ILIPOISHIA:
Nilipofika, na mimi nilijifanya ni
mwombolezaji wa kawaida tu, nikawasalimia baadhi ya watu kisha nikajichanganya
na waombolezaji wengine. Ghafla nilishtuka baada ya kuona kitu ambacho
sikukitarajia, nikahisi kijasho chembamba kikianza kunitoka, mara hirizi yangu
ikaanza kunibana kwa nguvu, kufumba na kufumbua kamba yake ikakatika,
ikadondoka chini!
SASA ENDELEA...
“Mungu wangu!” nilijikuta nimetamka kwa
sauti, hali iliyofanya watu wote washtuke, hata wale ambao hawakuwa wameniona
nikiwasili eneo hilo, waligeuka na kunitazama, nikajihisi mwili ukiishiwa nguvu
na kunyong’onyea kama nimepigwa na shoti ya umeme.
Sikujua nifanye nini kwa wakati huo,
watu wakawa bado wamenikazia macho, kila mtu akiwa na shauku kubwa ya kutaka
kujua mimi ni nani na nini kimetokea mpaka nikashtuka kiasi hicho.
“Wasalimu watu wote kwa heshima kisha
wape pole,” nilisikia sauti ya baba masikioni mwangu, ghafla nikajikuta
nimepata nguvu na kuwa na imani kubwa kwamba hata iweje, baba ameshajua
kinachoendelea kwa hiyo atanisaidia.