Sunday, December 28, 2014

MY REPENTANCE (KUTUBU KWANGU)- 4


ILIPOISHIA:
Kwa kuwa nilikua nimevaa taiti na sidiria tu huku juu nikiwa nimejifunga mtandio mwepesi, umbo langu lilionekana vizuri kabisa, uzalendo ukamshinda Ibrahim, akanitamkia:
“Kumbe umeumbika hivi? Loh, mpenzi wako anafaidi.” Nikacheka sana kwa furaha kwani nilichokuwa nakitaka, kilikuwa kimetimia. Tayari Ibrahim alishaanza kuonesha dalili za kunitaka kimapenzi.
SASA ENDELEA...
Unajua sisi wanawake wengi huwa tunapenda sana kusifiwa, na mtu akishaanza kukusifia, basi ukijirahisisha kwake, lazima mwisho muishie kuwa wapenzi. Baadhi ya wanaume wanaujua udhaifu wetu huu na wamekuwa wakipitia humohumo kukidhi haja za miili yao.
Basi nikazidi kuringa mtoto wa kike, nikamtoa wasiwasi kwamba hakuna mtu yeyote anayenimiliki, nipo ‘singo’.
“Unasema kweli upo singo?”
“Ndiyo, kwa nini huamini?”
“Unajua wanawake wazuri kama wewe mara nyingi huwa hawawezi kuwa singo, tena wengine wanakuwa na mpenzi zaidi ya mmoja.”
“Wala mimi sipo hivyo, wazazi wangu wakali sana na hawapendi kabisa nijihusishe na mambo hayo ndiyo maana nimeamua kuweka nguvu zangu zote kwenye masomo,” nilisema huku nikiyarembua macho yangu mazuri, kauli ambayo ilionesha kumfurahisha sana Ibrahim.
Kwa kuwa sikuwa na nguo nyingine za akiba, ilibidi nivae nguo zangu juu ya zile zilizoloana, tukatoka na Ibrahim na kuanza kutembea kuelekea kwenye gari. Tayari akili za Ibrahim zilishabadilika kabisa kwa sababu hata wakati tukitembea, alikuwa anataka nitangulie mbele kidogo halafu akawa ananitazama kwa nyuma kwa kuibia. Nililijua hilo, nikazidisha vituko.
Basi tulifika kwenye gari, tukaingia na safari ya kurudi nyumbani ikaanza, mazungumzo kati yangu na Ibrahim yalianza kubadilika taratibu, akawa ananiuliza mambo mbalimbali kuhusu maisha yangu kuanzia vitu ninavyovipenda, nisivyovipenda, ratiba yangu ya maisha ya kila siku na mambo mbalimbali kuhusu maisha yangu.

Nilimjibu kila kitu alichotaka kukijua, hatimaye tukafika Morocco. Akasimamisha gari kituoni kisha tukaagana, nilipotaka kushuka, aliniita jina langu, nikageuka na kumtazama.
“Kuna jambo nitakwambia baadaye kwenye simu, tafadhali usikatae,” alisema huku akiwa amevaa uso uliokuwa na ujumbe mzito kwangu, nilitabasamu na kumtoa wasiwasi, nikashuka.

“Chukua hizi zitakusaidia matumizi yako madogomadogo,” alisema Ibrahim huku akinipa noti kadhaa za shilingi elfu kumikumi. Nilizipokea na kumshukuru, nikabeba furushi langu la mchanga na kuanza kuondoka kuelekea nyumbani. Naye aliwasha gari lake na kuondoka.
Kwa kuwa ule mchanga wala sikuwa na kazi nao, nilipofika mbele kidogo niligeuka na kumuangalia Ibrahim, nilipoona ameshaondoka, niliutupa ule mchanga na kuanza kuchekelea ujanja nilioutumia mpaka kumuingiza Ibrahim kwenye mtego.
Nilipofika nyumbani, nilipitiliza bafuni kuoga kisha nikabadilisha nguo na kutulia chumbani kwangu, nikiendelea kumuwaza Ibrahim. Mara simu yangu iliita, nilipotazama namba ya mpigaji, alikuwa ni Ibrahim, nikatabasamu na kuipokea nikiwa na shauku kubwa ya kutaka kumsikia anachotaka kuniambia.
Alianza kwa kunisalimia, ila safari hii alikuwa akizungumza kwa sauti tulivu iliyobeba hisia nzito ndani yake. Nikamchangamkia kama kawaida yangu, akaniuliza kama nimeshalala, nikamjibu bado nasubiri nile chakula cha usiku kisha nifanye kazi niliyopewa chuoni.
“Ooh! Napenda sana mtu anayejali masomo, kazania elimu si unajua ndiyo urithi wetu?” alisema Ibrahim kisha tukaendelea na mazungumzo ya hapa na pale, bado shauku yangu ya kutaka kusikia anataka kuniambia nini ikiwa kubwa.
Cha ajabu, mpaka ananiaga, wala hakuniambia kitu ambacho aliniahidi jioni ile wakati akinishusha kwenye gari kwamba ataniambia na akanisihi nisimkatalie. Mtoto wa kike uvumilivu ukanishinda, ikabidi nimuulize. Maskini Ibra! Alibabaika sana na kuishia kuchekacheka mpaka alipokata simu.
Nilichokigundua ni kwamba Ibrahim alinipenda na alikuwa akitaka kunitongoza lakini aibu zilimjaa mkaka wa watu. Inavyoonekana hakuwa fundi wa kutongoza kama walivyo wanaume wengine. Hata hivyo kwa kuwa mimi ndiyo nilikuwa nyota wa mchezo, nilijiapiza kumfanya aweze kutongoza ili azma yangu itimie.
Alipokata simu, nilianza kumchokoza kwa meseji, nikamwambia kama ameshindwa kuniambia basi anitumie meseji. Akanijibu kwamba jambo lenyewe ni la kawaida wala nisiwe na wasiwasi. Bado sikukubali, nikaendelea kumganda kama ruba.
Wakati mwingine nilianza kuhisi kwamba Ibrahim hakuwa mwanaume wa kawaida kwa kile alichokuwa amekifanya. Mategemeo yangu yote nilidhani kwamba Ibrahim angenitongoza lakini matokeo yake, mwisho wa siku akakata simu bila kunitongoza na hata tulipokuwa tukichati hakutaka kufanya hivyo.
Mwanamke mimi, wakati mwingine nilijishtukia, nilitamani kukutana naye na kumwanzishia mazungumzo ya kimapenzi, sikupenda kabisa kila tunapokutana au kuongea simuni, alikuwa akisisitizia sana suala la elimu.
Nilimpenda Ibrahim na kila siku niliamini kwamba hata yeye mwenyewe alinipenda japokuwa hakutaka kuweka wazi. Hisia kali za mapenzi bado ziliendelea kuuchoma moyo wangu, nilikuwa nikimtamani Ibrahim leo kesho aniambie maneno ya kimapenzi na mwisho wa siku tuwe wapenzi, tupendane kama walivyokuwa wapenzi wengine.
“Ibrahim, mbona unanifanyia hivi? Mbona hautaki kuniambia ukweli kila siku unanirusha roho tu jamani?” nilijiuliza kana kwamba Ibrahim alisimama mbele yangu.
Sikujua kitu gani kilichomfanya Ibrahim kuchukua muda mrefu kabla ya kuniambia ukweli juu ya hisia alizokuwa nazo juu yangu. Si kwamba Ibrahim hakuwa akinipenda, hapana, alinipenda sana kwani hata macho yake yalikuwa yakidhihirisha hilo.
“Sasa anataka kuniambia nini?” nilijiuliza.
Wakati mwingine sikutaka Ibrahim anitongoze kwa sababu sisi wanawake unapomfanyia mwanaume mambo mengi ya kimapenzi huku ukimuoneshea ishara zote za kimahaba, hatakiwa kukutongoza bali anatakiwa kufanya mambo yote kama wapenzi, yaani leo kukushika kiuno na kesho kukubusu mdomoni.
Hiyo ndiyo hulka yetu. Kama unapata nafasi ya kumuoneshea mwanaume kila kitu halafu baadaye akaja na kukutogoza, huwa tunashangaa kwa sababu kitu ambacho huwa tunakitarajia ni kuona akianza kuonyesha mapenzi kwa vitendo, yaani kutushika hapa na pale na mambo mengine mengi ya kimahaba.
Mpaka kufikia hapo, tayari nilimuoneshea Ibra ishara zote, aliishia kunisifia tu. Japokuwa nilizifurahia sifa zake lakini bado nilitaka atamke maneno ya kimapenzi, ajaribu kunitongoza na mimi kumkubalia tu.
Ibrahim hakutaka kufanya hivyo, kitu ambacho kilikuwa kikinikera zaidi ni pale tunapokutana au kuongea halafu kuniuliza kuhusu masomo yangu tu.
Ibrahim hakutakiwa kufanya hivyo, alitakiwa kunioneshea kwamba yeye ni mwanaume anayejiamini, alitakiwa kuniambia maneno ya kimapenzi kwa sababu hicho ndicho kilikuwa kitu pekee nilichokuwa nikikitarajia kutoka kwake.
“Au hanitaki? Lakini haiwezekani, mbona kila nikimwambia twende sehemu tunakwenda? Mbona kila nikimwambia fanya hiki anafanya? Sasa kwa nini hataki kunitongoza? Au nimekuwa mbaya?” nilijiuliza maswali mengi lakini sikupata jibu.
Kuna kipindi nilikuwa nikiinuka kutoka kitandani na kukifuata kioo changu, ninapokifikia ninaanza kujiangalia huku nikiwa na nguo na mwisho wa siku navua nguo zote.
Umbo langu bado lilikuwa bora, sura yangu bado ilikuwa ikivutia na nilikuwa na uhakika wa kumteka mwanaume yeyote ambaye alikuwa akiniona kwa mara ya kwanza.
Sasa kwa haya yote, sura yangu na umbo langu bado tu Ibrahim hakuona kwamba ninatakiwa kuwa msichana wake, anipende na kunithamini? Bado Ibrahim hakuona kwamba nilikuwa msichana ninayestahili kutongozwa na mtu kama yeye?
Bado kichwa changu kilikuwa na maswali mengi yasiyokuwa na majibu, niliendelea kumfikiria huyu Ibrahim ambaye kila siku alinifanya kuwa na presha kubwa lakini hakuonekana kujali.
Kioo kilinitia moyo, ni kweli nilikuwa mrembo haswa lakini ukimya wa Ibrahim wa kutotaka kunitongoza ulinifanya nimshangae kila siku.
Wakati mwingine nilijitahidi sana kusoma makala mbalimbali za mapenzi ili kuona ni kwa jinsi gani unaweza kumtongoza mwanaume ambaye ulikuwa ukimpenda lakini yeye hakukwambia kitu japokuwa macho yake yalionesha kila kitu.
“Au nimtongoze mimi? Lakini yeye si ameshindwa bwana, kama vipi nimtongoze mimi mwenyewe,” nilijisemea.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...