ILIPOISHIA:
Naomba umpe namba yangu mwambie
anitafute au nipe yake nijue namna ya kumfikishia mzigo wake,” alisema dereva
wa ile Carina kwa sauti ya kiungwana mno.
Nilishusha pumzi ndefu na kuachia
tabasamu, nikamwambia kwamba mimi ndiyo Flaviana, nikamsikia akicheka kidogo
kisha akaniuliza nipo wapi kwa wakati huo. Nilipomuelekeza, aliniambia nimsubiri
hapohapo anakuja.
SASA ENDELEA...
Kweli baada ya kama dakika tano hivi,
ile Carina ilipaki upande wa pili wa barabara, akanipigia simu na kuniuliza
kama nilikuwa naliona gari. Nikatoka mbiombio na kukimbia kuvuka barabara. Kwa
kuwa bado mvua ilikuwa inanyesha, nilipolifikia gari lake, alinifungulia
mlango, nikaingia na kukaa kwenye siti ileile niliyokuwa nimekaa awali,
nikamgeukia, na yeye akanitazama, macho yetu yakagongana.
“Pole kwa usumbufu,” aliniambia kwa
sauti ya kiungwana, nikaachia tabasamu hafifu huku nikiendelea kujifuta maji ya
mvua, nikwamwambia mimi ndiyo napaswa kumpa yeye pole kwani licha ya kunipa
lifti bure, nilimpa kazi nyingine ya kunitafuta.
Alinipa begi langu na kuniuliza
nilikokuwa nakwenda.
“Naenda chuo, pale jirani na mnara wa
askari.”
“Unasomea nini?”
“Nasomea uhasibu.”
“Ooh! Safi sana, mimi pia nilisomea
uhasibu pale IFM sasa hivi nafanya kazi benki,” alisema yule dereva huku na
yeye akiachia tabasamu, akaniomba kama sitajali anisindikize jirani na chuo ili
nisiendelee kulowa.
Nilikubali haraka na kumshukuru sana.
Akawasha gari na kwenda mpaka mbele kidogo, akageuza gari na kurudi barabarani,
akawa anaendesha gari taratibu huku tukipiga stori za kawaida.
Ndani ya kipindi kifupi tu nilichokaa
naye, niligundua kuwa yule kaka alikuwa mtu mmoja mstaarabu sana, asiye na
maneno mengi, anayejiheshimu na anayeheshimu watu wengine pia bila kujali umri,
jinsia au hali ya kiuchumi.
Alinisogeza mpaka jirani na chuoni
kwetu, akalitoa gari barabarani na kupaki pembeni huku mvua kubwa ikiendelea
kunyesha. Nilitaka kushuka lakini akaniambia nisubiri mvua ipungue kidogo kwani
yeye hakuwa na haraka sana kwani ofisi anayofanyia kazi ni jirani na pale.
Tofauti na wanaume wengi niliokuwa
nakutana nao kila siku katika pilikapilika zangu, yeye wala hakuonesha papara ya
kuniomba namba yangu ya simu wala hakuonesha kabisa nia ya kutaka kunitongoza
hasa ukizingatia kwamba licha ya umri wangu mdogo, nilikuwa nimejaliwa uzuri wa
kipekee kuanzia sura mpaka umbo.
Mvua ilipungua na hatimaye ikaisha
kabisa, nikarudia tena kumshukuru yule kaka ambaye mpaka muda huo wala sikuwa
nikilijua jina lake. Tukaagana, nikashuka kwenye gari lake na kuanza kutembea
harakaharaka kuelekea chuoni bila hata kugeuka nyuma.
Japokuwa nilikuwa nimechelewa,
nilipoingia darasani, nilikuta wanafunzi wachache tu wakiwa wameshafika,
nikajua ni kwa sababu ya hali ile ya hewa. Kwa kuwa jana yake sikumaliza kazi
tuliyopewa chuo, sikutaka kupoteza muda, nikakaa kwenye kompyuta yangu na
kuendelea na kazi.
Bado kumbukumbu za yule kaka zilikuwa
zikiendelea kuja na kupotea kwenye kichwa changu. Sijui ni kwa sababu gani
lakini nahisi ni kwa sababu ya uungwana alionionesha. Ndani ya muda mfupi tu
niliokaa naye, nilijikuta nikianza kumzoea na kutamani kama niendelee kumuona
au kuisikia sauti yake nzuri.
Haikuwa kawaida yangu kuvutiwa
kirahisi namna hiyo na mwanaume, katika historia ya maisha yangu, wanaume ndiyo
walikuwa wakinipapatikia kutokana na uzuri wangu, wala mimi sikuwahi kufanya
hivyo hata mara moja, nikabaki najishangaa.
Nilijitahidi kujitoa kwenye mawazo hayo
bila mafanikio, kila nilipofumba macho, sura ya yule kaka ilinijia akili mwangu
na kujikuta nikitabasamu.
Kibaya zaidi, wala hakunipa namba yake
ya simu na sikuwa nikijua anafanya kazi wapi zaidi ya kuniambia kuwa ofisi yao
ilikuwa jirani na chuo chetu. Ghafla nilikumbuka kitu kilichonifanya
nitabasamu. Nilikumbuka kwamba yeye ndiye aliyenipigia simu wakati niliposahau
mkoba wangu kwenye gari lake.
Harakaharaka nikatoa simu yangu na
kuanza kuangalia kwenye namba zilizoingia. Macho yangu yalitua kwenye namba
yake, nikaitazama kwa muda kisha nikaiandika pembeni ya kitabu changu cha
Financing. Nikafanya kama najaribu kumtumia hela kwa njia ya mtandao wa simu
ili nione jina gani litatokea.
Baada ya kubonyezabonyeza namba
fulani, likatokea jina la Ibrahim Mnasy, nikatabasamu tena na kushusha pumzi
ndefu.
“Kumbe anaitwa Ibrahim!” nilijisemea
huku nikiisevu namba yake. Kama kuna mtu angekuwa ananifuatilia ninachokifanya,
angeweza kudhani nataka kurukwa na akili. Angalau sasa roho yangu ilitulia
kwani nilijua naweza kumpata endapo nikihitaji kuwasiliana naye.
Mvua ilikuwa imekatika kabisa,
wanachuo wengi wakawa wanakuja darasani na baadaye kidogo, walimu waliwasili,
tukaanza masomo japo kwa kuchelewa. Masomo yaliendelea mpaka saa nane mchana,
tukatoka kwa ajili ya chakula cha mchana kisha tukarejea tena darasani mpaka
saa kumi ambapo kwa kawaida ndiyo ulikuwa mwisho wa vipindi.
Tukatawanyika na mimi kuongoza mpaka
kwenye kituo cha daladala cha Posta ambacho kila siku huwa napandia magari ya
kurudi kwetu, Kinondoni. Kama ilivyokuwa asubuhi, usafiri ulikuwa wa shida sana
jioni hiyo. Hatimaye nilipanda daladala ingawa ilikuwa ni kwa kugombania sana,
safari ya kurudi nyumbani ikaanza.
Njiani bado kumbukumbu juu ya Ibrahim
ziliendelea kunisumbua, nikajiapiza kuwa jioni nikimaliza kazi zangu zote,
lazima nimpigie simu japo nisikie sauti yake. Baada ya kusota kwa muda mrefu
kwenye foleni, hatimaye tuliwasili Morocco, nikashuka na kuvuka barabara,
nikatembea kidogo kuelekea nyumbani kwani hatukuwa tukiishi mbali sana na kitu
hicho.
Nilipofika nyumbani, siku hiyo
sikutaka stori na mtu, nilipitiliza chumbani kwangu, baada ya kupumzika kidogo
nikaenda kuoga na kurudi sebuleni kusubiri chakula cha usiku kwani tulikuwa na
desturi ya kukusanyika familia nzima kila jioni.
Tulipomaliza kula, harakaharaka
nilirudi chumbani kwangu na kujifungia, nikachukua simu na kujitupa kitandani,
nikatafuta namba ya Ibrahim na kumpigia huku nikiwa nimeshajiandaa nini cha
kuongea.
Simu ilipoita kidogo tu, ilipokelewa,
nikajikuta nikisisimka mno baada ya kuisikia sauti ya Ibrahim, mapigo ya moyo
wangu yakawa yananienda mbio mno.
“Haloo!”
“Haloo kaka Ibrahim.”
“Naam! Naongea na nani?” Ibrahim
alizungumza kwa sauti iliyotulia mno, nikazidi kuchanganyikiwa mtoto wa kike.
Nilishusha pumzi ndefu na kujitambulisha, nilipomkumbusha tu mazingira
tuliyokutania, alinikumbuka na kunichangamkia.
“Umelijuaje jina langu?”
“Si ulinitajia mwenyewe, au umesahau,”
nilidanganya, nikamsikia akiguna kama anayekumbuka kitu kisha tukaendelea na
mazungumzo. Nilimwambia nimempigia simu ili kumshukuru kwa wema wote
alionifanyia siku hiyo, akafurahi na kuniambia nisijali.
Tuliendelea kuzungumza mambo ya hapa
na pale, mimi nikiwa ndiyo mzungumzaji sana, nilichokuwa nakitaka ilikuwa ni
ukaribu wake na kumzoea, jambo ambalo lilishaanza kuonekana kuwa litafanikiwa
kwa jinsi alivyokuwa ananichangamkia.
Baadaye mazungumzo yaliisha,
nikamtakia usiku mwema kisha nikakata simu. Nilishusha pumzi ndefu na kuanza
kushangilia moyoni, sijui kwa nini nilifurahi sana kuongea na Ibrahim.
Kama hiyo haitoshi, nilimtumia ujumbe
mfupi mzuri wa kumtakia usiku mwema, naye akanijibu ndani ya muda mfupi tu,
nikalala na kuukumbatia mto wangu huku joto tamu likiendelea kuzunguka kwenye
mwili wangu.
Niseme tu wazi kwamba nilishampenda
sana Ibrahim tangu nilipomuona kwa mara ya kwanza tu, na sasa nilikuwa tayari
kufanya chochote, hata ikibidi kujitongozesha ilimradi awe mpenzi wangu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue. Unaweza kuisoma pia Facebook kwa ku-like page ya Simulizi za Majonzi.
No comments:
Post a Comment