Thursday, August 30, 2018

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 2


ILIPOISHIA:
Bado nilikuwa nazikumbuka namba za siri nilizotumia kukifunga, macho yangu yakatua juu ya kitu kilichosababisha nitabasamu! Siyo tabasamu la furaha, la hasha! Tabasamu la kifo, tabasamu ambalo huwa linaonekana usiku wa giza totoro pekee.
SASA ENDELEA...
Unaweza kujiuliza nilikuwa nimeona nini kilichosababisha nitoe tabasamu la aina hiyo? Kihulka mimi ni mpole sana na pengine upole wangu wa nje ndiyo unaosababisha wakati mwingine watu kunionea waziwazi, wakiwa hawajui ndani ya moyo wangu kumejificha kitu.
Ilikuwa ni bunduki ninayoipenda sana, AK47 ambayo ilikuwa imekatwa kitako na mtutu na kuifanya iwe na uwezo wa kubebeka vizuri mikononi. Jinsi nilivyoipata silaha hii hatari, ambayo kisheria haitakiwi kabisa kumilikiwa na raia, isipokuwa wanajeshi tu, ni stori ndefu sana na yenye kusisimua kwelikweli.
Wakati mwingine binadamu wanakuwa wepesi wa kuwalaumu wenzao kwa matokeo ya mwisho, lakini ni wachache wanaokuwa wanaujua ukweli wa nini kinachosababisha mtu fulani akafanya tukio fulani. Sikuwahi kudhani hata mara moja kwamba itafika siku nitakuwa nikiutegemea mtutu wa bunduki kufanya kile ninachokitaka.

Kwa kipindi kirefu ndoto zangu zilikuwa ni kusoma na kuja kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na watoto, na nilisukumwa kuupenda udaktari kutokana na jinsi nilivyokuwa namuona mama yangu akiteseka kwa kipindi kirefu kitandani, akiwa hana uwezo wa kufanya kitu chochote kutokana na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua.
Hata hivyo, ndoto zote hizo ziliyeyuka kutokana na matatizo niliyopitia na japokuwa baadaye niliamua kuachana na mambo hayo, siku hiyo nilijikuta nimetamani tena kufanya jambo kwa ajili ya kujitetea.
Hakuna kitu ambacho nilikuwa nakichukia kwenye maisha yangu kama kuonewa, shida na matatizo niliyopitia maishani mwangu vilinifanya niwe na roho ya aina yake, ambayo wakati mwingine nikikasirika utaona ni bora ukutane na mnyama mkali wa porini kuliko mimi.
Niliendelea kuitazama ile bunduki huku tabasamu la kifo likiwa bado limetanda kwenye uso wangu, nikainua macho na kutazama juu angani huku ile bunduki nikiwa nimeishikilia vilevile, nikaitazama tena na kujaribu kuikoki, ikakubali na kutoa mlio fulani ambao kwa kipindi kirefu ulikuwa unaashiria jambo baya na kila nilipousikia ujue kuna jambo baya lilikuwa linaenda kutokea.
Unaweza kujiuliza, nini hasa kilichotokea kwenye maisha yangu kiasi cha kufanya ndoto zangu za udaktari ziyeyuke na kujikuta nikiishia kuwa mtumiaji mzuri wa bunduki za kivita wakati hata jeshini sijawahi kupitia?
Nikisema mtumiaji mzuri wa bunduki namaanisha hivyo, kwenye suala zima la kulenga shabaha na kufanya mashambulizi ya kushtukiza, wenyewe wanaita ‘ambush’ nilikuwa vizuri kwelikweli kiasi kwamba kipindi nilipoamua kujikita kwa asilimia mia moja kwenye kazi hiyo, licha ya umri wangu mdogo nilikuwa tegemeo kwelikweli.
Ilikuwa ikitokea ‘kazi’, basi lazima nitakuwa miongoni mwa watu wawili au watatu ambao ndiyo wanaoongoza msafara. Baada ya hapo, niligeuka huku na kule kutazama kama kuna mtu alikuwa ananitazama, nilipogundua kwamba niko peke yangu, harakaharaka nililirudisha lile sanduku palepale lilipokuwa na kulifunga vizuri, kwa kutumia ‘chepe’ nikafukia na kuparudishia kama palivyokuwa awali.
Kwa muda wote huo, zana yangu nilikiwa nimeivaa begani. Nilirudishia miche ya mipapai ambayo ilikuwa juu ya eneo hilo kama njia ya ‘kuwazuga’ askari wasijue chochote kilichokuwa kinaendelea kisha harakaharaka nikarudi mpaka ndani, nikachukua begi dogo lililokuwa darini na kutoka nje.
Begi hilo lilikuwa na vifaa maalum ambavyo kwa harakaharaka ungeweza kudhani labda ni vya ufundi wa umeme, lakini kimsingi vilikuwa ni vifaa kwa ajili ya kusafishia bunduki.
Harakaharaka nilianza kuifungua silaha hiyo na kwa sababu tayari nilikuwa na uzoefu wa namna ya kuifungua na kuifunga upya kwa muda mfupi, ndani ya dakika chache tu nilikuwa nimeshaifungua, nikaanza kuisafisha kwani haikuwa imetumika kwa muda mrefu kiasi.
Wakati nikiendelea na kazi hiyo, kwa mbali nilianza kusikia muungurumo kama wa gari au pikipiki kubwa ukija kwa kasi kubwa. Kengele ya hatari ikalia ndani ya kichwa changu, kwa kuwa nilikuwa nakaribia kumaliza, niliamua kuifunga hivyohivyo, harakaharaka nikairudishia na kuivaa begani.
Nikachukua koti langu la kazi, refu na jeusi kisha nikafunga mlango na kuzunguka nyuma ya nyumba, nikakimbia na kuyapita yale makaburi na kutokomea kwenye vichaka vilivyokuwa mita kadhaa kutoka pale nyumbani.
Nikaenda kupanda juu ya mti mrefu wa mkaratusi, nikawa natazama kwa mbali kuangalia muungurumo niliokuwa nausikia ulikuwa unatokea wapi kwa sababu haikuwa kawaida kwa magari kuja huko tulikokuwa tunaishi.
Nilichokuwa nimekihisi ndicho kilichokuwa kimetokea, niliona pikipiki mbili aina ya Honda, zile kubwa kama zinazotumika kwenye mashindano zikija kwa kasi kubwa huku wanaume wanne wenye miili mikubwa wakiwa wamepakizana wawili wawili.
Walikuja kwa kasi kubwa mpaka pale nyumbani kwetu, ile pikipiki ya kwanza ikasimama upande wa kulia na ile nyingine upande wa kushoto kisha wote wanne wakateremka huku wakiwa wamevaa kofia maalum za kuficha nyuso zao.
Japokuwa walikuwa wamejiziba nyuso zao, niliweza kuhisi moja kwa moja kwamba ni watu niliokuwa nawafahamu kwa jinsi miili yao ilivyokuwa na jinsi walivyokuwa wakitembea. Unajua kama mtu umewahi kufanya naye kazi kwa karibu, hata ikitokea akajaribu kujibadilisha, ni rahisi sana kumgundua, hivyo ndivyo ilivyotokea kwangu.
Nitakuja kueleza kwa kirefu baadaye ni kwa namna gani mimi na watu hawa tulifahamiana lakini chanzo cha yote, kilikuwa ni mtu mmoja tu. Mtu ambaye awali niliamini kwamba anaweza kunisaidia kuutua mzigo mzito niliokuwa nao kichwani lakini mwisho akaishia kunibadilisha na kuwa kiumbe mwingine tofauti kabisa.
Basi nikiwa pale juu ya mti, niliwashuhudia watu wale wakigonga mlango kwa fujo kama walivyofanya jana yake, na walipoona kimya, walivunja mlango na kuingia ndani kibabe.
Nikiwa sielewi hili wala lile, nilimuona mmoja kati yao akirudi pale kwenye pikipiki, nikamuona akifungua kidumu kilichokuwa na kimiminika ndani yake ambacho kwa mbali sikuweza kugundua ni nini. Akarudi ndani kwa wenzake na kufumba na kufumbua, nilishtuka kuona moshi mwingi ukianza kutokea madirishani napembeni ya paa.
Wale watu wakatoka haraka nje, wakadandia pikipiki zao na kuziwasha, wakasogea mita kadhaa na kugeuka tena nyuma, nadhani ili kuhakikisha kama walichokusudia kukifanya kinaenda kama walivyokuwa wamepanga.
Nilishindwa kujizuia pale juu ya mti kutokwa machozi, baada ya kuona nyumba yetu kuukuu ikiteketea kwa moto huku wale washenzi wakigongesheana mikono kwa furaha na kuondoka kwa kasi kubwa na pikipiki zao.
Nilikuwa na uwezo wa kufanya kitu lakini niliona si busara kwa sababu naweza kujikuta naharibu zaidi mambo. Basi niliendelea kushuhudia nyumba yetu ikiteketea huku moshi mkubwa ukiwa umetanda angani, na kwa jinsi moto ulivyokuwa mkali, sikuweza kuokoa chochote.
Nilishuka na kukaa nje, mita kadhaa kutoka moto ulipokuwa unawaka kwa nguvu, nikawa nimejishika tama huku moyoni nikiwa na uchungu usiomithilika. Kwa ilivyoonesha, mtu aliyekuwa nyumaya matukio yote hayo, alikuwa akitamani kuniona napata shida kubwa pengine kuliko binadamu yeyote aliyewahi kuishi.
Kilichonifikirisha zaidi, kama mtu au watu waliokuwa wanayafanya haya walikuwa na lengo la kuniua, kwa nini jana yake walipokuja hapo nyumbani na kumteka Saima, hawakunipiga risasi na kuniua kabisa wakati walikuwa na uwezo wa kufanya hivyo? Kwa nini waliniacha niendelee kuishi?
Kwa jinsi nyumba zilivyokuwa zimejengwa hapo kijijini kwetu, na kwa sababu sikupiga kelele zozote za kuomba msaada, wanakijiji walikuja kuanza kukusanyika wakati moto ukiwa unaelekea kuzimika baada ya kuwa umeteketeza kila kitu. Kwa sababu ninazozijua mwenyewe, sikutaka kuzungumza na mtu yeyote, nikawahi kuondoka kabla hawajafika na kurudi kule vichakani.
Nilikuwa nahitaji muda wa kukaa peke yangu, kutafakari juu ya kilichotokea na kuchukua uamuzi wa nini cha kufanya. Kwa hiyo niliendelea kujichimbia kule vichakani, machozi yakinitoka na kuulowanisha uso wangu, nikawa natafakari nini cha kufanya.
Nilikaa huko mpaka giza lilipoanza kuingia, nikavaa koti langu na kuhakikisha kama kitendea kazi changu kipo kwenye hali nzuri, nikaianza safari ya kuelekea mjini kwa sababu katika kutafakari, niliamua kwamba dawa ya tatizo siyo kulikimbia, ni kukabiliana nalo.
Kwa kuwa nilikuwa na picha ya watu waliokuja kuchoma ile nyumba yetu na nilikuwa nafahamu wapi kwa kuwapata, niliamua kuwafuata hukohuko ili kama mbwai iwe mbwai!
Huu ni uamuzi wa kijasiri sana ambao unahitaji kweli uwe na moyo wa kishujaa kuuchukua kwa sababu watu niliokuwa nawafuata hawakuwa wa mchezomchezo lakini ilikuwa ni lazima niende.
Niliamua kutembea kwa miguu kwa sababu kwa hali niliyokuwa nayo, kama ningeamua kupanda gari basi ingekuwa rahisi kwa watu kunishtukia kwamba nilikuwa na chuma begani na pengine kunikamatisha kwa polisi.
Baada ya kutembea kwa muda mrefu, hatimaye niliwasili jijini Dar es Salaam na moja kwa moja nilienda Manzese Tip Top, kwenye maskani ya mmoja kati ya wale vijana aitwaye Ismail au Suma Baunsa kama tulivyozoea kumuita.
Suma alikuwa akiendesha biashara ya kuuza vinywaji kwenye grosari moja pale Manzese Tip Top na sifa kubwa ya grosari yake ilikuwa ni kuuza kila aina ya pombe unayoitaka, kwa saa ishirini na nne. Kwa nje ungeweza kudhani kwamba ni nyumba ya mtu lakini kumbe ndani kulikuwa na ukumbi mkubwa ambako pombe zinauzwa usiku kucha na mchana kutwa.
Nilijua kwa vyovyote lazima Suma atakuwa kwenye ofisi yake akisherehekea na wenzake kwa sababu mara zote, hata kipindi ambacho tulikuwa tukishiriana nao kabla sijaamua kuachana na hayo mambo na kuendelea na maisha yangu, tulikuwa tukipiga ‘ishu’, tunakaa nao kwenye chimbo hilo kuwakwepa polisi na kiukweli hapo ndipo nilipojifunzia kunywa pombe, kula mirungi na kuvuta bangi.
Baada ya kufika eneo hilo, nilijua nikipitia mlango wa mbele, ni rahisi mabaunsa wake kunishtukia na pengine kunizuia kuingia, kwa hiyo kwa sababu nilikuwa nazijua njia za mkato za kuingilia ndani, nilitazama huku na kule na nilipojiridhisha kwamba hakuna aliyekuwa akinifuatilia, niliruka ukuta mrefu wa uani, nikatua ndani kimyakimya.
Nikaingia kwenye moja kati ya vyoo vya wanaume vilivyokuwa huko uani, nikaikoki vizuri bunduki yangu na kuikamata vizuri mkononi, nikatoka huku nikitembea kwa staili ya kuyumbayumba ili watu waamini nilikuwa miongoni mwa wateja na nilikuwa nimelewa. Muziki ulikuwa ukipigwa kwa sauti ya juu huku watu wengi wakiwa wanakunywa pombe, kutafuna mirungi, kujidunga madawa ya kulevya na kila aina ya ufuska, huku wengine wakifanya matendo yasiyostahili kufanywa hadharani na wanawake waliokuwa ndani ya grosari hiyo ya aina yake.
Nilichezesha macho kwa kasi kubwa na hatimaye nilifanikiwa kumuona Suma akiwa amekaa na mwanamke mmoja mnene aliyevalia nusu utupu, wakiwa wananyonyana ndimi. Nikateleza kama nyoka na kumfikia, kufumba na kufumbua tulikuwa tukitazamana naye, ana kwa ana huku bomba la AK47 nikiwa nimelikandamiza kwenye ubavu wake wa kushoto.
“Inuka na ufanye ninachokueleza, ukizingua unajua nini kitatokea,” nilisema kwa sauti ya chini lakini yenye mamlaka, yule mwanamke akakurupuka akiwa ni kama haamini kilichotokea, Suma naye akawa anatetemeka akiwa haelewi nimeingiaje pale.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Championi Jumatatu.  

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...