Furaha ya maisha ya mzee Khalfan na familia yake inaanza kuingia doa baada ya kupokea barua ya vitisho ikiwataka kuhama ndani ya nyumba yao katika kipindi cha siku saba.
Hakuna anayetaka kuona hilo likitokea. Khalfan na mkewe wanajadiliana usiku kucha nini cha kufanya mara bada ya kupewa barua ile.
Wanaona njia muafaka ni kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi japokuwa barua ile iliwaonya juu ya kufanya kitu kama hicho.
Wanaamua kujitoa sadaka kwa kwenda kutoa taarifa polisi bila kujali nini kitakachotokea kwani wanaamini polisi ipo kwa ajili ya kuwalinda raia kama wao.
Baada ya siku saba walizopewa kuisha , polisi hawaji kuwapa msaada kama walivyowaahidi, na usiku wa manane nyumba yao inavamiwa na majambazi yenye silaha nzito a kuafanya maangamizi makubwa.
Je nini kitafuatia? twende pamoja…
***
Kulipopambazuka tu, Khalfani na mkewe wakaanza safari ya kwenda kutoa taarifa kwenye kituo kikuu cha polisi cha Blazinia “Blazinia Central police post”. Walienda na barua ile waliyoletewa kama ushahidi wao. Dakika chache baadae walikuwa wameshafika kituoni na wakashuka na kuingia ndani mpaka kaunta ambapo waliomba kukutana na mkuu wa kituo. Muda mfupi baadae wakawa ndani ya ofisi ya mkuu wa kituo, Luteni Lauden Kambi, aliyekuwa akifahamika kwa jina la utani kama “Luteni Fuvu” kutokana na ukatili wake.
Mzee Khalfan alianza kueleza kila kitu kuanzia mwanzo mpaka mwisho, na Luteni akawa anaandika kila kitu kwenye faili jeusi. Alipomaliza kueleza, Luteni Lauden Kambi aliwajibu kwa kifupi kuwa waende nyumbani kwao baada ya kuacha maelezo yote ya msingi ya mahali na mtaa wanakoishi, jeshi litawapa ulinzi baada ya siku hizo saba kupita. Aliwatoa hofu kuwa vile ni vitisho vya kawaida ambavyo vinahitaji ujasiri kuweza kukabiliana navyo. Aliwapa pia maelezo kuwa warudi siku ya sita hapo kituoni ili waambiwe nini cha kufanya. Baada ya kuridhika na maelezo waliyopewa, Khalfan na mkewe waliaga na kurudi nyumbani kwao wakiwa na matumaini makubwa ya kupewa msaada na jeshi la polisi
Siku zikawa zinasonga mbele kwa haraka mno, mara ikafika siku ya sita…yakiwa yamesalia masaa Ishirini na nne tu kabla ya siku ya mwisho waliyoambiwa kuwa wanatakiwa wawe wameondoka katika eneo lile, siku ya Jumapili. Hawakuwa na wasiwasi tena wakiamini wako salama wa kuwa walishahakikishiwa kuwa watapewa ulinzi. Walichokifanya ni kwenda kutoa ripoti Polisi siku moja kabla, yaani Jumamosi Kama walivyokuwa wameelekezwa na mkuu wa kituo cha polisi, Luteni Lauden kambi “Fuvu”.
Wakajitayarisha kwa safari ya kwenda tena Blaziniar Central Police post wakiwa na matumaini makubwa ya kupewa ulinzi. Safari hii gari lao liliendeshwa na Bi Miriam huku Khalfan akiwa ametulia siti ya pembeni. Walipofika waliomba tena kuonana na Mkuu wa kituo. Yule Askari aliyekuwa pale kaunta aliwapa taarifa kuwa Mkuu wa kituo ameanza likizo yake ya mwezi mzima kuanzia siku ya Ijumaa, yaani jana yake na kwa muda huo alikuwa ameshasafiri kurudi kwao alikoenda kuimalizia likizo yake.
Alizidi kuwaambia kuwa shughuli za ukuu wa kituo alikuwa amepewa mtu mwingine ambaye naye alikuwa safarini kikazi. Maelezo yale yalionekana kuwachanganya mno Khalfan na mkewe. Yale matumaini waliyokuwa nayo yakawa yamepotea Kama barafu inavyoyeyuka kwenye moto mkali. Walionyesha hofu na woga waziwazi vikiambatana na kupoteza matumaini Kiasi cha kumfanya yule Askari aliyewapa taarifa ile kushtuka. “Kwani kuna tatizo gani mzee! niambieni labda naweza kuwasaidia hata kama Mkuu hayupo”
Ilibidi mzee Khalfan aanze tena kueleza upya kuanzia mwanzo. Baada ya maelezo yake
yule Askari aliwaomba waongozane mpaka kwenye Ofisi ya Mkuu wa Kituo, wakatafute faili ambalo maelezo yao yalihifadhiwa pamoja ile barua waliyokuwa wameileta kama uthibitisho. Dakika chache baadae wakawa tayari ndani ya Ofisi ya Mkuu wa Kituo. Yule Askari akaanza kutafuta faili lenye maelezo yao.
‘’Unasema mlikuja kutoa ripoti siku gain?” Yule askari alimhoji mzee Khalfan.
‘’Jumatatu iliyopita afande…‘’
Aliendelea kutafuta maelezo yale kwenye mafaili moja baada ya jingine.
‘’Aliweka maelezo yetu kwenye faili jeusi pamoja na ile barua’’ alizidi kusisitiza Bi Miriam huku wote wakimkodolea macho yule askari aliyekuwa akiendelea kupekua faili moja baada ya jingine. Baada ya kutafuta kwa muda mrefu karibu kila mahali, yule askari aliwageukia mzee Khalfan
na mkewe na akawaambia kuwa labda wasubiri kidogo ampigie simu bosi wake hata kama yuko likizo angewaelekeza alipolihifadhi faili lile.
Wakatoka Ofisini na kurudi kaunta ambako yule askari alinyanyua mkonga wa simu na kuanza kuongea na mkuu wa Luten Lauden Kambi. ‘’Amesema msiwe na wasiwasi, rudini nyumbani ila muache ramani ya mtaa mnakoishi, jina la mtaa, jina la balozi na namba ya nyumba eti ameshaacha maagizo na polisi watakuja kuwapa ulinzi wa kutosha kuanzia majira ya jioni.’’
Alimaliza yule Askari kuwapa maelezo aliyopewa na Mkuu wa kituo kwenye simu. Mzee Khalfan ali shusha pumzi ndefu kisha akamgeukia mkewe, wakatazamana kwa muda kisha yule askari akawapa
Karatasi kwa ajili ya kuacha maelezo ya mahali nyumba yao ilipo, jina la mtaa, jina la balozi na namba ya nyunba. Mzee Khalfan akaanza kuandika upya. Baada ya kuhakikisha kuwa maelezo waliyoyaacha ni sahihi mzee Khalfan na mkewe wakaaga na kuondoka.
Kengere ya hatari ilishalia kichwani mwa Khalfan, akahisi kuna mchezo mchafu unaotaka kuchezwa na askari wale askari. Iweje watoe maelezo mara ya pili ilhali walishahakikishiwa usalama wao?
Hakutaka kumwambia mkewe alichokihisi kwa kuogopa kumuongeza hofu. Wakapanda garini na safari ya kurudi kwao ikaanza safari hii pia hakuna aliyekuwa akimsemesha mwenzake… kimya kimya
mpaka nyumbani.
Masaa yakawa yanazidi kuyoyoma, saa kumi jioni… kumi moja… kumi mbili, mara saa tatu usiku… nne tano kasoro… Hakukuwa na dalili yoyote ya polisi kufika eneo hilo kama walivyoahidiwa na Luten Lauden ‘’Fuvu”. Kwa muda wote huo mzee Khalfan alikuwa nje pamoja na walinzi wake watatu na wengine wawili aliwakodi kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa eneo zima la kuzunguka nyumba yao ili kulinda usalama.
‘’Boss! hao polisi uliosema watakuja tusaidiane nao kazi mbona hawaji na muda ndio unazidi kwenda? saa tano usiku sasa!’’ Alihoji mlinzi mmoja kwa niaba ya wenzake. Mzee Khalfan hakuwa na jibu la kuwapa, zaidi swali lile lilionekana kumchanganya akili. Tangu saa moja jioni alikuwa akiwapa darasa walinzi wake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha bunduki wanazotumia (magobore) yako katika hali ya utayari kwa kazi muda wowote. Alihakikisha pia kuwa bastola yake aliyoachiwa na marehemu mzee Shamsi imejaa risasi za kutosha.
Wote wakawa wamejiandaa vya kutosha wakitegemea muda wowote polisi wangefika kuungana nao kuwasubiri hao wanaotaka kuwadhulumu mali zao kwa nguvu. Walijiandaa kutoa upinzani wa kutosha kwa yeyote ambaye angethubutu kuleta ujeuri wa aina yoyote ile katika eneo lile. Bi Miriam naye alikuwa amewahi kuwaingiza watoto wake ndani mapema kuliko siku yoyote. Wakawahi kula chakula cha usiku kisha wote wakaenda kulala. Alihakikisha milango yote na madirisha yamefungwa ipasavyo.
Mzee Khalfan hakutaka kuingia ndani. Alitaka ashirikiane bega kwa bega na walinzi hata kama polisi hawatafika. Walinzi walimshauri aende ndani kwani walikuwa wakijiamini kuwa wanaweza kazi. Baada ya mabishano kidogo, hatimaye mzee Khalfan alikubali kurudi ndani huku bastola yake ikiwa mkononi “standby” kwa lolote. Muda ukazidi kuyoyoma…mara saa sita usiku… Saa saba na hatimaye saa nane.
Eneo zima lilikuwa kimya kabisa huku giza nene likiwa limetanda kila sehemu. Walinzi walikuwa waki zunguka huku huko kuhakikisha hakuna mtu anayesogelea eneo lile. Bunduki zao zilikuwa “standby” mikononi wakisaidiwa na mbwa mkubwa wa mzee Khalfan. Giza lilikuwa likizidi kushamiri na kufanya hali
ya eneo lile izidi kutisha. Ilishatimia saa tisa usiku huku bado kukiwa kimya kabisa.
Ghafla zilianza kusikika kelele za mbwa aliyekuwa akibweka na kukimbilia kwenye geti kubwa la kuingilia. Walinzi wakajua mambo yameanza, kwa umakini mkubwa nao wakaanza kunyata kuelekea kule mbwa alikokuwa anakimbilia. Alizidi kubweka na walinzi nao wakawa wanazidi kusogea kuelekea kule getini. Mara walishtukia kuona mbwa akipigwa risasi nyingi kichwani kisha akadondoka chini, Puuuh! Ile milio ya risasi ilitosha kuwamaliza kabisa ujasiri wote waliokuwa nao wale walinzi, kwani ilionekana dhahiri maadui zao wamekuja na bunduki nzito za kivita.
Hawakuelewa risasi zimetokea upande gani wakawa wanaangalia huku na huko. Wakiwa bado wanashangaa walishtukia kujikuta wote wamemulikwa na tochi kali kisha mvua ya risasi ikaanza kuwanyeshea. Sekunde chache baadae walinzi wote watano walikuwa chini wakitapatapa kukata roho baada ya shambulizi la ghafla risasi zilikuwa zimepenya vichwani mwao kisawasawa.
Kelele za shambulizi lile ziliwafanya wote waliokuwa ndani ya nyumba ya mzee Khalfan kushtuka. Watoto walianza kupiga mayowe hovyo ya kuomba msaada. Bi Miriam naye alikuwa hajitambui kwa hofu. Mzee Khalfan akapiga moyo konde na kunyanyua bastola yake, akaikamata kisawasawa. Akafungua mlango wa chumbani na kuanza kutoka huku akinyata kwa tahadhari kubwa. Mkewe alijaribu kumzuia asitoke lakini wapi! Akanyatia mpaka sebuleni. Akiwa katikati ya sebule, alishuhudia mlango wa nje ukivunjwa kwa jiwe kubwa kisha watu wapatao saba, wote wakiwa wamevalia makoti marefu meusi, usoni wakiwa wamevaa vitambaa vya kuficha sura zao (masks) , mikononi wakiwa na bunduki nzito za kivita kila mtu ya kwake wakiingia kwa kasi na kumzunguka pale aliposimama…
‘’Weka silaha chini! ‘’ Mmoja wa majambazi yale alimuamuru mzee Khalfan kwa sauti ya ukali mno. Akajikuta akitetemeka mwili mzima kiasi cha kuhisi haja ndogo ikimtoka bila ya ridhaa yake. Hakuwa na cha kufanya zaidi ya kudondosha bastola yake chini kisha kuinua mikono juu kusalimu amri. Yale majambazi yakaanza kumshambulia kama mpira wa kona. Alipigwa na kitako cha bunduki kichwani akadondoka chini kama mzigo.
Yakaanza kumshushia kipigo cha nguvu kwa zamu zamu. Alijitahidi kujitetea lakini alizidiwa nguvu. Majambazi wengine wakaingia vyumbani na kuwatoa Bi Miriam na watoto wake wote. Kipigo kikaendelea kwa wote… hata mtoto wao mdogo wa mwisho ambaye na miaka miwili tu! Ikawa ni kichapo mtindo mmoja.
Mtoto wa kwanza wa Mzee Khalfan, Khaleed, ambaye kwa kipindi hicho alikuwa na miaka kumi na tatu, alifanikiwa kujificha chini ya meza kabla ya majambazi hayajamuona. Aliendelea kushuhudia jinsi baba’ake, mama’ake na wadogo zake walivyokuwa wakisulubiwa. Uchungu ulimuingia mno kiasi cha kushindwa kuvumilia. Kwa haraka alitoka chini ya meza na kunyanyua chuma kilichokuwa sakafuni, kisha akakinyanyua kwa nguvu zake zote na kukirusha kwa jambazi mmoja. Kilitua sawia kichwani kiasi cha kufanya jambazi lile lidondoke chini.
Akajikuta amedakwa juu juu kama kifaranga cha kuku mbele ya mwewe. Kisha naye akaanza kusulubiwa. Sekunde chache tu baadaye naye akawa ameloa damu mwili mzima kama wenzake. Kichapo kiliendelea mpaka wote wakawa hoi taabani. Yale majambazi yakawafunga wote kwa kamba, mikononi na miguuni na kuwajaza matambara midomoni mwao. Kisha yakaanza kuwaburuza mpaka nje ambako yalianza kuwapakiza kwenye gari yaliyokuja nayo. Yalikuwa yakiwarusha kama magunia,wakati yaiwapakia kwenye Landrover. Gari likawashwa na kuanza kuondoka kwa kasi ya ajabu kuelekea kusikojulikana. Eneo zima liliachwa likiwa limetapakaa damu na maiti tano za walinzi zikiwa zimelala chini. Ukimya ukatawala eneo zima, tena safari hii kukiwa kunatisha zaidi kwani hakuna aliyekuwa amesalia akiwa hai eneo lile.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1
Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...
-
Ni wiki nyingine ambapo mwenyezi Mungu ametujaalia kukutana katika busati letu la mahaba ambapo tunajadiliana mambo mbalimbali yanayohusu ...
-
HASH POWER 7113 NI matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa. Ni wiki nyngine tunapokutana kwenye busati letu ambapo tunajuzana na kuja...
No comments:
Post a Comment