Baada ya mambo kuzidi kuwa magumu kwa Geneviv, anaamua kutoroka nyumbai kwao, muda mfupi kabla ya mama yake hajarudi kutoka Hospitalini alikokuwa amelazwa kwa siku nyingi. Hakutaka mama yake agundue kuwa alikuwa ametoa ujauzito, kwani alijua fika kuwa angeumia sana na huenda shinikizo la damu lililokuwa likimsumbua lingejirudia upya, hali ambayo hakuwa tayari kuona ikitokea. Anaacha ujumbe mzito kitandani kwake, kisha anaodoka kuelekea kusikojulikana. Muda mfupi baadae mama yake anarudi akiwa ameongozana na Alice aliyemsaidia kubeba vitu vyake kutoka Hospitali. Je nini kitaendelea? Twende kazi.
“Geneviv….Genny… where are you my dear? im back,”…(uko wapi mwanangu, nimerudi?) alikuwa akiita Bi Patricia huku akizunguka huku na huko kumtafuta Geneviv kwenye vyumba vyote bila mafanikio. Nyumba ilikuwa kimya kabisa.
Alienda mpaka chumbani kwake lakini hakumkuta. Akiwa huko alishangaa jinsi chumba cha mwanae kilivyobadilika. Alikuwa amenunua vipodozi vingi na kuvijaza mezani, pia alikuwa amenunua nguo nyingi alizozijaza kwenye begi kubwa. Mashuka na mablanketi nayo yalikuwa mapya!…Bi Patricia akabaki mdomo wazi.
Alishindwa kuelewa ni nani aliyemnunulia Geneviv vitu hivyo ambavyo kwa harakaharaka aliviona kuwa na thamani kubwa. Akiwa bado anashangaa mabadiliko makubwa aliyokuwa nayo Geneviv, aliona ujumbe kitandani na kwenda kuusoma. Ulikuwa umeandikwa na Geneviv akieleza kuwa wasimtafute na chochote ambacho kingemtokea kisihusishwe na mtu yeyote.
Bi Patricia hakuyaamini macho yake baada ya kuusoma ujumbe ule. Akiwa bado amepigwa na butwaa, aliona kiboksi kidogo chenye dawa kikiwa pembeni ya kitanda cha Geneviv. Akakisogelea na kukichukua. Alipokitazama vizuri alijikuta akisisimkwa na mwili kupita kawaida. Zilikuwa ni dawa ambazo alizigundua haraka kuwa ni za kusafisha kizazi na nyingine zikiwa ni vidonge vya kuzuia mimba, alijikuta akiishiwa nguvu. Mpaka hapo alishapata picha kamili ya kilichokuwa kikiendelea.
Akatoka na kurudi sebuleni ambako alimkuta Alice akiendelea kusafisha na kupanga vyombo. Alimtazama kwa hasira akiamini yeye ndie chanzo cha Geneviv kuharibika.
“Hebu niambie ukweli, mwenzio yuko wapi?” Bi Patricia alimbana Alice na kutaka amueleze ukweli aliko Geneviv. Alice akawa anatetemeka kwa hofu. Akazidi kubanwa kwa maswali mfululizo na mwisho akajikuta akitoa siri.
“Mama ukweli ni kwamba Geneviv anaumwa sana tumbo…tusamehe ni shetani alitupitia, mimi ndio niliempeleka kutoa mimba tukiogopa kukuumiza zaidi kwa kuwa ulikuwa bado hujapona vizuri, lakini kwa bahati mbaya daktari alimkosea, tusamehe mama.” Whaaat! Geneviv ametoa ujauzito, Mungu wangu wee, ni nani aliyempa? Bora angejifungua tu ningelea mjukuu, si ameshaharibika moja kwa moja sasa, Oooh My Lord, kwanini matatizo hayaniishii mimi? Nimekosa nini kwa Mungu maskini mimi! Bi Patricia aliongea kwa uchungu na kuanza kulia.
“Mama usilie, utaanza kuumwa tena, Geneviv atapona tu, mbona hata mimi iliwahi kunitokea na nikapona” alikuwa akiongea Alice akimbembeleza Bi Patricia. Kauli ile ilimfanya Bi Patricia amtazame usoni Alice kwa hasira. Pamoja na kuwa yeye ndio alikuwa chanzo, alijikuta akimuonea tena huruma. Hakuna kitu ambacho kilikuwa kikimuogopesha kama kutoa ujauzito.
Akajikuta akijifikiria jinsi watoto wa siku hizi walivyoharibika. Enzi wakati yeye akikua, ilikuwa ni vigumu sana kwa watoto wadogo kama Alice kujihusisha na umalaya na kujikuta wakitoa mimba zisizohesabika. Ilikuwa ni kama laana. Akapiga moyo konde na kuamua kuangalia njia ya kumsaidia Geneviv ingawa tayari alikuwa amechelewa. Wakaanza kumtafuta na kazi haikuwa ngumu kwani Alice alimpigia simu na kumuuliza alipo huku mama yake akisikiliza.
Geneviv alijibu huku akilia kuonyesha kuwa hali yake ndio inazidi kuwa mbaya. Kwa haraka Bi patricia akiongozwa na Alice wakatoka na kuanza kukimbia kuelekea kule walikoelekezwa na Geneviv. Alikuwa ameenda kujificha kwenye nyumba moja ya kulala wageni iliyokuwa mbali kidogo kutoka pale walipokuwa wanaishi. Wakawa wanamfuata mbio mbio ili kuwahi kumuokoa.
Kila aliyemuona Bi Patricia akikimbia mitaani alishangaa na wengine wakawa wanahisi kuwa labda amerukwa na akili kwani ni siku hiyohiyo ndio alikuwa ametoka Hospitali. Baadae wakafika pale walipoelekezwa. Wakaingia mpaka mapokezi ambapo baada ya kuulizia waliambiwa kuwa binti huyo aliingia muda mchache uliopita ingawa alikuwa akionekana amezidiwa sana.
“Yuko chumba gani jamani, ni mwanangu…” Aliongea Bi Patricia huku akihema kwa nguvu. Nguo alizozivaa aliziona kama mzigo, akawa anahaha huku na kule kama aliyepagawa. Yule mhudumu wa mapokezi alitoka na kuwapeleka chumba alichoingia Geneviv. Walipofika karibu na mlango walisikia Geneviv akilia kwa uchungu na ghafla akanyamaza, kukawa kimya…
“Geneviv! Geneviv! Fungua mlango, ni mimi mama yako… fungua please, sikufanyi chochote mwanangu…”
Bi Patricia alikuwa akigonga mlango kwa nguvu huku akimsihi mwanae Geneviv afungue kwani alikuwa amejifungia kwa ndani. Pamoja na kugonga kwa nguvu kwa muda mrefu, bado kulikuwa kimya kabisa.
“Tuvunje mlango…inawezekana amepoteza fahamu ndani. Tumuwahi asije akapoteza maisha.”
“Ngoja nikachukue funguo ya akiba,msivunje kwanza mlango.”
Mhudumu alitoka mbio kwenda kuchukua ufunguo wa akiba. Bi Patricia alikuwa hajiwezi kwa wasiwasi. Hakujua mwanae ana hali gani mle ndani. Sekunde chache baadae mhudumu alirejea na funguo mkononi. Wakafungua mlango na wote wakaingia ndani.
“Mungu wangu weee! Mwanangu jamani…uuuuwii!” Bi Patricia alianza kupiga mayowe kwa sauti. Geneviv alikuwa amejilaza sakafuni akiwa amelalia tumbo,mwili wake ukiwa umetulia tuli. Ilionekana kama maumivu yalikuwa yamemzidia kiasi cha kumfanya apoteze fahamu.
Je nini kitaendelea? Tukutane wiki ijayo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1
Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...
-
Ni wiki nyingine ambapo mwenyezi Mungu ametujaalia kukutana katika busati letu la mahaba ambapo tunajadiliana mambo mbalimbali yanayohusu ...
-
HASH POWER 7113 NI matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa. Ni wiki nyngine tunapokutana kwenye busati letu ambapo tunajuzana na kuja...
No comments:
Post a Comment