Baada ya vijana wa kihuni kumfanyia kitu mbaya Geneviv,wanaondoka na kumuacha akiwa amepoteza fahamu kutokana na maumivu makali aliyoyapata. Anakuja kuzinduka usiku sana na kujikuta akiwa peke yake porini,palepale chini ya mti.Hawezi hata kusimama kutokana na maumivu makali anayoyahisi…anaamua kulala hapohapo mpaka asubuhi bila kujali kuwa ni porini.
Nyumbani kwao nako baba na mama yake wameyamaliza matatizo yao kiutu uzima,lakini wanaanza tena kulumbana na kila mmoja amechanganyikiwa baada ya kuona muda unazidi kuyoyoma na usiku unaingia huku Geneviv akiwa hafahamiki aliko.
Je nini kitatokea?
Ungana nami,twende sasa…
****
Baada ya kumkosa chumbani kwake, Bi Patricia alirudi na kumpa mumewe taarifa.
“Atakuwa ameenda wapi? Maskini malaika wangu…”
Aliongea mzee Rwakatare akijifanya kumsikitikia mwanae.Kwa kifupi,zile tofauti zilizokuwepo baina ya Bi Patricia na mumewe zilionekana kama zimekwisha kabisa na sasa wote wakawa wanamfikiria binti yao Geneviv.
Muda ulizidi kwenda bila ya Geneviv kurudi nyumbani.Hawakujua yuko wapi na amepatwa na nini.
“Ningekuwa na nguvu ningeenda kumuulizia kwa wenzake,mwanangu hana tabia ya kuchelewa kurudi nyumbani namna hii! Sijui kapatwa na balaa gani maskini”
aliongea Bi Patricia kwa masikitiko baada ya kuanza kuhisi kuwa huenda mwanae amepatwa na jambo baya baada ya usiku kuzidi kuingia.Mwili wake wote ulikuwa bado una maumivu kutokana na kipigo cha mumewe kiasi cha kumfanya ashindwe hata kutoka nje kwenda kumtafuta mwanae.Saa ya ukutani iliyokuwa mle chumbani ilionyesha kuwa ni tayari saa nne za usiku.
Wasiwasi ulizidi kuwaingia kiasi cha kila mtu kubaki kimya akiwaza kivyake.
“kwani alivyoondoka aliaga anakwenda wapi?”
Mzee Rwakatare aliuliza swali la kijinga kiasi cha kumkumbusha mkewe yaliyotokea asubuhi ya siku ile na kumfanya Geneviv atoroke pale nyumbani bila kuaga.
“Si ujinga wako uliokuwa unaufanya asubuhi,unafikiri mwanao bado mtoto sio, namtaka mwanangu! Amka kamtafute mwanangu…!”
Bi Patricia alianza kucharuka na kumshinikiza mumewe aende kumtafuta Geneviv.Mzee Rwakatare naye hakuweza kutoka nje kwani bado alikuwa na maumivu sehemu ya kichwani baada ya kupigwa na stuli asubuhi.Wakabaki kulaumiana wenyewe kwa wenyewe.Mzee Rwakatare alijihisi kushtakiwa na dhamira yake sana,kwani ukweli aliujua kuwa yeye ndio chanzo cha matatizo na hata kama mwanae angepatwa na jambo baya,basi yeye ndiye aliyemsababishia.Alijikuta akisononeka sana moyoni hasa baada ya kumuona mkewe akizidi kulia kwa kuomboleza.
“Mke wangu jikaze jamani,unavyolia anamchulia mwanetu,atapatwa na matatizo bure,yote tumwachie Mungu”
Mzee Rwakatare alijifanya kuongea kwa busara.Bi Patricia hakuamini kusikia maneno kama yale kutoka kwa mumewe.Ilibidi ainue macho na kumtazama usoni kwa mshangao,alihisi mumewe anamkejeli kwani tangu aachishwe kazi hakuwahi kulitaja jina la Mungu kutoka kinywani mwake zaidi ya matusi ambayo sasa alishaanza kuyazoea.
Waliendelea kutazamana kwa muda mrefu huku kila mmoja akiwa kimya.Masaa yalizidi kuyoyoma na hatimaye saa ya ukutani ikawa inasoma saa sita za usiku. Bi patricia alishindwa kujikaza na akawa anaendelea kulia kwa kilio cha kwikwi.Pia alikuwa akisali kimoyomoyo akimuomba Mungu wake amnusuru mwanae Geneviv.
****
Manyunyu ya mvua yalianza kudondoka huku wingu zito likitanda angani kuashiria mvua kubwa inataka kunyesha.Geneviv alizinduka kutoka usingizini baada ya kuona ameanza kuloana.Aliposhtuka mwili wake ulikuwa ukitetemeka kwa baridi kali ya usiku huku akiwa hajajifunika kitu chochote zaidi ya nguo alizokuwa amezivaa ambazo nazo zilikuwa zimechanwachanwa. Alijaribu tena kuinuka kutoka pale chini na safari hii alifanikiwa kusimama kwani maumivu yalikuwa yamepungua kidogo.Alijaribu kuinua mguu na kupiga hatua lakini akajikuta akishindwa kutembea.
“I must die hard, I need to move out of this place”
(lazima nife kigumu,nahitaji kuondoka mahali hapa)
Alijiambia Geneviv kimoyomoyo wakati akijikaza na kuanza kupiga hatua fupifupi kuelekea barabarani ambako aliamini anaweza kupata msaada.Japokuwa alikuwa akisikia maumivu makali alijitahidi kujikongoja kiupande-upande na akawa anajongea taratibu kuelekea upande iliko barabara. Manyunyu ya mvua yalikuwa yakiongezeka na kuanza kuuloanisha mwili wake mchanga.Kadri manyunyu yalivyokuwa yanaongezeka na kumloanisha ndivyo Geneviv alivyozidi kupata nguvu ya kutembea na kuongeza mwendo. Baada ya kitambo kirefu akawa amefika barabarani.
Hakutaka kupoteza muda zaidi,akaanza kuifuata barabara akiwa haelewi anakoelekea. Hakutamani tena kurudi nyumbani kwao kwani chuki dhidi ya baba yake ilizidi kukua na kumfanya amchukie kama shetani. Akiwa bado anazidi kusonga mbele akielekea asikokujua,aliona mwanga wa taa za gari likija kutokea mbele yake.Hakujua ni gari gani na lilikuwa likielekea wapi ila akapiga moyo konde na kuamua kulisimamisha.
“Haroo afande hebu simamisha ‘Defender’ ,naona kama kuna rimutu rinasimamisha gari,sijui ni rinani na rimetokea wapi usiku wote huu Mura!”
aliongea Koplo Marugu kwa Kiswahili kibovu akimuamuru dereva wake kusimamisha gari.Walikuwa wako katika doria ya usiku pamoja na askari wengine watatu waliokuwa wamekaa nyuma ya gari.
Geneviv aliendelea kulipungia lile gari mikono kwa nguvu zake zote na taratibu akaanza kuliona likipunguza mwendo na kusimama karibu yake.
Liliposimama Geneviv akagundua kuwa lilikuwa ni gari la polisi,alishusha pumzi ndefu na kumshukuru Mungu wake kwani aliamini angekuwa salama mikononi mwa wanausalama wale.Hakutaka kuwaambia ukweli wa kilichomtokea kwani alijisikia vibaya kueleza kuwa amebakwa kwani alihisi ni aibu kubwa kwake.Akaamua kutunga uongo…
Baada ya lile gari kusimama,askari walishuka na kuanza kumhoji ametoka wapi na anakwenda wapi usiku wote ule,ukizingatia yeye ni mtoto wa kike na hapo alipo ni porini.
“Tulikuwa tumetoka shambani na dada,tukavamiwa na watu walioanza kutupiga mpaka wakanichania nguo.Dada alikimbia na kuniacha peke yangu huku.”
Geneviv aliongea uongo mtakatifu huku akitoa machozi na kuwafanya wale askari waamini alichokuwa anakisema.Bila hata kumhoji maswali mengi,walimpakia ndani ya Defender na kuanza kurudi naye mjini ambapo alielezwa kuwa atapewa sehemu ya kulala mpaka asubuhi ambapo ataandikisha maelezo yake kituoni ili watuhumiwa waanze kusakwa.Hakuna hata mmoja aliyehisi kuwa maelezo ya Geneviv ni uongo.
Gari likawashwa na kuanza kurudi mjini.Muda mfupi baadae tayari walikuwa wameshafika kituo kikuu cha polisi cha Blaziniar ambapo Geneviv alikabidhiwa kwa askari wawili wa kiume waliokuwa zamu na wale polisi wengine wakaendelea na doria. Wale askari walimpokea Geneviv na kumuweka kaunta,huku wakijifanya kumuonea huruma. Walimuonyesha sehemu ya kukaa na wao wakaendelea na shughuli zao.
“Haloo afande haka kabinti ni kazuri mno,hebu kaangalie vizuri”
wale askari walikuwa wakinong’onezana kwa sauti ya chini na mara wote wakaanza kumtolea macho Geneviv ambaye alikuwa ameanza kusinzia pale alipokaa na hakuwa na habari kama wale askari wanamtazama kwa macho ya husda.
“Aisee kweli bwana,unajua nilikuwa sijakaangalia vizuri…halafu unajua mke wangu alisafiri wiki ya pili sasa…natamani niwe fataki japo kidogo tu!”
Waliendelea kunong’ona wale askari na wakajikuta wakicheka kwa pamoja na kugongesheana mikono.Kelele za vicheko zilimshtua Geneviv aliyekuwa anasinzia kwenye kiti alichokuwa amekalia.
Mmoja kati ya wale askari aliinuka na kumfuata pale alipokuwa amekaa na kumshika begani.
“Binti naona umechoka sana, pole! amka basi nikakuonyeshe sehemu ya kulala,usiwe na wasiwasi hapa uko mikononi mwa chombo cha dola…tutakulinda mpaka asubuhi”
Aliongea yule askari akimshika mkono Geneviv na kutoka nae nje ya jengo la kituo cha polisi. Geneviv hakuwa na wasiwasi kwani aliamini kazi ya jeshi la polisi ni kuwalinda raia wake. Wakatoka na kuelekea kwenye kibanda kidogo kilichokuwa mita chache pembeni.
****
Hakuna hata mmoja kati ya Mzee Manuel Rwakatare na mkewe Bi Patricia aliyepata hata tone la usingizi. Mpaka inagonga saa nane usiku, Geneviv alikuwa hajarejea nyumbani na hakukuwa na dalili za yeye kurudi. Bi Patricia alikuwa akizidi kulia hali iliyomfanya aanze kuhisi maumivu makali ya kichwa kwani alikuwa bado hajapona. Baada ya kuona mkewe hataki kutulia, ilibidi mzee Rwakatare ajiandae kwenda kutoa taarifa polisi usiku huohuo. Na yeye alionekana kuchanganyikiwa mno, akawa anajilaumu kwa yote aliyoyafanya ambayo ndiyo yaliyopelekea kuibuka kwa tatizo hilo.
Alipiga moyo konde na kujifariji kuwa hakuna binadamu asiyekosea. Baada ya kumaliza kujiandaa alimuaga mkewe ambaye hakumjibu kitu zaidi ya kuendelea kumwaga machozi.Alitoka na safari ya kuelekea kituo kikuu cha polisi cha Blaziniar ikaanza. Ilimbidi abebe mwamvuli kwani mvua nayo ilikuwa imechachamaa kunyesha.Baada ya safari ya takribani dakika arobaini, tayari alishawasili kwenye eneo la kituo cha polisi.
Tangu asimamishwe kazi serikalini,Mzee Rwakatare alikuwa hapendi kabisa kuonekana na polisi kwa kuhofia kukamatwa kwa makosa yake ya uhujumu ambayo bado upelelezi ulikuwa unaendelea, lakini kwa sababu ya mwanae alijikuta hofu ikimuishia. Akawa anapiga hatua za taratibu kusogelea eneo la kituo.
Akiwa hatua chache kabla ya kuufikia mlango mkubwa wa kuingilia kituoni,alisikia sauti ambayo ilimfanya mapigo ya moyo yaanze kumwenda kasi mithili ya injini ya jeti.
Ilikuwa ni sauti ambayo aliitambua vizuri kuwa ni ya mwanae Geneviv ikitokea kwenye kibanda kidogo pembeni ya kituo cha polisi.
Geneviv alikuwa akilalama kwa maumivu makali aliyokuwa anayapata wakati yule askari aliyejifanya kumpeleka kulala akimuingilia kimwili kwa nguvu. Kwa mara nyingine tena, Geneviv alikuwa akibakwa,tena safari hii na Askari polisi.
Mzee Rwakatare hakutaka kuyaamini masikio yake kuwa ile sauti kweli ilikuwa ni ya Geneviv.Ikabidi asogee mpaka karibu ya kile kibanda na kuchungulia ndani kupitia tundu dogo chini ya dirisha.
Hakuyaamini macho yake kwa alichikiona…
“Sh*t, what the hell are you doin with my daughter…im gonna kill you!”
Mzee Rwakatare aliongea kwa hasira kali, na kwa nguvu zake zote aliukanyaga mlango wa kile chumba na kuingia ndani mzima-mzima.
Yule askari alishtuka kuona mlango ukivunjwa na kumharibia starehe yake.Akawa anahangaika kuvaa suruali yake vizuri.
Mzee Rwakatare alimuwahi kwa kipigo kikali cha kushtukiza mpaka yule askari akadondoka chini.Alipotazama pembeni alikiona kipande cha bomba la chuma kilichokuwachini. Alikiokota na kuanza kumuadhibu vikali yule askari kichwani mpaka akazimia.
Kwa haraka alimuinua mwanae Geneviv ambaye bado alikuwa akilia kwa uchungu kutokana na maumivu makali aliyokuwa anayapata huku damu ikimchuruzika kutoka katikati ya miguu yake.Alimuweka begani na akatoka naye kwa spidi ya ajabu na kuanza kukimbia nae kutokomea gizani.
Hakuna askari aliyeelewa kinachoendelea.Mvua nayo ilikuwa ikizidi kupamba moto na sasa zilianza kusikika radi kali zikipiga na kuufanya usiku uzidi kutisha.Mzee Rwakatare hakujali kitu,akawa anazidi kutimua mbio huku Geneviv akiwa begani.
Akiwa umbali wa mita kadhaa,alishtukia kuona anamulikwa na taa za gari lililokuwa likiingia kituo cha polisi. Kwa haraka akamrusha Geneviv chini na yeye akarukia pembeni ya barabara kwenye mtaro.
Kutokana na mvua kubwa iliyokuwa inaendelea kunyesha ikiambatana na ukungu,hakuna mtu yeyote kutoka kwenye lile gari aliyewaona.
Gari ambalo aliligundua kuwa ni la polisi likapita na kuingia pale kituoni.Kwa haraka aliinuka na kumnyanyua mwanae na kumuweka tena begani.Akawa anatimua mbio kurudi nyumbani kwake, safari hii akipitia njia za vichochoroni kukwepa kuonekana tena na polisi.Baada ya kama nusu saa akawa ameshafika nyumbani kwake. Geneviv alikuwa akiendelea kulalama kwa maumivu na hakuelewa kilichofuatia mpaka alipojikuta anaingizwa ndani mwao.
Bi Patricia alishtuka kusikia mlango ukigongwa.
“Nini tena jamani?” Bi Patricia aliuliza kwa sauti iliyokauka kutokana na kulia, na akawa anajikongoja kwa uchovu kwenda kufungua mlango. Alishakata tamaa ya kumuona mwanae Geneviv usiku huo.
“Fungua mke wangu!”
Aliongea mzee Rwakatare kwa sauti iliyomaanisha kuna jambo. Bi Patricia aliharakisha kufungua mlango.
“Ooooh My God!.....”
Bi Patricia alishtuka kupita kiasi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1
Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...
-
Ni wiki nyingine ambapo mwenyezi Mungu ametujaalia kukutana katika busati letu la mahaba ambapo tunajadiliana mambo mbalimbali yanayohusu ...
-
HASH POWER 7113 NI matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa. Ni wiki nyngine tunapokutana kwenye busati letu ambapo tunajuzana na kuja...
No comments:
Post a Comment