ILIPOISHIA:
Kama hiyo haitoshi, nilimtumia ujumbe
mfupi mzuri wa kumtakia usiku mwema, naye akanijibu ndani ya muda mfupi tu,
nikalala na kuukumbatia mto wangu huku joto tamu likiendelea kuzunguka kwenye
mwili wangu.
SASA ENDELEA...
Niseme tu wazi kwamba nilishampenda
sana Ibrahim tangu nilipomuona kwa mara ya kwanza tu, na sasa nilikuwa tayari
kufanya chochote, hata ikibidi kujitongozesha ilimradi awe mpenzi wangu.
Naomba watu wasinielewe vibaya kwa
sababu najua kwa mila za Kitanzania, ni vigumu sana mwanamke kueleza hisia zake
za kimapenzi, tumezoea kwamba sisi ni watu wa kutongozwa tu.
Wapo wengi tu ambao walikuwa
wakiwapenda watu fulani ila kwa sababu ya kukosa ujasiri, wakajikuta wakiolewa
na watu ambao wala hawakuwahi kuwafikiria kwenye maisha yao.
Niliamua kujitoa mhanga mtoto wa kike,
nikajiapiza kuwa lazima nimpate Ibrahim. Wala kilichonizuzua halikuwa gari lake
au kusikia kwamba anafanya kazi benki, walaa! Ni mapenzi ya dhati ndiyo
yaliyonisukuma mpaka kupata ujasiri wa namna ile.
Niliendelea kumfikiria Ibrahim mpaka
usingizi uliponipitia, kesho yake asubuhi nikawahi kuamka kama kawaida yangu na
kujiandaa kwa ajili ya kwenda chuo. Nilipomaliza kuvaa, niliwaaga baba na mama
kama ilivyo kawaida yangu kila siku kisha nikatoka na kuanza kutembea kuelekea
kituo cha daladala.
Siku hiyo hakukuwa na mvua kama jana
yake ingawa kila kona kulikuwa na matope. Kumbukumbu juu ya Ibrahim zikanijia
na kujikuta nikitabasamu mwenyewe. Nilitoa simu yangu kwenye mkoba na kutafuta
namba yake, nikampigia.
Muda mfupi baadaye alipokea,
nikamsalimia kwa adabu na kumuuliza kama ameamka salama. Alinijibu kwamba yupo
poa na kwa muda huo anajiandaa kwenda kazini.
“Mi mwenyewe naelekea Morocco kupanda
daladala.”
“Ahaa! Sasa kwa nini usinisubiri
nikupe lifti?”
“Hutachelewa sana,” nilijibaraguza ili
asinione najirahisisha sana kwake, akaniambia kuwa wala hatachelewa, baada ya
dakika kumi tu atakuwa ameshafika. Tuliagana, nikakata simu huku nikiwa na
furaha ya ajabu ndani ya moyo wangu.
Nilitembea harakaharaka mpaka kituoni,
nikatafuta sehemu tulivu na kukaa huku macho yote yakiwa upande ule Ibrahim
alikotokea jana yake. Nilitoa kioo changu kidogo ninachotembea nacho kwenye
mkoba na kujikagua usoni, nikajiweka sawa na kuendelea kumsubiri.
Kweli dakika kumi baadaye, gari la
Ibrahim lilifika pale kituoni, akapunguza mwendo na kusimama huku akishusha
kioo. Kwa kuwa tayari nilishamuona, niliinuka harakaharaka na kumfuata,
akanifungulia mlango wa mbele, nikaingia na kukaa.
“Mambo!” Ibrahim alinisabahi huku
tabasamu pana likiwa limeupamba uso wake. Kiukweli Ibrahim alikuwa na mvuto wa
kipekee machoni pa mtu yeyote. Nikajihisi mkondo kama wa umeme ukipita mwilini
mwangu na kusambaa kwenye kila kiungo.
Nilimjibu huku na mimi nikiachia
tabasamu pana, akaondoa gari na safari ya kuelekea Posta ikaanza. Mazungumzo ya
kawaida yaliendelea huku mara kwa mara nikigeuka na kumtazama Ibrahim usoni.
Kila macho yetu yalipogongana, moyo
wangu ulikuwa ukinilipuka mno mpaka nikawa najishtukia. Kwa kuwa siku hiyo
hakukuwa na foleni kubwa, baada ya dakika kadhaa tayari tulikuwa Posta.
Akanipeleka mpaka jirani na chuoni kwetu, tukaagana kisha akaondoa gari kwenda
kazini kwake.
Nilimsindikiza kwa macho mpaka
alipopotea kwenye upeo wa macho yangu, nikatembea harakaharaka kuingia chuoni
huku moyo wangu ukiwa na furaha ya ajabu. Siku hiyo hata akili zangu hazikuwepo
kwenye masomo kabisa, nilikuwa nikiwaza jinsi ya kumuingiza Ibrahim kwenye kumi
na nane zangu! Moyo wangu ulishampenda.
Muda wa lanchi ulipofika, nilimtumia
meseji Ibrahim na kumwambia kama ana nafasi aje tule wote mi nitamlipia,
akanijibu kwamba alikuwa na kazi nyingi hivyo isingekuwa rahisi kuonana.
“Kwani kazini unatoka saa ngapi?”
“Saa kumi na moja.”
“Kuna mahali nataka unisindikize,
utakuwa na nafasi?”
“Yaa, nikitoka kazini huwa naenda
nyumbani moja kwa moja kwa hiyo usijali nitakusindikiza,” alisema Ibrahim bila
hata kuhoji ni wapi nilipokuwa nataka anisindikize. Wala sikuwa na safari
yoyote, nilitaka tu ukaribu wake.
Kichwani nikapata akili kwamba
nitamwambia anisindikize ufukweni kuchukua mchanga kidogo wa bahari kwa ajili
ya kumpelekea mama. Nilipanga kwamba tukifika ufukweni, nitamfanyia vituko
mpaka mwenyewe achanganyikiwe na mimi. Muda wa lanchi ulipopita, nilirudi
darasani, nikawa naona kama saa haziendi haraka.
Hatimaye muda wa kutoka ulifika,
nikakusanya kila kitu changu na kutoka, nikampigia simu Ibrahim kwamba
atanikuta namsubiri palepale aliponishusha asubuhi. Kwa kuwa mimi niliwahi
kidogo kutoka chuo, ilinibidi nimsubiri Ibrahim kwa zaidi ya dakika arobaini.
Kwangu hiyo wala haikuwa kazi kubwa,
hatimaye nikaliona gari lake likija taratibu pale nilipokuwa nimekaa, akashusha
kioo na macho yetu yakagongana, wote tukatabasamu. Harakaharaka niliingia
kwenye gari na kukaa pembeni ya Ibrahim, nikamgeukia, na yeye akanigeukia,
tukawa tunatazamana.
“Mambo!” alivunja ukimya, nikamjibu
huku nikiachia tabasamu pana, na yeye akatabasamu na kuyafanya meno yake meupe
yaonekane vizuri. Siyo siri nilijikuta nikizidi kumpenda Ibrahim.
Nilimwambia kuwa nataka anisindikize
baharini nikachukue mchanga mama kaniagiza, wala hakuwa na kipingamizi chochote.
Akawasha gari na kuanza kuendesha taratibu, tukawa tunaelekea baharini, upande
wa Hospitali ya Ocean Road. Njiani tulikuwa tukipiga stori za hapa na pale,
akawa ananiuliza kuhusu masomo yangu na kunisisitiza kuwa nikazane kwani elimu
ndiyo ukombozi wetu.
Tulifika baharini, akatafuta sehemu
nzuri na kupaki gari, pembeni ya barabara kisha tukashuka. Nikaona huo ndiyo
muda muafaka wa kufanya nilichokuwa nakitaka.
“Samahani, nikitaka kuogelea kidogo
utanisubiri?”
“Wala usiwe na wasiwasi, kwani huwa
unapenda kuogelea?”
“Napenda sana,” nilisema huku moyoni
nikifurahi kwani nilichokuwa nakitaka kilikaribia kutimia. Ibrahim
alinisindikiza, tukashuka kwenye ngazi za ukingo wa bahari mpaka chini ambako
haikuwa rahisi kwa wapita njia kutuona.
“Geukia kule nibadilishe nguo,”
nilisema huku nikijichekeshachekesha, kweli Ibrahim akageuka na kunipa mgongo,
nikavua suruali niliyokuwa nimevaa na kubaki na taiti, juu nikavua blauzi na
kubaki na sidiria tu kisha nikachukua mtandio mwepesi na kujifunga juu kidogo
ya kifua.
Nilifanya vile kwa makusudi kwani
nilijua nitakapoingia kwenye maji na ule mtandio, utanichora mwilini na
kulifanya umbo langu zuri la kuvutia lionekane vizuri. Nikaanza kutembea
taratibu kumfuata Ibrahim ambaye bado alikuwa amenipa mgongo.
“Tayari,” nilisema huku nikimgusa
begani, akageuka na kunitazama. Mshtuko alioupata haukuweza kujificha,
alinitazama kuanzia juu mpaka chini kama ndiyo kwanza anakutana na mimi kwa
mara ya kwanza, nikajua ameshaingia kwenye mtego.
“Vipi mbona umeduwaa,” nilimuuliza
lakini hakuwa na jibu zaidi ya kutabasamu. Nikageuka na kuanza kutembea kwa
maringo kuelekea kwenye maji, huku nikijitingisha kwa makusudi. Ibrahim akazidi
kupagawa.
Nilipoingia kwenye maji, nilianza
kuogelea kihasarahasara huku nikimuita Ibrahim naye aje tuogelee naye lakini
alikataa, bado akawa anaendelea kunitazama kwa macho yaliyokuwa yamebeba ujumbe
mzito.
Sikuogelea sana, nikachukua mchanga
kidogo na kuuweka kwenye mfuko kama geresha tu kisha nikatoka kwenye maji. Kwa
kuwa nilikua nimevaa taiti na sidiria tu huku juu nikiwa nimejifunga mtandio
mwepesi, umbo langu lilionekana vizuri kabisa, uzalendo ukamshinda Ibrahim,
akanitamkia:
“Kumbe umeumbika hivi? Loh, mpenzi
wako anafaidi.” Nikacheka sana kwa furaha kwani nilichokuwa nakitaka, kilikuwa
kimetimia. Tayari Ibrahim alishaanza kuonesha dalili za kunitaka kimapenzi.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue. Unaweza pia kuisoma Facebook kwa ku-like page ya Simulizi za Majonzi.
No comments:
Post a Comment