda kujisaidia baba,” nilimdanganya baba, akanitazama usoni kisha akaendelea na kazi yake. Nilitoka na kwenda chooni ambako nako nilizunguka nyuma, nikatokomea huko na kwenda kutokea upande wa pili, nyumbani kwa mzee Mwankuga.

MAKABURI YA WASIO NA HATIA (GRAVES OF THE INNOCENTS)- 1


JINA langu naitwa Togolai Mahimba, ni mtoto wa mwisho kati ya watoto saba wa baba yetu, Sinai Mahimba ambaye kwa sasa ni marehemu. Baba yetu alifariki miaka mitatu iliyopita baada ya kuugua ghafla.
Kifo chake kilitawaliwa na utata mkubwa na hata siku ya mazishi yake, kulitokea mambo mengi ya ajabu ambayo mpaka leo siwezi kuyaeleza. Ninayo mambo mengi ambayo ningependa kukusimulia ndugu msomaji lakini kwa kuanzia, naomba nikueleze mambo machache yaliyotokea kabla ya kifo cha baba yetu ambaye mimi ndiye nilikuwa mtoto anayenipenda zaidi.
Kabla hajafikwa na mauti, baba yetu alikuwa mtu maarufu sana kijijini kwetu, Makongorosi, Chunya mkoani Mbeya tulikokuwa tukiishi. Kilichofanya awe maarufu kiasi hicho, ni kazi yake ya uganga aliyokuwa anaifanya ambapo mbali na mambo mengine, alikuwa akiwafanyia matambiko wachimbaji wengi wa dhahabu ili wakiingia mgodini, wapate dhahabu kwa urahisi sambamba na wafanyabiashara wengine.

Umaarufu wa baba ulisababisha hata sisi watoto wake tuwe maarufu sana, hasa mimi ambaye muda mwingi nilikuwa nikiongozana naye kila alikokuwa anakwenda, kuanzia kwenye matambiko maporini, kwenye mazindiko migodini, kuchimba dawa msituni mpaka kilingeni kwake alikokuwa akifanyia shughuli zake za uganga.

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...