Mwandishi: Hashim Aziz
“Sukuma! Sukumaaa! Jikaze mwanangu...
moja... mbili... tatu... haya sukumaaa!” sauti ya mkunga wa jadi, Mama Anunu
ilisikika kutoka ndani ya kibanda cha nyasi na miti, akimhimiza msichana mdogo
aliyekuwa na ujauzito mkubwa, Adelina kujitahidi ili hatimaye ajifungue.
Licha ya ujauzito wake kutimiza umri
wa miezi kumi na moja, Adelina alishindwa kabisa kujifungua. Alishahangaika
sana kwenye hospitali mbalimbali bila mafanikio, alishapewa dawa za kuongeza
uchungu mara kadhaa bila mafanikio, mwisho ndipo aliposhauriwa kwenda kwa mama
Anunu.
Mwanamke huyo, licha ya kuzuiwa na
serikali kufanya shughuli za ukunga nyumbani kwake na badala yake akaambiwa awe
anawapa washauri waende hospitali na kwenye vituo vya afya kwa usalama wao,
bado aliendelea na kazi yake kwa siri, akiwasaidia wengi ambao ujauzito wao
ulikuwa na matatizo na wale ambao hawakuwa na uwezo wa kusafiri mpaka
hospitalini, kilometa nyingi kutoka eneo hilo.
“Kwani mume wako yuko wapi?” mama
Anunu alimuuliza msichana huyo ambaye alishindwa kutoa majibu zaidi ya
kuendelea kulia kwa maumivu makali kutokana na uchungu wa kujifungua kumzidia.
“Si nakuuliza, kwani mumeo yuko wapi?”
“A...li..ni...ka..taa.”
“Alikukataa? Kwa nini alikukataa?”
“Mke wa...ke ali...jua ka...ma
ana...msaliti...”
“Mungu wangu, we mtoto, kumbe ulikuwa
unatembea na mume wa mtu?”
“Nisa...idie ma...ma na...ku...fa,”
alilalamika Adelina huku akilishika tumbo lake.
“Nitakusaidia mwanangu lakini kwa
uzoefu wangu, lazima utakuwa umefungwa kitanzi na mwenye mume wake ndiyo maana
mpaka leo hujajifungua. Inabidi nikupe dawa nyingine za kienyeji ili kufungua
hicho kitanzi,” alisema mama Anunu na kukimbilia chumbani kwake. Muda mfupi
baadaye alitoka akiwa na kibuyu cheusi na kuanza kukitingisha kwa nguvu.
Alipokifungua, kilitoa gesi kama ile
inayotoka kwenye chupa ya soda inapofunguliwa kisha akamnywesha Adelina na dawa
nyingine akaimimina kwenye kiganja cha mkono wake na kumpaka kwenye viungo
vyake vya uzazi.
Muda mfupi baadaye, chupa ya uzazi
ilipasuka na kusababisha maji yaanze kumtoka kwa wingi, yakafuatiwa na damu
nyingi zilizoambatana na maumivu makali ya tumbo hasa eneo la kiunoni
yaliyosababisha msichana huyo aanze kupiga kelele kwa nguvu.
“Ukilia unapoteza nguvu za kumsukuma
mtoto, jikaze huo ndiyo uanamke, sukumaaa... sukumaaa,” mama Anunu aliendelea
kumhimiza msichana huyo mdogo asukume mtoto.
Licha ya kumuelekeza hata mkao wa
kukaa ili iwe rahisi kujifungua, bado Adelina hakuweza kufanikiwa kujifungua, kibaya
zaidi damu nyingi zikawa zinaendelea kumtoka, hali iliyoanza kutishia uhai
wake.
Licha ya ukongwe wake katika kazi ya
ukunga hasa kuwazalisha wanawake ambao mimba zao zilikuwa zimepitiliza umri,
hali ilionekana kumuelemea mama Anunu kiasi cha kumfanya kijasho chembamba kiwe
kinamtoka licha ya baridi kali iliyokuwa inapenya mpaka ndani ya nyumba hiyo.
“Jamani msaada! Naombeni msaada, mzee
Mtwivila... msaada jamani,” Mama Anunu alisema huku akitoka na kutimua mbio
kuelekea kwa jirani yake, Mzee Mtwivila ambaye ndiye pekee aliyekuwa na usafiri
wa pikipiki au bodaboda kama wengi wanavyopenda kuuita.
“Kuna nini tena jirani?”
“Kuna mgonjwa amezidiwa, anapoteza
damu nyingi anaweza kupoteza maisha.”
“Kwani hujaacha kuzalisha watu hapo
nyumbani kwako? Kweli wewe unataka kwenda kuozea jela.”
“Jirani nikiacha unafikiri nitakula
wapi? Nisaidie, huu siyo muda wa kunisimanga.”
“Sasa tutamsafirishaje kwenye
bodaboda?”
“Twende hivyohivyo tutajua mbele ya
safari, washa pikipiki,” alisema mama Anunu huku kijasho chembamba kikizidi
kumtoka kiasi cha kulowanisha gauni alilokuwa amelivaa.
***
Dr. Richard Mkisi, alikuwa ni daktari
maarufu wa magonjwa ya wanawake ambaye licha ya kufanya kazi katika hospitali
kubwa ya wazazi ya Meta jijini Mbeya, pia alikuwa akimiliki kituo maarufu cha
afya alichokiita Saint Camilius Health Centre, kilichokuwa kikitoa huduma
mbalimbali za afya.
Licha ya udogo wa kituo hicho,
kilikuwa na chumba maalum cha kuhifadhia maiti kilichokuwa na majokofu ya
kisasa na vifaa vyote muhimu vilivyokuwa vinahitajika kwa ajili ya kuhifadhi
maiti bila kuharibika.
Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa mtu
yeyote wa nje kugundua kwamba ndani ya kituo hicho kidogo lakini maarufu,
kulikuwa na mochwari ya kisasa namna hiyo. Ni watu wachache tu ndiyo waliokuwa
wakijua kuhusu suala hilo.
Kutokana na kituo hicho kujengwa
katika eneo lenye mkusanyiko mkubwa wa watu la Mbalizi, Mbeya, muda wote
wagonjwa walikuwa hawaishi ndani ya kituo hicho ambacho pia kilikuwa na wodi
kadhaa kwa ajili ya kulaza wagonjwa waliozidiwa.
Pia kilikuwa msaada mkubwa kwa wakazi
wa maeneo mengine ya mbali hasa Chunya ambapo wananchi wengi walikuwa
wakilazimika kusafiri umbali mrefu, tena kwenye barabara ya vumbi kufuata
huduma za afya katika kituo hicho.
“Mwingine aingie,” Dokta Mkisi alisema
akimaanisha mgonjwa mwingine aingie ndani ya chumba cha daktari baada ya kuwa
ameshamaliza kumhudumia mgonjwa wa awali.
“Dokta! Dokta, kuna dharura.”
“Dharura? Dharura gani tena?”
“Kuna mdada kaletwa sasa hivi kutoka Makongolosi,
Chunya, ana hali mbaya sana.
“Yuko wapi?”
“Yuko hapo nje ndiyo wanamshusha, anashindwa
kujifungua na amepoteza fahamu kabisa,” alisema nesi mmoja huku akitweta,
harakaharaka wote wakatoka mpaka nje.
Je, nini kitafuatia? Usikose next
issue.
No comments:
Post a Comment