Tuesday, September 7, 2010

TOFAUTI KATI YA MWANAMKE NA MWANAUME


Ni ukweli usiopingika kuwa wanaume na wanawake hatufanani. Japokuwa sote tunafahamu kuwa hatufanani, bado wengi wetu hatujajua tofauti yetu iko wapi, au ni nini. Ni kwa kosa hili kubwa, wanaume wameendelea kuamini kuwa wao ni kundi bora kuliko wanawake, huku wanawake, nao kwa kutojua ukweli, kukubali kuwa wao ni viumbe dhaifu na wanaostahili kuongozwa katika kila jambo.

Nasema tena kuwa tofauti kati ya mwanaume na mwanamke zipo na hazikwepeki, lakini ni wajibu wa kila mmoja kutambua kuwa binadamu wote ni sawa katika mantiki ya “Ubinadamu”. Kuwa mwanaume au mwanamke hakukuongezei wala kukupunguzia chochote.


Kila mmoja amekamilika kwa vile alivyo,
Na thamani yetu kama binadamu inabaki kuwa palepale. Maisha yanakuwa na maana zaidi pale mwanaume na mwanamke wanapoungana na kuishi pamoja katika muunganiko ambao kila mmoja anafahamu yeye ni nani na mwenzake ni nani. Ukifanya utafiti utagundua kuwa hata kama familia ina mafanikio makubwa kiasi gani, kama mwanaume (baba) hajajua kuwa yeye ni nani na mwenzake (mama) ni nani na anahitaji nini, familia kama hiyo haiwezi kuwa na amanai na maisha kwao yanapoteza maana kabisa.

Kwa kushindwa kuelewa sisi ni nani na wenzetu ni nani, wengi tumeendelea kuwa wahanga wa nmaisha huku kila mmoja akimsingizia mwenzake kuwa ndio sababu ya yeye kushindwa kufikia malengo. Utakuta mwanaume analalamika kuwa mke wake ndio chanzo cha yeye kutofanikiwa, huku mke nae akilalamika kuwa mumewe ndio sababu ya yeye kushindwa kufikia malengo.

Tofauti kubwa kati ya mwanamke na mwanaume kwa sehemu kubwa zipo kwenye maumbile, jinsi mwili unavyofanya kazi, utashi, homoni, hisia, mahitaji na jinsi tunavyoyatazama mambo (Perception).

Ni kutokana na ujinga wa kutojua tofauti hizi, ndio maana ndoa nyingi zinaingia kwenye matatizo na migogoro kila kukicha, kuna kuumizana kwingi ndani ya mahusiano na mwisho kutengana kwa sababu kila mmoja (Mwanaume na mwanamke) anategemea mwenzake afanye na kutenda kama yeye bila kujua kuwa hili ni jambo ambalo haliwezekani kwa kuwa tunatofautiana katika mambo kadha wa kadha.

Ni makosa makubwa kwa mwanaume kutarajia mwanamke afanye kama yeye anavyotaka, au mwanamke kutegemea mwenzi wake amfanyie kama anavyotaka. Ni vizuri kila mmoja azifahamu tofauti zilizopo ili aweze kuishi kwa amani na mwenzake. Iwapo kila mmoja atafahamu tofauti zetu zipo wapi, migogoro na mifarakano isiyo ya lazima itaepukwa kwa kiwango kikubwa sana.

Wataalamu wengi wa mambo ya jinsia wamefanya utafiti kwa miaka mingi na kwa pamoja wamebaini tofauti zifuatazo:

UELEWA WA WANAUME
Kihulka, wanaume ni viumbe wasiopenda kufundishwa wala kushauriwa kitu kwa namna ambayo itawafanya wahisi kudharauliwa au hawajui jambo. Mwanamke anaweza kumshauri vizuri sana mumewe, kwa mfano “Mshahara wako au pesa unazopata tuzitumie kidogo na nyingine zinazobaki tuweke akiba kwa ajili ya kujenga nyumba au kusomesha watoto.”

Kimantiki huu ni ushauri wa busara sana ambao wanawake wengi huwapa wenzi wao, lakini mwanaume anapoambiwa hivi na mkewe, hasa kama mke nae hajui tofauti kati yake na mumewe, matokeo huwa ni kwa mwanaume kuhisi mkewe ameona yeye hawezi kupangilia mambo vizuri na ndio maana ameamua kumfundisha. Kitakachoendelea hapa itakuwa ni ugomvi mkubwasana na pengine mwaamke atabaki kujiuliza ni wapi alipokosea mpaka mumewe amjie juu wakati ametoa ushauri ambao ni mzuri.

Kinachosababisha ugomvi hapa ni kutojua kuwa wanaume sio watu wakufundishwa kama unavyomfundisha mtoto. Ushauri kama huu unaweza kuwa mzuri na kumfanya mwanaume ajihisi ni mwenye thamani kubwa endapo ataambiwa na mkewe wakiwa faragha, wakiwa wametulia kabisa, hali ambayo itamfanya mwanaume kujiona kama shujaa.

Wanawake wanaoijua siri hii, huwashauri waume zao mambo mazuri wakiwa vyumbani mwao, tena hufanya hivi baada ya kuhakikisha wamewafurahisha vya kutosha kwa mambo mazuri kama vile kwa chakula kizuri na tendo la ndoa lililopangiliwa vizuri. Pia mwanamke anatakiwa kuanza kutoa ushauri wake kwa kumsifia mumewe kwa yale mazuri ambayo amekwisha yafanya hata kama ni machache na madogo.

Kitu kingine ambacho kihulka ni tabia ya wanaume ni kupenda kutoa au kupewa suluhisho la moja kwa moja. Mwanaume anapoamua kumweleza mkewe hukusu jambo Fulani ambalo linamtatiza, anataka kupewa suluku ya moja kwa moja na sio kuonewa huruma. Inapotokea mwanaume anamuomba ushauri mkewe na badala ya mke kumpa ufumbuzi wa nini cha kufanya anaanza kumuonea huruma na kumsikitikia, huhisi kama hadhi yake imeshushwa sana.

UELEWA WA WANAWAKE
Tofauti na wanaume, wanawake ni viumbe wanaopenda sana kuelekezwa na kufundishwa hasa na waume zao au watu wao wa karibu. Unapomuelekeza mwanamke jambo kwa upole na ukarimu, utakuwa na nafasi nzuri ya kupendwa sana na mwanamke huyo.

Wanawake pia kupenda sana kusikilizwa wanapoeleza matatizo yao. Pamoja na hayo, hupenda sana pia kusaidiwa mambo yanayowasumbua hata kama ni madogo. Utashangaa sana kwamba hata yale mambo ambayo wanaume huyaona kuwa ni kawaida na yasiyo na uzito wowote, kuwa na maana kubwa sana kwa wanawake.

Nimewahi kusimuliwa na ndugu yangu mmoja ambaye alikuwa akinisimulia insi alivyokutana na mke wake wa sasa. Alinieleza kuwa walikutana katika kituo cha daladala wakisubiri usafiri, na daladala ilipofika kutokana na msongamano wa abiria, yule mwanamke aligongwa na mwanamke mwenzake mpaka akadondosha simu na mkoba wake chini.

Ndugu yangu anasema alipoona yule mwanamke akiwa ameduwaa akiwa hajui nini cha kufanya, aliwani na kumsaidia kuokota vitu vyake chini na kumkabidhi, kisha akamsaidia kupada ndani ya daladala.
Kwa msaada huo ambao kwa mwanaume angeuona wa kawaidsa nap engine asingekumbuka hata kusema asante, yule mwanamke alijikuta akimshukuru sana ndugu yangu na walipofika mwisho wa safari, alimuomba ndugu yangu namba ya simu na huo ukawa ndio mwanzo wa uhusiano wao mpaka wakaja kufunga ndoa na kuoana.

Huo ni mfano mdogo tu wa namna wanawake wanavyopenda kusaidiwa, kusikilizwa na kuonewa huruma.
……………………………………………………………………………………………………………………………………………

Kwa kutojua tofauti hii, wanaume wengi hujikuta wakiwaudhi wake zao kutokana na kuchukulia mambo kirahisi hali ambayo husababisha manun’guniko makubwa kwa wenzi wao.

Ni vizuri wanaume wakajenga utaratibu wa kuwasikiliza wake zao au wenzi wao kwa upole na umakini wa hali ya juu. Makosa ambayo wengi huyafanya bila ya wao kujua ni pamoja na kusoma gazeti au kuangalia Tv wakati mkeo anakueleza jambo akihitaji umsikilize na pengine anahitaji umpe msaada wa nini cha kufanya (Umfundishe).

Kwa mwanaume ataona ni jambo la kawaida kusoma gazeti wakati mkewe akimueleza kero zake wakati kiuhalisia wanawake hujisika vibaya sana na kuamini kuwa hawana thamani tena na ndio waume au wenzi wao hawawasikilizi kwa makini.

WANAUME HUPENDA KUSIFIWA
Miongoni mwa vitu ambavyo wanaume wanavipenda maishani mao basi ni kusifiwa. Kwa kawaida mwanaume husikia fahari kubwa sana kusifiwa, wakati mwanamke akisifiwa sana hujihisi aibu.

Mwanaume anaposifiwa hasa na mtu anayempenda kama mke wake au mpenzi wake, yuko tayari hata kufa akitaka azidi kusifiwa zaidi. Hakuna sumu kali kama mwanamke kumkosoa mwanaume, hususani mbele ya watu wengine. Hili ni kosa ambalo wanawake wengi kulifanya pia. Unakuta mke anamkosoa na kumcheka mumewe mbele ya watoto au majirani huku akiwa hana wasiwasi kabisa kuwa anafanya makosa makubwa.

Watafiti wa mambo ya mahusiano wanaeleza kuwa tatizo la wanawake kuwahosoa wanaume, huwaumiza sana wanaume kisaikolojia na ni miongoni mwa sababu inayopelekea wanaume wengi kukosa au kupungukiwa nguvu za kiume. Pia kukosolewa huku hupelekea wanaume kushindwa kujiamini hata mbele ya wanaume wenzao na huhisi kuwa thamani yao ina walakini. Hii ni sumu mbaya sana ambayo wanawake wanapaswa kuikwepa ili kudumisha uhusiano bora na wenye kudumu.

WANAWAKE HUPENDA KUONESHWA KAMA WANAPENDWA
Inawezekana ikawa ni vigumu sana kujibu swali kuwa ni kwa nini wanawake ndio wanaotakiwa kutongozwa, wakati mwanamke akimtongoza mwanaume anaonekana hajatulia. Kihulka, imani hii inatokana na ukweli kwamba mara zote wanawake ni viumbe wanaotakiwa kupendwa kwanza ndipo nao waoneshe upendo wao.

Ni vigumu sana kuishi bila kukwaruzana na mwanamke kama anahisi kuwa humpendi wala humjali. Wakati wanaume wao wanapenda sana sifa, wanawake wanapenda sana kupendwa na wako tayari kufanya lolote ili kumfurahisha mtu anayeonesha mapenzi ya hati kwao.

Ni rahisi sana kwa mwanamke kushawishika kutembea nje ya ndoa endapo atahisi kuwa mume aliyenaye hampendi kwa dhati, wahati kuna mwingine wa nje anayeonesha mapenzi ya kweli. Ukifanya utafiti, utagundua kuwa wanaume wengi huwa wepesi wa kuwatamkia wanawake kuwa wanawapenda katika siku za mwanzo za uhusiano, lakini wakishaingia ndani ya ndoa huwa ni wagumu sana kutamka neno “Nakupenda”.

Mwanamke mmoja alikuwa akitoa ushuhuda kuwa mumewe alimtamkia neno nakupenda siku moja tu wakati anamtongoza, lakini baada ya kumkubali na kuolewa naye, yapata miaka kumi na tatu sasa hajawahi kusikia tena neno hilo kutoka kwa mumewe, na hata pale yeye anapomwambia kuwa anampenda, huwa anamjibu kwa kifupi kuwa anajua kuwa anampenda.

WANAUME HUPENDA KUJITENGA WAKIWA WAMECHOKA
Kuna usemi maarufu unaotumika duniani kote unaoelezea kuwa wanaume wametokea katika sayari ya Mars wakati wanawake wanatoka katika sayari ya Venus. Msemo huu una maana kubwa sana kwamba, mara nyingi hulka za wanaume huwa zinakinzana na za wanawake. Wataalamu wanaeleza kuwa mara nyingi wanaume akili zao zinapochoka, huwa wanahitaji kukaa peke yao mpaka akili itulie ndipo waweze kuendelea na shughuli nyingine. Wanawake wengi huwa hawaliekewei hili na kwa ujinga wao hujikuta wakizidi kuwakera waume zao.

Mfano unakuta mwanaume anarudi kazini jioni kichwa kikiwa kimechoka. Badala ya mke kumpokea kwa maneno matamu yatakayomfanya uchovu wake upungue, anaanza hoja za kichokozi huku akitoa lawama kibao, mara kwa nini ulikuwa hpokeai simu, kwa nini umechelewa kurudi, ulikuwa umeongozana na nani, na kauli nyingine zilizojaa lawama.

Ni dhahiri kuwa kwa kuwa akili ya mwanaume inakuwa imeshachoka, atakuja juu kama mbogo na uwezekano wa kumpiga mwanamke wa aina hii huwa ni mkubwa. Ukichunguza kwa makini, wanawake wanaolalamika kuwa huwa wanapigwa na waume zao, wao ndio huwa sababu kubwa ya kupigwa kwao kutokana na kushindwa kuwasoma waume zao.

WANAWAKE HUPENDA KUBEMBELEZWA WANAPOKUWA WAMECHOKA
Tofauti na wanaume ambao wakichoka hupenda kujitenga peke yao, wanawake wanapokuwa wamechoka hupendwa kubembelezwa na kufarijiwa kwa karibu. Hupenda kuwa jirani na mtu ambaye atawapa maneno matamu yatakayowafanya wasahau maswaibu na uchovu wa kutwa nzima.
Hali kuwa inakuwa mbaya katika nyumba ambayo mwanaume na mwanamke wote ni wafanyakazi. Unakuta mwanaume amerudi kazini akiwa amechoka na anahitaji muda wa kukaa peke yake mpaka akiliyake itakapotulia, upande wa pil mwanamke nae amerudi kazini akiwa amechoka sana na anahitaji kukaa jirani na mumewe kwa ajili ya kubembelezwa baada ya kazi za kutwa nzima.

Kitakachotokea hapa ni kwa mwanaume kutafuta uhuru wa kuwa peke yake. Atatoka na kwena kukaa peke yake sebuleni , ukumbini au chumbani. Kitendo hiki kitamfanya mwanamke ahisi kuwa huenda amemuuzi mumewe na ndio maana anajitenga, na ataanza kumfuatafuata kila anakokwenda. Matokeo yake ni kila mmoja kuishia kuboreka na mwenzake na hapo ndipo maudhi madogomadogo yanapoanza, na kwa wasipokuwa makini wanaweza kuishia kwenye ugomvi mkuba saa ambao chanzo chake hakieleweki.

Itaendelea

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...