ILIPOISHIA:
“Ndiyo, lakini mambo yenyewe ndiyo kama
hivi, hatupati hata dakika chache za kuwa pamoja, mi nimechoka bwana,” alisema
Shamila na kunisogelea mwilini, nikawa naiona hatari iliyokuwa mbele yetu
endapo Junaitha atageuka na kugundua kwamba tulibaki koridoni tumesimama, tena
tukiwa tumesogeleana mithili ya majogoo yanayotaka kupigana.
SASA ENDELEA...
“Please Shamila, huu siyo muda muafaka,
kama inawezekana tutafute muda baadaye,” nilisema kwa sauti ya chini, akashusha
pumzi ndefu na kunitazama usoni kwa macho yake mazuri, tukaendelea kutembea
lakini alionesha kweli amemaanisha kile alichokisema.
Tuliingia kwenye kile chumba ambacho
tulikuwa tukikutania kila panapokuwa na shughuli maalum, Junaitha akatuelekeza
kukaa kwa duara kama ilivyokuwa kawaida yetu kisha akatuambia wote tuanze
kuvuta hewa kwa wingi kwa kutumia pua na kuitoa kwa kutumia mdomo.
“Inatakiwa wote tufumbe macho na
tuendelee kupumua taratibu, vuta pumzi ndefu kwa kutumia tumbo na sio kifua,
unajua kuna watu wengi wanaishi lakini hawajui hata namna ya kupumua, badala
yake wao wanahema,” alisema Junaitha na kuanza kutufafanulia kile alichokisema.