NILIJIUNGA NA DINI YA SHETANI- 1

Jina langu naitwa Mkanwa Sebastian au Saba kama wengi walivyozoea kuniita, mkazi wa Itete, Tukuyu wilayani Rungwe, Mbeya. Baba yangu mzazi, Sebastian Mwambenja alikuwa ni mchungaji wa Kanisa la Wokovu lililokuwa kwenye kijiji nilichozaliwa huku mama yangu akiwa ni muuguzi katika Zahanati ya Lufingo iliyokuwa kijiji cha pili kutoka pale tulipokuwa tunaishi.


Mimi nilikuwa ni mtoto wa mwisho kuzaliwa katika familia yetu iliyokuwa na watoto saba. Baba yangu alikuwa akitokea kwenye ukoo wa kichifu wa Mzee Mwambenja ingawa baada ya babu yetu kufariki, aliamua kuokoka na ndipo alipoupata uchungaji wa kanisa hilo.

Tangu nikiwa mdogo, wazazi wangu walinilea katika misingi ya kumuabudu na kumtukuza Mungu huku mara kwa mara wakinieleza kuwa Yesu alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi zangu. Kila Jumapili nilikuwa nikiongozana na wazazi wangu kuelekea kanisani na baba alikuwa akitaka nikae mbele kabisa, jirani na madhabahu ambayo alikuwa akiyatumia kutangazia Injili na kuhubiri Neno la Mungu.

Mara kwa mara alikuwa akiniambia kuwa imani ndiyokitu pekee kinachoweza kumkomboa mwanadamu kutoka kwenye kifungo cha mateso ya dunia.
Watu wengi walikuwa wakimheshimu sana baba, kila alipokuwa anapita alikuwa akiitwa baba mchungaji, mama yeye akawa anaitwa mama mchungaji huku mimi nikiitwa mtoto wa mchungaji.

Nakumbuka wakati baba anaanza kushika cheo cha mchungaji, nilikuwa na umri wa kati ya miaka sita au saba. Katika siku za mwanzo, hakuwa na uwezo wowote wa kufanya miujiza na kanisa lake halikuwa na waumini wengi zaidi ya ndugu zetu wa karibu na majirani ambao walikuwa wakijumuika nasi kila muda wa ibada ulipofika.

Mimi kazi yangu ilikuwa ni kumbebea baba Biblia, sadaka na vifaa vingine vilivyokuwa vinatumika kwenye sala na wakati mwingine nilikuwa nikibeba zawadi ndogondogo alizokuwa anapewa na waumini wake.

Kwa kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele na mimi kuwa mkubwa, baba alianza kubadilika kwa vitu vingi, nilianza kumshuhudia akiwa na uwezo wa kufanya miujiza na mambo ambayo katika hali ya kawaida ni vigumu kuyaelezea. Kila Jumapili, alikuwa akifanya miujiza ya kuwaponya watu wenye matatizo mbalimbali yakiwemo magonjwa sugu, kuwaombea watu wenye shida mbalimbali na kutoa huduma ya kiroho.

Kila nilipokuwa nikimuuliza anapata wapi nguvu za kufanya miujiza kama ile ambayo awali nilizoea kuiangalia kwenye mkanda wa video wa Yesu, aliniambia kuwa alikuwa amefikia hatua ya ukomavu wa kiimani na ndiyo maana alikuwa na uwezo wa kufanya chochote na kikatokea kweli kama alivyotaka.

“Sasa baba, kama una uwezo wa kufanya chochote, kwa nini usiombee familia yetu tukawa matajiri na kumiliki mashamba makubwa ya migomba na magari ya kusafirishia mizigo kama baba yake Angenile?” nilimuuliza siku moja, akanitazama usoni kisha akanijibu kuwa umri wangu ulikuwa mdogo kuuliza maswali kama yale, akaniambia nikikua nitayaona mwenyewe.

Sikuridhika na majibu yake, nikaona njia pekee inayoweza kuniridhisha nafsi yangu ni kuutafuta ukweli mimi mwenyewe. Siku ziliendelea kusonga mbele, kanisa la baba likawa linazidi kuwa maarufu pale kijijini, vijiji vya jirani na wilaya nzima ya Rungwe.

Ilifika mahali watukutoka Tukuyu Mjini, Ushirika, Katumba, Kiwira na sehemu nyingine wakawa wanakuja kijijini kwetu na kujaa kwenyekanisa la baba. Kwa kuwa awali kanisa lilikuwa dogo na lisilo na ubora wowote, baada ya waumini kuanza kuongezeka, nilimsikia baba akijadiliana na watu fulani kwenye simu, akawaomba wamjengee kanisa kubwa na la kisasa.

Baadaye baba aliniambia kuwa wale ni Wamisionari waliokuwa wanaishi Ulaya ambao alifahamiana nao katikakazi yake ya kutangaza injili.

Siku iliyofuatia, tukamtafuta mpiga picha ambaye alilipiga picha lile kanisa la zamani na maeneo ya kuzunguka eneo hilo, tukasafairi na baba hadi Tukuyu mjini ambapo nilimsaidia kuzituma zile picha kwa njia ya mtandao kwenda kwa Wamisionari hao wa nchini Denmark.

Wiki kadhaa baadaye, wale wamisionari walimpigia simu baba na kumweleza kuwa fedha zilikuwa tayari, tukaenda tena mjini kufungua akaunti benki kisha tukasubiri baada ya siku tatu, fedha nyingi zikaingia kwenyeakaunti hiyo.
Baada ya hapo, baba alisaidiana na wazee wa kanisa pamoja na wauminji wengine kupanga namna kanisa jipya litakavyokuwa.

Baada ya mipango kukamilika, kanisa zuri la kisasa lilijengwa pembeni kidogo ya lile la zamani. Watu wengi wakavutiwa nalo, hali iliyosababisha waumini wazidi kuongezeka.

Kila baada ya misa kumalizika, kama kawaida yangu ya siku zote, nilikuwa nikibeba boksi lenye sadaka na kulipeleka nyumbani. Safari hii sadaka ziliongezeka kuliko kawaida, kila Jumapili watu wakawa wanamtolea Mungu wao kwa sana, noti za shilingi elfu kumikumi zikawa zinatolewa kwa wingi, tofauti na zamani ambapo waumini wa kiwango cha juu walikuwa wakitoa shilingi mia tano au elfu moja.

Maisha yetu nayo yalizidi kubadilika kila siku, tukaachana na kula mbalaga (ndizi zinazopikwa na kupondwa), sasa tukawa tunakula vyakula vizuri huku tukibadilisha milo kila siku.
Mama naye alianza kuvaa vitenge vya wax na kupaka mafuta yanayonukia vizuri.https://www.facebook.com/simulizizamajonzi

No comments:

Post a Comment