Niliolewa na mume wangu kipenzi, Ibrahim au Ibra kama mwenyewe nilivyozoea kumuita ambaye alikuwa akifanya kazi kwenye benki moja maarufu ambayo sitaitaja jina kwa sababu maalum, iliyopo hapa jijini Dar es Salaam.
Kabla Ibra hajanioa, tulidumu kwenye uchumba kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja, kipindi hicho nikiwa nasoma chuo kimoja cha uhasibu kilichopo Posta, katikati ya Jiji la Dar es Salaam, nikiwa ndiyo kwanza nimeanza mwaka wa kwanza.
Baada ya ndoa, mimi na Ibra tulihamia Mbezi Beach kwenye nyumba yetu ambako tuliishi pamoja mpaka tulipokuja kutengana kwa sababu ambazo ndizo hasa zilizonifanya nitafute nafasi hii ya kutubu hadharani na kukiri kwa kinywa changu yote niliyowahi kuyafanya.
Nimesukumwa kuja kusimulia mkasa wangu huu kwa sababu nataka watu wajifunze kupitia maisha yangu na Ibra. Najisikia aibu sana, najikaza tu kwa sababu nataka wanawake wenzangu waelewe kilichonitokea na kamwe wasifuate njia kama ambazo mimi nilipita. Pia iwe funzo kwa wanaume, hasa wale ambao wapo ndani ya ndoa.
Nasikitika kwamba nimekuwa kikwazo kikubwa katika maisha ya Ibra, mwanaume niliyetokea kumpenda kwa moyo wangu wote lakini kwa sababu ya mapungufu ya kibinadamu ambayo nitayaelezea, nikageuka na kuwa mwiba mkali kwenye maisha yake.
Nilisema tangu awali na nitaendelea kusema kwamba sijawahi kutokea kumpenda mwanaume kama nilivyompenda Ibra ila hata sielewi ni kitu gani kilichosababisha haya yote yatokee.