Tuesday, August 31, 2010

THE SMELL OF THE DEAD
(Harufu ya wafu)
Utangulizi
Tamaa ya kumiliki mali kwa nguvu ya uchawi na ushirikina, vinamfikisha kijana Elisante Katembo katika shimo la mauti. Imani kali za kishirikina alizorithishwa na marehemu bibi yake, zinamfanya atamani kufanya mambo makubwa kuliko uwezo wake. Anafanikiwa kupata utajiri mkubwa ambao hakuna anayefahamu ameupata wapi kutokana ana umri wake kuwa bado mdogo.

Hamu ya kumiliki mali inamfanya akubali kuwa mtumwa mzuri wa shetani, anawatoa kafara wanawake wengi, lakini bado mambo yake yanazidi kwenda mrama, hatimaye anakubali kuwatoa kafara wanae,wake zake, mama yake mzazi, majirani na marafiki zake wote wanawake, ikiwa ni kutimiza agano la kishetani, linalowataka wafuasi wote wa nguvu za giza kutoa sadaka ya damu na viungo vya wanawake wanaowapenda.

Anafanya ushetani mkubwa nyuma ya pazia jeusi, huku uzuri wa sura yake na upole vikiificha taswira halisi ya moyo wake, anajificha nyuma ya mwavuli wa ulokole akijifanya ni mcha Mungu, anaudanganya ulimwengu na hakuna anayemshtukia, hali inayompa nafasi ya kutenda ushetani mkubwa. Kwa nje, anaonekana mtakatifu, lakini ndani ya nafsi yake, ushetani mkubwa unachipua na kuota mizizi.


Utanashati wake na busara anazozionesha kwa nje, zinafanya watu wanamuamini na kumpa uongozi wa kanisa, akiwa mshauri wa vijana anayetegemewa. Anautumia mwanya huo kutembea na wanawake wengi, wakiwemo waimba kwaya wa kanisa lake, na baada ya kutimiza lengo lake, anawaua na kuwakata baadhi ya viungo vyao, anavyovitumia katika shughuli zake za uchawi na kujiongezea utajiri maradufu.

Hakuna anayejua kinachoendelea upande wa pili wa maisha yake… hata mke wake anayelala naye kitanda kimoja haelewi chochote juu ya mumewe. Lakini kwa bahati mbaya anakosea miiko na masharti na mambo yanaanza kumuendea mrama. Harufu ya wafu inaanza kumuandama kila anakokwenda.

Hakubali kufa peke yake, anataka kuondoka na wengi, na kama masharti yake ya kichawi yalivyokuwa, njia pekee ya kurejesha nguvu za kichawi zilizopotea ni kulala na wanawake wengi zaidi wa kadri awezavyo, na baada ya kumaliza tendo, kuwaua na kuondoka na viungo vyao nyeti, ambavyo vinatumika katika matambiko maalum ya kurudisha nguvu za kishirikina na kuulinda utajiri haramu aliokuwa anaumiliki.

Pamoja na kuwa hakuna mtu yeyote anayefahamu matendo ya Katembo, dhamira yake inamshtaki kila anakokwenda. Kama walivyosema wahenga, hakuna marefu yasiyo na ncha. Harufu ya wafu wote waliopoteza maisha yao mikononi mwake, inamfuata kila anakokwenda. Damu ya kisasi inamuwakia katika kila analolifanya. Japokuwa utajiri wake unazidi kukua kila kukicha, anakosa kabisa amani ya nafsi. Uchawi unashindwa kumlinda tena, visasi vya walioonewa vinawaka moto mkali. Harufu ya maisha inabadilika kutoka kwenye marashi ya kifahari mpaka kwenye harufu inayonuka vibaya, ni harufu ya wafu… The smell of the dead. Anza nayo ujionee maajabu ya dunia….

Ilikuwa ni usiku wa manane, wingu zito likiwa limetanda kila sehemu na kulifanya giza totoro lililokuwa limetanda, lizidi kutisha. Rasharasha za manyunyu ya mvua zilikuwa zikipungua taratibu baada ya mvua kubwa iliyofululiza kunyesha usiku mzima, tangu majira ya jioni.

Mitaa yote ilikuwa kimya kabisa huku viambaza vya nyumba za watu vikifunikwa na giza nene. Kwa mbali zilikuwa zikisikika sauti za kutisha za milio ya bundi na ndege wa usiku, waliozidi kuupamba usiku wa manane.

Mvua kubwa ambayo sasa ilikuwa inakatika ilikuwa imesababisha maafa makubwa kwani radi za nguvu na upepo mkali viliharibu nyumba kadhaa huku miti ikiangukia barabarani na kufunga njia zote za mitaa. Nguzo za umeme nazo zilianguka ovyo, hali iliyosababisha umeme kukatika mji mzima na kuacha kila kona ya mji ikiwa giza tupu.


Hii siyo ya kuikosa. Tukutane wiki ijayo.

THE SMELL OF THE DEAD
(HARUFU YA WAFU)-2
Tamaa ya kumiliki mali kwa nguvu ya uchawi na ushirikina, vinamfikisha kijana Elisante Katembo katika shimo la mauti. Imani kali za kishirikina alizorithishwa na marehemu bibi yake, zinamfanya atamani kufanya mambo makubwa kuliko uwezo wake. Anafanikiwa kupata utajiri mkubwa ambao hakuna anayefahamu ameupata wapi kutokana ana umri wake kuwa bado mdogo.

Hamu ya kumiliki mali inamfanya akubali kuwa mtumwa mzuri wa shetani, anawatoa kafara wanawake wengi, lakini bado mambo yake yanazidi kwenda mrama, hatimaye anakubali kuwatoa kafara wanae,wake zake, mama yake mzazi, majirani na marafiki zake wote wanawake, ikiwa ni kutimiza agano la kishetani, linalowataka wafuasi wote wa nguvu za giza kutoa sadaka ya damu na viungo vya wanawake wanaowapenda.

Anafanya ushetani mkubwa nyuma ya pazia jeusi, huku uzuri wa sura yake na upole vikiificha taswira halisi ya moyo wake, anajificha nyuma ya mwavuli wa ulokole akijifanya ni mcha Mungu, anaudanganya ulimwengu na hakuna anayemshtukia, hali inayompa nafasi ya kutenda ushetani mkubwa. Kwa nje, anaonekana mtakatifu, lakini ndani ya nafsi yake, ushetani mkubwa unachipua na kuota mizizi. Lakini mwisho wa yote, harufu ya wafuinaanza kumuandama.
Shuka nayo mwenye.

Kijana Elisante Katembo alikuwa amejifungia kwenye chumba chake cha siri, muda mfupi baada ya kurejea kutoka makaburini walikokuwa na sherehe ya kichawi, ambapo wachawi wote walikutana kujadili mambo mbalimbali yanayowahusu, kama ilivyokuwa kawaida yao.

Tofauti na vikao vyao vya siku zote, cha usiku huu kilikuwa na lengo moja kubwa, lililokuwa likimhusu Katembo. Kilikuwa ni kikao maalum kwa ajili ya kufanya tambiko kwa ajili ya Katembo kutokana na matatizo makubwa yaliyokuwa yakimuandama. Kwa kuwa shughuli ya tambiko hilo haikuwa nyepesi kama ilivyodhaniwa, ilibidi kafara ya damu itolewe ili kulipa nguvu tambiko.

Watoto wachanga watatu, akiwemo mziwanda wa Katembo aliyekuwa na miezi saba tu, walichinjwa kisha damu na nyama zao kutumika kama kinga maalum dhidi ya mikosi na matatizo yaliyokuwa yakimuandama Katembo. Viungo vyao, ikiwemo nywele, mikono, miguu na mafuvu ya vichwa vyao viliwekwa kwenye jeneza dogo alilopewa Katembo kwa ajili ya kwenda kulificha kwenye chumba chake cha siri.

Wakati Katembo akiwa kwenye chumba chake cha siri, mkewe alikuwa amelala usingizi wa pono, akiwa hajui chochote kinachoendelea. Mwanae mchanga aliyekuwa na umri wa miaka saba tu alikuwa amepatwa na ugonjwa wa ajabu na ndani ya siku mbili tu na hali yake ilikuwa imebadilika sana, hali iliyomkosesha raha kabisa. Usiku uliopita hakulala hata kidogo kutokana na mwanae huyo kukesha akilia. Akisaidiana na mumewe Katembo walimbembeleza bila mafanikio mpaka kulipopambazuka.

Hata kulipokucha bado alikuwa akilia sana hali iliyosababisha sauti kukauka. Japokuwa alikuwa na hali mbaya, Katembo alimkataza mkewe kumpeleka Hospitali.
“Usiwe na wasiwasi atapona tu, watoto huwa wanasumbua sana hasa wakiwa wachanga,” Katembo alikuwa akimpa moyo mkewe aliyeonekana kuchanganyikiwa. Masaa yalizidi kuyoyoma huku hali ya mtoto wao ikizidi kuwa mbaya. Usiku wa pili ulipofika, hali ya mtoto ilibadilika ghafla na kuwa nzuri, mama yake akaamini amepona. Kwa kuwa alikuwa hajalala kwa siku mbili mfululizo aliutumia muda huo kulala kwa ni alikuwa na uchovu wa hali ya juu.

Hakujua kuwa mumewe alikuwa na ajenda ya siri nyuma ya pazia. Walilala pamoja huku mtoto wao akiwa katikati. Mkewe alipopitiwa na usingizi, Katembo aliutumia muda huo kutimiza azma yake ya kwenda kumtoa mtoto huyo kafara ili kumaliza matatizo na mikosi iliyokuwa inamuandama kutokana na imani kali za kishirikina alizokuwa akijihusisha nazo.

Katembo alimchukua mwanae kichawi na kumuacha mkewe akiwa amelala, ambapo alimpeleka makaburini ambako wachawi walikuwa wakikutana kila usiku kwa ajili ya sherehe zao za kichawi. Kilichoendelea ikawa ni tambiko kubwa lililohusishwa kuchinjwa kwa watoto wachanga watatu, akiwemo na yule wa Katembo aliyemchukua kutoka kwake bila ya mkewe kujua.

Itaendelea wiki ijayo.

THE SMELL OF THE DEAD
(HARUFU YA WAFU)-3
Tamaa ya kumiliki mali kwa nguvu ya uchawi na ushirikina, vinamfikisha kijana Elisante Katembo katika shimo la mauti. Imani kali za kishirikina alizorithishwa na marehemu bibi yake, zinamfanya atamani kufanya mambo makubwa kuliko uwezo wake. Anafanikiwa kupata utajiri mkubwa ambao hakuna anayefahamu ameupata wapi kutokana ana umri wake kuwa bado mdogo.

Anafanya ushetani na mkubwa nyuma ya pazia jeusi, huku uzuri wa sura yake na upole vikiificha taswira halisi ya moyo wake, anajificha nyuma ya mwavuli wa ulokole akijifanya ni mcha Mungu, anaudanganya ulimwengu na hakuna anayemshtukia, hali inayompa nafasi ya kutenda ushetani mkubwa. Kwa nje, anaonekana mtakatifu, lakini ndani ya nafsi yake, ushetani mkubwa unachipua na kuota mizizi. Lakini mwisho wa yote, harufu ya wafuinaanza kumuandama.
Shuka nayo mwenye.

Baada ya tambiko lililodumu kwa masaa matatu mfululizo, Katembo aliruhusiwa kurudi nyumbani kwake, ila akapewa vifaa vya kumlinda na kumuongezea nguvu za kichawi zilizokuwa zimeanza kupungua. Vifaa hivyo vilijumuisha viungo vya watoto wachanga waliochinjwa makaburini, vikiwemo nywele, mikono, miguu na mafuvu ya vichwa vyao ambavyo viliwekwa kwenye jeneza dogo alilopewa Katembo kwa ajili ya kwenda kulificha kwenye chumba chake cha siri.

Kwa mujibu wa masharti aliyokuwa amepewa, hakutakiwa mtu yeyote kuona kilichokuwa ndani ya jeneza lile, na endapo angevunja masharti basi madhara yake yangekuwa makubwa sana. Katembo aliapa kuwa atafuata masharti yote aliyopewa ili nguvu zake za kichawi zirudi na kuwa kali kama zamani. Alisafiri kichawi mpaka nyumbani kwake akiwa na lile jeneza alilopewa kule makaburini.

Aliliingiza mpaka kwenye chumba chake cha siri bila ya mtu yeyote kujua na baada ya kufanya mizungu maalum kwa ajili ya kulisalia tambiko, aliliweka lile jeneza dogo ndani ya kile chumba, akakifunga kwa uangalifu mkubwa kisha akaenda kuoga bafuni. Kwa muda wote huo mkewe alikuwa bado amelala akiwa hajui kinachoendelea.
****
“Jamani mmesikia kwamba nyumbani kwa mchungaji Katembo kuna msiba, eeh! yule mwanae mchanga aliyeanza kuumwa ghafla jana amefariki,” walisikika wakina mama wakipeana taarifa juu ya kifo cha mtoto mchanga wa ‘Mchungaji’ Elisante Katembo. Hakuna ambaye aliamini kuwa ni kweli mtoto wa Katembo amefariki dunia kwani alikuwa na afya njema na hakuwahi kuumwa hata siku moja tangu azaliwe, na homa iliyomuanza ghafla siku mbili zilizopita ndiyo iliyomuondoa uhai wake.

Hakuna aliyekuwa anafahamu nyuma ya kifo kile cha kichanga wa Katembo kuna nini. Hata mkewe mwenyewe hakuelewa chochote kilichokuwa kinaendelea. Taratibu za mazishi ziliharakishwa kuliko kawaida, zikiongozwa na Katembo mwenyewe, na baada ya masaa sita akawa tayari ameshazikwa.

“Lakini mbona mazishi ya huyu mtoto yamefanywa haraka sana, yaani kafariki alfajiri saa hizi ameshazikwa?” waombolezaji waliokuwa makaburini walikuwa wakihojiana. Hakuna aliyekuwa na jibu la nini kilichokuwa kinaendelea. Kwa jinsi Katembo alivyokuwa anaheshimika mbele ya jamii, hakuna ambaye angeweza kuhisi tofauti.

Mazishi yakawa yamefanyika bila ya mtu yeyote kushtukia mchezo mzima. Baada ya taratibu zote kukamilishwa, wito ulitolewa makaburini kwamba hakutakuwa na msiba kwani kwa kawaida watoto wenye umri wa chini ya mwaka mmoja misiba yao ilikuwa inaishia makaburini baada ya mazishi. Hii haikuwa mara ya kwanza kwa Katembo kuharakisha mazishi ya vifo vilivyotokea katika mazingira tata kama yale.

Mke wake wa kwanza naye alipoteza maisha katika mazingira tata kama yale, na mazishi yake yakafanywa katika mazingira ambayo yaliwaacha wengi na viulizo. Hata wanae wakike wawili waliokufa vifo vya ghafla miaka kadhaa iliyopita, nao walizikwa kinyemela huku wakiacha maswali na viulizo vingi kwa waliokuwa wanawafahamu.

“Siamini kama mwanangu ametutoka, jamani mziwanda wangu, rudi mwanangu,” alikuwa akiongea kwa uchungu mke wa Katembo akiwa amemkumbatia mumewe.

Itaendelea wiki ijayo.


THE SMELL OF THE DEAD-4

Kwa mwonekano wa nje, ilikuwa ni vigumu sana kufahamu namna nafsi yake ilivyo. Imani kali za kishirikina na nguvu za giza vinamfanya awe mtumwa wa shetani. Anafanya maasi makubwa kwa wanawake na watoto wachanga kwa tamaa ya kumiliki mali, huku akijificha nyuma ya pazia la uchungaji. Lakini hatimaye, harufu ya wafu inaanza kumuandama. Je nguvu za kichawi zitamuokoa? Shuka nayo…

Maombolezo ya kifo cha mtoto mchanga wa Bwana Elisante Katembo yanavuta hisia za wengi kutokana na jinsi mke wake alivyokuwa na uchungu. Japokuwa ilishatangazwa kuwa hakutakuwa na msiba, bado watu wengi walikuwa wakimiminika nyumbani kwake kwenda kumpa pole kutokana na umaarufu aliokuwa nao.

“Siamini kama mwanangu ametutoka, jamani mziwanda wangu, rudi mwanangu!” alikuwa akiongea kwa uchungu mke wa Katembo akiwa amemkumbatia mumewe.
“Nyamaza mke wangu, ukilia sana utakufuru, kazi ya Mungu haina makosa, Bwana alitoa na sasa ametwaa, jina lake lihimidiwe,” alisema Katembo akijifanya kondoo wa Mungu.”

Kila aliyekuwa akimfahamu, alikuwa akienda kumpa pole kwa msiba. Hakuna aliyejua kuwa yeye ndiye aliyekuwa mhusika mkuu wa kifo cha mwanae. Maombolezo yaliendelea kwa wiki nzima, huku kila aliyekuwa akimjua Katembo akienda kumpa pole. Kilichowachanganya wengi ni mfululizo wa matukio ya Bwana Katembo kufiwa na wanae wachanga, pamoja na wanawake anaowaoa. Hakuna aliyekuwa na jibu juu ya tatizo lile, ikabaki kuwa siri yake mwenyewe.

Siku zilizidi kusonga na hatimaye taratibu kumbukumbu za kufiwa na mwanae zikaanza kufutika. Kwa kadri siku zilivyokuwa zinasonga, Katembo alizidi kuandamwa na mikosi na mabalaa kuliko hata awali. Kwa jinsi ilivyoonekana, tambiko alilolifanya kwa kushirikiana na wachawi wenzake lilikuwa halijamsaidia chochote zaidi ya kumuongezea matatizo.

Ilibidi mkutano wa washiriki wa nguvu za giza uitishwe upya, na safari hii wachawi wote walikutana nyumbani kwa Bwana Katembo. Uamuzi uliofikiwa ilikuwa ni kukamilisha idadi ya wanawake saba, ambao Katembo alitakiwa kuvunja nao amri ya sita na kisha kuwaua kabla ya kuwakata baadhi ya viungo vya miili yao. Alipangiwa muda wa siku 30 kuwa ameikamilisha kazi ile, na bila kupoteza muda akaanza kazi.
******
“Jamani mbona leo tumekuwa wazito sana kwenye maombi, hata saa sita za usiku hazijafika tayari wote tumechoka, kuna nini?” aliongea kiongozi wa maombi akiwauliza vijana wenzake waliokuwa wamekutana kwa ajili ya maombi ya usiku, ndani ya kanisa la Holly Gospel, alilokuwa akisali Katembo. Ilionekana ni kama wamefungwa na nguvu fulani ingawa hakuna aliyejua ni nini kimetokea.

Katembo alikuwa ni miongoni mwa watu waliohudhuria kipindi cha maombi ya usiku, na kilichomfanya awepo kanisani hapo usiku ule, ilikuwa ni kuanza kutekeleza kazi aliyokua amepewa. Ili kuficha ukweli, akawa anawahimiza vijana wenzake kuzidi kusali ili kuzishinda nguvu za giza zilizokuwa zinawanyemelea.

Muda mfupi baadae walijikuta wote wakipitiwa na usingizi mzito wakiwa ndani ya kanisa, akabakia Katembo peke yake akiwa macho. Usingizi ule haukuwa wa kawaida, bali ulikuwa ni mtego maalum ulioandaliwa na kundi la wachawi ili kumrahisishia Katembo kazi yake, ulikuwa ni mpango wa siri. Akaanza kuchagua mwanamke wa kuanza naye kazi kati ya waumini waliokuwa wamehudhuria misa ya usiku ule.

Macho yake yalitua kwa Getrude, binti mpole aliyekuwa akisifika kwa haiba yake ya upole na unyenyekevu, hususan awapo ndani ya nyumba ya ibada.Kwa kutumia nguvu za kichawi, Katembo alimgusa Getrude mabegani, ambaye alikuwa amepitiwa na usingizi, na kwa ghafla ukatokea mwanga mkalikama wa radi, na wote wawili wakapotea kimiujiza.


****
Kikao cha wachawi kilikuwa kikiendelea ndani ya nyumba ya Katembo, ambapo idadi kubwa ya wachawi walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya kumsaidia mwenzao ambaye alionekana kuishiwa nguvu za kichawi hali iliyosababisha aanze kuandamwa na mabalaa chungu mzima.

Wakiwa kwenye kikao chao cha wachawi, ilifahamika kuwa Katembo anaandamwa na mikosi kwa sababu alikuwa amekosea masharti, na zaidi kwa sababu alikuwa akiishi kwenye nyumba za kanisa ambapo kulikuwa na nguvu zinazoshindana kati ya nguvu za kichawi na nguvu za Mungu. Na ilu kuubomoa ukuta wa nguvu hizo, Katembo alitakiwa kuanza kazi yake ya kutoa kafara kwa mtu ambaye alikuwa muumini mzuri.

“Na ndio maana nimemchagua huyu Getrude, ni muumini mzuri sana na bila shaka nguvu zake zitatusaidia kwa kiwango kikubwa,” Katembo alikuwa akijieleza mbele ya wachawi wenzake, huku mwili wa Getrude ambaye alikuwa hana fahamu ukiwa umelazwa mbele yake.

“Mbona anaonekana kama alishawahi kuzaa? Mtu wa kufungua tambiko lazima awe kigori,” alisikika mchawi mmoja akiongea kwa sauti ya mamlaka.

“Hajawahi kuzaa kiongozi, bado ni binti mdogo tu, ila umbo lake ndio linalomfanya aonekane mkubwa.”
“Nadhani atatufaa sana, kazi ianze mara moja.”
“Sawa mkuu!”.

BAADA ya kutoroka naye kichawi, Katembo anamsafirisha kichawi Getrude mpaka ufukweni mwa bahari, ambako alifanya kama alivyoelekezwa na wenzake, kuvunja naye amri ya sita kasha kuchukua viungo kadhaa vya mwili wake. Baada ya kumaliza kufanya unyama ule, Katembo aliubeba mwili wa Getrude na kuingia nao ndani ya bahari, na kuanza kutembea kuelekea mbele, mpaka alipofikia maji yenye kina cha mabegani. Alipofika, alitabana maneno kadhaa ya kichawi, kisha akautupa ule mwili na kugeuka, akaanza kutembea kiupandeupande kuelekea ufukweni.

Alifanya ishara za kichawi, kisha akatoweka kimiujiza. Wale waumini walioachwa wamepitiwa na usingizi mzito kanisani wakati wakiwa kwenye ibada, waliendelea kuwa katika hali ya unusu kaputi mpaka alfajiri. Baada ya kumaliza tambiko lao, wakitumia damu ya binti aliyechaguliwa na Katembo, wachawi wote walitawanyika na kuanza kurudi makwao. Katembo alibeba vitu vyake alivyopewa usiku ule, na kuvisafirisha kichawi mpaka nyumbani kwake, kisha akarudi kanisani na kujirudisha katika hali kama aliyokuwa nayo awali. Akajifanya naye amepitiwa na usingizi kama waumini wengine.

“Hee! Mungu wangu, yaani kumeshapambazuka? Mbona haya maajabu!”
“Haijawahi kunitokea hali kama hii, nipitiwe na usingizi mpaka asubuhi kanisani, lazima kuna jambo.”
“Kwani kumetokea nini? Mbona mi sijielewi…
Waumini walianza kuzinduka kutoka usingizini huku kila mmoja akijishangaa imekuwaje mpaka apitiwe na usingizi mzito isivyo kawaida.


THE SMELL OF THE DEAD-6!
Tukio la ajabu la waumini wa kanisa la kiroho analosali Katembo, kupitiwa na usingizi wakati wakiwa kwenye maombi ya usiku hadi asubuhi, kunawashangaza wengi na kuvuta hisia za wengi, kila mmoja akiwa haamini kilichotokea. Wakati fahamu zikianza kuwarudia mmoja mmoja baada ya kuachiwa na nguvu za kichawi, waumini wanagundua kuwa mwenzao mmoja, Getrude amepoteza fahamu tangu usiku, na mwili wake umetulia sakafuni mithili ya mtu aliyekufa. Nini kitafuatia? Shuka nayo mwenyewe!

“Getrude! Getrude! Amka wewe, wenzako wote tumeshaamka.”
“Lakini kwanini yeye hajazinduka mpaka muda huu wakati wenzake wote tumeshaamka?”
“Yawezekana amepatwa na tatizo kubwa, tumsaidieni jamani!”

Waumini walikuwa wakijiuliza bila kupata majibu baada ya kuona wengine wote wamezinduka isipokuwa Getrude. Kwa hofu waliyokuwa nayo waumini baada ya kurudiwa na fahamu zao, hakuna aliyeweza kutoka nje ya jengo la kanisa. Kila mmoja alikuwa akijificha nyuma ya mwenzake, isipokuwa mtu mmoja tu, Katembo.

“Wapendwa mi nafikiri Mungu aliyapokea maombi yetu tuliyokuwa tunayafanya usiku na ndio maana tukapitiwa na usingizi. Itabidi kila mmoja atoe ushuhuda wa alichokiona akiwa kwenye usingizi mtakatifu,” Aliongea Katembo akiwa hana wasiwasi hata kidogo, hali iliyowafanya waumini wale washindwe kugundua kuwa yeye ndiye aliyesababisha yote yale.

“Ni kweli mtumishi, lakini mi nafikiri kwa muda huu tumshughulikie mwenzetu Getrude ambaye bado hajazinduka. Mengine yatafuata baadae.”
“Ni kweli kabisa, hatuwezi kufanya lolote mpaka tuhakikishe Getrude amezinduka.”
Waumini wote waliweka msimamo wao kufanya kila linalowezekana kuhakikisha Getrude anazinduka kutoka kwenye usingizi wa kifo. Walimuweka katikati na kuanza upya maombi, kama walivyokuwa wakifanya usiku, lakini asubuhi hii ilikuwa maalum kwa ajili ya kumuombea Getrude.

Mwili wa Getrude ulilazwa katikati, waumini wakauzunguka na kushikana mikono, kisha wakaanza kumuombea. Kabla hawajaanza kuomba, Katembo alijifanya kapatwa na dharula, akawaomba waumini wenzake atoke nje ya kanisa, lakini akaahidi kuwa angereja baada ya muda mfupi. Walimruhusu na kuendelea na maombi.

“Hebu sikiliza mapigo yake ya moyo!”
“Mapigo ya moyo hayasikiki, lakini mwili wake bado wa moto!”
“Heee! Tazameni jamani, damu imeanza kumtoka masikioni, mdomoni na puani! What the hell is this?” (Hili ni balaa gani?)
Waumini walizidi kupigwa na butwaa baada ya kuona dalili za ajabu kwenye mwili wa Getrude.
“Jamani mi nashauri tumkimbize hospitali ili kunusuru maisha yake!”
“Huo ni uhaba wa imani mtumishi, tuendelee kumuombea kwa Mungu atapona tu, hakuna linaloshindikana.”
Baada ya kutoka kanisani, Katembo aliharakisha kurejea nyumbani kwake, na alipofika hakutaka kusalimiana na mtu yeyote, akapitiliza mpaka kwenye chumba chake cha siri alikohifadhi zana zake za kichawi. Alienda mpaka mahali alipoficha viungo alivyovikata kichawi kutoka kwenye mwili wa Getrude , akavishika na kuanza kutabana kichawi, ili Getrude asirudiwe na fahamu zake.

Ilikuwa ni lazima afanye vile kwani kama angechelewa, maombi ya waumini kanisani yangeweza kuzishinda nguvu za giza, na Getrude angezinduka hali ambayo ingesababisha matatizo makubwa kwa Katembo na wachawi wenzake.

Alichokifanya ilikuwa ni kupulizia dawa ya usingizi kwa waumini wale waliokuwa wakiendelea na maombi kanisani, kisha kuwafunga akili na kuwafanya washindwe kuuona ukweli. Haikumuwia vigumu kutokana na nguvu kubwa za kichawi alizokuwa nazo.
***
Kwa mara nyingine, baadhi ya waumini wakajikuta wakianza kuhisi dalili za usingizi mzito kama ule uliowapata usiku.Wakaanza kupitiwa na usingizi mmoja baada ya mwingine. Baada ya kupulizia kichawi dawa ya usingizi, Katembo alianza kuchimba shimo ndani ya chumba chake cha siri, ili kuvifukia vile viungo vya Getrude, hii ikiwa na maana ya kumzika kabisa na kuhalalisha kifo chake.

Alipomaliza kazi yake, alirejea kanisani kwa haraka, akakuta waumini wenzake baadhi wakiwa wamepitiwa na usingizi mzito, huku baadhi wakiwa bado anaendelea na maombi mazito. Aliingia kwa haraka na kujichanganya nao, akawa anafanya kazi ya kuendelea kutabana kichawi ili wote wapitiwe na usingizi kama usiku uliopita.
Itaendelea wiki ijayo.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...