Wednesday, October 21, 2009

MY HEART IS BLEEDING (MOYO WANGU UNAVUJA DAMU)-4

Mafanikio ya haraka aliyoyapata Khalfan maishani mwake yanaanza kumletea matatizo. Baadhi ya watu wameanza kumonea wivu na wameanza kupanga mbinu za kumuangamiza. Japokuwa anajitahidi kuishi vizuri na kila mtu, maadui wanazidi kuongezeka siku baada ya siku, wengi wakiwa ni marafiki zake wa karibu.

Hilo halimpi hofu kabisa kwa kuwa anaamini hana kosa lolote mbele ya maulana na anaishi maisha ya haki kila siku. Familia yake nayo inazidi kukua huku mtoto wake wa kiume Khaleed akizidi kukua na kuwa na akili za kiutu uzima akiwa angali bado mdogo.

Wanaendelea kuyafurahia maisha yao na kamwe hawako tayari kuona mtu mwingine akipata taabu. Wanawasaidia wote wenye shida na Mungu anazidi kuwabariki. Lakini ghafla mambo yanaanza kwenda mrama.
Twende pamoja…
***

Baada ya miaka kadhaa kupita, walikuwa na jumla ya watoto watano, wazuri wenye furaha na afya njema. Khalfan sasa akiitwa “mzee” khalfan na mkewe Bi Miriam waliyafurahia sana maisha yao na familia yao. Muda mwingi walikuwa sambamba na watoto wao wakiwafundisha maadili mema . Utajiri ukawa unazidi kuongezeka kila kukicha, familia yao ikiwa gumzo kila kona ya mtaaa . Wengine waliendelea kuamini na kuhusisha mafanikio yale na ushirikiana , huku wengine wakiamini kwamba mzee khalfan alikuwa amebahatisha

Lakini ukweli ni kuwa juhudi na maarifa ndivyo vilivyofanya maisha yao yawe gumzo kila sehemu . Siku zikawa zinakwenda, lakini kama walivyosema waswahili penye riziki hapakosi chuki , na ili ufanikiwe zaidi unahitaji kuishi vizuri na kila mtu ingawa huwezi kukwepa kuwa na maadui, taratibu mzee Khalfan akaanza kuhisi kuwa na maadui wasiopenda mafanikio yake, alianza kuhisi marafiki zake anaoshirikiana nao katika shughuli zake za biashara wameanza kumfanyia hila kutokana na mafanikio anayoyapata, hakukosea kabisa . Hivyo ndivyo ilivyokuwa.

Wengi wa marafiki zake waliokuwa wakija kumtembelea pale nyumbani kwake walikuwa wakiyamezea mate mafanikio yake. Wengi walimwona kama hastahili kumiliki mali nyingi na za thamani kama alizokuwa nazo, wakaanza kupanga njama kila mmoja kwa wakati wake , wote wakitaka kumiliki mali zilizokuwa chini ya uangalizi wa khalfan na mkewe Bi Miriam. Hilo halikuwapa sana hofu khalfan na mkewe kwani waliamini Mola wao atawapigania kwa haki kwa kwa hakuna lolote baya walilomfanyia , wala hawakuwa na roho mbaya kwa mtu yeyote yule. Wote waliokuja kuomba misaada ya kimaisha walipewa walichohitaji kwa moyo wa ukarimu.

Ilikuwa ni kawaida ya familia yao kwenda kubarizi ufukweni mwa bahari kila mwisho wa wiki , siku za jumamosi na jumapili wakipendelea kukaa sehemu tulivu wakipunga upepo mwanana wa baharini huku wakibadilishana mawazo na kucheza na watoto wao.

Ilikuwa ni jumapili tulivu , majira ya jioni kabla ya jua halijazama… Khalfan na mkewe walikuwa wakirudi kutoka ufukweni walikokuwa wamekwenda kubarizi pamoja na watoto wao . Bi Miriam ndiye aliyekuwa akiendesha gari huku mumewe akiwa amekaa pembeni yake na watoto wakiendelea kucheza siti ya nyuma , baada ya muda mfupi wakawa wamefika kwenye geti la kuingia kwenye himaya yao . Bi Miriam alipiga honi mfululizo na mlinzi akatoka mbio kuja kuwafungulia.

Baada ya mlinzi kufungua mlango Bi Miriam aliingiza gari mpaka sehemu ya maegesho , akashuka na kumfungulia mumewe mlango naye akashuka kisha wakawashusha watoto wao. Kwa muda wote huo mlinzi alikuwa amesimama pembeni yao akionekana kuwa na jambo alilotaka kumwambia bosi wake, mzee Khalfani. Alisubiri wamalize kushushana ndipo ampe ujumbe aliokuwa amepewa muda mfupi uliopita kabla hawajarudi .

Khalfan aligundua kuwa mlinzi hayuko katika hali ya kawaida ikabidi amsogelee palepale alipokuwa amesimama . Mlinzi alitoa ujumbe aliokuwa amepewa na kumkabidhi mzee Khalfan, ilikuwa ni bahasha ya ukubwa wa kati iliyokuwa imefungwa vizuri. Nje ya bahasha ile hakukuwa na anuani wala jina la mtu aliyetumiwa , ila yalisomeka maandishi makubwa ya wino mwekundu “SIRI”.

Kilichomshtua khalfan ni jinsi mlinzi alivyokuwa na hofu wakati akimkabidhi ujumbe ule, alijaribu kumhoji juu ya mtu aliyeileta barua ile lakini akawa anamjibu kwa kubabaika. Alieleza kuwa muda mfupi uliopita gari ndogo nyeusi na ya kifahari ikiwa na vioo “TINTED” vya rangi nyeusi iliwateremsha wanaume wawili waliovalia makoti marefu meusi na kofia kubwa zilizoficha sura zao, mmoja akaenda mpaka pale mlangoni na mwingine akawa amebakia kwenye gari.

“Bila hata salamu akanipa bahasha na kusema nikupe wewe ukirudi!” Aliendelea kueleza mlinzi. Khalfan hakutaka kuhoji zaidi, akachukua ile bahasha na kuingia nayo ndani. Muda huo mkewe alikuwa ameshatangulia ndani na watoto akawa anaendelea kuwaandalia chakula cha jioni. Akapitiliza mpaka chumbani na kwenda kuifungua bahasha ile.

Alijikuta mikono ikianza kutetemeka alipoanza kuifungua bahasha ile akakutana na maandishi ya wino mwekundu ambayo yalisomeka vizuri. Ulikuwa ni ujumbe uliojaa vitisho na maneno ya kibabe, ukimtaka eti ‘ahame hapo nyumbani kwake yeye na familia yake yote bila kuchukua kitu chochote kwa sababu yeye Khalfan hakuwa mmiliki halali wa eneo hilo. Ujumbe ule ulizidi kutishia kwamba wanampa siku saba za kuwa ameshaondoka na onyo kali likatolewa kuwa asijaribu kutoa taarifa sehemu yoyote kwa kuwa kwa kufanya hivyo angehatarisha uhai wake.’

Alijikuta akicheka kwa dharau na kisha akatoka na ile bahasha mpaka sebuleni alikokuwa amekaa mkewe na watoto wake wakiangalia luninga. Mkewe alishtuka kumuona mumewe ameanza kubadilika, ingawa usoni alikuwa akicheka lakini alionekana kuchanganyikiwa sana akampa ule ujumbe ili na yeye ausome.

“Unatakiwa uhame hapo unapoishi wewe na familia yako bila kuchukua kitu chochote. Huna haki ya kumiliki eneo zuri kama hilo, wamiliki halali tupo na tulikuwa tunangoja muda ufike tukuambie.

Usijaribu kutoa taarifa sehemu yoyote , polisi wala jeshini kwani kwa kufanya hivyo utahatarisha usalama wako na hizo takataka zako (mkeo na watoto) unapewa siku saba za kutekeleza amri hii na ukiipuuza utaona matokeo yake”

NB. Uhai hautafutwi ila mali zinazotafutwa
By
Wamiliki

Bi Miriam alishusha pumzi ndefu baada ya kumaliza kuisoma, huku akiwa amepigwa bumbuwazi asijue nini cha kufanya. Kwa muda wote huo Khaflan alikuwa akizunguka-zunguka pale sebuleni akiwa haelewi anatafuta nini . watoto walikuwa hawana habari wakawa wanaendelea kucheza na kuruka kwenye masofa ya kisasa yaliyokuwepo pale sebuleni.

Khaflan alirudia kuisoma barua ile kisha akatoka kwa kasi kumfuata mlinzi nje. Alianza kumhoji upya ni nani aliyeleta ujumbe ule na mlinzi akarudia maelezo kama aliyoyatoa mara ya kwanza. Safari hii alionekana kuhofia zaidi baada ya kumuona bosi wake amechanganyikiwa.

Hakujua mle ndani mliandikwa nini lakini kwa hal aliyokuwa nayo bosi wake ilionyesha kuna jambo baya. Mzee Khalfan alirudi ndani na kumuelekeza mkewe awape chakula watoto haraka kisha akawalaze . Alipitiliza mpaka chumbani na kujitupa kitandani kama mzigo.

Maswali mengi yalikuwa yakipishana kichwani kama umeme wa gridi ya taifa . Alijalibu kuwaza na kuwazua ni akina nani walioleta ujumbe ule, hakupata jibu. Muda mfupi baadae mkewe akawa ameshamaliza kuwapa chakula wanae na akaenda kuwalaza kwenye chumba chao. Ama kwa hakika usiku huo ulikuwa ni usiku wa mauzauza kwao. Mpaka jogooo la kwanza linawika kuashiria mapambazuko, Khalfani na mkewe walikuwa hawajapata hata tone la usingizi.

Usiku kucha walikuwa wakijadiliana wafanye nini, hakuna aliyekuwa na jibu. Mwisho wakafikia uamuzi wa kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi ingawa barua ile iliwaonya vikali juu ya uamuzi huo.
“Lakini mume wangu , si ni bora tuondoke tu tuwaachie wafanye wanachotaka ? nahofia usalama wa wanangu, tuondoke tu Mungu atatusimamia huko tuendako kwani mali hutafutwa lakini uhai hautafutwi.”
Wazo hilo halikuingia akilini mwa mzee Khalfani, kwani kufanya hivyo kungemaanisha yeye ni mwanaume dhaifu asiyeweza kuilinda familia yake aliamua kutetea msimamo wake.

”Mke wangu siko tayari hata kwa mtutu wa bunduki kuruhusu watu wengine wayaharibu maisha yetu! niamini nitafanya kila niwezalo kukulinda mke wangu na wanangu na mali zangu zote! Hakuna wa kuchukua chochote kutoka mikononi mwetu, siwezi kusalimu amri kirahisi namna hii, niamini…”

Kwa jinsi alivyokuwa akiongea kwa kujiamini, mkewe akapata imani kuwa usalama wao utalindwa kwa kila namna. Kulipopambazuka tu, mzee Khalfani na mkewe wakaanza kujiandaa kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi cha Blazinia Central Police Post”.

Walichukua barua ile kama ushahidi wa maelezo yao. Mzee Khalfan aliendesha gari lao huku mkewe akiwa pembeni yake. Hakuna aliyemsemesha mwenzake! Kila mtu alikuwa kwenye lindi zito la mawazo, maneno ya barua ile yalikuwa yakijirudiarudia vichwani mwao.
***

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...