Wednesday, August 19, 2015

CRUEL WORLD (DUNIA KATILI)- 1

Mwandishi: Hashim Aziz
“Sukuma! Sukumaaa! Jikaze mwanangu... moja... mbili... tatu... haya sukumaaa!” sauti ya mkunga wa jadi, Mama Anunu ilisikika kutoka ndani ya kibanda cha nyasi na miti, akimhimiza msichana mdogo aliyekuwa na ujauzito mkubwa, Adelina kujitahidi ili hatimaye ajifungue.
Licha ya ujauzito wake kutimiza umri wa miezi kumi na moja, Adelina alishindwa kabisa kujifungua. Alishahangaika sana kwenye hospitali mbalimbali bila mafanikio, alishapewa dawa za kuongeza uchungu mara kadhaa bila mafanikio, mwisho ndipo aliposhauriwa kwenda kwa mama Anunu.
Mwanamke huyo, licha ya kuzuiwa na serikali kufanya shughuli za ukunga nyumbani kwake na badala yake akaambiwa awe anawapa washauri waende hospitali na kwenye vituo vya afya kwa usalama wao, bado aliendelea na kazi yake kwa siri, akiwasaidia wengi ambao ujauzito wao ulikuwa na matatizo na wale ambao hawakuwa na uwezo wa kusafiri mpaka hospitalini, kilometa nyingi kutoka eneo hilo.


“Kwani mume wako yuko wapi?” mama Anunu alimuuliza msichana huyo ambaye alishindwa kutoa majibu zaidi ya kuendelea kulia kwa maumivu makali kutokana na uchungu wa kujifungua kumzidia.
“Si nakuuliza, kwani mumeo yuko wapi?”
“A...li..ni...ka..taa.”
“Alikukataa? Kwa nini alikukataa?”
“Mke wa...ke ali...jua ka...ma ana...msaliti...”
“Mungu wangu, we mtoto, kumbe ulikuwa unatembea na mume wa mtu?”
“Nisa...idie ma...ma na...ku...fa,” alilalamika Adelina huku akilishika tumbo lake.
“Nitakusaidia mwanangu lakini kwa uzoefu wangu, lazima utakuwa umefungwa kitanzi na mwenye mume wake ndiyo maana mpaka leo hujajifungua. Inabidi nikupe dawa nyingine za kienyeji ili kufungua hicho kitanzi,” alisema mama Anunu na kukimbilia chumbani kwake. Muda mfupi baadaye alitoka akiwa na kibuyu cheusi na kuanza kukitingisha kwa nguvu.
Alipokifungua, kilitoa gesi kama ile inayotoka kwenye chupa ya soda inapofunguliwa kisha akamnywesha Adelina na dawa nyingine akaimimina kwenye kiganja cha mkono wake na kumpaka kwenye viungo vyake vya uzazi.
Muda mfupi baadaye, chupa ya uzazi ilipasuka na kusababisha maji yaanze kumtoka kwa wingi, yakafuatiwa na damu nyingi zilizoambatana na maumivu makali ya tumbo hasa eneo la kiunoni yaliyosababisha msichana huyo aanze kupiga kelele kwa nguvu.
“Ukilia unapoteza nguvu za kumsukuma mtoto, jikaze huo ndiyo uanamke, sukumaaa... sukumaaa,” mama Anunu aliendelea kumhimiza msichana huyo mdogo asukume mtoto.
Licha ya kumuelekeza hata mkao wa kukaa ili iwe rahisi kujifungua, bado Adelina hakuweza kufanikiwa kujifungua, kibaya zaidi damu nyingi zikawa zinaendelea kumtoka, hali iliyoanza kutishia uhai wake.
Licha ya ukongwe wake katika kazi ya ukunga hasa kuwazalisha wanawake ambao mimba zao zilikuwa zimepitiliza umri, hali ilionekana kumuelemea mama Anunu kiasi cha kumfanya kijasho chembamba kiwe kinamtoka licha ya baridi kali iliyokuwa inapenya mpaka ndani ya nyumba hiyo.
“Jamani msaada! Naombeni msaada, mzee Mtwivila... msaada jamani,” Mama Anunu alisema huku akitoka na kutimua mbio kuelekea kwa jirani yake, Mzee Mtwivila ambaye ndiye pekee aliyekuwa na usafiri wa pikipiki au bodaboda kama wengi wanavyopenda kuuita.
“Kuna nini tena jirani?”
“Kuna mgonjwa amezidiwa, anapoteza damu nyingi anaweza kupoteza maisha.”
“Kwani hujaacha kuzalisha watu hapo nyumbani kwako? Kweli wewe unataka kwenda kuozea jela.”
“Jirani nikiacha unafikiri nitakula wapi? Nisaidie, huu siyo muda wa kunisimanga.”
“Sasa tutamsafirishaje kwenye bodaboda?”
“Twende hivyohivyo tutajua mbele ya safari, washa pikipiki,” alisema mama Anunu huku kijasho chembamba kikizidi kumtoka kiasi cha kulowanisha gauni alilokuwa amelivaa.
***
Dr. Richard Mkisi, alikuwa ni daktari maarufu wa magonjwa ya wanawake ambaye licha ya kufanya kazi katika hospitali kubwa ya wazazi ya Meta jijini Mbeya, pia alikuwa akimiliki kituo maarufu cha afya alichokiita Saint Camilius Health Centre, kilichokuwa kikitoa huduma mbalimbali za afya.
Licha ya udogo wa kituo hicho, kilikuwa na chumba maalum cha kuhifadhia maiti kilichokuwa na majokofu ya kisasa na vifaa vyote muhimu vilivyokuwa vinahitajika kwa ajili ya kuhifadhi maiti bila kuharibika.
Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa mtu yeyote wa nje kugundua kwamba ndani ya kituo hicho kidogo lakini maarufu, kulikuwa na mochwari ya kisasa namna hiyo. Ni watu wachache tu ndiyo waliokuwa wakijua kuhusu suala hilo.
Kutokana na kituo hicho kujengwa katika eneo lenye mkusanyiko mkubwa wa watu la Mbalizi, Mbeya, muda wote wagonjwa walikuwa hawaishi ndani ya kituo hicho ambacho pia kilikuwa na wodi kadhaa kwa ajili ya kulaza wagonjwa waliozidiwa.
Pia kilikuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa maeneo mengine ya mbali hasa Chunya ambapo wananchi wengi walikuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu, tena kwenye barabara ya vumbi kufuata huduma za afya katika kituo hicho.
“Mwingine aingie,” Dokta Mkisi alisema akimaanisha mgonjwa mwingine aingie ndani ya chumba cha daktari baada ya kuwa ameshamaliza kumhudumia mgonjwa wa awali.
“Dokta! Dokta, kuna dharura.”
“Dharura? Dharura gani tena?”
“Kuna mdada kaletwa sasa hivi kutoka Makongolosi, Chunya, ana hali mbaya sana.
“Yuko wapi?”
“Yuko hapo nje ndiyo wanamshusha, anashindwa kujifungua na amepoteza fahamu kabisa,” alisema nesi mmoja huku akitweta, harakaharaka wote wakatoka mpaka nje.
Wakaenda kwenye gari lililomleta mgonjwa huyo ambapo harakaharaka kitanda chenye magurudumu kilisogezwa, msichana mdogo akateremshwa na kulazwa juu yake, akiwa ameshapoteza fahamu kutokana na kutokwa na damu nyingi.
“Mungu wangu, kwa nini mmemchelewesha namna hii?” Dokta Mkisi alimuuliza mwanamke aliyekuwa ameongozana na mgonjwa huyo ambaye naye nguo zake zote zilikuwa zimelowa damu.
“Tumetoka mbali dokta, tumetoka Makongolosi, Chunya na kama unavyojua usafiri wa kwetu ni mgumu sana.
“Mgonjwa anaitwa nani?”
“Anaitwa Adelina.”
“Jina lake la pili?”
“Silijui, ni msamaria mwema tu nimemkuta amezidiwa ndiyo nimejitolea kumsaidia.”
“Wewe unaitwa nani?”
“Naitwa Safina Musa ila wengi wamenizoea kwa jina la mama Anunu,” Dokta Mkisi alikuwa akimhoji mwanamke huyo huku wakitembea harakaharaka kuelekea chumba cha kujifungulia (labour) ambako msichana yule mdogo aliingizwa.
Dokta Mkisi alipoingia tu, alikuta tayari manesi wake wenye ari na kazi wameshaandaa vifaa vyote muhimu vilivyokuwa vinahitajika kwa ajili ya kumsaidia msichana huyo kujifungua.
Harakaharaka akaanza kumpima vipimo mbalimbali, yakiwemo mapigo yake ya moyo, shinikizo la damu na vipimo vingine muhimu, akatundikiwa dripu na kazi ya kumzalisha ikaanza.
Hata hivyo, Dokta Mkisi alikumbana na kikwazo kikubwa kwa sababu licha ya kumpa dawa za kumzindua msichana huyo, hakurejewa na fahamu zake hivyo hakuwa na uwezo wa kusukuma mtoto wala kufanya chochote.
“Hali ni mbaya, kuna uwezekano mkubwa tukawapoteza wote wawili,” Dokta Mkisi alisema huku akishusha pumzi ndefu. Kutokana na uzeofu mkubwa aliokuwa nao katika kazi yake, alijua kuwa kwa mujibu wa sheria za kidaktari, ana machaguo matatu kwa wakati huo.
Chaguo la kwanza lilikuwa ni kuwaokoa wote wawili, mama na mwanaye aliyepo tumboni. Chaguo la pili lilikuwa ni kumuokoa mama pake yake na kama hilo nalo lingeshindikana, basi angelazimika kutumia chaguo la tatu ambalo lilikuwa ni kumuokoa mtoto.
Kazi iliendelea kwa muda mrefu ndani ya wodi hiyo, kila mbinu aliyoitumia kujaribu kuokoa maisha ya wawili hao ilionekana kushindikana kwani Adelina hakuwa na fahamu hata kidogo na kadiri muda ulivyokuwa unazidi kusonga mbele, ndivyo mapigo ya moyo wake yalivyokuwa yakizidi kushuka kutokana na kupoteza damu nyingi.
“Inabidi tumfanyie upasuaji haraka iwezekanavyo, vinginevyo tutawapoteza wote wawili,” alisema Dokta Mkisi, ikabidi harakaharaka Adelina ahamishwe kutoka ‘labour’ na kukimbizwa kwenye chumba cha upasuaji ambapo aliandaliwa na muda mfupi baadaye, Dokta Mkisi akawaongoza wenzake kumfanyia upasuaji msichana huyo.
Kwa bahati nzuri, walifanikiwa kumtoa mtoto wa kiume akiwa hai japokuwa alikuwa amechoka sana. Akakimbizwa kwenye chumba maalum huku Dokta Mkisi akiendelea na kazi ya kumshona Adelina ambaye bado hakuwa amerejewa na fahamu zake. Jeraha likashonwa vizuri kisha msichana huyo akarudishwa wodini lakini kadiri muda ulivyokuwa unazidi kusonga mbele ndivyo hali yake ilivyozidi kuwa mbaya, chupa nyingi za damu zikawa zinatiririka kuingia kwenye mishipa yake kufidia kiwango kikubwa alichopoteza wakati wa kujifungua lakini bado haikusaidia kitu.
“Dokta! Dokta! Hali ya mgonjwa inazidi kuwa mbaya, twende ukajionee mwenyewe,” alisema nesi mmoja na kumshika mkono Dokta Mkisi, wakatoka mbiombio mpaka kwenye wodi aliyokuwa amelazwa msichana huyo.
Walipofungua mlango tu, walipokelewa na mlio wa mashine kadhaa alizokuwa ameunganishiwa msichana huyo, zikitoa mlio kuashiria kwamba tayari mgonjwa alikuwa amekata roho.
“Mungu wangu, amekufa?” Dokta Mkisi alisema kwa mshtuko, akiwa ni kama haamini alichokuwa anakiona mbele ya macho yake. Msichana huyo alikuwa amelala kimya kabisa kitandani, akamsogelea akiwa na kifaa cha kupimia mapigo moyo, akamgusisha kifuani na kusikiliza kwa sekunde kadhaa, akatingisha kichwa akimaanisha tayari roho yake ilikuwa imeshatengana na mwili.
Baada ya ukimya uliotawala kwa zaidi ya dakika tatu, hatimaye Dokta Mkisi aliwaamuru manesi wafanye taratibu zao za kawaida mtu anapokata roho. Kitanda alichokuwa amelazwa Adelina kikazungushiwa mapazia ya rangi ya kijani kisha vifaa vyote vilivyokuwa vinatumika kumtibu vikatolewa na kupelekwa sehemu maalum ya kuvisafishia kabla ya kurudishwa stoo.
Kitanda kilichokuwa na mwili wa Adelina kikaanza kusukumwa taratibu kuelekea kwenye mochwari kubwa na ya kisasa iliyokuwa ndani ya kituo hicho cha afya.
***
“Eeeh! Bosi, vipi habari za kazi?”
“Nzuri dokta, vipi kuna habari mpya?”
“Yaah! Nimekupigia kukupa taarifa kwamba tumepata mzigo mpya mmoja, nafikiri utafaa kwa kazi yetu.”
“Ooh! Safi sana, ndiyo maana nakupenda dokta, ni wa aina gani?”
“Mwanamke, amefariki akijifungua.”

Je, nini kitafuatia? Usikose next issue!

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...