Wednesday, May 19, 2010

MADHARA YA KUVAA VIATU VYENYE VISIGINO VIREFU

KULINGANA na utafiti uliofanywa hivi karibuni na wataalamu wa magonjwa ya miguu kwa binadamu, imebainika kuwa watu wengi huwa wanazaliwa wakiwa hawana matatizo ya miguu. Hata hivyo, kwa kupuuza taratibu za kiafya na ushauri wa wataalamu, watu wengi hupata magonjwa ya miguu wakiwa watu wazima. Taarifa hiyo inazidi kueleza kuwa, kundi lililopo kwenye hatari kubwa ni wanawake ambao inakadiriwa kuwa wanasumbuliwa na matatizo ya miguu, mara nne zaidi ya wanaume.

Wanawake huwa katika hatari kubwa kutokana na mazoea ya kuvaa viatu vyenye visigino virefu. Inaelezwa kuwa asilimia 90 ya wanawake wanaofanyiwa upasuaji mdogo au mkubwa wa miguu, huwa ni kwa sababu ya uvaaji wa viatu usiozingatia kanuni za afya kwa kuvaa viatu vyenye visigino virefu.
Sababu za wanawake kuvaa viatu vyenye visigino virefu, ni kutaka waonekane warefu, wawe na mvuto zaidi na kwenda na fasheni. Licha ya sababu hizo, uvaaji wa viatu vyenye visigino virefu (kuanzia inchi 2) huwa na madhara makubwa kuliko faida.

Kulingana na utafiti wa kitaalamu, mwanamke wa kawaida ana uwezo wa kutembea wastani wa hatua 10,000 kwa siku. Visigino virefu hufanya nguvu inayotumika kutembea hatua moja kuwa kubwa kuliko kawaida, huku vikimnyima raha ya kutembea kwa uhuru.
Visigino virefu huhamisha uzito wa mwili kutoka kwenye visigino vya miguu mpaka kwenye magoti, mapaja na kiuno, na nguvu kubwa inayotumika huishia katika viungio vya mifupa (balls and socket) na kusababisha viwe vinasuguana na kuleta maumivu.

Kwa kawaida, miguu ya binadamu, hasa visigino, vimeumbwa ili kuutegemeza uzito wa mwili juu ya ardhi. Uvaaji wa viatu virefu hufanya uzito wa mwili kubebwa na kisigino kirefu, hivyo uzito wa mwili kushindwa kusawazika.

Matokeo yake husababisha misuli na mishipa ya miguu, kiuno, mgongo na shingo kufanya kazi kubwa ya kujaribu kusawazisha uzito, kazi ambayo kwa kawaida hufanywa na visigino. Hii husababisha miguu, kiuno, na mgongo kuwa katika hatari kubwa ya kupatwa na matatizo ya kiafya, ikiwemo kuteguka na kuvunjika.

Visigino virefu hubadili muundo wa mifupa ya miguu, hivyo kusababisha magoti na misuli ya mapaja (tendons) kufanya kazi ya ziada ili kuupa mwili balansi. Kwa kuwa misuli inakuwa inafanya kazi kubwa, uwezekano wa kupatwa na maumivu makali ya miguu na kushindwa kutembea katika siku za baadae huwa mkubwa.

Visigino virefu husababisha maumivu ya visigino, damu kuvilia ndani ya miguu, mpangilio wa mifupa ya vidole kuvurugika, mishipa na misuli ya tendon kuwa mifupi, neva za fahamu kufungana na kushindwa kufanya kazi yake. Tatizo huendelea kwa vifundo vya miguu (ankle) , magoti, na mifupa ya kwenye mapaja kushindwa kujivuta na kulegea (stretch and relax) na hivyo kusuguana wakati wa kutembea, hali ambayo kama haikudhibitiwa mapema, madhara yake huwa ni makubwa kwa siku za baadaye.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...