MANYUNYU ya mvua yalianza kudondoka huku wingu zito likiendelea kujikusanya angani, kuashiria mvua kubwa iliyokuwa inataka kunyesha. Japokuwa ilikuwa bado ni mapema, giza lilitanda angani na kufanya watu karibu wote kukimbilia majumbani mwao kabla mvua hiyo haijaanza kunyesha.
Radi kali na ngurumo za kutisha zilikuwa zikisikika huku na kule na kuzidi kuifanya hali kuwa tete. Manyunyu yaliongezeka na muda mfupi baadaye, mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali ilianza kumwagika. Watu wote walikimbilia majumbani mwao, huku wengine wakijibanza kwenye viambaza vya nyumba na maduka kujisitiri na mvua hiyo.
“Kaka amka tunataka kufunga baa.”
“Niongeze bia moja baridi na kiroba.”
“Inamaana hii mvua wewe huisikii au?”
“We mhudumu, nimekwambia ongeza bia, kwani wewe ndiyo umenileta hapa, sitaki kuwahi kurudi nyumbani kwani moto unawaka.”
“Kivipi?”
“Naishi na mwanamke ambaye ni tatizo kubwa maishani mwangu, yaani muda mwingine natamani kujifia niepuke mateso haya,” kijana mmoja mdogo alikuwa akijibizana kilevi na mhudumu wa baa ndogo ya Mpakani. Licha ya mvua kubwa iliyokuwa inamwagika, kijana huyo hakuonekana kujali, pombe zilikuwa zimemzidi lakini bado alikuwa anataka kuendelea kunywa.
Mhudumu alipoona hamuelewi, alibeba vifaa vyote na kuvifungia ndani, akamuachia kiti alichokuwa amekalia pekee. Kutokana na mvua kuambatana na upepo mkali, alianza kulowana na mvua lakini hakujali. Ndiyo kwanza aliinamisha kichwa chake na kuuchapa usingizi, palepale alipokuwa amekaa.
Mvua iliendelea kunyesha kwa muda mrefu, radi kali zikasababisha umeme kukatika, mji mzima ukamezwa na giza totoro. Baada ya kunyesha kwa takribani saa mbili mfululizo, mvua ilikatika, maji yakawa yanapita kwa kasi kwenye mitaro na kuzoa vitu mbalimbali.
Brighton, alizinduka kutoka kwenye usingizi mzito na kujikuta amelala kwenye matope, mwili mzima akiwa amelowa chapachapa. Akili yake haikuweza kumpa majibu ya haraka ni kwa nini amelowa kiasi kile na kulala kwenye matope.
Alipojaribu kuinuka, ndipo alipoanza kurejewa na fahamu kuwa kilichosababisha akawa kwenye hali ile ni kiasi kikubwa cha pombe alichokunywa. Alijilaumu kwa kushindwa kujidhibiti lakini hakuwa na namna, maisha yaligeuka na kuwa mzigo mkubwa sana kwake.
Alijikongoja na kuinuka, akasogea kwenye dimbwi la maji yaliyokuwa yametuama na kuanza kunawa, akajisafisha matope yaliyokuwa yametapakaa mwilini kama nwendawazimu. Baada ya hapo, alivua nguo zake na kuzikamua kisha akaanza kujikongoja kuelekea nyumbani kwake.
Bado pombe hazikuwa zimemuisha kichwani, hali iliyosababisha awe anaingia kwenye madimbwi ya maji na kuanguka mara kwa mara. Mpaka anafika nyumbani kwake, uso ulikuwa umejaa michubuko aliyoipata baada ya kuanguka na kujiburuza mara kadhaa njiani.
“Ngo ngo ngo ngooo!” Brighton alibisha mlango kwa nguvu, akawa anasubiri kufunguliwa. Alipoona kimya alirudia tena, safari hii akianza kuita kwa sauti ya kilevi.
“Umetoka wapi?”
“Nimetoka kazini.”
“Kazi gani mpaka alfajiri? Kama umechoka kuishi na mimi si bora unirudishe kwetu? Mwanaume gani unashindwa kuwa na huruma? Yaani na hali yangu niliyonayo unashindwa kunithamini badala yake unaendekeza pombe na wanawake?”
“Sijafanya lolote baya mpenzi wangu, nilipitia kuchangamsha kichwa kidogo kwa bahati mbaya nikapitiwa mpaka muda huu.”
“Muongo mkubwa wewe, sasa kwa taarifa yako, hapa ndani huingii, kalale hukohuko ulikotoka,” alisema mwanamke aliyekuwa na tumbo kubwa kuashiria kuwa alikuwa mjamzito na kumsukuma Brighton mpaka nje, akadondoka kama mzigo na kutulia kimya. Mlango ukafungwa na eneo lote likatawaliwa na ukimya wa ajabu.
Baada ya kusukumwa kwa nguvu, Brighton alijibamiza kwenye kipande cha tofali na kupoteza fahamu, akalala palepale kama mfu mpaka kulipoanza kupambazuka.
“We mlevi, wewe! Amka kumekucha,” sauti ya mwanamke ilisikika ikimwamsha Brighton lakini hakuinuka. Mwanamke yule mjamzito alirudi mpaka ndani na kuchukua ndoo ya maji, akamwagia Brighton huku akimtingisha kwa miguu lakini hakuinuka. Aliendelea kumuamsha lakini hakuinuka, ikabidi akimbie mpaka kwa jirani yake na kumuamsha.
“Jirani kuna nini tena alfajiri yote hii?”
“Kuna tatizo, Brighton ameanguka na kupoteza fahamu,” alisema mwanamke huyo mjamzito huku akionekana kuwa na hofu, wakatoka pamoja na kuelekea eneo la tukio.
“Mungu wangu, inaonekana amejibamiza kwenye jiwe, inabidi tumkimbize hospitali,” alisema jirani yule na kurudi haraka ndani kwake, akawaamsha majirani wengine ambapo kwa pamoja walisaidiana kumbeba Brighton mpaka kwenye hospitali iliyokuwa jirani.
Harakaharaka akapewa huduma ya kwanza na kutundikiwa dripu huku jeraha lake la kichwani likianza kutibiwa.
“Kwani ilikuwaje?”
“Alikunywa sana pombe ndiyo akaanguka na kupoteza fahamu.”
“Ilikuwa saa ngapi?”
“Sikumbuki kwa sababu sikumsikia wakati akirudi, nimekuja kushtukia asubuhi na kumkuta akiwa amelala chini, nikawaita majirani ambao ndiyo wamenisaidia kumleta hapa.”
“Huyu ni nani yako?”
“Ni mchumba wangu na baba wa mwanangu mtarajiwa.”
“Itabidi aendelee kupatiwa matibabu mpaka atakapozinduka,” alisema daktari aliyekuwa akimtibu Brighton huku akiandika maelezo kwenye faili la mgonjwa. Aliendelea kupatiwa matibabu na baada ya saa sita tangu afikishwe hospitalini hapo, Abeid alizinduka na kujikuta sehemu tofauti.
“Unajisikiaje Brighton,” sauti ya muuguzi wa kike ilisikika masikioni mwa Brighton lakini badala ya kujibu, alianza kububujikwa na machozi kwa uchungu. Kwa jinsi ilivyoonesha, alikuwa na tatizo kubwa lililokuwa linautesa moyo wake.
“Mbona unalia kaka, kwani kuna tatizo?”
“Nesi we niache tu, acha nilie ili kupunguza uchungu uliomo ndani ya mtima wangu.”
“Jikaze usilie kwani hali yako bado siyo nzuri, utajizidishia matatizo,” nesi alimwambia Brighton kwa upole huku akiwa amemuinamia pale kitandani. Brighton aliendelea kuugulia ndani kwa ndani mpaka usingizi ulipompitia. Alipozinduka, alimkuta Matilda, msichana aliyekuwa na ujauzito wake akiwa amekaa pembeni ya kitanda chake, uso akiwa ameukunja kwa hasira.
“Umeona faida za ulevi? Mwanaume huna haya wewe… najuta kukubebea ujauzito,” alisema Matilda kwa jazba na kuamsha uchungu uliokuwa umeanza kupoa kwenye mtima wa Brighton.
“Kwa nini usiniulize ninavyoendelea kwanza ndiyo mengine yafuate? Huu siyo muda wa kulaumiana.”
“Huna lolote, starehe uponde na wanawake zako halafu mimi naambulia kazi ya kukuuguza, mwanaume huna shukrani wewe… najuta!” Matilda aliendelea kumnanga Brighton bila kujali hali aliyokuwa nayo, ikabidi nesi aliyekuwa anamhudumia aingilie kati na kumtaka Matilda kutoka nje ya wodi. Aliondoka huku akiendelea kuporomosha mvua ya matusi, hali iliyofanya kila mmoja amshangae.
“Hivi huko nyumbani kwenu mnaishije kaka? Amani ipo kweli? Mbona mwenzio anaonekana mkali sana,” aliuliza nesi kwa upole mara baada ya Matilda kutoka, Brighton hakujibu kitu zaidi ya kuendelea kutokwa machozi.
Licha ya kusikia watu wa rika mbalimbali wakisifia utamu wa mapenzi kila kukicha, kwa Brighton hali ilikuwa tofauti, aliishia kusimuliwa tu. Hakuwahi kufurahia mapenzi hata siku moja tangu alipokutana na Matilda, kila siku ilikuwa ni maumivu, mateso, vilio na uchungu ndani ya mtima wake, hali iliyomfanya Brighton abadilike sana kitabia.
Hakuwa Brighton yule ambaye watu walikuwa wanamfahamu, kijana mpole, mstaarabu, mtanashati na mtiifu kwa watu wa rika zote. Hakuwa Brighton ambaye kila mtu alikuwa anapenda kukaa karibu naye kutokana na ucheshi, uchapa kazi na tabia njema aliyokuwa nayo! Alibadilika kabisa na kuwa mtu mwingine tofauti.
Ghafla alianza tabia ya ulevi wa kupindukia, akawa anatumia muda mwingi kwenye vilabu vya pombe za kienyeji na mara mojamoja alipopata fedha, alikuwa akikesha baa. Mara kwa mara alikuwa mtu wa mwisho kuondoka vilabuni, akiwa amelewa tilalila.
Kulala kwenye mitaro ya maji machafu halikuwa jambo geni tena kwake, uso wake ulichakaa kwa pombe, kila sehemu akawa na makovu ya michubuko na majeraha aliyokuwa anayapata baada ya kulewa. Kwa watu waliokuwa wanamfahamu, walikuwa wakimuonea huruma sana kwani alionesha kupoteza dira ya maisha akiwa bado kijana mdogo sana.
Hata muda wa kumpa ushauri wa nini cha kufanya haukupatikana tena kwani muda wote alikuwa amelewa, si asubuhi, mchana wala usiku. Aligeuza pombe kuwa starehe yake kubwa, akaharibu kazi na kila kitu kwenye maisha yake! Alitia huruma.
Akiwa amelala juu ya kitanda kilichotandikwa mashuka meupe, dripu ikitiririka taratibu kuingia mishipani mwake, machozi yakilowanisha kichwa chake na mashuka, kumbukumbu zake zilimrudisha nyuma, siku aliyokutana kwa mara ya kwanza na Matilda.
No comments:
Post a Comment