ILIPOISHIA:
Kwa kuwa nilikua nimevaa taiti na
sidiria tu huku juu nikiwa nimejifunga mtandio mwepesi, umbo langu lilionekana
vizuri kabisa, uzalendo ukamshinda Ibrahim, akanitamkia:
“Kumbe umeumbika hivi? Loh, mpenzi
wako anafaidi.” Nikacheka sana kwa furaha kwani nilichokuwa nakitaka, kilikuwa
kimetimia. Tayari Ibrahim alishaanza kuonesha dalili za kunitaka kimapenzi.
SASA ENDELEA...
Unajua sisi wanawake wengi huwa
tunapenda sana kusifiwa, na mtu akishaanza kukusifia, basi ukijirahisisha
kwake, lazima mwisho muishie kuwa wapenzi. Baadhi ya wanaume wanaujua udhaifu
wetu huu na wamekuwa wakipitia humohumo kukidhi haja za miili yao.
Basi nikazidi kuringa mtoto wa kike,
nikamtoa wasiwasi kwamba hakuna mtu yeyote anayenimiliki, nipo ‘singo’.
“Unasema kweli upo singo?”
“Ndiyo, kwa nini huamini?”
“Unajua wanawake wazuri kama wewe mara
nyingi huwa hawawezi kuwa singo, tena wengine wanakuwa na mpenzi zaidi ya
mmoja.”
“Wala mimi sipo hivyo, wazazi wangu
wakali sana na hawapendi kabisa nijihusishe na mambo hayo ndiyo maana nimeamua
kuweka nguvu zangu zote kwenye masomo,” nilisema huku nikiyarembua macho yangu
mazuri, kauli ambayo ilionesha kumfurahisha sana Ibrahim.
Kwa kuwa sikuwa na nguo nyingine za
akiba, ilibidi nivae nguo zangu juu ya zile zilizoloana, tukatoka na Ibrahim na
kuanza kutembea kuelekea kwenye gari. Tayari akili za Ibrahim zilishabadilika
kabisa kwa sababu hata wakati tukitembea, alikuwa anataka nitangulie mbele
kidogo halafu akawa ananitazama kwa nyuma kwa kuibia. Nililijua hilo,
nikazidisha vituko.
Basi tulifika kwenye gari, tukaingia
na safari ya kurudi nyumbani ikaanza, mazungumzo kati yangu na Ibrahim yalianza
kubadilika taratibu, akawa ananiuliza mambo mbalimbali kuhusu maisha yangu
kuanzia vitu ninavyovipenda, nisivyovipenda, ratiba yangu ya maisha ya kila
siku na mambo mbalimbali kuhusu maisha yangu.
Nilimjibu kila kitu alichotaka
kukijua, hatimaye tukafika Morocco. Akasimamisha gari kituoni kisha tukaagana,
nilipotaka kushuka, aliniita jina langu, nikageuka na kumtazama.
“Kuna jambo nitakwambia baadaye kwenye
simu, tafadhali usikatae,” alisema huku akiwa amevaa uso uliokuwa na ujumbe
mzito kwangu, nilitabasamu na kumtoa wasiwasi, nikashuka.
“Chukua hizi zitakusaidia matumizi
yako madogomadogo,” alisema Ibrahim huku akinipa noti kadhaa za shilingi elfu
kumikumi. Nilizipokea na kumshukuru, nikabeba furushi langu la mchanga na
kuanza kuondoka kuelekea nyumbani. Naye aliwasha gari lake na kuondoka.
Kwa kuwa ule mchanga wala sikuwa na
kazi nao, nilipofika mbele kidogo niligeuka na kumuangalia Ibrahim, nilipoona
ameshaondoka, niliutupa ule mchanga na kuanza kuchekelea ujanja nilioutumia
mpaka kumuingiza Ibrahim kwenye mtego.
Nilipofika nyumbani, nilipitiliza
bafuni kuoga kisha nikabadilisha nguo na kutulia chumbani kwangu, nikiendelea
kumuwaza Ibrahim. Mara simu yangu iliita, nilipotazama namba ya mpigaji,
alikuwa ni Ibrahim, nikatabasamu na kuipokea nikiwa na shauku kubwa ya kutaka
kumsikia anachotaka kuniambia.
Alianza kwa kunisalimia, ila safari
hii alikuwa akizungumza kwa sauti tulivu iliyobeba hisia nzito ndani yake.
Nikamchangamkia kama kawaida yangu, akaniuliza kama nimeshalala, nikamjibu bado
nasubiri nile chakula cha usiku kisha nifanye kazi niliyopewa chuoni.
“Ooh! Napenda sana mtu anayejali
masomo, kazania elimu si unajua ndiyo urithi wetu?” alisema Ibrahim kisha
tukaendelea na mazungumzo ya hapa na pale, bado shauku yangu ya kutaka kusikia
anataka kuniambia nini ikiwa kubwa.
Cha ajabu, mpaka ananiaga, wala
hakuniambia kitu ambacho aliniahidi jioni ile wakati akinishusha kwenye gari
kwamba ataniambia na akanisihi nisimkatalie. Mtoto wa kike uvumilivu
ukanishinda, ikabidi nimuulize. Maskini Ibra! Alibabaika sana na kuishia
kuchekacheka mpaka alipokata simu.
Nilichokigundua ni kwamba Ibrahim
alinipenda na alikuwa akitaka kunitongoza lakini aibu zilimjaa mkaka wa watu.
Inavyoonekana hakuwa fundi wa kutongoza kama walivyo wanaume wengine. Hata
hivyo kwa kuwa mimi ndiyo nilikuwa nyota wa mchezo, nilijiapiza kumfanya aweze
kutongoza ili azma yangu itimie.
Alipokata simu, nilianza kumchokoza
kwa meseji, nikamwambia kama ameshindwa kuniambia basi anitumie meseji.
Akanijibu kwamba jambo lenyewe ni la kawaida wala nisiwe na wasiwasi. Bado
sikukubali, nikaendelea kumganda kama ruba.
Wakati mwingine nilianza kuhisi kwamba
Ibrahim hakuwa mwanaume wa kawaida kwa kile alichokuwa amekifanya. Mategemeo
yangu yote nilidhani kwamba Ibrahim angenitongoza lakini matokeo yake, mwisho
wa siku akakata simu bila kunitongoza na hata tulipokuwa tukichati hakutaka
kufanya hivyo.
Mwanamke mimi, wakati mwingine
nilijishtukia, nilitamani kukutana naye na kumwanzishia mazungumzo ya
kimapenzi, sikupenda kabisa kila tunapokutana au kuongea simuni, alikuwa
akisisitizia sana suala la elimu.
Nilimpenda Ibrahim na kila siku
niliamini kwamba hata yeye mwenyewe alinipenda japokuwa hakutaka kuweka wazi.
Hisia kali za mapenzi bado ziliendelea kuuchoma moyo wangu, nilikuwa
nikimtamani Ibrahim leo kesho aniambie maneno ya kimapenzi na mwisho wa siku
tuwe wapenzi, tupendane kama walivyokuwa wapenzi wengine.
“Ibrahim, mbona unanifanyia hivi?
Mbona hautaki kuniambia ukweli kila siku unanirusha roho tu jamani?” nilijiuliza
kana kwamba Ibrahim alisimama mbele yangu.
Sikujua kitu gani kilichomfanya
Ibrahim kuchukua muda mrefu kabla ya kuniambia ukweli juu ya hisia alizokuwa
nazo juu yangu. Si kwamba Ibrahim hakuwa akinipenda, hapana, alinipenda sana
kwani hata macho yake yalikuwa yakidhihirisha hilo.
“Sasa anataka kuniambia nini?”
nilijiuliza.
Wakati mwingine sikutaka Ibrahim
anitongoze kwa sababu sisi wanawake unapomfanyia mwanaume mambo mengi ya
kimapenzi huku ukimuoneshea ishara zote za kimahaba, hatakiwa kukutongoza bali anatakiwa
kufanya mambo yote kama wapenzi, yaani leo kukushika kiuno na kesho kukubusu
mdomoni.
Hiyo ndiyo hulka yetu. Kama unapata
nafasi ya kumuoneshea mwanaume kila kitu halafu baadaye akaja na kukutogoza,
huwa tunashangaa kwa sababu kitu ambacho huwa tunakitarajia ni kuona akianza
kuonyesha mapenzi kwa vitendo, yaani kutushika hapa na pale na mambo mengine
mengi ya kimahaba.
Mpaka kufikia hapo, tayari
nilimuoneshea Ibra ishara zote, aliishia kunisifia tu. Japokuwa nilizifurahia
sifa zake lakini bado nilitaka atamke maneno ya kimapenzi, ajaribu kunitongoza
na mimi kumkubalia tu.
Ibrahim hakutaka kufanya hivyo, kitu
ambacho kilikuwa kikinikera zaidi ni pale tunapokutana au kuongea halafu
kuniuliza kuhusu masomo yangu tu.
Ibrahim hakutakiwa kufanya hivyo, alitakiwa
kunioneshea kwamba yeye ni mwanaume anayejiamini, alitakiwa kuniambia maneno ya
kimapenzi kwa sababu hicho ndicho kilikuwa kitu pekee nilichokuwa nikikitarajia
kutoka kwake.
“Au hanitaki? Lakini haiwezekani,
mbona kila nikimwambia twende sehemu tunakwenda? Mbona kila nikimwambia fanya
hiki anafanya? Sasa kwa nini hataki kunitongoza? Au nimekuwa mbaya?”
nilijiuliza maswali mengi lakini sikupata jibu.
Kuna kipindi nilikuwa nikiinuka kutoka
kitandani na kukifuata kioo changu, ninapokifikia ninaanza kujiangalia huku
nikiwa na nguo na mwisho wa siku navua nguo zote.
Umbo langu bado lilikuwa bora, sura
yangu bado ilikuwa ikivutia na nilikuwa na uhakika wa kumteka mwanaume yeyote
ambaye alikuwa akiniona kwa mara ya kwanza.
Sasa kwa haya yote, sura yangu na umbo
langu bado tu Ibrahim hakuona kwamba ninatakiwa kuwa msichana wake, anipende na
kunithamini? Bado Ibrahim hakuona kwamba nilikuwa msichana ninayestahili
kutongozwa na mtu kama yeye?
Bado kichwa changu kilikuwa na maswali
mengi yasiyokuwa na majibu, niliendelea kumfikiria huyu Ibrahim ambaye kila
siku alinifanya kuwa na presha kubwa lakini hakuonekana kujali.
Kioo kilinitia moyo, ni kweli nilikuwa
mrembo haswa lakini ukimya wa Ibrahim wa kutotaka kunitongoza ulinifanya
nimshangae kila siku.
Wakati mwingine nilijitahidi sana
kusoma makala mbalimbali za mapenzi ili kuona ni kwa jinsi gani unaweza
kumtongoza mwanaume ambaye ulikuwa ukimpenda lakini yeye hakukwambia kitu
japokuwa macho yake yalionesha kila kitu.
“Au nimtongoze mimi? Lakini yeye si
ameshindwa bwana, kama vipi nimtongoze mimi mwenyewe,” nilijisemea.
No comments:
Post a Comment