Tuesday, July 8, 2014

DIAMOND, ‘MCHAWI’ WAKO HUYU HAPA

Makala: Hashim Aziz
Jamaa anaitwa Kevin Liles, alizaliwa Februari 27 pande za Baltimore, Maryland nchini Marekani. Japokuwa jina na sura yake havijulikani kiivyo, Kevin ndiye ‘mastermind’ wa wasanii wakubwa wanaopeta kwenye levo za kimataifa wakiwemo Jay Z, Diddy, Kanye West, Trey Songz, Big Sean, Rick Ross, Rihanna na wengine wengi kibao.
KEVIN NI NANI HASA?


Naamini wengi hawamjui Kevin lakini ukweli ni kwamba jamaa ndiye ‘mchawi’ wa muziki wa Hip Hop, R&B na Pop, akimpenda
msanii na kumkubali, akaamua kumsimamia kimuziki, lazime atusue na kupaa levo za mbalai sana, hiyo haina ubishi.


ALIKOTOKEA
Alianza kujihusisha na muziki akiwa meneja wa wasanii mbalimbali miaka kibao iliyopita lakini nyota yake ilianza kung’ara mwaka 1999 alipochaguliwa kuwa rais wa kampuni kubwa ya kurekodi muziki, Def Jam Recordings na makamu wa rais wa kampuni mama, The Island Def Jam Music mpaka mwaka 2004.


Baada ya hapo, Kevin alihamia kwenye kampuni nyingine kubwa zaidi ya kurekodi muziki, Warner Music Group ambako alisimama kama makamu wa rais akiwa chini ya bosi wake wa zamani, Lyor Cohen.
MJASIRIAMALI WA MUZIKI
Baadaye, Septemba 2009 baada ya kuiongoza kampuni hiyo kwa mafanikio makubwa na kuwaibua wasanii kibao kutoka sifuri mpaka kuwa mastaa wakubwa duniani, Kevin aliamua kuachana na ajira, akajiajiri kwenye ujasiriamali wa muziki.
Kutokana na heshima kubwa aliyoipata katika kipuindi chote alipokuwa anafanya kazi na kampuni hizo kubwa, Kevin ambaye ni mume halali wa Erika, aliendelea kutusua kivyakevyake, akaendelea kuzalisha wasanii wapya na kuwapa mafanikio makubwa kila kukicha huku akikodiwa na kampuni nyingine kibao kama Sony na Atlantic Music.
YEYE NA DIAMOND
Juni Mosi, 2014 , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete akiwa ziarani nchini Marekani, ‘aligumiana’ na Diamond ambaye naye alikuwa kwenye mishemishe zake za kimuziki.
Wakala chakula cha jioni pamoja ambapo mbali na mambo mengine, usiku huo mheshimiwa alimkutanisha Diamond na Kevin (tazama picha), wakajadili kwa kirefu jinsi ya kumsaidia bwa’ mdogo huyo pamoja na wasanii wengine wa Kitanzania katika Bongo Fleva na Bongo Muvi.
NYOTA NJEMA KWA DIAMOND
Kitendo cha rais kumkutanisha mkali huyo wa Ngololo na mtu mkubwa duniani kama Kevin, ilikuwa ni sawa na nyota njema iliyowaka kwenye maisha ya Diamond. Kumbuka nimeeleza kwamba Kevin akimpenda msanii na akakidhi viwango anavyovitaka, lazima ambadilishe na kuwa staa mkubwa duniani kama ilivyotokea kwa Jay Z, Rihanna, Trey Songz, Big Sean na wengine kibao.
KWAKO DIAMOND
Ninachotaka kushadadia hapa ni kwamba, kama Diamond kwa miaka mingi ulikuwa ukihangaika kwa waganga wa kienyeji kung’arisha nyota yako kama ambavyo baadhi ya watu wanakutuhumu (sina hakika na madai hayo yasiyo na msingi), basi ulikuwa ukipoteza muda.
Mganga au mchawi wako ambaye unapaswa kumng’ang’ania kwa sasa ni Kevin. Mheshimiwa Rais Kikwete ameshakufungulia milango, kazi ni kwako sasa.
KEVIN ANAKUJA BONGO
Katika salamu zake alizozitoa  katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Juni 14, 2014 kwenye tamasha kubwa lililoandaliwa na Clouds Media Group, Rais Kikwete aliahidi kumdondosha Bongo Kevin pamoja na wadau wengine, akiwemo mmiliki wa kituo cha runinga cha E! News pamoja na msanii Usher Raymond kuwanoa wasanii wa nyumbani ili nao wapae kimataifa.
Wasanii wa Bongo, mpewe nini tena? Changamkieni fursa ili Bongo Movie ifike Hollywood na Bongo Fleva ipae kimataifa zaidi, ‘mchawi’ anakuja, mtumieni kusafisha nyota zenu.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...