Naitwa Flaviana Joel, mwanamke mwenye
umri wa miaka ishirini na nane. Nilibahatika kuolewa miaka kumi iliyopita,
nikiwa bado msichana mbichi katika umri wa miaka kumi na nane tu.
Niliolewa na mume wangu kipenzi,
Ibrahim au Ibra kama mwenyewe nilivyozoea kumuita ambaye alikuwa akifanya kazi
kwenye benki moja maarufu ambayo sitaitaja jina kwa sababu maalum, iliyopo hapa
jijini Dar es Salaam.
Kabla Ibra hajanioa, tulidumu kwenye
uchumba kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja, kipindi hicho nikiwa nasoma chuo
kimoja cha uhasibu kilichopo Posta, katikati ya Jiji la Dar es Salaam, nikiwa
ndiyo kwanza nimeanza mwaka wa kwanza.
Baada ya ndoa, mimi na Ibra tulihamia
Mbezi Beach kwenye nyumba yetu ambako tuliishi pamoja mpaka tulipokuja
kutengana kwa sababu ambazo ndizo hasa zilizonifanya nitafute nafasi hii ya
kutubu hadharani na kukiri kwa kinywa changu yote niliyowahi kuyafanya.
Nimesukumwa kuja kusimulia mkasa wangu
huu kwa sababu nataka watu wajifunze kupitia maisha yangu na Ibra. Najisikia
aibu sana, najikaza tu kwa sababu nataka wanawake wenzangu waelewe
kilichonitokea na kamwe wasifuate njia kama ambazo mimi nilipita. Pia iwe funzo
kwa wanaume, hasa wale ambao wapo ndani ya ndoa.
Nasikitika kwamba nimekuwa kikwazo
kikubwa katika maisha ya Ibra, mwanaume niliyetokea kumpenda kwa moyo wangu
wote lakini kwa sababu ya mapungufu ya kibinadamu ambayo nitayaelezea,
nikageuka na kuwa mwiba mkali kwenye maisha yake.
Nilisema tangu awali na nitaendelea
kusema kwamba sijawahi kutokea kumpenda mwanaume kama nilivyompenda Ibra ila
hata sielewi ni kitu gani kilichosababisha haya yote yatokee.
Najisikia uchungu sana ndani ya moyo
wangu hasa nikiwatazama wanangu Joel, James na Mahiza ambao bado walikuwa
wakihitaji malezi ya baba na mama lakini kwa kukosa akili kwa mama yao (mimi)
leo wanateseka mno.
Siwezi kumlaumu Ibra kwa sababu
alijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kufanya yale ambayo mwanaume anapaswa
kuyafanya katika ndoa yake ingawa pia alikuwa na udhaifu mkubwa ambao ndiyo
uliosababisha leo hii nipate nguvu ya kuja kutubu hadharani na kuwa sauti ya
wengine ambao waume zao wana matatizo kama aliyokuwa nayo mume wangu Ibra
lakini hawana pa kusemea.
Naamini kutubu kwangu na kueleza
ukweli wa kila kitu kwenye maisha yangu, kutakuwa chachu ya mabadiliko katika
nyumba nyingi na kutaokoa ndoa nyingi.
Ukimya unaua, naamini kuna wanawake
wengi sana ambao wanakufa taratibu kwa sababu hawataki kuyasema matatizo ya
ndoa zao hadharani, matokeo yake wanazalisha matatizo mengine kwa waume zao
ambayo mwisho wake ni kama huu ulionitokea.
Kama kujiua isingekuwa dhambi, hakika
ningeyakatisha maisha yangu lakini naogopa nitakachokutana nacho siku ya
kiyama. Naamini kwa kuyasimulia haya, angalau kidogo nitapunguza mzigo
unaonielemea ndani ya nafsi yangu.
Nawaomba radhi wote mlioumizwa na
matendo yangu na mtakaoumizwa na ushuhuda huu, hasa kipenzi changu Ibra, watu
wote wanaotufahamu na kubwa zaidi kwa mama yangu ambaye matendo yangu
yamemfanya adharaulike na kila mtu kwani inaonekana alishindwa kunilea katika
maadili mema.
Pia naomba Mungu wangu anisamehe na
nitaendelea kumlilia kila siku kama nilivyofundishwa na mtumishi wa Mungu,
Mchungaji Mwakatobe ambaye ndiye aliyeniongoza katika sala ya toba.
***
April 8, 2003
Dar es Salaam.
Ilikuwa ni asubuhi yenye mvua kubwa
ambayo ilisababisha hali ya taharuki kwa wakazi wengi wa Jiji la Dar ambao
tulikuwa tukitegemea usafiri wa daladala. Nakumbuka vizuri ilikuwa ni tarehe 8
ya mwezi wa nne, mwaka 2003. Naikumbuka vizuri tarehe hii kwa sababu ambayo baadaye
nitaielezea.
Nilikuwa nimebeba begi langu begani na
kujikunyata pembeni ya kituo cha daladala cha Morocco, kwenye makutano ya
Barabara za Ali Hassan Mwinyi na Old Bagamoyo Road, nikisubiri usafiri wa
kuelekea chuoni, Posta.
Daladala siku hiyo zilikuwa za taabu
sana kwa sababu ya hali ya hewa iliyosababisha foleni kubwa karibu kwenye
barabara zote za Jiji la Dar es Salaam. Kama ujuavyo Jiji la Dar mvua ikinyesha
kidogo tu basi barabarani hakupitiki kutokana na foleni.
Ilikuja daladala ya kwanza iliyokuwa
inaelekea Posta lakini ilikuwa imejaza mno kiasi cha watu wengine kuwa
wananing’inia mpaka mlangoni. Nikashindwa kupanda. Ikaja ya pili nayo ikiwa
katika hali hiyohiyo, ikanibidi niendelee kusubiri.
Mvua nayo ilikuwa inaendelea kunyesha,
safari hii ikiambatana na upepo uliosababisha wote tuliokuwa tumejibanza pale
kituoni kuanza kulowa. Nilitamani kurudi nyumbani kwani ukiachilia mbali kero
ya mvua, muda nao ulikuwa umeenda sana.
Nikiwa najishauri cha kufanya, gari
dogo aina ya Toyota Carina lilikuja na kusimama pale kituoni, jirani kabisa na
pale nilipokuwa nimesimama. Kioo cha upande wa kushoto kikashushwa kisha
tukamsikia dereva akituambia kuwa kama kuna wanaoenda Posta, anataka kuwabeba
watu wanne tu kwa sababu daladala zinasumbua.
Mimi nilikuwa wa kwanza kulifikia gari
hilo dogo lakini zuri, nikawahi kufungua mlango wa mbele na kujitoma ndani.
Abiria wengine wengi wakafuata na kuanza kugombania lakini kwa sababu gari
lilikuwa na uwezo wa kubeba abiria wanne tu, watatu nyuma na mmoja mbele,
ilibidi wengine wabaki.
Nilijiona kuwa na bahati kubwa,
nikamgeukia dereva na kumsabahi huku nikimshukuru kwa msaada wake. Abiria
wengine nao walifanya hivyohivyo, akaondoa gari na safari ya kuelekea Posta
ikaanza. Kwa kuwa sote tulikuwa tumelowa, hakuna aliyekuwa na stori na
mwenzake, kila mmoja akawa anajifuta maji.
Safari iliendelea taratibu kutokana na
foleni na baada ya muda mrefu, hatimaye tulifika Posta. Kila mmoja alifungua
nauli na kutaka kumpa dereva lakini mwenyewe alikataa na kutuambia kuwa
ametusaidia tu kwa hiyo tusimlipe.
Tulimshukuru sana, sote tukashuka na
kila mmoja akaendelea na hamsini zake. Baada ya lile gari kuondoka, nilikumbuka
kuwa nilikuwa nimesahau begi langu lenye madaftari, vitabu na vifaa vyangu
vingine vya kusomea. Nilijikuta nikichanganyikiwa ghafla, nikawa najilaumu kwa
uzembe nilioufanya.
Ilibidi nianze kulifukuzia lile gari
kwa nyuma lakini tayari nilikuwa nimechelewa, lilishajichanganya na magari
mengine, hali iliyonipa wakati mgumu kulitambua kwani kulikuwa na magari mengi
aina ya Carina Posta, tena yote yakiwa yanafanana.
Nilitoa simu yangu mfukoni lakini
nilishindwa kuitumia kwa sababu sikuwa nikizijua namba za dereva. Nikajikuta
nikiishiwa nguvu kabisa. Safari yangu yote haikuwa na maana tena kwa sababu
nisingeweza kwenda chuo nikiwa sina vifaa vya kusomea.
Kwa kuwa bado mvua ilikuwa ikimwagika,
nilisogea kwenye korido ndefu za Posta Mpya na kujibanza hapo pamoja na watu
wengine wengi waliokuwa wamejisitiri mvua. Nikiwa bado najiuliza cha kufanya,
simu yangu ilianza kuita. Nilipotazama namba ya mpigaji, ilikuwa ngeni kwangu.
Sina kawaida ya kupokea namba za simu
nisizozijua lakini siku hiyo niliipokea haraka ilipoita mara moja tu.
“Halloo!”
“Haloo, nani mwenzangu.”
“Samahani, unamfahamu Flaviana Joel?”
“Ndiyo namfahamu, kwani vipi?”
“Kuna watu niliwapa lifti kwenye gari
langu muda mfupi uliopita sasa kuna mmoja amesahau begi lake la vitabu,
nilipopekua ndiyo nikaikuta hii namba imeandikwa nyuma ya kitabu kimoja. Naomba
umpe namba yangu mwambie anitafute au nipe yake nijue namna ya kumfikishia
mzigo wake,” alisema dereva wa ile Carina kwa sauti ya kiungwana mno.
Nilishusha pumzi ndefu na kuachia
tabasamu, nikamwambia kwamba mimi ndiyo Flaviana, nikamsikia akicheka kidogo
kisha akaniuliza nipo wapi kwa wakati huo. Nilipomuelekeza, aliniambia
nimsubiri hapohapo anakuja.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue. Unaweza pia kuisoma kwenye Facebook kwa kulike page ya Simulizi za Majonzi.
No comments:
Post a Comment