Manyunyu ya
mvua yalikuwa yakiendelea kudondoka taratibu kuashiria kumalizika kwa mvua
kubwa iliyonyesha mfululizo usiku kucha. Tofauti na siku zote, watu walikuwa
wachache sana barabarani japokuwa tayari kulishapambazuka. Ubaridi ulioambatana
na mvua hiyo, ulimfanya kila mmoja kutamani kuendelea kuvuta shuka na kuuchapa
usingizi.
“Hee! Tayari
ni saa moja? Mungu wangu, nitachelewa kazini,” Edmund Katera ‘Mundi’, kijana
mdogo aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni kubwa ya mawasiliano ya Hashcom
Mobile kwenye kitengo cha Teknolojia ya Mawasiliano (Information Technology) alikurupuka
kutoka usingizini na kukimbilia kwenye kabati lake la nguo kwa lengo la
kuchukua taulo.
Harakaharaka
akatoka mpaka nje na kuchukua ndoo ya maji ya kuoga huku mswaki ukiwa mdomoni,
akatembea kwa hatua za haraka mpaka bafuni ambapo alijimwagia maji bila kujali
ubaridi uliokuwepo asubuhi hiyo kutokana na mvua iliyokuwa inaishia.
Muda mfupi
baadaye, tayari alikuwa amerejea chumbani kwake, akavaa na baada ya dakika
chache, alikuwa ameshajiandaa, akajitazama kwenye kioo kikubwa cha ‘dressing
table’ iliyokuwa ndani ya chumba chake na baada ya kuridhishwa na mwonekano
wake, alitoka na kufunga mlango wa nyumba aliyokuwa anaishi, akatoka na kuianza
safari ya kuelekea kazini.
Kwa jinsi
barabarani kulivyokuwa na matope na foleni kubwa ya magari barabarani kutokana
na mvua hiyo kama ilivyo desturi ya Jiji la Dar es Salaam hasa nyakati za mvua,
ukizingatia kwamba tayari alikuwa nyuma ya muda kutokana na kuchelewa kuamka,
hakuwa na ujanja zaidi ya kukodi bodaboda.
“Naenda
Bamaga, Mwenge.”
“Buku nne tu
mwanangu.”
“Aaah! Buku
nne mi sina, nitakupa buku mbili jero.”
“Unaua
mwanangu, ok poa twenzetu,” dereva wa bodaboda alimwambia Edmund ambaye bila kupoteza
muda, alikwea kwenye bodaboda na safari ikaanza. Dereva huyo wa bodaboda akawa
anapenya kwenye foleni, wakati mwingine akilazimika kupita katikati ya magari
yaliyokuwa yamefungana kwa lengo la kumuwahisha mteja wake sehemu aliyokuwa
anaenda.
Hata hivyo,
haraka hizo zilienda kuishia eneo la Sinza Afrika Sana ambapo magari kutoka
kila upande, yalikuwa yamefungana eneo hilo lililokuwa na makutano ya barabara
nne, moja inayotokea Shekilango, nyingine inayotokea kwenye taa za kuongozea
magari za Bamaga, inayotokea kituo cha polisi cha Mabatini na ile iliyokuwa
inatokea Mwenge kwa kupitia ofisi za TRA.
Kwa jinsi
magari hayo yalivyokuwa yamefungana, haikuwa rahisi hata kwa mwenda kwa miguu
kukatisha katikati ya magari hayo, manyunyu ambayo yalikuwa yamepungua yakaanza
kuongezeka na kusababisha kero kubwa kwa wasafiri waliokuwa wakitumia bodaboda,
akiwemo Edmund ambaye tayari shati lake nadhifu alilokuwa amelivaa lilianza
kulowa.
“Pipiiii!
Pipiiii... Poooopooo!” milio ya honi nyingi za magari iliendelea kusikika eneo
hilo, kila dereva akijiona yeye yupo sahihi isipokuwa wengine ndiyo wanavunja
sheria za barabarani, hali iliyosababisha taharuki kubwa eneo hilo.
Ilibidi Edmund
aanze kumshinikiza dereva wake afanye kila linalowezekana kuhakikisha
wanajinasua eneo hilo kwani ukiachilia mbali ukweli kwamba alikuwa anaendelea
kuloa, alikuwa pia anaendelea kuchelewa kazini.
Wakati dereva
wa bodaboda akihangaika kuitoa pikipiki pale ilipokuwa imezingirwa na magari,
kwa bahati mbaya alijikuta akilikwangua gari lililokuwa nyuma yao na
kulibonyeza eneo kubwa na kukwangua rangi.
“Mungu wangu,
tumeharibu gari la watu,” alisema dereva wa bodaboda huku akiendelea kuhangaika
kutafuta upenyo wa kukimbia kabla mwenye gari hajashuka lakini alikuwa
amechelewa kwani mwenye gari alishashtukia kwamba amegongwa na bodaboda.
Msichana mdogo
mwenye umri wa kati ya miaka ishirini na mbili hadi ishirini na tano, mrefu
wastani, mwenye umbo lenye mvuto wa aina yake, akiwa amevalia mavazi ya kisasa
kama mtu anayefanya kazi kwenye ofisi moja kubwa mjini, chini akiwa amevaa suruali
nyeusi ya kitambaa iliyomshika kisawasawa maungo yake makubwa na shati jeupe
nadhifu, usoni akiwa amevaa miwani ya kisasa ya rangi nyeusi, aliteremka kwenye
gari la kifahari, Jeep Grand Cherokee la rangi ya fedha na kuzunguka upande ule
bodaboda iliyokuwa imembeba Edmund ilipokuwa.
“You stupid
poor boys, do you know how much it cost to buy this type of car?” (Nyie
wavulana maskini wapumbavu, mnajua inagharimu kiasi gani kununua gari kama
hili?) alisema msichana huyo kwa jazba huku akivua miwani yake aliyokuwa
amevaa, akainama kuangalia pale dereva wa bodaboda alipoligonga gari lake
wakati akirudi nyuma.
Kwa kuwa
Edmund na dereva wake ndiyo waliokuwa na makosa na ni kweli kwamba waliharibu
gari hilo ambalo hata wangeambiwa walipe gharama za kutengeneza sehemu
waliyoigonga hawakuwa na fedha, ilibidi waufyate mkia. Wakawa wanatazamana huku
kila mmoja akijisikia aibu kubwa kutokana na jinsi msichana huyo alivyokuwa
akiendelea kuwachambua, akichanganya lugha, Kiingereza cha Kimarekani na
Kiswahili.
“Please
forgive us ladyboss, its just an accident,” (Tafadhali tusamehe bosi, ni ajali
tu) alisema Edmund, kauli iliyomfanya yule msichana amgeukie na kumtazama kwa
jicho la ukali.
“Ajali?
Unazijua ajali wewe? Mtazame kwanza, nikikwambia ulipe gharama za uharibifu
alioufanya huyo maskini mwenzio utaweza? Go to hell! (Nenda kuzimu!)” alisema
msichana huyo kwa hasira, kauli iliyomfedhehesha mno Edmund.
Tayari
madereva wa magari mengine walikuwa tayari wameteremka kwenye magari yao na
kuanza kumsihi msichana huyo awasamehe Edmund na dereva wake. Kwa nyodo na
dharau akageuka na kuanza kutembea kuelekea kwenye gari lake huku akiivaa
miwani yake. Akaingia kwenye gari na kukaa nyuma ya usukani.
Edmund
aliyekuwa ameshuka kwenye bodaboda, aliendelea kulitazama gari lile, hasa pale
bodaboda yao ilipopagonga. Akiwa anaendelea kushangaa, aliona kitu chini kwenye
lami chini ya gari, bila kuonekana na mtu yeyote akainama na kukiokota.
Ilikuwa ni
simu ya kisasa iliyokuwa imedondoka chini, bila hata kuuliza akajua kwa
vyovyote lazima yule msichana aliiangusha alipoinama kuangalia gari lake.
Tayari askari wa usalama barabarani walikuwa wameshafika eneo hilo kusaidia kufungua
njia ambayo ilikuwa imefungwa na magari yaliyofungamana kila upande.
Wakati Edmund
akiwa bado anajishauri kama amrudishie msichana yule simu yake au la, tayari
barabara ilishafunguliwa na magari yakaanza kuondoka kwa kasi. Akashuhudia yule
msichana naye akibadili gia kwenye gari lake la kifahari na kuondoka kwa
mbwembwe za hali ya juu.
“Oyaa twende
mwanangu!” dereva wa bodaboda alimuita Edmund kwa sauti ya juu ambayo
ilimzindua kutoka kwenye hali aliyokuwa nayo, akaiweka simu hiyo mfukoni na
kusogea hadi pale dereva wa bodaboda alipokuwa anamsubiri, akapanda na
kuendelea na safari.
Kwa kuwa eneo
hilo halikuwa mbali na ofisini kwao, dakika chache baadaye tayari walishawasili
Bamaga, akashuka kwenye bodaboda na kumlipa dereva fedha zake kisha akaanza kutembea
harakaharaka kuelekea kazini kwao huku akiwa anaendelea kutafakari juu ya tukio
hilo lililotokea muda mfupi uliopita na jinsi alivyotolewa nishai na msichana
yule mrembo.
Je, nini
kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment