“Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!”
“Nanii?”
“Fungua!”
“Jitambulishe kwanza, wewe nani?”
“Nimesema fungua! Fungua kwa hiyari yako!”
“Huyo ni nani?”
“Shiii! Rudi ndani kalale!”
“What is going on? Please let me know!” (Nini kinaendelea? Tafadhali naomba nieleweshe).
“Ngo! Ngo! Ngo!”
Kufumba na kufumbua, kishindo kikubwa kilisikika, mlango ukaja kunibamiza kwa nguvu na kunirusha mpaka ukutani, nikajibamiza na kudondoka chini kama mzigo. Wanaume watatu waliokuwa wamevalia makoti meusi, walinifuata na kunikaba pale chini huku wakinimulika kwa tochi zenye mwanga mkali usoni.
“Tulia, vinginevyo tunakumwaga ubongo sasa hivi,” alisema mmoja kati yao, nikashtuka kusikia akikoki bunduki yake na kuninyooshea. Sikuwahi kuona bunduki halisi katika maisha yangu hata mara moja, nilizoea tu kuziona kwenye TV lakini sasa, mtutu ulikuwa ukinitazama.
“She is innocent! Please leave her alone!” (Hana makosa! Tafadhali muacheni) nilisema kwa sauti ya kutetemeka, nikashtukia mmoja kati yao akinipiga kwa nguvu kichwani na kitako cha bunduki kisha akanisindikizia kwa kunipiga na buti gumu alilokuwa amevaa, nikasikia kizunguzungu kikali kisha giza nene likatanda kwenye uso wangu, sikuweza tena kugundua chochote kilichoendelea.
Nilipokuja kuzinduka, tayari kulikuwa kumepambazuka. Nikakurupuka pale chini nilipokuwa nimelala na kusimama, nikasikia kichwa kikiwa kinanigonga kuliko kawaida. Kilichonishtua ni kwamba pale chini nilipokuwa nimelala, palikuwa na damu nyingi ambazo sasa zilikuwa zimekauka.
Nikajishika sehemu mbalimbali za mwili wangu, nikagundua kwamba mdomo wangu ulikuwa umevimba sana, harakaharaka nilisogea kwenye kioo kidogo kilichokuwa ukutani na kujitazama, nikashtuka kwa jinsi nilivyokuwa natisha.
Jicho moja lilikuwa limevimba sana na kuweka kama alama za weusi kwa chini yake, mdomo nao ulikuwa hautamaniki. Kwa jinsi ilivyoonesha, ni kwamba wale wanaume walionivamia usiku uliopita, waliendelea kunipiga tena hata baada ya kuwa nimepoteza fahamu.
“Lakini kwa nini? Why? Nimefanya kosa gani kwa Mungu wangu kustahili adhabu kali kiasi hiki?” nilijisemea huku nikianza kumwaga machozi. Harakaharaka nikaenda mpaka chumbani, macho yangu yakatua juu ya kitanda cha chuma au banco kama wenyewe tulivyokuwa tumezoea kukiita, Saima hakuwepo!
Nikageuka kutazama huku na kule, nikagundua kwamba hata begi lake pia halikuwepo, uchungu usioelezeka ukanikaba kooni kiasi cha kunifanya nishindwe hata kumeza mate.
Nilitoka nje huku nikipepesuka maana maumivu ya kicha yalikuwa makali sana, nikatazama huku na kule, hakukuwa na dalili yoyote ya kuwepo kwa Saima, nikarudi ndani huku nikiendelea kulia kwa uchungu usioelezeka.
Niliwasha moto kwenye jiko la kuni, nikabandika maji na kuchochea mpaka yalipochemka, nikaanza kujikanda maeneo yote yaliyokuwa na majeraha. Nilikuwa nasikia maumivu makali lakini ilikuwa ni lazima nifanye hivyo.
Nilisukutua mdomo kwa maji yaliyochanganywa na chumvi, maumivu niliyokuwa nayasikia yalikuwa hayaelezeki. Nilijisafisha puani ambako damu ilikuwa imegandia, nikaanza pia kujikanda kwenye jicho. Ama kwa hakika nilikuwa nikisikia maumivu makali sana lakini ilikuwa ni lazima nifanye hivyo ili angalau nipate ahueni.
Tangu nifahamiane na Saima, kila kitu changu kilikuwa kimebadilika kabisa, nilishapoteza kila kitu na sasa hata usalama wangu wenyewe ulikuwa ni mtihani mgumu.
Nasema mtihani kwa sababu kama watu wameweza kujua mahali tulipokimbilia na kujificha, tukiishi maisha kama ya wanakijiji kabisa, lakini watu wameingia mpaka ndani, wamenipiga na kunijeruhi vibaya lakini kama hiyo haitoshi wameondoka na Saima, hiyo ilikuwa ni ishara ya hatari sana kwenye maisha yangu.
Sasa kama hata sehemu ya kujificha haipo tena, nini ityakuwa hatma yangu? Nilijiuliza maswali mengi sana wakati nikiendelea kujikanda. Baada ya kumaliza kazi hiyo, nilienda kuanza kurekebisha mlango uliokuwa umevunjwa usiku uliopita na watu wale walioondoka na Saima.
Niliifanya kazi hiyo huku nikiendelea kujiuliza maswali mengi sana ndani ya kichwa changu. Nilipomaliza, tumbo lilikuwa likitetemeka kwa sababu ya njaa, ikabidi nifanye maarifa ili kutuliza njaa yangu.
Kwa bahati nzuri, unga tulionunua mjini na Saima siku tulipoamua kufunga safari kwenda kujificha, bado ulikuwepo. Nikapika ugali harakaharaka na kwa sababu kulikuwa na mboga kidogo tulizobakisha usiku uliopita, sikupata tabu.
Baada ya kumaliza kula, nilitoka na kujaa nje, nikawa naendelea kutafakari nini cha kufanya kwa sababu ndani ya muda mfupi tu nilikuwa nimeingia kwenye matatizo makubwa sana ambayo hata sikuwa najua nawezaje kutoka.
Sikuwa na kazi tena, kazi pekee ambayo ndiyo iliyokuwa inanipa jeuri ya kuishi jijini Dar es Salaam kwa uhuru, ilikuwa imeshapotea katika mazingira ya kushangaza sana.
Sikuwahi kuwa na wasiwasi kuhusu utendaji kazi wangu na japokuwa wakati akinipa barua ya kunisimamisha kazi, meneja wetu alisisitiza kwamba wamefikia hatua hiyo kutokana na sababu za kiutendaji, moyoni nilikuwa najua wazi kwamba hiyo siyo sababu bali kuna jambo jingine kubwa ambalo mimi na yeye tulikuwa tunalijua.
Nilikumbuka jinsi nilivyojikuta nikiwa nimezungukwa na watu wanaonitakia mambo mabaya, watu wanaotamani kusikia au kuona nimedondoka na kupoteza maisha papo hapo! Nilishangaa kwa nini watu ambao kipindi cha nyuma ndiyo waliokuwa watu wangu wa karibu, wamenigeuka kiasi hicho?
Uchungu uliponizidia, niliinuka na kuzunguka nyuma ya nyumba yetu, mahali kulipokuwa na makaburi mawili, moja la marehemu baba na lingine la marehemu mama. Nilipiga magoti na kuyainamia, machozi yakawa yananitoka kwa wingi huku uchungu mkali ukizidi kunitesa moyoni mwangu.
“Naomba mnisamehe wazazi wangu! Yawezekana napitia haya kwa sababu sikuyatilia maanani mafundisho yenu, nateseka mtoto wenu, sina mahali pa kuegamia, imefika mahali sioni tena sababu ya kuendelea kuishi,” nilisema huku machozi yakiendelea kunitoka kwa wingi sana.
Waliosema kulia ni dawa hawakukosea, baada ya kulia kwa muda mrefu angalau nilianza kujihisi kama kuna mzigo fulani mkubwa umepungua ingawa macho nayo sasa yalikuwa yamevimba na kuwa mekundu sana. Niliinuka na kuanza kutembea taratibu kurudi ndani huku moyoni nikijiambia kwamba sikuzaliwa kufeli.
Haiwezekani nisome kwa taabu, baadaye Mungu anisaidie nipate kazi nzuri, niwe na familia nzuri na kupata kila ninachokitaka lakini baadaye kila kitu kigeuke na kunifanya nirudi tena kwenye mateso! Niliona ni kitu kisichowezekana na kutoka ndani kabisa ya moyo wangu, niliamua kupambana kiume.
Kwanza nilipata ujasiri wa kukabiliana na tatizo kubwa la Saima, ambaye mpaka muda huo nilikuwa sijui huko aliko kama yuko hai au la! Lakini pia ilikuwa ni lazima nipambane kurejesha kila kilichokuwa changu kisha kikapotea.
Ilikuwa ni kazi ya hatari lakini hakukuwa na jinsi, sikuwa tayari kurudi kwenye mateso yale niliyokulia tangu nikiwa mdogo. Nilikuwa naijua hatari ambayo naenda kukabiliana nayo lakini sikuwa na namna, ilikuwa ni lazima nipambane.
Kwa jinsi nilivyokuwa nimeamua kuishi, sikuwa mtu wa matatizo kabisa na niliamua kuwa hivyo kutokana na historia yangu kutokuwa nzuri kwenye suala zima la maisha yangu binafsi lakini hiki kilichokuwa kinaendelea kwa sasa, kilinikumbusha maisha yangu ya nyuma, nikajikuta nikitamani kurudi kwenye maisha yangu ya zamani, ambayo huwa ni chukizo kubwa kwa wanadamu mpaka kwa Mungu.
“Hata Mungu wangu utakuwa shahidi wangu kwa hili, sina namna! Itabidi tu iwe hivyo,” niliwaza huku machozi yakinitoka tena. Nilisimama na kutembea kikakamavu mpaka nyuma ya nyumba yetu ambayo sasa ilikuwa imechakaa sana.
Nikasogea mpaka pembeni ya mti wa mjohoro, nikaanza kufukua kwa kutumia panga nililokuwa nimelishika. Baada ya kufukua kwa muda, hatimaye nilikutana na kitu nilichokuwa nakitafuta. Nilikitoa kisanduku kidogo cha plastiki, nikageuka na kutazama huku na kule, nilipohakikisha hakuna anayeniona, harakaharaka nilikibeba kisanduku hicho mpaka ndani.
Nikakiweka mezani, nikakifutafuta udongo kwa sababu kilikuwa kimekaa kwa muda mrefu ardhini na baada ya kuridhika na hali yake, hatimaye nilikifungua.
Bado nilikuwa nazikumbuka namba za siri nilizotumia kukifunga, macho yangu yakatua juu ya kitu kilichosababisha nitabasamu! Siyo tabasamu la furaha, la hasha! Tabasamu la kifo, tabasamu ambalo huwa linaonekana usiku wa giza totoro pekee.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Championi Ijumaa.
No comments:
Post a Comment